Wednesday, 5 March 2014

Mahojiano Kati ya Deus Gunze wa Radio Butiama Columbus, Ohio USA na Mohamed Said Akizungumza Kutoka Tanga 2006


Mwaka 2006 mwandishi alichapa makala kuadhimisha uhuru wa Tanganyika 9 Desemba 1961. Katika makala ile mwandishi alimzungumza Dossa Aziz kwa kirefu na mchango wake kwa Nyerere na TANU. Akamaliza kwa masikitiko jinsi Dossa alivyokufa masikini Hospitali ya Tumbi, Kibaha akiwa hawezi hata kumudu kununua shati siku zake za mwisho akiishi maisha ya upweke shamba Mlandizi. Makala hii ilivuta hisia za wengi na watu wakajiuliza mengi kuwa inawezekanaje Dossa akaachiwa ateseke ilhali Nyerere rafiki yake yu hai? Radio Butiama ni radio iliyoanzishwa Ohio Marekani kwa nia ya kumuenzi Mwalimu Nyerere. Mwanzilishi wa radio hiyo Deus Gunze akanipigia simu kutoka Marekani kutaka mahojiano na mimi kuhusu historia ya uhuru wa Tanganyika. Hayo chini ndiyo mazungumzo yetu:

460>_632240
Katika kitabu chake cha "The life and Times of Abdulwahid Sykes (1924-1968): The untold story of the Muslim Struggle against British Colonialism in Tanganyika" mwandishi Mohamed Said anaangalia mchango wa waislam katika harakati za kuleta uhuru wa Tanganyika. Je waislam ndio walioanzisha TAA na TANU? Je ni kweli Mwalimu Nyerere alinyakua TANU toka kwa waislam na kukifanya kuwa chombo cha kanisa? Nani alisaidia sana kuleta uhuru wa Tanganyika kati ya Mwalimu Nyerere na Abdul Sykes? Sikiliza zaidi.
[PLAY]

Historia ya TANU kama inavyoelezwa na wenyewe waliokujachukua madaraka baada ya uhuru mwaka 1961 ni sawasawa na mchuzi uliokosa viungo. Mchuzi wa aina hiyo huwa umepooza. Sasa katika historia hii hii iliyokosa ladha ukaieleze vingine kwa kuileta timu ya Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, Hamza Kibwana Mwapachu, Dk. Luciano Tsere, Dk. Joseph Mutahangarwa, Dr. Vedasto Kyaruzi, Dk. Wilbard Mwanjisi, Steven Mhando, Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Suleiman Takadir, Dossa Aziz, Mwinjuma Mwinyikambi, Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate, Said Chamwenyewe, Tatu bint Mzee, Idd Faiz Mafongo, Idd Tosiri, Idd Tulio, Titi Mohamed...majina ni mengi huo mchuzi uliopooza na kuchujika hupata ladha. Na hii ni timu kutoka Dar es Salaam na ukileta wengine kutoka katika majimbo hapo mambo ndiyo huchangamka khasa...utampata Ali Migeyo, Yusuf Olotu, Bilali Rehani Waikela, Sheikh Yusuf Badi, Salum Mpunga, Yusuf Chembera, Hamisi Kheri, Mohamed Kajembe, Dharura bint Abdulrahmani, Shariffa Bint Mzee, Mama Bint Maalim...majina hakika ni mengi na hawa ndiyo walipigania uhuru wa Tanganyika lakini historia imewasahau.

No comments: