Friday, 17 April 2015

KUMBUKUMBU MIAKA 60 YA HOTOBA YA MWALIMU NYERERE UNO MARCH 1955



Mwandishi Akihojiwa na Hassan Abdulla Khamis wa Radio Kheri

Kushoto: Rashid Sisso,Robert Makange, Zuberi Mtemvu, Iddi Faiz Mafongo, Julius Nyerere, 
John Rupia na Bi. Titi Mohamed Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam Kumsindikiza Nyerere Akienda Umoja wa Mataifa New York, 1955


"Baraza la Wazee wa TANU chini ya Mwenyekiti wake Sheikh Suleiman Takadir lilichukua mafanikio ya safari ya Nyerere kwenda UNO kuwa  jukumu lao binafsi. Sehemu ya kwanza ya maandalizi ilitakiwa ifanyike kwa siri sana. Uongozi wa TANU ulikabidhi Idd Faiz kazi ya kuandaa, kukusanya na kusimamia mfuko wa safari ya rais wa TANU kwenda Umoja wa Mataifa, New York. Safari ilikuwa ifanyike mwezi wa Februari, 1955.

Mwaka wa 1953 Idd Faiz alikuwa na umri wa miaka arobaini na tatu, mwenye ari na nguvu tele. Alipokuwa katika kamati kuu ya  ya TANU mwaka wa 1959 aliteuliwa kuwa mweka hazina  wa taifa wa TANU pamoja na kuwa mjumbe wa kamati kuu. Idd Faiz alikuwa mmoja wa viongozi wa chama walioanzisha TANU Press iliyokuwa katika njia panda ya Mtaa wa Mchikichi na Livingstone mjini Dar es Salaam. TANU Press ndiyo ilikuwa ikichapisha na kusambaza jarida  la TANU, Sauti ya TANU lililohaririwa na rais wa chama, Julius Nyerere, na baadaye kuchapisha Mwafrika  chini ya uhariri wa Rashid Heri Baghdelleh na Robert Makange. Kampuni hiyo ya kupiga chapa ilimilikiwa na Mwananchi Development Corporation TANU ilimteua Abdul Faraj kuiongoza kampuni hiyo.

TANU ilihitaji takriban shilingi elfu kumi na mbili kumwezesha Nyerere kusafiri kwenda Umoja wa Mataifa, New York. Kamati ya Abdu Kandoro, Japhet Kirilo na Abbas Sykes ilikuwa imekusanya kiasi cha fedha kutoka majimboni ambacho kilitumika katika ile safari ya Ally na Phombeah kwenda kwenye Pan African Congress mjini Lusaka. Kilichosalia hakikutosha kumpeleka Rais wa TANU, Nyerere Amerika. Ilibidi fedha za ziada zitafutwe kutoka kwa wananchi ili kumwezesha Nyerere kufanya safari hiyo. John Rupia alichangia zaidi ya theluthi moja ya fedha zilizotakikana. Wanachama wengine walichangia kwa uwezo wao wote lakini TANU katika siku zile ikiwa bado changa ilikuwa maskini, kiasi hicho kilikuwa bado kiko nje ya uwezo wake.  Ikitambua ule upungufu wa fedha za safari ya Nyerere, Idd Faiz aliombwa na uongozi wa Al Jamiatul Islamiyya kutoa fedha katika mfuko wa Al Jamiatul Islamiyya na kuzitia katika hazina ya TANU kukiwezesha chama kumpeleka Nyerere New York. Hata pamoja na fedha zile kutoka Al Jamiatul Islamiyya hizo hazikuweza kukidhi haja.

Al Jamiatul Islamiyya haikuwa na jingine isipokuwa kumuomba Idd Faiz asafiri kwenda Tanga na kupata fedha zaidi kutoka huko. Mwalimu Kihere alikuwa tayari amekusanya fedha hizo na alikuwa anasubiri tu zije zichukuliwe na kupelekwa makao makuu.  TANU ilipata habari kwamba yeyote ambaye angeenda Tanga kuchukua fedha hizo kwa ajili ya safari ya Nyerere angekamatwa. Kabla ya kuondoka, Oscar Kambona, Katibu Mkuu wa TANU, na John Rupia, Makamo wa Rais wa TANU, walikwenda kuonana na Idd Faiz nyumbani kwake Ilala kumuaga, kumtakia safari njema na kumpa maelezo kwa ufupi. Safari ya kwenda Tanga haikuwa na tatizo lolote, lakini katika wakati wa kurudi basi ambalo Idd Faiz alikuwamo lilisimamishwa njiani Turiani na makachero. Idd Faiz alikamatwa, akavuliwa nguo na kupekuliwa, lakini hakukutwa na fedha. Hili lilimshangaza na kumchanganya yule afisa aliyemkamata kwa sababu walikuwa na taarifa kwamba Idd Faiz alikuwa amechukua fedha kutoka kwa Mwalimu Kihere kule Tanga. Idd Faiz aliwekwa chini ya ulinzi na kupelekwa Dar es Salaam kwa usaili zaidi wakati wote akiwa analindwa na askari wenye silaha. Baadaye Idd Faiz aliachiliwa huru. Zile fedha za TANU zilifika makao makuu ya TANU Dar es Salaam, salama salimini. Zilizokuwa  zimepewa kubeba msichana mdogo aliykuwa abiria ndani ya basi lile alimokuwa Idd Faiz.

Mnamo tarehe 17 Februari, 1955 Nyerere aliondoka kwenda New York kuhutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa. Nyerere aliiweka wazi nia ya TANU kuwa alikuwa ametumwa na wananchi wa Tangayika kuwasilisha ujumbe ufuatao:

“Kuona kanuni ya uchaguzi ikianzishwa na Waafrika kujiwakilisha katika taasisi zote za umma... Hii tunaamini, ni kwa mujibu wa masharti ya Makubaliano ya Udhamini na Ibara ya 76 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.”

 Mbele ya Umoja wa Mataifa, TANU haikuwa ikidhihirisha tamko lolote jipya, yale yote yaliyowasilishwa pale yalikuwa ni maoni ya kamati ndogo ya siasa ya TAA yaliyowakilishwa kwa Constitutional Development Committee ya Gavana Edward Twining mwaka wa1950. Gavana Twining aliyapuuza mapendekezo ya TAA na badala yake aliendelea na mipango yake ya kuwa na wawakilishi wa  rangi zote katika Baraza la Kutunga Sheria. Ili kuupa msukumo msimamo wake huo serikali ilituma ujumbe wake Umoja wa Mataifa kuipinga TANU uliowakilishwa na I. C. Chopra, Mwasia; Sir Charles Phillips, Mzungu na Liwali Yustino Mponda, mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria wa Newala.

Nyerere alirudi kutoka New York Jumamosi, tarehe 19 Machi, 1955 na alipokelewa uwanja wa ndege na halaiki ya watu. Dossa Aziz anakumbuka kuwa aliruhusiwa pale uwanja wa ndege kuingiza gari yake hadi ndani ya uwanja chini ya  ndege ili kumrahisishia Nyerere kuingia ndani ya gari na kuepuka msongamano wa watu. Dossa Aziz anasema kama isingekuwa kwa msaada huo Nyerere angesongwa sana na watu. Watu walikuwa kila mahali wakisukumana na kusongamana wakijaribu angalau kumtia Nyerere machoni. Watu walikuwa wakiimba na kucheza ëmgandaí, ngoma ya Kizaramo, wakiimba: ëBaba Kabwela Yunoí. Jambo la kushangaza ni kwamba hakuna mtu aliyewahi kuusikia wimbo huu kabla ya siku ile na hakuna ajuaye lini ulitungwa. Ile gari ya Dossa Aziz aliyopanda Nyerere ilisukumwa kutoka uwanja wa ndege hadi nyumbani kwa Nyerere, Magomeni Majumba Sita, kiasi cha kama kilomita ishirini.

Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili. TANU ilifanya mkutano wa hadhara Mnazi Mmoja ambao ulihudhuriwa na umati ambao kamwe haukupata kuonekana Dar es Salaam. Inakisiwa zaidi ya watu 40,000 walikuja kutoka kila upande wa mji kumsikiliza Nyerere. Hakuna mtu aliyekuwa na raha ya kuandika kuhusu mkutano ule na safari ya kihistoria ya Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa kuliko Mashado Plantan katika gazeti lake Zuhra. Mtambo wa gazeti wa Mashado uliokuwa Mtaa wa Ndanda, Mission Quarters ulichapisha nakala za ziada za gazeti hilo na toleo lote liliuzika."

(Kutoka kitabu cha Abdul Sykes)

Chambuzi za historia zinaeleza katika harakati za kudai ukombozi wa Tanganyika haukuhusisha wanaume pekee, bali hata wanawake walikuwa mstari wa mbele kwa hali na mali wakiongozwa na vuguvugu la kisiasa kuanzia Chama cha Waafrika yaani Tanganyika African Association(TAA) na hadi Chama cha TANU-Tanganyika African National Union. Kinara wa kundi la wanawake aliyebakia kwenye kumbukumbu ya kizazi hiki ni Bibi Titi Mohammed. Huyu alikuwa sehemu ya mafanikio ya TANU kisiasa kwa wakati huo.

Mwanamke mwingine ni Mtumwa Kitete, mpika vitumbua na uji aliyekuwa akiishi Mtaa wa “New Street” sasa Lumumba. Huyu alitoa michango mingi ya hali na mali kuchangia TANU. Ndiye anayetajwa na wachambuzi kuwa alitoa mchango wa pesa za mwisho za kuchangia safari ya Mwalimu Julius Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa (UNO), Marekani kueleza kwamba watu wa Tanganyika wapo tayari kwa uhuru na wanaweza kujitawala wenyewe.

Pia Mwamvua Mrisho aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Umoja wa Wanawake wa TANU, ambaye pia ni mke wa Abdulwahidi Sykes, ndiye aliyewapa mawazo kina Abdulwahidi, Dossa Aziz na Abass wamwendee Mtumwa Kitete na kumjulisha juu ya hatihati ya kukwama kwa safari ya Mwalimu Nyerere kwenda UNO.

Nyumba ya Mtumwa Kitete ilipovunjwa katika mtaa wa “New Street” (Lumumba) pahali ulikopita mtaa wa Mkunguni, alipewa kiwanja akajenga Mwananyamala hadi kifo chake.Wanawake wengine ni Tatu Mzee. Katika kitabu chake cha “TANU Woman: Gender and Culture in the Making of Tanganyika Nationalism, 1955-1965” kilichoandikwa na Susan Geiger anawataja wanawake walioshiriki harakati za ukombozi kuwa ni Halima Khamis, Mwamvita Mnyamani, Salma Ferouz, Mashavu binti Kibonge, Binti Kipara, Mwasaburi Ali na Fatma Abdallah.

Wengine ni Halima Selengia Kinabo, Mwamvita Salim and Zainab Khatibu, Mario Kinabo, Violet Njiro, Elizabeth Gupta, Kanasia Tade Mtenga, Natujwa Daniel Mashamba na Lucy Lameck.Wanawake wanaungana na akina Bibi Titi Mohammed kwenye mapambano ya uhuru ni pamoja na Agnes Sahani, Aziza Lucas, Tunu Nyembo, Halima Ntungi, Mwajuma Msafiri, Pili Juma, Mwamvua Kibonge, Zuhura Mussa na Chausiku Mzee.

Lakini kwa baadhi ya upande wa wanaume waliofanya kazi kwa karibu na Nyerere wakati wa harakati za ukombozi wa Tanganyika ni Saadani Abdul Kandoro, John Rupia, Dk Luciano Tsere, Makisi Mbwana, Mwinjuma Mwinyikambi, Idd Tulio, Jumbe Tambaza, Idd Tosiri, Fauzi Mafongo, Salum Abdallah, Dk Joseph Mutahangarwa, Abubakar Mwilima, Dk Vedasto Kyaruzi, Dk Wilbard Mwanjisi, George Magembe, Dunstan Omari na Zuberi Mtemvu.
Chanzo: http://www.kiongozi.co.tz/miaka-53-ya-uhuru-wa-tanganyika/



Jamaa wengi wametaka kujua nini kilitokea baada ya safari ya
 Nyerere UNO. 
Kwa heshima yao naongeza kitu kidogo ili kukamilisha historia hii muhimu ingawa mimi naamini somo limeeleweka. Hapa chini ndipo nilipomalizia safari ya Nyerere UNO 1955:

“Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili. TANU ilifanya mkutano wa hadhara Mnazi Mmoja ambao ulihudhuriwa na umati ambao kamwe haukupata kuonekana Dar es Salaam. Inakisiwa zaidi ya watu 40,000 walikuja kutoka kila upande wa mji kumsikiliza Nyerere. Hakuna mtu aliyekuwa na raha ya kuandika kuhusu mkutano ule na safari ya kihistoria ya
 Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa kuliko Mashado Plantan katika gazeti lake “Zuhra.” Mtambo wa gazeti wa Mashado Plantan uliokuwa Mtaa wa Ndanda, Mission Quarters ulichapisha nakala za ziada za gazeti hilo na toleo lote liliuzika."

Mashado Plantan
 inaaminika ndiyo mwandishi wa kwanza kumwandika Nyerere katika gazeti
lake la Zuhra akimtambulisha kwa kwa wananchi kama ndiyo kiongozi mkuu wa TANU. Hii ilikuwa Agosti 1954 baada ya mkutano wa kwanza wa TANU pale Arnautoglo Hall. (Nakala za gazeti hili zinapatikana Maktaba ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, East Africana).
 

Baada ya mapokezi yale ya
 Nyerere na mwamko mpya uliogubika Tanganyika, Waingereza walijua kuwa siku zao zilikuwa zinahesabika. Father Walsh alimwambia Nyerere achague siasa au kazi ya ualimu. Kwa muda mrefu Abdul Sykes alikuwa akimwambia Nyerere ajiuzulu kazi na ashughulike na TANU lakini Nyerere alikuwa bado hajaamua.

Baada ya kuelezwa hivyo na kuandikiwa barua rasmi
 Nyerere aliichukua barua ile hadi kwa Mzee Mtamila ambae ndiye alikuwa rais wa TANU na Mzee Mtamila akaitisha mkutano wa Halmashauri Kuu na ile barua ikasomwa mbele yao. 

Uamuzi uliofikiwa ulikuwa
 Nyerere na ajiuzulu na TANU itakuwa nyuma yake kwa hali na mali. Kati ya wajumbe wa Halmashauri Kuu walikuwa John Rupia, Bi Titi Mohamed na Bi. Tatu biti Mzee. Mkutano huu muhimu katika historia ya Nyerere ulifanyika nyumbani kwa Mzee Mtamila Mtaa wa Kipata na Sikukuu. Nyumba hii ilikuwa kwenye kona. Hivi sasa nyumba ile haipo tena imejengwa ghorofa. 

Nyerere
 alijiuzulu ualimu na siku alipokuja mjini kutoka Pugu na basi la “Majigo” (basi hili lilipewa jina “Majigo” kwa kuwa mwenye basi lile alikuwa Muhindi ambae abiria akipanda anamnadia kwa kusema, “Majigo juu, majigo juu.” Yaani mzigo juu, mzigo juu) Nyerere moja kwa moja alikwenda ofisini kwa Abdul Sykes Kariakoo Market si mwalimu tena. Kituo cha basi la Majigo kilikuwa Mtaa wa Msimbazi na Agrrey. Nyererealikaa nyumbani kwa Abdul Sykes na mkewe Bi. Mwamvua Mtaa wa Aggrey na Sikukuu kwa muda hadi TANU ilipompatia nyumba Magomeni.

Hapa ndipo katika nyumba ile miaka michache nyuma
 Abdul alijitahidi sana kumshawishi Chief David Kidaha Makwaia ajitoe alikokuwa aje TAA wamchague kuwa rais na kisha waunde TANU na yeye atakuwa rais wadai uhuru na ukipatikana yeye Chief Kidaha atakuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika.

Hii ndiyo historia ya TANU niijuayo mimi na nimeiandika katika kitabu cha
 Abdul Sykes (1998) kwa ajili ya kizazi kijacho.

Naamini ni baada ya kuandika historia hii ndipo katika kumbukumbu ya miaka 50 ya uhuru viongozi wetu waliamua kumtunuku Abdul Sykes medali pamoja na mdogo wake
 Ally.




2 comments:

Unknown said...

hongera sana sheikh muhammad said

Anonymous said...

Hongera kwa kudumisha hati, nyaraka na taarifa za kihistoria Bw Mohammed Said. Hizi kumbukumbu na "visa vya zamani" ni muhimu sana kuchapwa. Ni kazi ngumu kwa anayejua. Unatotwa jasho la maana. Unaujua wajibu wako. Daima tuko nawe na tunakutakia maisha mema , marefu na majaaliwa uendelee kutujuza historia ya watu wetu na nchi yetu ya Tanzania.