Video ya mazungumzo na Kumbukizi ya Mwl. Nyerere In Sha Allah itawekwa...
Waliokuwa Katika Picha Hii na Ndilo lilikuwa Baraza la Wazee wa TANU
(Wengine: Hawapo)
- Abdallah Shomari (Tandamti No. 3)
- Nassoro Kalumbanya (Simba)
- Said Chamwenyewe (Aggrey/Congo)
- Mtoro Ally (Muhonda)
- John Rupia (Misheni Kota)
- Julius Nyerere (Pugu Sekondari)
- Said Chaurembo (Congo/Mkunguni)
- Jumbe Tambaza (Upanga)
- Sheikh Suleiman Takadir (Mafia/Swahili)
- Dossa Aziz (Mbaruku/Somali Kipande)
- Mshume Kiyate (Tandamti)
- Juma Sultani (Kitchwele Karibu na Kanisa Dogo)
- Maalim Shubeti (Masasi/Likoma)
- Rajab Simba (Kiungani)
- Waziri Mtonga (Kilosa 18, Ilala)
- Mwinjuma Mwinyikambi (Mwananyamala)
- Makisi Mbwana (Aggrey/Congo)
- Usia Omari (Sungwi, Kisarawe)
- Sheikh Issa Nasir (Bagamoyo).
Baraza
la Wazee wa TANU lilichukua mafanikio ya safari ya Nyerere UNO kuwa jukumu lao binafsi. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU alikuwa Sheikh Suleiman Takadir. Sehemu ya kwanza ya
maandalizi ilitakiwa ifanyike kwa siri sana. Uongozi wa TANU ulimkabidhi Idd
Faiz kazi ya kuandaa, kukusanya na kusimamia mfuko wa safari ya rais wa rais wa
TANU Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa, New York. Safari ilikuwa ifanyike mwezi
wa Februari, 1955.
 |
Kushoto: Sheikh Suleiman Takadir, John Rupia na Julius Nyerere, 1955 |
 |
Mwenye miwani na kofia ni Abdul Faraj kama alivyo hivi sasa |
Mwaka wa 1953 Idd Faiz alikuwa na umri wa
miaka arobaini na tatu, mwenye ari na nguvu tele. Alipokuwa katika Kamati kuu ya
TANU mwaka wa 1959 aliteuliwa kuwa Mweka Hazina
wa Taifa wa TANU pamoja na kuwa mjumbe wa Kamati Kuu. Idd Faiz alikuwa
mmoja wa viongozi wa chama walioanzisha TANU Press iliyokuwa katika njia panda
ya Mtaa wa Mchikichi na Livingstone mjini Dar es Salaam. TANU Press ndiyo
ilikuwa ikichapisha na kusambaza jarida
la TANU, Sauti ya TANU lililohaririwa na rais wa chama, Julius Nyerere,
na baadaye kuchapisha Mwafrika chini ya
uhariri wa Rashid Heri Baghdelleh na Robert Makange. Kampuni hiyo ya kupiga
chapa ilimilikiwa na Mwananchi Development Corporation TANU ilimteua Abdul
Faraj kuiongoza kampuni hiyo.
 |
Kushoto: Kanyama Chiume, Mwl. Julius Nyerere na Robert Makange miaka ya 1980 |
 |
Kushoto: Idd Faiz, Sheikh Mohamed Ramia, Julius Nyerere, Saadan Abdul Kandoro
na Haruna Taratibu Dodoma 1956
|
TANU
ilihitaji takriban shilingi elfu kumi na mbili kumwezesha Nyerere kusafiri
kwenda Umoja wa Mataifa, New York. Kamati ya Abdu Kandoro, Japhet Kirilo na Abbas
Sykes ilikuwa imekusanya kiasi cha fedha kutoka majimboni ambacho kilitumika
katika ile safari ya Ally na Phombeah kwenda kwenye Pan African Congress mjini
Lusaka. Kilichosalia hakikutosha kumpeleka Rais wa TANU, Nyerere Amerika.
Ilibidi fedha za ziada zitafutwe kutoka kwa wananchi ili kumwezesha Nyerere
kufanya safari hiyo. John Rupia alichangia zaidi ya theluthi moja ya fedha
zilizotakikana. Wanachama wengine walichangia kwa uwezo wao wote lakini TANU
katika siku zile ikiwa bado changa ilikuwa masikini, kiasi hicho kilikuwa bado
kiko nje ya uwezo wake. Ikitambua ule
upungufu wa fedha za safari ya Nyerere, Idd Faiz aliombwa na uongozi wa Al
Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) kutoa fedha
katika mfuko wa Al Jamiatul Islamiyya na kuzitia katika hazina ya TANU
kukiwezesha chama kumpeleka Nyerere New York. Hata pamoja na fedha zile kutoka
Al Jamiatul Islamiyya fedha hizo hazikuweza kukidhi haja.
Al
Jamiatul Islamiyya haikuwa na jingine isipokuwa kumuomba Idd Faiz asafiri
kwenda Tanga na kupata fedha zaidi kutoka huko. Mwalimu Kihere alikuwa tayari
amekusanya fedha hizo na alikuwa anasubiri tu zije zichukuliwe na kupelekwa
makao makuu. TANU ilipata habari kwamba
yeyote ambaye angeenda Tanga kuchukua fedha hizo kwa ajili ya safari ya Nyerere
angekamatwa. Kabla ya kuondoka, Oscar Kambona, Katibu Mkuu wa TANU, na John
Rupia, Makamo wa Rais wa TANU, walikwenda kuonana na Idd Faiz nyumbani kwake
Ilala kumuaga, kumtakia safari njema na kumpa maelezo kwa ufupi. Safari ya
kwenda Tanga haikuwa na tatizo lolote, lakini katika wakati wa kurudi basi
ambalo Idd Faiz alikuwamo lilisimamishwa njiani Turiani na makachero wa Special
Branch. Idd Faiz alikamatwa, akavuliwa nguo na kupekuliwa, lakini hakukutwa na
fedha. Hili lilimshangaza na kumchanganya yule afisa aliyemkamata kwa sababu
walikuwa na taarifa kwamba Idd Faiz alikuwa amechukua fedha kutoka kwa Mwalimu
Kihere kule Tanga. Idd Faiz aliwekwa chini ya ulinzi na kupelekwa Dar es Salaam
kwa usaili zaidi wakati wote akiwa analindwa na askari wenye silaha. Baadaye
Idd Faiz aliachiliwa huru. Zile fedha za TANU zilifika makao makuu ya TANU Dar
es Salaam, salama salimini. Zilizokuwa
zimepewa kubeba msichana mdogo aliyekuwa abiria ndani ya basi lile
alimokuwa Idd Faiz.
 |
Mwalimu Kihere |
Mnamo
tarehe 17 Februari, 1955 Nyerere aliondoka kwenda New York kuhutubia Baraza la
Udhamini la Umoja wa Mataifa. Nyerere aliiweka wazi nia ya TANU kuwa alikuwa
ametumwa na wananchi wa Tangayika kuwasilisha ujumbe ufuatao:
‘’Kuona
kanuni ya uchaguzi ikianzishwa na Waafrika kujiwakilisha katika taasisi zote za
umma... Hii tunaamini, ni kwa mujibu wa masharti ya Makubaliano ya Udhamini na
Ibara ya 76 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.’’
Mbele
ya Umoja wa Mataifa, TANU haikuwa ikidhihirisha tamko lolote jipya, yale yote
yaliyowasilishwa pale yalikuwa ni maoni ya kamati ndogo ya siasa ya TAA
yaliyowakilishwa kwa Constitutional Development Committee ya Gavana Edward
Twining mwaka wa 1950. Gavana Twining aliyapuuza mapendekezo ya TAA na badala
yake aliendelea na mipango yake ya kuwa na wawakilishi wa rangi zote katika Baraza la Kutunga Sheria.
Ili kuupa msukumo msimamo wake huo serikali ilituma ujumbe wake Umoja wa
Mataifa kuipinga TANU uliowakilishwa na I. C. Chopra, Mwasia; Sir Charles
Phillips, Mzungu na Liwali Yustino Mponda, mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria
wa Newala.
Nyerere
alirudi kutoka New York Jumamosi, tarehe 19 Machi, 1955 na alipokelewa uwanja
wa ndege na halaiki ya watu. Dossa Aziz anakumbuka kuwa aliruhusiwa pale uwanja
wa ndege kuingiza gari yake hadi ndani ya uwanja chini ya ndege ili
kumrahisishia Nyerere kuingia ndani ya gari na kuepuka msongamano wa watu.
Dossa Aziz anasema kama isingekuwa kwa msaada huo Nyerere angesongwa sana na
watu. Watu walikuwa kila mahali wakisukumana na kusongamana wakijaribu angalau
kumtia Nyerere machoni. Watu walikuwa wakiimba na kucheza ‘’mganda,’’ ngoma ya
Kizaramo, wakiimba: ‘’Baba Kabwela Yuno,’’ yaani baba amerudi kutoka UNO. Jambo
la kushangaza ni kwamba hakuna mtu aliyewahi kuusikia wimbo huu kabla ya siku
ile na hakuna ajuaye lini ulitungwa. Ile gari ya Dossa Aziz aliyopanda Nyerere
ilisukumwa kutoka uwanja wa ndege hadi nyumbani kwa Nyerere, Magomeni Majumba
Sita, kiasi cha kama kilomita ishirini.
 |
Dossa Aziz |
Siku
iliyofuata ilikuwa Jumapili. TANU ilifanya mkutano wa hadhara Mnazi Mmoja ambao
ulihudhuriwa na umati ambao kamwe haukupata kuonekana Dar es Salaam. Inakisiwa
zaidi ya watu 40,000 walikuja kutoka kila upande wa mji kumsikiliza Nyerere.
Hakuna mtu aliyekuwa na raha ya kuandika kuhusu mkutano ule na safari ya
kihistoria ya Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa kuliko Mashado Plantan katika
gazeti lake Zuhra. Mtambo wa gazeti wa Mashado uliokuwa Mtaa wa Ndanda, Mission
Quarters ulichapisha nakala za ziada za gazeti hilo na toleo lote liliuzika.
 |
Mkutano wa TANU Jangwani Miaka ya Mwanzoni 1950 |
 |
Kushoto: Dossa Aziz, Julius Nyerere, Abdul Sykes na Lawi Sijaona Ukumbi wa Arnautoglo katika tafrija ya kumuaga Nyerere kwenda UNO safari ya mwaka 1957 |
 |
Kushoto waliokaa wa kwanza ni Japhet Kirilo |
 |
Kushoto Abdulwahid Ally Sykes na Mwandishi Nyumbani kwa Japhet Kiriko Usa River 1989 nilikuwa nimekwenda kumfanyia mahojiano lakini nikamkuta amesafiri amekwenda Nairobi. Japhet Kirilo ndiyo Mtanganyika wa kwanza kuzungumza UNO mwaka wa 1952
|
No comments:
Post a Comment