Ndugu msomaji ingia hapo chini kwa somo kamili:
Bonyeza Kiungo Iki >> : #post12605365
Bonyeza Kiungo Iki >> : #post12605365
MAKALA YA PROF. IBRAHIM NOOR
Siku
zote, lengo kuu la propaganda ni kuzibaka akili za watu na kugandisha katika
bongo zao yale wanayoyataka wana-propaganda; na wana propaganda hupendelea sana
kuwapata watoto wakiwa wangali wadogo kuwajaza hizo propaganda zao ili hata
wakiwa watu wazima uwe mgando huo umeshatapakaa kama kensa katioka bongo za
walengwa ili zisiweze tena kuganduka. Hawakukosea wavyele wetu waliponena kuwa
“udongo upatilize ungali umaji.”
Na vipi
unaweza kumtambua mtu aliyelishwa propaganda kali, khasa za ubaguzi/ugozi na za
udini? Kwanza utamwona ni mtu ambaye huwezi kumwambia lolote tafauti na zile
sumu alizolishwa akalikubali, hata likiwa na ukweli na mantiki ya hali ya juu
kabisa. Propaganda walizogandishwa bongoni mwao tokea utotoni huwafanya wajione
wanajua kila kitu na wewe huelewi chochote! Wakati ni wao walioseelea na
mtizamo finyu.
Mawazo
ya mtu kama huyo hakika ni ya kusikitisha sana khasa kwa vile wengi wao, baada
ya kuharibiwa akili zao shuleni, uwezo wao wa kufikiri kama bin Adam
anavyotakiwa afikiri kwa kutumie akili yake ili kumtafautisha na mnyama, hupewa
nafasi na wadhifa wa kuweza kuwaathiri watu wengi kwa fikra zao zilizojaa
ubaguzi, kwani fikra zao hujikita katika ufinyu wa propaganda walizomiminiwa
bongoni mwao tokea walipokuwa shuleni utotoni mwao na kuwafanya wakawa hawana
haja ya kujua mengineyo ambayo huenda yakawatoa katika gereza la mawazo mgando
waliyonayo; yaani, wametosheka na yale waliyosomeshwa shuleni hata yakiwa si ya
kweli na yamejaa ubaguzi na udini na yana khatari kwa nchi. Kwa mfano, kiwango
na mgando wa “ilimu” alionao Pasco umempelekea kuandika yafuatayo:
“Tangu
Mlango wake wa Kwanza unaohusu “Taarikh ya Kuwasili Kwa Wabantu, Washirazi na
Waarabu Pwani ya Afrikaya Mashariki.” ameanza na maurongo yaliyokubuhu!”
Anatuelezea
haya hata kitabu hajakisoma! Lakini tusistaajabu, kwani, kama nilivyoeleza, hii
ndio athari na lengo khasa la propaganda.
Waliotekwa na propaganda hawahitajii kusoma chochote kwanza, wao
wameshafanywa, kwa njia za kipropaganda, waamini tokea utotoni mwao fikra
fulani, basi wametosheka nayo. Bila ya kuzisoma hoja na ushahidi uliotolewa
kitabuni na bila ya yeye kututolea ushahidi wowote wenye kuonesha kuwa
yaliyoelezewa kitabuni ni ya “maurongo yaliyokubuhu!” anatutaka tuzikubali
kauli zake kama yeye alivyokubali kumiminiwa propaganda za udini na ubaguzi
alipokuwa shuleni hata ikamfanya yeye binafsi, kuwa na chuki kubwa sana dhidi
ya wale alioambiwa awachukie na kuwabagua. Soma barua yake kwa makini na
utamuona vipi alivyotopea katika chuki na vipi yeye (na wengine kama yeye)
alivyokuwa hahitajii kusoma kwanza kabla hajaamua kumshambulia mwandishi wa
kitabu pamoja na anayodhania ameyaandika! Ni muhimu kwake binafsi kuendelea na
fikra mgando za chuki kuliko kuutafuta ukweli na kuwa mtu huru kimawazo.
La
kusikitisha pia ni kumwona mtu huyohuyo anajinata kuwa kasoma sana na anaelewa
vya kutosha hadi kufika kuwa na “sixth sense.” Mahabusi wa propaganda, khasa
zikiwa za udini na ubaguzi, hawezi kabisa kutumia akili yake na akili hiyo
kumwongoza hadi kufikia uamuzi unaokubali ushahidi wowote wala hoja yoyote
inayopingana ufinyu wa propaganda za ubaguzi na za udini alizojazwa nazo.
Nakariri, propaganda haimruhusu hata kuwa na “comon sense” wacha kuwa na “sixth
sense” kwani mtu huyo huwa kama kasuku anayerejelea yaleyale ya chuki alizojazwa
nazo tokea utotoni mwake. Jinginelo lolote, hata likitolewa ushahidi gani,
hawawezi kulikubali kwani propaganda huwaondoshea hata “common sense."
Sifa ya
pili waliyonayo ni kuwa daima kiumbe kama huyo anataka kulazimisha tukubali tu
yale anayoyaamini yeye. Kwa mfano, lazima iwe ni Wabantu
ndio wenyeji asilia wa pwani ya Afrika Mashariki. Wala hana hamu ya kutaka
kujua nini wameandika mabigwa wa taarikh ya uhamiaji wa Wabantu na lini
wamewasili katika upwa huo, ingawa siku hizi huna haja ya kuvitafuta na
kuvisoma vitabu vya mabingwa wenye kuijua taarikh ya Afrika. Fungua hata
mitandao na uangalie wajuzi wanatuelezea nini kukhusu uhamiaji wa Wabantu na
khasa wapi walipotokea. Hakuna hata mmoja katika mabingwa hao anayedai kuwa
Wabantu walitokea Afrika Mashariki na kuelekea Afrika Magharibi. Wote
wanatuelezea kuwa ama wametoka Afrika Kati na kuelekea mashariki na Kusini, au
wametokea Afrika Magharibi na kuelekea Mashariki na Kusini, na mabingwa wenye
kusema haya ndio wengi zaidi. Fungua mtandao uandike “Bantu Migration” ujionee
mwenyewe kwa maneno na kwa ramani kukhusu uhamiaji wao Wabantu. Lakini, kama
nilivyosema kabla, waliolishwa vidonge vya sumu ya propaganda za udini na
ubaguzi hawawezi kukubali lolote hata likiwa na ukweli wa aina gani ila propaganda
ile ile waliosomeshwa tokea utototoni. Inasikitisha kushuhudia namna na kadiri
ya vidonge vya sumu na chuki zilivyofanya kazi ya kuharibu akili za watoto wetu
katika kuwasomesha historia.
Jambo
linalomuuma zaidi ni kwanini Waarabu waweze kuwa wenyeji wa pwani ya Afrika
Mashariki; hawezi kukubali Mwarabu awe raia wa Tanzania wa daraja ile ile moja
sawa na Mbantu na Mtanzania yoyote yule. La! Hasha. Wao walivyokuwa wabaguzi
kweli, wanataka pawe na matabaka ya uraia. Angalia mfano wa manenno yake
mwenyewe:
“Yaani
hapa huyu Mwarabu, anataka kuwafanyia Afrikanization hawa wavamizi wa Kiarabu
ili kuwahalalisha eti na wao, ni wenyenyeji halali wa Afrika Mashariki…”
Angalia
na mfano mwingine wa ugozi wake:
“Lengo
ni kuzuia kinachoweza kuja kuwapata Waarabu wa Afrika Mashariki na sana sana
Waarabu wa Zanzibar ambao wametoka kwao Omani juzi juzi tuu mwaka 1832
wakiongozwa na Sultan Sayyid Said aliye yahamisha makao yake makuu toka Oman
hadi Zanzibar! Huyu sio tuu ni mvamizi bali pia ndiye mporaji mkuu,
aliyejitwalia visiwa hivyo kama ameviokota as if hakumkuta mtu yoyote ili hali
wenyeji walikuwepo! Siku ile ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar, siungi mkono
mauaji yoyote ya Waarabu, bali wangeambiwa tuu kistaarabu, wafungashe kilicho
chao, wao na wazalio wao, wajirudie kwao Omani walikotoka na kutuachia visiwa
vyetu!”
Yaani
huyu mbaguzi kutoka Bara ambaye Zanzibar si kwao hata chembe anafika kusema kwa
ujeuri kabisa na kwa kinywa kipana kuwa mwenye asili ya Kiarabu hata akiwa ni
wa kizazi cha ngapi hapo Zanzibar asiwe na haki yoyote ya uraia na uananchi,
bali yeye Pasco mzalia na mkaazi wa Bara ana haki zaidi na kamili Zanzibar
kuliko huyo Mzanzibari! Kama maneno haya ya Pasco na wenziwe kama Wahishimiwa
akina Lukuvi na Sitta si onyo kubwa sana kwa Wazanzibari kukhusu nia zao na
lengo lao hawa Wabara wenye chuki dhidi ya Wazanzibari, basi Wazanzibari
endeleeni kulala mkione cha mtema kuni. Ishara zote za ubaguzi wao ziko wazi
kabisa, na mwenye macho haambiwi “tazama.”
Waarabu
wengi, na wengi walikuwa watu wa kawaida tu na wengine walikuwa mafakiri,
waliuwawa kwa ghadhabu kubwa sana na wabara kama hawa, kwa bunduki, mapanga na
mashoka kama nguruwe mwitu, ikisha anatuambia kuwa yalikuwa “Mapinduzi
matukufu.” Yatakuwaje matukufu na ilihali roho za raia wengi sana ziliteketezwa
na wavamizi kutoka Tanganyika ambao tumewashuhudia kwa macho yetu na kuwasikia
kwa lafdhi zao za kibara wakipita mitaani mwetu na kunadi: “Arabu uwa, Muhindi
uwa Muzungu siguse.” Utukufu ni sifa ya Mwenye-enzi Mungu. Mauwaji ya halaiki
ya raia na uraruwaji wa wanawake, ufungwaji wa wengi bila ya sababu,
unyanyasaji, unyang’anyi wa mali za raia, uadhibishwaji wa watu waliokuwa
hawana kosa lolote ila kuwa hawakubaliani na siasa za Karume na Kambarage,
zinakhusiana nini na “utukufu”? Nini kilichotukuka katika kutenda maovu haya
yaliyokatazwa na Mwenye-enzi Mungu Mtukufu?
Pasco
anendelea na haya yafuatayo:
“Prof.
Ibrahim Noor Shariff, ni 'ill motive!' Tangu Mlango wake wa Kwanza unaohusu
“Taarikh ya Kuwasili Kwa Wabantu, Washirazi na Waarabu Pwani ya Afrikaya Mashariki,”
ameanza na maurongo yaliyokubuhu!, hapa anadanganya wazi mchana kweupe kwa
maushahidi yake ya uongo kwamba eti Waarabu wamefika Pwani ya Afrika Mashariki
maelfu ya miaka iliopita kabla ya Wabantu, tangu karne ya 16 B.K! The ill
motive ya mlango huu ni kuonesha kwamba Waarabu si wageni bali ni wenyeji wenye
haki hapa sawasasa kwenye Pwani ya Afrika Mashariki sawa na wenyeji wengineo.”
Kwanza
anaanza kwa kunishambulia binafsi kwa dhana zake mwenyewe wala si kwa hoja
nilizozitoa alipoandika kuwa mimi “ni 'ill motive!'” Tukiacha na Kiingereza
chake chenye makosa, suala ni: amejuaje kama mimi nina sifa mbovu hiyo? Kitabu
hajakisoma alau akadai kuwa amenisoma vizuri kabla hajautoa uamuzi wake huo,
maajabu haya! Aliyekuwa "ill-motivated" ni nani hapa!
Anaonesha
wazi kuwa taarikh ya Waarabu haijui zaidi ya hiyo aliyosomeshwa shuleni
iliyojazwa chuki ndani yake. Hajui kabisa kuwa Waarabu ni watu walioanza
kusafiria Bahari ya Hindi miaka elfu nyingi kabla, na walielewa taratibu za
pepo za Musim na kufikia nchi zote ziliko pwanipwani ya Bahari ya Hindi.
Haelewi kuwa taarikh ya Bara Arabu na nchi za Afrika kama Habash/Ethiopia
zimefungamana kwa zaidi ya miaka elfu kumi. Taarikh kama hiyo haingii katika
hisabu za akili yake! Kama sabini katika mia ya Waarabu wanaasili ya Afrika na
wanaishi Afrika kama ni wenyeji makwao kutoka Sudan hadi Moroko.
Haelewi
pia kuwa Waarabu wengi ni Wasemiti, na jamaa zao wako kutoka nchi za Ghuba hadi
Nigeria. Kuwa Wahausa wa Afrika Magharibi ni katika jamaa zao Waarabu, na
Waethiopia ni jamaa zao wa karibu sana, na hawa wote wako mbali kabisa kiujamaa
na Wabantu. Afrika haina watu wa asili moja tu. Kuna makundi mengi mbalimbali
ambayo Waingereza huita “race.” Nikupe mfano mmoja utakaokufanya ufikiri.
Unadhani Wabaka (mbilikimo) na Watutsi wana asili moja kwa sababu rangi za
ngozi zao zimekoza?
Barua
yake yote Pasco ni mfano dhahiri kabisa wa mtu aliyefunzwa propaganda za udini
na chuki zilizotopea khasa dhidi ya wenye asili ya Kiarabu. Soma na haya
aliyoyaandika kwa kifua mbele:
“Hili swali la Waarabu wamekujaje Pwani ya
Afrika Mashariki, litakuja kurudi tuu mbele ya safari hivyo ushauri wangu, ni
kujituliza tuu na kuishi kwa unyenyekevu wa hali ya juu sana kwa kujihesabu
wanaishi hapo kwa hisani tuu, vinginevyo watatimuliwa warudi kwao Oman
walikotoka, wao na vizalia vyao!.”
“Hizi historia za kutunga tunga kutaka
kuwahalalisha madhalimu hawa waliowauza mababu zetu kama bidhaa! hazitasaidia
kitu! no wonder kila siku wanashinda uchaguzi lakini kamwe hawatakabidhiwa
nchi, na 2015 watashinda tena na moto ni ule ule! Mwarabu atoke kwao, aje
akutawale, babu zako awauze, kisha mumpindue halafu leo mumrudishe eti kisa
amechaguliwa! hii haitakaa itokee!.”
Huyu
kiumbe kutoka Bara anawaambia Wazanzibari wenye asili ya Kishirazi, Kiarabu,
Kihindi na nyinginezo, kuwa hawana haki yoyote ile kwao Zanzibar. Wenye haki ni
wao Wabara! Kama huu si ujeuri mkubwa sana na ubeberu akhasi ya ukoloni, basi
sijui tuuitaje! Ikisha anawaambia Wazanzibari hao kuwa hata wakishinda chaguzi
vipi, wao wakoloni ndio watakaoamua, na wameamua kuwa Zanzibar itabakia kuwa
koloni lao hata Wazanzibari wote wakitaka kutokana na ubeberu huo
unaowakandamiza. Kwa hivyo akina Sefu na Jussa na Mansuri na Moyo na wafuasi
wenu ndiyo mmeshapewa tahadhari na mabeberu wakoloni wepya kutoka bara
wanaotaka kukutieni nyote vitanzi wakunyongeni, msiseme hamkutahadharishwa na
waliyoyakusudia. Kivitendo wameshawauwa Wazanzibari 1961, 1964 na kuendelea.
Wanadhani ukhabithi wao na mauwaji wanayoyafanya mara kwa mara ndiyo
yatawawezesha kuitawala Zanzibar milele. Yaguju!
Huwezi
kuzungumza na mtu ambaye kwake yeye taarikh ya Waarabu Zanzibar na pwani ya
Afrika Mashariki imeanzia na Sayyid Said mnamo Karne ya Kumi na Tisa tu! Ni
shida kubwa sana kumsomesha mtu taarikh asiyotaka kuisikia, na hakuna viziwi
zaidi kuwashinda wale wasiotaka kusikia. Na uziwi unakufika upesi sana iwapo
utotoni umepikwa na propaganda za chuki zinazokusudia kuufunga ubongo wako
usiweze kufikiri kama mwana Adamu anavyotakiwa afikiri.
Ibrahim
Noor
No comments:
Post a Comment