Saturday, 21 February 2015

Twende mbele na turudi nyuma na Ben Rijal



Twende mbele na turudi nyuma
na Ben Rijal

Msemo wa Twende mbele na turudi nyuma ulikuwa ukitumiwa na wazee wetu katika siku za kugombania Uhuru na hata wengine kuhoji nakusema iweje tushakwenda mbele kisha turudi nyuma kipi tuanchokitafuta huko nyuma? Ukiziangalia hoja mbili hizo kila moja ina mantiki iweje ushafika mbele unaangalia nyuma kuna nini unachokitafuta? Kwa mazungumzo ya kawaida utasema hivyo ndivyo, lakini ndani ya maendeleo nikusema kuwa lazima ushafika mbele urudi nyuma kujitathmini, ikiwa umefuzu au umeharibikiwa ndipo utapofanikiwa.

Wengi huwenda mbele tu mithili ya nguruwe mwitu asiojua kwenda mbele na kurudi nyuma. Nilipokuwa nashiriki katika usasi wa nguruwe mwitu mahasidi wa mazao ya wakulima ilikuwa tukifukuza nguruwe saa nyengine humuachia kisha tukafwatilia njia yake ile aliopita nakuweza kumkamata kwa kirahisi kwa kuwa nguruwe mwitu anajua kwenda mbele tu hajui kurudi nyuma. Siku zote kwenye usasi mukimkosa  kumkamata nguruwe aliokuponyokeni kumua inabidi muifwate ile njia muliomkuta kabla kisha kumsubiri siku nyengine mtamkuta kapita hapo hapo bila ya kubadilisha upande ndio saa nyengine utawasikia weledi wakisema umekuwa kama nguruwe mwitu njia yako hio kwa hio?

Najaribu kujenga hoja ili nilitakalo kukieleza kieleweke, katika kwenda mbele na kurudi nyuma, nitaanza na Mapinduzi, neno Mapinduzi kila mwenye lugha yake amelita kwa namna yake mfano Kiafrikana hutamkwa Rewolusie, Ki-Albanian Revolucion, Ki-Arabu Thawra ( ثورة), Ki-Indonesia Revolusi, Ki-Persia Inkilabu (انقلاب), Ki-Vietnam Cuc cách mng, Ki-Welsh Chwyldro neno hilo lina maana mmoja na lengo moja nalo nikufanya na kuleta mabadiliko lakini kila mmoja analitamka kivake.

John Adams Rais wa pili wa Marekani aliyafafanua Mapinduzi  kwa kusema  “mapinduzi  huleta athari kabla hayajatekelezwa, siku zote mapinduzi yapo katika fikra za watu, mapinduzi sio chochote sio lolote lile ila ni mabadiliko yaliomuhimu yakiwa na misingi, hisia na furaha kwa watu hayo ndio mapinduzi ya kweli ya Amerika” na mwanaharakati wa mapinduzi aliojizatiti kutaka kuona haki na usawa katika ulimwengu uliogubikwa na madhila na ubeberu raia wa Argentina aliojiunga na vugu vugu la mapinduzi ya Cuba huyo sio mwengine ni Che Guevera anayachambua mapinduzi kwa kusema “mapinduzi sio tunda la epuli (apple) huanguka wakati linapoiva, ukweli lazima ulifanye lianguke,” na akaendela kusema “moja ya kazi nzito na ya mwanzo ya mapinduzi ni kuelimishwa watu. (“The first duty of a revolutionary is to be educated.” Mapinduzi yametekelezwa kwingi tu duniani kwa lengo kuu lakuleta mabadiliko ya haraka na kuweza kuwaelimisha na kuwafunza wananchi kupata maendeleo na kuishi katika maisha ya matumaini. Mapinduzi yamefanyika Marekani, Urusi, Ufaransa, Nigeria, Ghana hata Zanzibar na kwengineko.

Zanzibar ilijaribu kufwata mkondo ule ule wa kimapinduzi duniani na kujitahidi kuyafanya maisha ya wananchi wake kulingana na kutoa matumaini, kati ya hayo ilikuwa elimu, kilimo, afya, biashara na sekta mbalimbali ziliwekwa mikononi mwa Serikali na kuweza kuiweka nchi ya Kimapinduzi kwa mwananchi wake kuwa na matumaini na maisha yake ya baadae ya kujiweza kujikimu.

Moja kati ya matunda hayo Serikali hio ya mapinduzi ilianzisha kitu kiitwacho BIZANJE ambacho kiliwaweka wananchi kutohangaishwa na maisha yao ya kula na kuvaa, maana ya BIZANJE ni Biashara za Nje na fikra hii iliasisiwa na muumini wa Mapinduzi halisi katika visiwa hivi naye ni Dr. Ahmed Rashid aliokuwa daktari mahiri wa wanyama, msomi huyu aliobobea fikra, yake ilikubalika na Rais wa kwanza wa Zanzibar bada ya mapinduzi, Mheshimiwa Abeid A. Karume kumtaka kuanzishwe kitu hicho nacho ni Biashara za Nje na kilichokuweko kikitekelezwa ni ile dhana ya kijamaa wananchi wote mnatumia kitu cha aina moja au vinavyolingana tena viliopo kwenye viwango, hapo ikawa Michele mizuri ikiliwa na kila Mzanzibari, unga bul bul, sabuni za kila aina iwe Lux, Night Castle, Life Buoy, Pears, Baby Soap zote zikipatikana, maziwa ya kibati yawe Tweco, Ng’ombe wanne n.k. Samli za kila aina bila ya kuisahau Kismayou, kisha aina mbalimbali za nafaka iwe Njugu mawe, Kunde, Maharagwe, sabuni za kufulia Omo, Sunlight na nyenginezo, vitambaa vya suruali kina terelini. Mabuku ya kuandikia na kalamu za kila aina na penseli zake zikiuzwa na kukaribia kusema ni bure.

BIZANJE ilimuwezesha mnunuzi kuona sio ananunua anaona kama anatunukiwa kwani kila mmoja alikuwa awe wa juu au yule hoe hahe wote wakimudu kuvinunua hivyo vitu na kuvifurahia na kusema Shabasha sasa haya ndio maisha.

Bahati mbaya fikra hizi huwa hazikubaliki na wale ambao unyang’anyi na ubepari umewazunguka katika magenzi yao kwahio bahati mbaya ikatokea kwani wale waliokabidhiwa kuendesha BIZANJE ndio waliokuwa wanafuja na hata yale maduka yaliokuwa yakiendeshwa na Serikali yakawa kila siku zikenda zikiwakatisha tama watu kwa kuwa kunaanza kukosekana yale mahitaji ambayo wananchi wakiyafaidi. Ureda ukapotea mambo yakawa ni msege mnege.

Nilizungumza na mmoja kati ya washika usukani katika uongozi nikamwambia wakati umefika kurudisha BIZANJE alinistaajabu na kunambia “watu wanakwenda mbele wewe unarudi nyuma, sasa ni biashara huria, biashara huru anayetaka anaingia kwenye ushindani, siku za Serikali kufanya biashara ziko wapi?” Hakuwa tena anataka kunisikiliza na fikra za kijamaa akaja na mazungumzo mengine kabisa na nikajiona nimepwelewa.

Ukweli sio mwenye kupinga juu ya biashara huru nitasema biashara huru ziwepo na waendelee wananchi kuziendesha hizo biashara lakini bado Serikali ingeweza kuleta vile vya mahitaji yalazima na kuviwekea katika maduka maalumu na kuona hivyo vilivyoletwa vinauzwa katika bei hio iliopangwa itakayowezwa kila mmoja wetu kuimudu, hapo kina Pangu pakavu mithili yangu tungesema Shabash tunarudi tulikotoka kutokana na kujitathmini pale tulipo kwa kurudi nyuma.

Ukiangalia katika pande zote mbili za Muungano fikra kama hizi zilipoasisiwa wengi walishindwa kuzifahamu badala yake wakawa mstari wa mbele kuzivuruga, wengi wanazitamani zirudi hawajui zitarudi kwa njia gani, lakini inawezekana tena sana kama alivyopata kutushauri aliokuwa Naibu Waziri Mkuu wa Malaysia pale ujumbe wa Visiwani ulipotembelea Malaysia mwandishi alikuwemo katika msafara huo, Anwar Ibrahim alitwambia “sio kila kitu mubinafsishe vyengine viendelee kubakia mikononi mwa Dola.” Malaysia waliweza kuwachukua wasomi katika fani mbalimbali nakuwataka waendeshe biashara matokeo yake nikuwa  kutokana na elimu na ujuzi waliokuwa nao walifanikiwa wao kuboresha maisha yao na kuiongezea kipato taifa la Malaysia kwanini nasi hatwendi huko?

Ndipo nilipokuwa nakubaliana na huu msemo Twende Mbele na Turudi Nyuma, kuna haja ya kujitathmini pakubwa sana namna kule nyuma kulivyokuwa patamu kwa wanyonge na sasa namna kulivyokuwa kuchungu kwa watu wa chini na wanyonge. Hebu nijikumbushe anuwani ya kitabu cha  Alan Paton wa Afrika Kusini “Cry, the Beloved Country” na kutafsiriwa katika Gazeti la Muongozi lilokuwa likitoka hapa Zanzibar kila wiki “Lia lia nchi ya Shida.” Mie nitasema Lia lia zamani nakutamani urudi. Haya baba Twende Mbele Turudi Nyuma ndio mafanikio yatapopatikana kinyume chake mambo yataendelea kuwa mazito.

No comments: