Thursday, 6 March 2014

UAMUZI WA BUSARA WA TABORA Kumbukumbu ya Uchaguzi wa Kura Tatu 1958 na Mohamed Said



UAMUZI WA BUSARA WA TABORA
Kumbukumbu ya Uchaguzi wa Kura Tatu 1958  

na Mohamed Said

 KITABU KIPYA KUHUSU HISTORIA YA KUDAI UHURU WA TANGANYIKA



Katika moja ya misiba ya Tanzania ni kutokuandikwa kwa ukweli historia ya wazalendo walopigania uhuru wa nchi hii. Vitabu vichache vilivyoandikwa vimejikita zaidi katika kujipendekeza kwa viongozi walio madarakani kuliko ukweli wenyewe ulivyokuwa. Hii imeifanya historia ya Tanzania kuwa sawasawa na mchuzi uliokosa viungo. Matokeo yake chakula kinakuwa doro hakina ladha. Sasa ni miaka hamsini toka siku ile kwa mara ya kwanza TANU katika mkutano uliofanyika Tabora ilipoamua kuingia katika uchaguzi mkuu wa kwanza licha ya masharti magumu yaliyowekwa na serikali ya kikoloni. Masharti ya kibaguzi na kudhalilisha ambayo TANU ilipania kuyakataa na kususa kushiriki katika uchaguzi ule kwa sababu mpiga kura alitakiwa ampigie kura Mzungu, Muasia na Mwafrika hna hapo ndipo lilipopatikana jina la kura tatu. Endapo hilo lingetendeka chama pinzani cha wazungu - United Tanganyika Party (UTP) ingepata mteremko na kuzoa viti vyote na hivyo kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. TANU ingebaki nje ya ulingo wa siasa na ikawa msemea pembeni.

Katika kitabu hiki mwandishi anaeleza yale ambayo hayafahamiki kwa wengi ni kwa nini suala la kura tatu lilitishia kuigawa TANU pande mbili. Moja likiwa na Mwalimu Nyerere rais wa TANU na jingine likiongozwa na Zuberi Mtemvu, Sheikh Suleiman Takadir, Said Chamwenyewe, Ramadhani Mashado Plantan na wazalendo wengineo. Katika kitabu hiki mwandishi anamchukua msomaji na kumkutanisha na wazalendo ambao lau kama wanahistoria wa leo wamewapuuza ukweli unabaki palepale kuwa bila ya kuwataja hawa katika historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika na hata historia ya Mwalimu Nyerere mwenyewe basi historia hiyo si tu itakuwa haijakamilka bali itakuwa historia ya uongo.

Mwandishi wa kitabu hiki kwa hakika ni mpiga hadithi kwa jinsi anavyohadithia visa na mikasa iliyowapata wazalendo pamoja na michango yao katika kurasa za kitabu. Mathalan anawajulisha wasomaji wake mzalendo ambae wala hayumo katika vitabu vya historia ya Tanganyika Mzee Mshume Kiyate, dalali wa samaki katika soko la Kariakoo lile la zamani la miaka ya 1950. Katika soko lile mkuu wa soko alikuwa Abdulwahid Sykes mmoja wa wazalendo 17 walioasisi TANU. Abdulwahid Sykes akiuza kadi za TANU pale sokoni. Kwa ajili hii pale sokoni ndipo palipotoa wanachama wa mwanzo wa TANU mmoja wapo akiwa Mzee Mshume Kiyate, mzee aliyeheshimika sana mjini. Pale sokoni Kariakoo ndipo palipokuwa kituo chake cha mwanzo Mwalimu Nyerere alipofikia kila alipotoka Pugu kuja Dar es Salaam akifika pale kumwona Abdulwahid Sykes ofisini kwake na kisha kukutana na wazee wengine wafanyabiashara pale sokoni kama Mzee Mshume Kiyate. Kitabu kinaeleza mchango wa hali na mali wa Mzee Mshume Kiyate kwa Mwalimu Nyerere binafsi na katika Baraza la Wazee wa TANU. 

Kitabu kinamrejesha katika historia Said Chamwenyewe mzalendo aliyetoa kwa niaba ya TANU taarifa ya hali ya siasa ya Tanganyika mbele ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaoshugulikia makoloni ulipozuru Tanganyika mwaka 1955. Said Chamwenyewe ndiye aliyeipatia TANU wanachama wake wa mwanzo kutoka Rufiji. Said Chamwenyewe akipanda baiskeli kutoka Dar es Salaam hadi Rufiji huku akiuza kadi za TANU katika vijiji vya njiani. Kitabu kimepambwa na picha hadimu sana ambazo hazijapata kuonwa na yeyote kabla. Kuna picha ya Mshume Kiyate akiwa na Mwalimu Nyerere, halikadhalika ya Sheikh Suleiman Takadir akiwa na Nyerere na John Rupia na picha ya pamoja ya Mwalimu Nyerere na Dossa Aziz wakiwa na Wazee wa Baraza la TANU ndani yake wakiwemo, Issa Nassir, Sheikh Haidar Mwinyimvua, Mwinjuma Mwinyikambi, Jumbe Tambaza, Sheikh Suleiman Takadir, Mshume Kiyate, Said Chamwenyewe na wengine wengi. Mwandishi kwa ufsaha na ustadi mkuu anaeleza historia ya Yusuf Olotu mzalendo mwingine aliyesahaulika kutokea Moshi ambae peke yake alitembea Kilimanjaro nzima kueneza TANU na ilipofika uchaguzi wa kura tatu ilibidi afanye kazi ya ziada kuwarai Wachagga kujiandikisha kama wapiga kura wakatim mwingine ikibidi ahutubie mikutano kwa Kichagga. Wachagga walikuwa na hofu kuwa endapo watajiandikisha basi serikali ya kikoloni itawaendea kuwadai kodi kwa mali walizonazo.

Mwandishi anahadithia kwa ufasaha mkubwa kisa ambacho kwa muda mrefu ilikuwa siri. Vipi Mwalimu Nyerere aliweza kuwapiku wapinzani wa kura tatu ambao walikuwa wengi katika TANU si tu pale makao makuu Mtaa wa New Street Dar es Salaam bali hata majimboni. Mwandishi anafichua  mkakati wa siri uliopitika Tanga kati ya Mwalimu Nyerere na Amos Kisenge kwa upande mmoja na viongozi wa TANU Tanga uliowakilishwa na  Mwalimu Kihere, Hamisi Heri, Sheikh Rashid Sembe na wengineo. Kitabu kinafichua ujanja wa Mwalimu Nyerere aliokuwanao kiasi cha kuweza kuwazidi maarifa si maadui zake bali hata marafiki zake wa karibu na kupata kile alichoamini yeye kuwa ndiyo mwelekeo unaofaa.

Mwandishi anaeleza jinsi TANU ilivyokuwa imetawaliwa na Uislam kiasi ambacho TANU haikufanya jambo lolote kubwa bila ya kutanguliza dua. Hapa msomaji anaingizwa katika yale ya ndani katika TANU ya wakati ule ya kufanya tawaswil na visomo Mwalimu Nyerere lau kama alikuwa Mkristo akishiriki sawia. Msomaji atapata mengi kwa kusoma kisa cha dua hii maalum kwa ajili ya kura tatu dua iliyosomwa katika kijiji cha Mnyanjani nje kidogo ya mji wa Tanga. Kitabu kinafichua ni ujanja gani aliotumia Nyerere kumwacha nyuma ofisini katibu wa TANU Mtemvu na kumchukua Amos Kisenge badala yake kwendanae Tanga kupanga mbinu ya kupambana na hila za Waingereza. Vipi Mtemvu ambae agenda ya kura tatu ilikuwa yake alikubali apokonywe na kuamini kuwa Nyerere ataitetea kwa niaba ya Waafrika wa Tanganyika ni swali linalotatanisha. Mtemvu aliposhtuka basi lilikuwa limeshamwacha na Nyerere kaondoka. Matokeo yake alijuzulu TANU na kuanzisha chama chake kipya Tanganyika African Congress akiwa na Said Chamwenyewe na wazalendo wengine waliokuwa na msimamo mkali ndanin ya TANU.

Lakini juu ya hayo yote msomaji atavutiwa sana na hotuba mbili za Mwalimu Nyerere alizotoa wakati wa sakata la kura tatu. Hotuba ya kwanza ni ile aliyotoa ndani ya mkutano kiasi ambacho aliweza kuzipiku hoja zote za wapinzani wa kura tatu na ya pili ni ile hotuba ya machozi Mwalimu alipozungumza katika mkutano wa hadhara Tabora sokoni na akalia na kuwaliza wasikizaji wake. Hata hivyo baadhi ya wana TANU hawakuridhika na uamuzi wa TANU wa kuingia katika kura tatu. Walihisi kuwa uamuzi ule haukuwa na maslahi na Waislam ambao ndiyo waliokuwa mstari wa mbele katika kudai uhuru. Walijitoa na kuanzisha chama kipya All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT).

Juu ya hayo yote sijui ni kwa utashi wake mwenyewe mwandishi au ni kwa sababu za uhariri kitabu kimekuwa kimya kwa jambo muhimu sana katika historia ya kura tatu. Mwandishi hakusema nani alipoteza katika kura tatu na nani alipata. Hofu kubwa katika kura tatu ilikuwa itakuwaje Waislam walio mstari wa mbele katika kupigania uhuru leo wanawekwa pembeni na Mwalimu Nyerere analeta watu kutoka nje na wengi wao Wakristo kugombea viti vya TANU? Nukta hii ni katika mambo muhimu sana ndani ya historia ya TANU. Ni katika jambo hili Sheikh Suleiman Takadir alipotofautiana na Mwalimu Nyerere na likapelekea kwa Sheikh Takadir kufukuzwa TANU kwa kosa la kuchanganya dini na siasa. Mwandishi hakugusa hata kwa mbali kisa hiki muhimu. Kwa wale ambao wanaoijua kalamu ya mwandishi huyu hili linaweza likawatatanisha sana. Lakini kitabu kina picha inayomwonyesha Sheikh Takadir akiwa na Mwalimu Nyerere na nyuma yao wamesimama wahamasishaji wa TANU waliokuwa wakijulikana kama Bantu Group iliyopigwa mwaka 1955. Picha hii ya pamoja baina na Sheikh Takadir na Mwalimu Nyerere ni moja ya hazina adhimu katika historia ya Tanganyika kwani inaaminika Sheikh Suleiman Takadir alifutwa kabisa katika historia ya TANU na hakuna popote picha yake inaonekana. Mwandishi anastahili pongezi kwa utafiti wake na kuandika kitabu hiki ambacho kitasaidia kizazi kipya kuwajua wazalendo waliopigania uhuru wa Tanganyika ambao leo hawatajwi. Hakika kitabu hiki kinatia nyama katika mifupa ya historia ya TANU na historia ya Mwalimu Nyerere mwenyewe.
Wednesday, 04 March 2009

Kitabu kinapatikana:
  1. Dar es Salaam Bookshop
  2. Duka la vitabu Chuo Kikuu
  3. Ibn Hazim Bookshop Mkabala na Msikiti Manyema
  4. Duka la vitabu mkabala na Msikiti Kipata
  5. Khartan Bookshop Swahili na Narung’ombe karibu na Kariakoo Bureau De Change
  6. Furaha Bookshop Msimbazi na Uhuru
  7. Amnet Bookshop Msimbazi na Livingstone
  8. Masomo Bookshop Zanzibar
  9. Duka la Maalim Masudi Br ya 12 Tanga
Kwa wanunuzi wa jumla: Abantu Publications Ltd Nyamwezi na Muhuro. Piga simu 0715 090 609 (Said Mrisho) E mai

No comments: