Udini Umeingia Kumbukumbu ya Nyerere –
M. Said
Na
Bakari Mwakangwale
Mohamed Ramadhani akimhoji Mwandishi |
IMEELEZWA kuwa si kwamba mambo yote yalikwenda
vuzuri katika historia ya Mwl. Julius Nyerere, bali pia yapo malalamiko kuhusu
mwanasiasa huyo wa Tanzania.
Hayo yamebainishwa na Mwanahistoria wa historia ya
Tanganyika, Sheikh Mohammed Said, katika mahojiano maalum ya kumbukumbu ya kifo
cha Mwl. Julius Nyerere, Oktoba 14, 2015, na kurushwa na Televisheni ya
Azam, Jumatano wiki hii.
Mohammed amesema ili kuweka kumbukumbu sahihi ya
Tanganyika (Tanzania) ni vyema historia ya Mwl. Nyerere, iandikwe au kusimuliwa
sambamba na wale alioshirikiana nao kwani sehemu kubwa ya historia hiyo
haijaandikwa kwa usahihi unaotakiwa.
Akizungumzia kuhusu malalamiko dhidi ya Mwl. Nyerere,
Mohammed Said amesema kuwa Waislamu hawakutegemea kwamba baada ya kudai Uhuru
kwa hali na mali zao, hali zao leo ziwe kama zilivyo sasa baada ya Uhuru.
Alisema, kabla na baada ya Uhuru Waislamu
hawakudhani kuwa watakuwa ni watu wa kutothaminiwa na kujikuta wanakuwa watu wa
chini ukilinganisha na wenzao.
Akasema, ni bora wakubwa wanaokamata nchi walitazame
suala hili la Waislamu, katika nchi hii, wajiulize je wameridhika na hali
waliyonayo (Waislamu) au kuna tatizo linalofanya wao kuwa katika hali hiyo.
Akijibu swali kwamba, inasemekana kuwa Waislamu
wenyewe hawakutaka kupata elimu na maendeleo, alisema haiwezekani watu
wasiotaka elimu na maendeleo waingie katika harakati na mipango ya kujenga Chuo
Kikuu mwaka 1968, ikiwa ni muda mfupi baada ya Uhuru.
“Mwaka huo Waislamu walitaka kujenga Chuo Kikuu cha
kwanza nchini, jambo ambalo lilileta mgogoro mkubwa na Serikali ya Mwl.
Nyerere, baada ya kuvurugiwa mipango na juhudi zao kwa makusudi na baada ya
hapo hawakuweza tena kunyanyuka.
“Kwa maana hiyo, tusijidanganye kuwa kila kitu
wakati wa Mwl. Nyerere, kilienda sawa yapo malalamiko mengi, laiti kama nisinge
andika kitabu cha ‘Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes’ usinge julikana
mchango na historia ya Waislamu katika kutafuta Uhuru wa Tanganyika.” Alisema Shkh. Mohammed.
Ama akizungumzia historia ya Mwl. Nyerere na
harakati za kudai Uhuru, Shkh. Mohammed Said aliweka bayana kwamba, historia ya
Mwl. Nyerere, haijaandikwa kwa usahihi unaotakiwa, pamoja na kuwa wapo
waliojitahidi kuandika lakini haijitoshelezi.
Mwanahistoria huyo, alisema kwamba suala hilo
amekuwa akilieza siku zote kwamba, historia ya Mwl. Nyerere, haiwezi kunoga
ikiwa atazungmzwa yeye Mwl. Nyerere, peke yake huku watu waliokuwa nae
wasielezewe au kutajwa.
Ili historia hiyo iwe sahihi ni vyema iandikwe
historia sambamba na wale alioshirikiana nao, ambao wapo wengi sana, huku
akimtaja Mzee Mshume Kiate,
ambaye alipambana sana katika kupigania Uhuru wa nchi hii.
Alisema, kwa kutambua mchango wake wakati huo Mzee
Kitwana Kondo, akiwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, alisema moja ya mitaa
Kariakoo upewe jina la Mzee Mshume, lakini akasema mpaka leo suala hilo
halijatekelezwa.
Alisema, moja ya mchango wake Mzee huyo, alikuwa ni
kulisha ama kutoa chakula kwa familia ya Mwl. Nyerere, akimtaka yeye (Nyerere)
aelekeze nguvu zake kupambana na Waingereza bila kuwaza familia yake watakula
nini.
Alisema, katika kutekeleza hilo, ilikuwa gari ya
Saidi Kamtawa (Said TANU), kila siku asubuhi linafika Sokoni Kariakoo (Dar es Salaam),
ambapo Mzee Mshume, anakusanya vyakula vya aina mbalimbali vinapelekwa
Magomeni, nyumbani kwa Mwl. Nyerere, zoezi alilolifanya mpaka Uhuru
unapatikana.
Alimtaja Mzee Idd Faizi Mafongo, na kuhoji leo hii
nani anayemjua, ambaye kadi yake ya TANU ilikuwa ni namba 25, alikuwa ndiye
mweka hazina wa TANU.
Alisema, katika mipango ya safari ya Nyerere kwenda
Umoja wa Mataifa, Bw. Mafongo, ndiye aliyekuwa akiratibu mipango ya fedha za
safari hiyo ambapo Waingereza walimkamata, kabla Mwl. hajafanya safari hiyo.
Aidha, aliwataja pia Tatu bint Mzee, Bw. Clement
Mtamila, na kueleza kwamba barua ya Mwl. Nyerere aliyoandikiwa na Waingereza
kuwa achague kati ya siasa au kazi, aliipeleka nyumbani kwa Mzee huyo
(Mtamila), Mtaa wa Kipata na Sikuku.
Alisema, hapo alikutana na wazee wa TANU, na
kujadili suala hilo ambapo walimwambia aachane na hiyo kazi na aungane nao moja
kwa moja na wao watamlipa mshahara ili wapambane na Waingereza wapate nchi yao
ya Tanganyika.
Katika harakati hizo za kudai Uhuru, Shkh. Mohammed,
alisema kwa mujibu wa Abas Sykes, wakati huo wazungumzaji wakuu walikuwa
watatu, alikuwepo Shkh Suleiman Takadir, akimtambulisha Mwl. Nyerere, katika
mikutano ya siasa, alikuwepo Bibi Titi Mohammed, nae alikuwa akizungumza baada
ya Shkh. Takadir, kisha Mwl. Nyerere, huongea mwishoni.
“Bibi Titi, ni mmoja wa wanawake waliomjenga sana
Mwl. Nyerrere, akiwa na mwenzake, akiitwa Bi Hawa bint Maftah, ambaye alikuwa
akiishi mtaa wa Mkunguni, Jijini Dar es Salaam.” Alisema Shkh. Mohammed.
Ama, kwa upande wa mikoani alisema, Mwl. Nyerere,
akiwa Lindi, aliongozana na Rajabu Diwani, na alifikia katika nyumba ya Mzee
Suleiman Mnyumvi, Mtaa wa Makonde, (Nyumba hiyo hadi sasa ipo), ambapo, Mjini
Moshi, nyumba ya Bi. Halima Selengia, aliyefariki miaka miwili iliyopita, ndio
alikuwa akifikia Mwl. Nyerere.
Alisema, hao pamoja wengine baadhi yao kama vile,
Salum Mpunga, Yusuph Chembera, Sharifa Bint Mzee, nao wana haki ya kutajwa na
kuenziwa sawa na Mwl. Nyerere kwa kuwa ndio walikuwa wakimsaidia katika
harakati hizo.
“Sasa tunaposema tunamuenzi Mwl. Nyerere, basi
na hawa wazee pia wapewe hadhi yao, watajwe au kama kuna khotuba zao ziwekwe
zisikike pia kwa kufanya hivyo tutakuwa tumefanya kumbukumbu yake kwa usahihi.
Huwezi kumuenzi Mwl. Nyerere bila kuwataja hawa
wasaidizi wake waliokuwa wakimsafishia njia na kumtambulisha kwa wenyeji wa
miji mbalimbali.” Alisema Shkh. Mohammed.
Akizungumzia uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2015,
alisema uchaguzi huu huwezi kuufananisha na chaguzi zozote zilizopita hapa
nchini ukitoa ule wa kura tatu, uliofanyika mjini Tabora, mwaka 1958, kutokona
na kuwa na hamasa kubwa.
Alisema, ukirejea vyama vilivyopigania uhuru katika
nchi jirani na Tanzania, ambavyo tayari vimeondolewa madarakani, kama vile kule
Kenya, Malawi na hata Zambia,
akasema sasa inaonyesha kuna uwezekano mkubwa hali hiyo ikaingia Tanzania.
No comments:
Post a Comment