Wednesday, 24 June 2015

KUTOKA RAIA MWEMA: SIASA KATIKA MJI WA DAR ES SALAAM MIAKA YA 1950

Dar es Salaam 1950

http://www.raiamwema.co.tz/siasa-katika-mji-wa-dar-es-salaam-miaka-ya-1950
Makala
Siasa katika mji wa Dar es Salaam miaka ya 1950

Mohamed Said
Toleo la 411
24 Jun 2015



NALIKUMBUKA eneo la Gerezani kama vile ilikuwa jana. Kuanzia mitaa yake hadi nyumba zilizokuwapo pale pamoja na wakazi wake ambao kwangu mimi walikuwa baba, mama, shangazi zangu na wajomba ukiachilia watoto wa rika langu tuliokua tukicheza pamoja. Mitaa takriban yote ilikuwa ni barabara za vumbi tupu lakini mchanga.

Kwa sisi watoto hii ilikuwa afueni maana tuliweza kucheza tukakimbizana bila ya madhara ya kuumia sana endapo mmoja wetu ataanguka.Mchezo tuliokuwa tukiupenda sana ulikuwa mpira wenyewe tukiita”chandimu”. Mtaa wetu ulikuwa unaitwa Kipata Street. Jina hili wengi hawalijui asili yake lakini ni moja ya vijiji ambavyo “mvumbuzi” David Livingstone alivipitia katika safari zake kwenda Nyasaland.
Mtaa wa mbele ya Kipata ni mtaa maarufu wa Kitchwele Street sasa unaitwa Mtaa wa Uhuru. Hakuna ajuaye hili neno “Kitchwele” nini maana yake. Lakini mtaa huu umepata heshima kubwa kwa kubadilishwa jina na kuitwa “Uhuru,” Tanganyika ilipojikomboa kutoka ukoloni wa Waingereza tarehe 9 Desemba 1961.

Nyuma wa Kipata Street ulikuwa mtaa wa Kirk Street sasa unaitwa Mtaa wa Lindi. Asili ya jina la Kirk ni Consular John Kirk aliyekuwa akitazama maslahi ya Waingereza Zanzibar. Sasa wazee wetu walikuwa hawawezi kulitamka jina hilo kama litakiwavyo badala yake wakawa wanasema “Kiriki” jina lililodumu hadi mtaa ulipobadilishwa jina.

Nakumbuka kibao chake cha mtaa kiliandikwa kwa wino mweupe kwenye kibao cheusi “Kirk Street.” Nyuma ya Kirk Street ulikuwa mtaa wa Somali na nyuma ya Somali kulikuwa “Kiungani Street.” Asili ya jina hili ni Kiungani Zanzibar ambako Universities’ Mission to Central Africa (UMCA) ilijenga kanisa lake la kwanza pwani ya Afrika Mashariki katika miaka ya 1800.

Sasa tuingie katika mitaa ya kukatisha. New Street ndiyo ilikuwa inatengeanisha Gerezani na Uwanja wa Mnazi Mmoja, kisha inafuatia mtaa wa Livingstone, Sikukuu, Swahili, Nyamwezi, Congo na mwisho Msimbazi. Kisha kulikuwa na mitaa miwili midogo, Somali Kipande na Mbaruku.
Kwa wakati ule kwa ajili ya udogo wangu ilikuwa shida sana kupambanua kuwa majina ya mitaa hiyo ya Kipata, Kirk, Livingstone na Kiungani ilikuwa ni kiashiria kuwa Tanganyika ilikuwa chini ya ukoloni wa Waingereza. Kwa Waingereza majina hayo yalikuwa yanawakumbusha mashujaa wao akina David Livingstone, Morton Stanley na ushawishi wao katika sehemu ambazo Waingereza walituma watu wao ama kuja “kuzivumbua” au kutawala.
Juu ya hayo, Gerezani ilijipambanua na mitaa mingine ya Dar es Salaam kwa kuwa na wapigania uhuru wengi waliokuja kutoa mchango mkubwa katika TANU. Lakini kwa bahati mbaya sana kwa hao wazalendo wote mchango wao haujathaminiwa wala hakuna leo mtu anayewafahamu au kuwakumbuka.
Sasa hebu tuanze matembezi ya nyumba kwa nyumba kuzipitia nyumba walokuwa wakiishi wazalendo wapigania uhuru wa Tanganyika ili tuwakumbuke na tueleze yale waliyofanya wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.
Sasa hebu tuanze Kipata Street inapoanza Gerezani. Kipata Street inaanzia kule Msimbazi. Pale kulikuwa na nyumba ya Abdallah Salum Matimbwa akifanya kazi Relwe. Nyumba yenyewe ya asili leo haipo. Mtoto wa MZee Abdallah Salum Matimbwa, Salum Matimbwa amejenga ghorofa. TANU ilipoanzishwa Abdallah Salum Matimbwa alikuwa mmoja wa wanachama wake wa mwanzo mwanzo lakini kwa kuwa wakati ule kudai uhuru lilikuwa jambo la hatari na yeye alikuwa mwajiriwa alijiunga TANU na kuwa mwanachama kwa siri. Halikadhalika alikuwa mwanachama wa Zaramo Union chama cha kikabila kikiendeshwa na Max Mbwana.
Vyama hivi vya kikabila Waingereza wakivipenda sana kwa kuwa viliwasaidia katika ile njama yao wa “wabague uwatawale” Salum Matimbwa anaingia katika historia ya ukombozi wa Tanganyika si tu kama mwanachama wa awali waliojiunga na TANU kabla ya 1958 bali kama mmoja wa wazalendo waliochanga fedha kuanzisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Fikra ya kuanzisha Chuo Kikuu inasemekana ilianza na Nyerere akiwa na Dossa.
Ilkuwa kawaida ya Dossa baada ya mikutano ya TANU pale Mnazi Mmoja kumchukua Nyerere na gari lake kumrudisha Pugu. Njia ya zamani kwenda Pugu ilikuwa inapita hapo kilipo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Sasa ilikuwa kiza kimeingia na walitaka kutoka nje ya gari kuangalia mandhari ya Dar es Salaam maana kutokea pale mji ulikuwa unapendeza sana kwa taa zilizokuwa zikiwaka barabarani.

Nyerere alimwambia Dossa, “Dossa tukipata uhuru wetu hapa lazima tujenge Chuo Kikuu.” Hili wazo lilifanyiwa kazi na wananchi wakahamasishwa kuchangia ujenzi wa Chuo hicho. Fedha zilichangwa na chuo kikajengwa pale New Street kwenye kiwanja cha John Rupia alichokitoa kuwapa TANU. Hapo ndipo kilipoanza Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Abdallah Salum alikuwa mmoja wa wachangiaji wa chuo hicho na mwanaye Salum Matimbwa hadi leo amehifadhi stakabadhi ya malipo ya shilingi 50 stakabadhi ambayo ina saini ya Joseph Nyerere. Wazee hawa walikuwa wazalendo wa kweli kabisa. Baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 na zilipokuwa zikianzishwa harakati za ushirika Abdallah Salum Matimbwa alitoa lori lake Commer Fargo DSY 435 kama mtaji kuingiza katika Coast Region Transport Company (CORETCO).
Pamoja naye katika kuanzisha CORETCO walikuwa wazee wengine kama Sharia Bofu na nduguye Ibrahim Bofu, Salum Kambi, Juma Mzee na wengineo.
Unateremka sasa Kipata unaelekea Mnazi Mmoja. Kipata kona na Congo kulikuwa na nyumba ya Ibrahim Hamisi mmoja wa waasisi wa African Association mwaka 1929. Huyu alikuwa Mnubi kutoka Darfur.
Baba yake alikuwa askari wa Kinubi waliokuja Tanganyika na Kamanda wa Kijerumani Von Wissman kuja kuwasaidia Wajerumani katika vita yao dhidi ya wazalendo wa Tanganyika akina Bushiri bin Harith wa Pangani na Chifu Mkwawa kutoka Kalenga.
Ibrahim Hamisi akifanya kazi Government Press kama “composer.” Wajerumani walikuwa wajanja na wepesi katika kulipa fadhila. Waliwasomesha vizuri sana watoto wa askari wao waliowaleta Tanganyika kuja kuwasaidia kutawala. Kwa njia hii waliweza kujenga tabaka la wageni lililokuwa juu kupita wenyeji wa Dar es Salaam, Wazaramo, Wamashomvi nk.

Hali hii kwa kiasi fulani ilileta migogoro baina Wamanyema, Wazulu na Wanubi kwa upande mmoja ambao walionekana kama “watu wa kuja” na wenyeji wazawa wa Dar es Salaam kwa upande mwingine.
Kwa wakati ule kazi ya “composer” ilikuwa kazi yenye hadhi kwa Mwafrika na ilihitaji mtu aliyesoma. Ibrahim Hamisi alikuwa mmoja wa waasisi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika chama cha Waislam kilichoanzishwa mwaka 1933 na kikajenga shule Al Jamiatul School New Street kona na Stanley Street ambayo jengo lake lipo hadi leo Mtaa wa Lumumba na Max Mbwana. Uongozi wa Al Jamiatul Islamiyya ndani yake mlikuwa na Waarabu, Wanubi, Wazulu, Wamanyema, Wazaramo na makabila mengine ya pwani na mara nyingi Wazulu na Wanubi ndiyo wakishika uongozi.
Na hii ilipata kuleta mgogoro mkubwa mwaka 1940 kiasi cha kufunga shule na kwa muda hadi Gavana akaingia kati kusuluhisha. Hii Ilikuwa katika Ali Aljamiatul Islamiyya lakini hata katika African Association mambo yalikuwa hivyo hivyo. Mwaka wa 1933 kulitokea ugomvi uliosababisha secretary Kleist Sykes asuse chama hadi alipoombwa na Mzee bin Sudi aliyekuwa Rais wa jumuiya hiyo ndipo aliporejea tena katika chama. Mzee Bin Sudi alikuwa Mmanyema. Hizi ndizo zililiwa siasa za wakati ule.
Mbele ya Kipata Street ukishapita Swahili Street unafika nyumba ya Hassan Machakaomo. Kizazi kingine cha wageni kutoka nje ya mipaka ya Tanganyika. Hassan Machakaomo ni mtoto wa Machakaomo Mzulu askari mamluki kama walivyokuwa Wanubi. Wazee wake waliletwa Tanganyika na Von Wissman kuja kuwasaidia Wajerumani kupigana vita dhidi ya wazalendo wa Tangnayika waliokuwa wanapinga utawala wa Wajerumani.
Hassan Machakaomo alijulikana zaidi kama kiongozi wa Young Africans Football Club katika miaka ya 1950 na harakati za kudai uhuru zilipoanza mwaka 1954 Young Africans, “Yanga” kama ilivyokuwa inajulikana ilijinasibisha moja kwa moja na bila ya kificho na TANU.
Si mbali na nyumba hiyo kwa mkono wa kulia Kipata kona na Sikukuu ilikuwa nyumba ya Clement Mohamed Mtamila ambaye katika miaka ya mwisho ya 1940 ndiye alikuwa Katibu wa TAA baada ya African Association kubadilisha jina na kuitwa TAA. Hapa itabidi tusimame kidogo.
Baada ya Vita ya Pili ya Dunia vijana askari waliokuwa katika King’s Africa Rifles (KAR) 6thBatallion waliopigana Burma katika wengi wao wakiwa Dar es Salaam walianza kuwachachafya viongozi wazee waliokuwa wakiongoza TAA.
Rais wa TAA wakati ule alikuwa Mwalimu Thomas Plantan mtoto wa Afande Plantan mkubwa wa askari mamluki wa Kizulu aliokuja Tanganyika na Von Wissman. Afande Plantan alikuwa ndiye kiongozi wa askari wa Kizulu na mkubwa wa Wazulu wote pale mjini.
Afande Plantan hakutoroka na Von Wissman kurudi kwao Msumbiji baada ya Vita ya Kwanza kumalizika na Jeshi la Wajerumani kushindwa wakawa sasa wanatoroka kukimbilia Msumbiji kupata hifadhi. Afande Plantan alibaki Dar es Salaam na kuweka makazi yake Mtaa wa Masasi Mission Quarter.
Mtoto wa Plantan, Thomas, akijulikana kwa jina lingine la Sauti alipata elimu nzuri katika shule ya Kijerumani akawa mwalimu wa shule. Thomas Plantan alistawi hadi kufikia kushika uongozi wa African Association. Sababu ya uongozi huu wa wazee kuchachafwa ni kuwa vijana walikuwa wakiona chama hakina malengo ya kudai uhuru wa Tanganyika.

Kwa hakika chama kilikuwa kimezorota sana. Mikutano ilikuwa haiitishwi na chama kilikuwa hakina fedha za kuweza kujiendesha. Hapa ndipo tunakutana na kijana Abdulwahid Sykes, mtoto wa Kleist Sykes, (Mzulu mwingine) yeye na kundi la vijana wenzake, Dossa Aziz, Hamza Mwapachu, Stephen Mhando, Dr Vedasto Kyaruzi wakawa wanatafuta njia za kuingia katika uongozi wa TAA. Tatizo lililowakabili ikawa wazee hawataki kuachia hatamu za uongozi wala kuitisha mkutano wa uchaguzi.
Thomas Plantan alikuwa mwindaji na alitumia muda wake mwingi porini kuwinda, hakuwa na muda na siasa za mjini. Hata miaka mingi baada ya kifo chake, bado kuta za nyumba yake Masasi Street, Mission Quarter zilipambwa na vichwa vya pofu na mbogo aliowaua porini. Hata hivyo walikuwapo wazee ambao ingawa walikuwa watu wazima lakini walikuwa wanataka kuona mabadiliko katika TAA.

Mmoja wa wazee hawa alikuwa Schneider Plantan, mdogo wake Thomas Plantan. Katika mkutano ulioitishwa Arnautoglo Hall mwaka 1950, Schneider alifanya vurugu mbele ya maofisa wa kikoloni kiasi ilibidi wazee wakubali kuitisha mkutano wa uchaguzi, lakini kabla ya uchaguzi kufanyika Abdulwahid Sykes na Hamza Mwapachu walivamia ofisi za TAA pale New Street na kuchukua uongozi kwa nguvu wakaitisha mkutano wa uchaguzi na Dk. Vedasto Kyaruzi akachaguliwa Rais na Abdulwahid Sykes akawa Katibu Mkuu. Hii ilikuwa mwaka 1950.
Inasemekana harakati za kupanga mipango ya kufanya mapinduzi katika TAA ilikuwa ikipangwa Ilala Welfare Centre ambako Hamza Mwapachu alikuwa akifanya kazi kama Welfare Officer, mahali pengine ilikuwa Kariakoo Market ambako Abdulwaihd alikuwa Market Master.
Tuachie hapa, tutakuja kuyazungumza haya huko mbele. Turudi kwenye nyumba ya Mzee Mtamila. Nyumba hii leo haipo, ilipokuwa nyumba ya Mzee Mtamila kuna gorofa na si watu wengi wanofahamu historia iliyopata kubebwa na nyumba ile.
Ilikuwa katika nyumba ile ndipo Julius Nyerere aliposhauriwa na Halmashauri Kuu ya TANU chini ya uenyekiti wa Mzee Mtamila ajiuzulu ualimu aiendeshe TANU. Hii ilikuwa baada ya Nyerere kurejea kutoka Umoja wa Mataifa mwaka 1954 na wakoloni wakaona jinsi TANU ilivyokuwa ikipata nguvu siku hadi siku.
Mmoja wa viongozi katika Halmashauri hii ya TANU ya 1955 waliomshauri Nyerere aache kazi ya ualimu aendeshe TANU alikuwa Tatu bint Mzee na Idi Faizi Mafongo. Mafongo ndiye alikuwa Mweka Hazina wa Al Jamiatul Islamiyya na Mweka Hazina wa TANU vilevile.
Leo hakuna anaewajua watu hawa wala historia haiwataji lakini walifanya kazi kubwa sana. Iddi Faizi Mafongo ndiye aliyefanikisha ukusanyaji wa fedha za TANU zilizotumiwa kumpeleka Nyerere Umoja wa Mataifa, New York na alichota fedha nyingine katika hazina ya Aljamitul Islamiyya kutunisha mfuko wa TANU.
Hili la kuchota fedha za Al Jamiatul Islamiyya halikuwa na shida yoyote kwani Katibu wake alikuwa Ali Mwinyi Tambwe mmoja wa watu wa mwanzo kujiunga na TANU. (Tutaona huko mbele Ali Mwinyi Tambwe aliingia vipi TANU na mchango wake katika kuiangusha serikali ya Zanzibar mwaka 1964 jambo lililokuja kumtia simanzi na huzuni kubwa kwa yale yaliyokuja kutokea – mauaji yaliyokuwa hayana sababu na maonezi ya kipuuzi kabisa).
Licha ya hilo, Abdulwahid na Ally walikuwa na sauti katika jumuia hiyo kwa kuwa ilianzishwa na baba yao na walisoma Al Jamiatul Islamiyya Muslim School.
Tatu bint Mzee, Bi Hawa Maftah, Bi Titi Mohamed, Mwalimu Sakina Arab na wanawake wengine wa mjini ndiyo waliotia nyimbo za Lelemama katika kwaya ya TANU nyimbo ambazo zilihamasisha watu kupita maelezo. Kuna nyimbo moja ilikuwa inaimbwa hivi:
“Muheshiwa nakupenda sana,
Wallahi sina mwinginewe,
Insha Allah Mungu yupo,
Tanganyika tutajitawala”

Hii ndiyo ilikuwa nyimbo ya mwanzo ya lelemama kutiwa katika harakati za kudai uhuru na baada ya hapo zikaja nyingine nyingi lakini maarufu na inayofahamika zaidi ni “Hongera Mwanangu”.
Mzee Mtamila ameacha hazina kubwa sana ya picha za siku za mwanzo za harakati za kudai uhuru zikionyesha wana TANU katika mikutano ya mwanzo Mnazi Mmoja. Inaaminika picha hizi zilipigwa na Mzee Shebe ambae studio yake ilikuwa Livingstone Street si mbali na nyumbani kwa Mzee Mtamila.
Baadhi ya picha zikimuonyesha Mzee Mtamila, Bibi Titi Mohamed, John Rupia wakiwa wamekaa katika jukwaa huku Mwalimu Nyerere akihutubia wananchi.
Ukivuka Kipata mbele unakutana na Livingstone Street, ukitazama mkono wa kulia kabla ya kufika New Street labda nyumba tatu kabla pale ndipo ilipokuwa nyumba ya Kleist Sykes, Mtoto wa Sykes Mbuwane, askari wa Kizulu aliyekufa maji Mto Ruaha akiwa anarudi vitani baada ya kumshinda Mkwawa.
Hii ilikuwa mwaka wa 1898. Kuna kisa kitatokea miaka 56 baadaye kati ya kizazi cha Mtwa Mkwawa na Sykes Mbuwane. Wajukuu wao watakuwa wamoja katika TANU kupambana na ukoloni. Nitakieleza kisa hicho kwa ufupi.
Mwaka 1954 fuvu la Mkwawa liliporudishwa Kalenga, Adam Sapi Mkwawa mjukuu wa Mtwa Mkwawa aliwaalika Abdulwahid Sykes mjukuu wa Sykes Mbuwane, adui wa babu yake na Dossa Aziz kuja katika sherehe ya kupokea fuvu lile.
Ilikuwa pale Kalenga ndipo Abdulwahid alipomuingiza Adam Sapi katika TANU kwa siri na kumfanya awe mmoja wa machifu wa mwanzo kabisa kuiunga mkono TANU. Wakati Chifu Adam Sapi anajiunga na TANU chama kilikuwa hakijamaliza hata mwezi moja katika uhai wake.
Tutazieleza habari za Abdulwahid Sykes na ushawishi mkubwa aliokuwa nao katika TAA na baadae TANU na katika wanasiasa wa wakati ule pamoja na machifu tutakapofika kusanifu makazi yake pale Stanley Street kona na Sikukuu Street. Baada ya Uhuru mtaa huu ulikuja kubadilishwa jina na kuitwa Aggrey. Ila ieleweke tu kuwa kwa wakati ule wa siku za mwanzo za harakati kuanzia enzi za TAA baadhi ya machifu hawakuitazama TAA na baadae TANU kwa jicho zuri sana.
Hofu kuu na ndiyo hofu aliyokuwanayo mshirika wao Muingereza katika ule mfumo “indirect rule” wa Lord Lugard ni kuwa TANU imekuja kuwanyang’anya madaraka yao.
Sasa turejee kwenye nyumba ya Kleist Sykes hapo Kipata. Kwa hakika Kleist alikuwa mtu wa mipango na mjengaji wa mikakati si tu katika maisha yake binafsi bali hata katika kupeleka mbele maslahi ya Waafrika katika Tanganyika. Kleist alizaliwa Pangani mwaka 1894. Akiwa na umri mdogo wa miaka 25 alikuwa keshaasisi African Association mwaka 1929 na kufikia mwaka 1933 aliasisi Al Jamiatul Islamiyya Fi Tanganyika, hicho ni Kiarabu (maana yake kwa Kiswahili ni “Umoja wa Waislam wa Tanganyika”).
Mwaka wa 1924, Dk. Aggrey alikuja Tanganyika kama mjumbe katika kamisheni moja ya elimu kuchunguza hali ya elimu kwa Waafrika wa Tanganyika. Kwa wakati ule Dk. Aggrey alikuwa mfano wa Mwafrika aliyeelimika sana. Alipokuwa Dar es Salaam, Aggrey alikutana na Kleist na katika mazungumzo Dk Aggrey alimshauri Kleist kuwa endapo Waafrika wanataka kupiga hatua ni lazima waunde umoja wao. Ilimchukua Kleist miaka mitano hadi kuja kufanikisha ushauri ule na kuunda African Association akiwa katibu muasisi.
African Association na Al JAmitul Islamiyya ndivyo vilivyokuja kuwa chimbuko la kuundwa kwa TANU kwa kutoa viongozi kama Abdulwahid na Ally Sykes, Ally Mwinyi Tambwe, Iddi Faizi Mafongo, Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Abdalla Iddi Chaurembo, Sheikh Suleiman Takadir na wengineo na wanachama wake wa mwanzo. Kleist alilelewa nyumba moja na Thomas, Schneider na Mashado Plantan baada ya kifo cha baba yake.
Hapa ningependa kidogo kuwaeleza wasomaji asili ya majina haya ya Kikristo na yenye asili ya Kijerumani. Hawa watoto baba zao walikuwa askari katika jeshi la Wajerumani. Wajerumani baada ya kuituliza Tanganyika kwa mtutu wakaliita lile jeshi lao la mamluki wa Kinubi na Wazulu “Germany Constabulary.” Mkubwa wa jeshi hili alikuwa Afendi Plantan, baba yao Thomas, Schneider na Mashado.

Sasa inasemekana wakizaliwa watoto, Wajerumani ndiyo walikuwa wakitoa majina kwa watoto hao na majina waliyowapa ni ya Kijerumani ndiyo kukawa na Kleist, Thomas, Schneider, Mashado na mengineyo. Lakini wakiondoka tu palepale baba zao wakawa wanatoa majina ya Kiislamu kwa kuwa wao walikuwa Waislamu hawakupenda sana watoto wao wajulikane kwa majina ya Kikristo.

Kwa mfano Kleist jina lake ni Abdallah, Shneider jina lake ni Abdillah na Mashado jina lake ni Ramadhani. Hadi leo kwenye kaburi la Kleist pale Makaburi ya Kisutu jina lake limeandikwa: “Kleist Abdallah Sykes.” Haieleweki kwa nini yeye hakupenda kujinasibu na jina lake la asili “Mbuwane” au “Abdallah” na kwa nini watoto wa Plantan kwa jina lao la asili la “Mohosh” ambae huko kwao Kwalikunyi Msumbiji alikuwa chifu wa Kizulu.
Sasa zaidi ya miaka mia moja ukoo wa Sykes umevuma na kujulikana katika siasa na biashara kwa jina hilo la Kijerumani na hadi leo ukoo wa Plantan ambao uko Mission Quarter, Mtaa wa Masasi ni katika koo maarufu sana Dar es Salaam nao wanajulikana kama akina Plantan.
Kleist alisoma shule ya Kijerumani na shule yenyewe ndiyo hii sasa Hospitali ya Ocean Road . Alisoma hadi darasa la sita na alipomaliza shule hapo alikuwa anasema Kijerumani, anajua short hand (hati mkato) na kupiga taipu. Huu ulikuwa ujuzi mkubwa sana kwa Mwafrika kuwa nao wakati ule.
Lakini alipomaliza shule Wajerumani hawakumwacha afanye kazi ofisini walimtia katika jeshi na Vita Vya Kwanza vilipoanza mwaka 1914 Kleist na ndugu yake Scheneider Plantan walijikuta wakielekea Tanga kupambana na majeshi ya Kiingereza. Mkuu wa majeshi ya Kijerumani alikuwa Von Lettow Voberk na Kleist ndiye alikuwa Aide De Camp wake. Cheo kizito sana wakati ule kwa Mwafrika kukibeba. Baada ya vita na kushindwa kwa Wajerumani baadhi ya askari wa Kizulu walikimbia na kamanda wao Vorbeck na kuingia Msumbiji. Wazulu waliobaki Tanganyika walikuwa wamepwelewa.
Kleist alikuwa mateka wa vita na alipoachiwa alianza kujifunza Kiingereza na hakutaka tena kujiunga na jeshi. Habari za Kleist ni nyingi sana na mengi katika maisha yake aliandika kwa mkono wake mwenyewe. Mwaka 1969 mjukuu wake, Daisy Sykes Buruku, kwa msaada wa baba yake, Abdulwahid Sykes na akiwa chini ya Profesa John Illife wa Chuo Kikuu Cha Cambridge wakati ule, Iliffe akisomesha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Daisy akiwa mwanafunzi wake alikuja kuandika upya maisha ya babu yake “Kleist Sykes The Townsman” katika kitabu “Modern Tanzanians” kilichohaririwa na John Illife.
Katika kitabu hicho Kleist anatoka kama mwanasiasa makini na muasisi wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Kleist alifanya mengi Dar es Salaam, alijenga shule Al JAmiatul Muslim School, jengo la TAA ambamo TANU ilikuja asisiwa mwaka 1954, alikuwa katika baraza la Manispaa, memba wa Dar es Salaam Maulid Committee, alikuwa kiongozi wa chama cha Wafanyakazi wa Relwe, alikuwa mfanya biashara mkubwa na mwanachama wa Chamber of Commerce na Mwafrika pekee katika chamber.
Kleist aliwanunulia vyombo vya muziki wanae wakati huo vijana wadogo baada ya Abdulwahid na Ally kurudi vitani Burma mwaka 1945 walipokwenda kupigana kama askari katika KAR. Wanae pamoja na vijana wenzao wa mjini kama Matesa, Said Kastiko, James Msikinya (huyu alikuwa ametokea Afrika ya Kusini), Dome Okochi Budohi na nduguye akiitwa Martin (hawa walikuwa wanatoka Kenya) wote hawa wakaanzisha bendi iliyojulikana kama “Skylarks.”
Baadaye walibadili jina na kujiita “Merry Blackbirds” Kleist mwenyewe akiwa mlezi wa bendi na akihudhuria maonyesho ya bendi hiyo. Kulikuwa na bendi kama hiyo siku zile Johannesburg ikiitwa “Skylarks.”
Hili ni kundi ambalo Miriam Makeba wakati huo msichana mdogo alikuwa akiimba. Bendi hii ikaja tena baadaye kubadili jina na kuitwa “Merry Makers.” Bendi hii ilipendwa sana na vijana wa mjini wa wakati ule hasa kwa kuwa wao walipiga ile mitindo ya Ulaya kama Waltz, Foxtrot, Quick Step nk.
Bendi hii ikipiga nyimbo zilizokuwa maarufu wakati ule wa vita si Tanganyika tu bali hata Ulaya kama “More,” Chacanuga Chouchou,” “Siboney,” “Siboney,” “Fly Me to The Moon,” “Perfidia” na nyinginezo, nyimbo ambazo zilipewa umaarufu na wanamuziki wakubwa wa Amerika na Uingereza kama Glenn Miller, Louis Armstrong, Charlie Parker, Benny Goodman, Andrew Sisters na wengineo.

Tufuatilie mtandaoni:

      
Wasiliana na mwandishi
Mohamed Said
msaid.ms94@gmail.com
Mwandishi ni mwanahistoria, mwandishi na mtafiti mashuhuri hapa nchini

Toa maoni yako


- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/siasa-katika-mji-wa-dar-es-salaam-miaka-ya-1950#sthash.bcxHulse.dpuf

No comments: