Thursday, 15 October 2015

LAMECK BUGOHE MUASISI WA TANU 1954 KAFARIKI NA KUZIKWA KIMYA KIMYA

Lameck Bugohe
Mwenyekiti wa United Democratic Party John Cheyo akizungumza katika maziko ya Lameck Bugohe
Picha ya kushora ya Waasisi wa TANU

Lameck Bugohe wakati wa uhai wake


Ijue Historia ya Kweli ya Kuasisiwa kwa TANU

Mohamed Said

Wasisi wa TANU tarehe 7 Julai 1954



Lameck Bugohe amefariki dunia tarehe 30 Aprili 2015 na amezikwa kimya kimya. Hakupata mazishi yanayomstahiki mzalendo aliyepigania uhuru na kuwa mmoja wa wazalendo 17 walioasisi TANU mwaka 1954. Mwaka wa 2010 Mzee Bugohe aliandika makala katika gazeti la Nipashe akilalamika kwa kupuuzwa kwa historia ya waasisi wa TANU. Kufuatia makala hii nilimuunga mkono na nikaandika makala hiyo hapo chini:

Nimesoma makala kuhusu Mzee Lameck Makaranga Bogohe (Nipashe Julai 7, 2010) iliyoandikwa na Denis Maringo ambae ametambilishwa kama Mwanahistoria na Mwanasheria kitaaluma na ni Mkurugenzi wa Kituo cha Haki na Demokrasia - Centre for Justice and Democracy (CJD).

Inaelekea nia ya makala hiyo ilikuwa kuwakumbusha wananchi historia ya kuasisiwa kwa TANU na waasisi wake hasa kwa kuwa tulikuwa katika sikukuu ya saba saba ambapo tunakumbuka siku TANU chama kilichopigania uhuru wa Tanganyika kilipoanzishwa tarehe 7 Julai 1954. Ajabu ni kuwa katika vitu vinavyostaajabisha sana ni kupuuzwa kwa historia hii iliyotukuka ya kudai uhuru wa Tanganyika pamoja na kupuuzwa kwa wazalendo walijitolea muhanga wakati ule kuhakikisha kuwa Tanganyika inajikwamua kutoka katika makucha ya ukoloni wa Waingereza. Mzee Bogohe analalamika kwa kusema kuwa “…katika vitabu kila Tanu iandikwapo ni Mwalimu Nyerere.” Kwa hakika Mzee Bogohe si wa kwanza kuliona hili hata mie kuna wakati hili jambo lilikuwa likinistaajabisha sana hata nikafikia kuona kuwa labda CCM chama kilichokuja baada ya TANU hawajipendi na hawawapendi mashujaa wao lakini nikajagundua kuwa si kama hawajipendi ila hawapendi historia ya wazalendo wengine wanapenda historia ya Julius Nyerere peke yake na atajwe pweke bila ya kumuhusisha na yeyote yule.

Mzee Bogohe amesema mengi kuhusu udhaifu huu lakini mie sitanukuu moja baada ya jingine katika masikitiko yake ila nitazungumza kwa ujumla tu na kujaribu kusahihisha yale ambayo nimeona labda kwa uzee, siku kuwa nyingi kupita na kwa kukosa nyaraka halisi za rejea za historia ya kuanzishwa kwa TANU kuna mengi mzee wetu ameyasahau au ameyakosea kwa tarehe na maudhui yenyewe katika matokeo yaliyopelekea kuundwa kwa African Association mwaka 1929 na katika kuigeuza African Association kuwa Tanganyika African Association (TAA) mwaka 1948 na mwishowe kuundwa kwa TANU 1954. Katika maelezo hayo nitaelezea vilevile harakati zilizokuwapo pale New Street Makao Makuu ya TAA wakati wazalendo viongozi wa TAA kati ya 1950 – 1953 walipokuwa wanapanga mikakati ya kuunda TANU. Wakati huo ni ukweli usiopingika kuwa hakuna kati yao ukimtoa Hamza Mwapachu na Joseph Kasella Bantu aliyekuwa amemsikia Julius Nyerere.

Imethibitika hivi sasa kuwa Nyerere hakupendezewa na historia ya kweli ya kudai uhuru wa Tanganyika ambayo ilianza miaka mingi nyuma kabla yake kiasi cha takriban nusu karne. Historia ya African Association (baadae chama kikaja kujulikana kama Tanganyika African Association - TAA) chama kilichokuja kuunda TANU 1954 inaanza katikati ya miaka ya 1920 na kinara wa harakati hizo alikuwa Kleist Sykes (1894 - 1949) baba yao marehemu Abdulwahid (1924 – 1968), Ally na Abbas Sykes.  Kumbukumbu za Kleist zinaonyesha kuwa alitiwa hamasa za kuanzisha African Association na Dr Dr James Kwegyir Aggrey kutoka Ghana aliyekuja kutembelea Tanganyika mwaka wa 1924. Kleist alikuwa Mwafrika msomi katika kiwango cha enzi zile akizungumza Kiingereza na Kijerumani. Dr Aggrey katika mazungumzo na viongozi wa Dar es Salaam Waafrika akiwamo Kleist Sykes aliwashauri viongozi wale kuwa ili kupata maendeleo haraka itakuwa busara kwa wao kama Waafrika kuwa na chama chao kitakachowajumuisha Waafrika wote. Ilimchukua Kleist na wenzake miaka mitano hadi kufikia kusajili African Association mwaka 1929 Kleist akiwa katibu mwanzilishi na Mzee Bin Sudi akiwa rais wake. Viongozi hawa baada ya kuasisi African Association wakaasisi chama kingine Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika mwaka 1933. Mingi ya mikutano ya kuanzisha African Association ikifanyika nyumba moja Mtaa wa Magila Mission Quarters, nyumba hii baadae ilikujanunuliwa na John Rupia. Hii nyumba bado ipo hadi leo. Wanahistoria bado wananafasi ya kwenda izuru nyumba hii kabla haijavunjwa na kujengwa ghorofa.

Historia ya TANU ukiitaka kwa undani inaanza miaka hii 1929 na mwanzoni mwa  1930. Sasa kupitia vyama hivi viwili viongozi wake wakajenga majengo mawili, moja ni hiyo nyumba ambayo hadi leo ipo ambayo yalikuwa makao makuu ya African Association Mtaa wa New Street. Jengo hili lipo na lilikuja kufunguliwa na Gavana Ronald Cameroon mwaka 1933. Bwana Ally Sykes ana picha ambayo inaonyesha sherehe za ufunguzi wa jengo hilo ikimwonyesha baba yake, Gavana Cameroon, Mwalimu Mdachi Shariffu, Machado Plantan na viongozi wengine wa African Association. Hii ndiyo nyumba iliyokuja kuasisiwa TANU mwaka 1954. Marehemu Abdulwahid Sykes katika kumbukumbu zake anasema yeye alikuwa akifuatana na baba yake kila siku za Jumapili pale New Street na akimuona baba yake na viongozi wenzake wakijenga nyumba ile kwa kujitolea. Jengo la pili ni hilo ambalo sasa ni shule ya Msingi ya Lumumba ambapo zamani ilikuwa makao makuu ya Al Jamiatuli Islamiyya na vilevile ilikuwa Al Jamiatul Islamiyya Muslim School. Viongozi wa mwanzao na wanachama wa awali wa TANU walitokana na vyama hivyo viwili. Taarifa hizo zote na kumbukumbu nyingine za harakati za siasa katika Tanganyika zipo mpaka leo katika hifadhi ya familia ya akina Sykes. Mwandishi wa makala hii zilimsaidia sana katika kuandika kitabu, The Life and Times of Abdulwahid Sykes 1924 -1968 The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika kitabu kilichochapwa London mwaka 1998 na tafasiri yake ya Kiswahili kuchapwa na Phoenix Publishers, Nairobi mwaka wa 2002.

Historia hii ya TANU kama ilivyo hapo juu ilikuja kuandikwa na Abdulwahid Sykes na Dr Wilbert Kleruu mwanzoni mwa miaka ya 1960 kwa ushauri wa Mwalimu Nyerere, Mwalimu Kihere na Dossa Aziz. Inasemekana historia ile kama alivyokuwa akiandika marehemu Abdulwahid Sykes ikawa kama inamtia unyonge kidogo Nyerere. Inasemekana Nyerere hakuipenda historia ile. Kwa hakika historia hii ambayo yeye hayumo hakuipenda kabisa na ikabidi mradi huo wa kuandika historia hiyo ufe kabla ya kazi kukamilika. Abdulwahid Sykes akajitoa katika kazi hiyo akamuuacha Dr Kleruu yeye aendeleenayo. Kleruu alimaliza kazi hiyo kwa namna inavyosemekana alivyoelekezwa na Nyerere lakini mswada ukabaki pale Makao Makuu ya TANU bila kuchapwa kwa muda mrefu. Inasemekana mswada uliibiwa na ukajachapwa kitabu bila ya ridhaa ya TANU. Hata hivyo haijulikani nyaraka zile za mwanzo kama zilivyoandikwa na Abdulwahid Sykes ziko wapi kwa  sasa kwani juhudi za mwandishi kuzipata katika maktaba ya CCM Dodoma ziligonga mwamba.

Baada ya wizi huo TANU ikaunda jopo la wataalamu wake ambalo lilikaa kitako na kuandika historia ya TANU  na kitabu kikachapwa (Historia ya Chama Cha TANU 1954-1977, Dar es Salaam, Kivukoni Ideological College, 1981). Kitabu hiki kilipotoka wengi hasa sie wazaliwa wa Dar es Salaam kikatustaajabisha kwani kwa kweli kilikuwa kitu kingine, ile haikuwa historia ya TANU na haitakujakuwa. Kwa uchache unaweza kusema ilikuwa historia yake Nyerere kuanzia mwaka wa 1954 na hata hivyo ilikuwa ikichagua nini la kuandika jina gani la kutaja na lipi la kukwepa. Kwa nini nasema kukwepa? Kitabu kizima hakuna hata sehemu moja ambako waasisi wa siasa za Tanganyika - ukoo wa akina Sykes ulipotajwa. Huwezi kuandika historia ya Nyerere ukaacha kuwataja watu hawa na wazalendo wa Dar es Salaam waliomtia katika siasa za TAA na TANU watu kama Mwinjuma Mwinyikambi, Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate, Iddi Tosiri na ndugu yake Iddi Faizi na kaka yao Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Suleiman Takadir, Dossa Aziz, Hamza Mwapachu, Clement Mtamila, Dr Michael Lugazia, John Rupia, Dr Vedasto Kyaruzi, Dr Luciano  Tsere, Dome Budohi, Dennis Phombeah, Zuberi Mtemvu, Ali Mwinyi Tambwe, Tatu binti Mzee, Titi Mohamed, Asha Ngoma na majina kwa kweli ni mengi ukisema uyataje hutoweza kuyamaliza kwa ukamilifu wake. (Titi Mohamed amehutubia mkutano wa TANU miezi michache baada ya kuundwa kwa TANU pale Mnazi Mmoja hamjui Nyerere wala hajaona sura yake inafananaje).  Ikawa sasa historia hii ya ukwepaji baadhi ya majina ya wazalendo Mwalimu akaipenda na ndiyo ikawa historia rasmi inayokubalika ya TANU na harakati za kudai uhuru hadi leo.

Katika hali kama hii ndipo ikawa watu kama Mzee Bogohe lau kama walikuwa na mchango wao katika siasa za kudai uhuru wa Tanganyika wakawa wamewekwa pembeni hawatajwi anatajwa Nyerere peke yake. Itoshe kumaliza kipengele hiki kwa kusema kuwa katika chaguzi za siasa za kusisimua katika historia ya Tanganyika ni ule uchaguzi wa TAA wa 1953 wakati Nyerere alipogombea nafasi ya urais wa TAA dhidi ya rais wake aliyekuwa anamaliza kipindi chake Abdulwahid Sykes pale katika ukumbi wa Arnatouglo tarehe 17 April 1953. Kukutana kwa Abdulwahid Sykes na Nyerere mwaka wa 1952 na siri za harakati alizozikuta Nyerere kwa Abdulwahid Sykes ni kisa cha kumsisimua mtafiti yeyote wa historia. Mama Maria Nyerere lazima atakuwa na kumbukumbu hizi za wao na akina Sykes pale mtaa wa Kipata nyumbani kwa Ally Sykes na Aggrey Street nyumbani kwa Abdulwahid Sykes na pilka pilika za hatari za kuwakwepa makachero wa Special Branch wakiongozwa na Amri Kweyamba na vijana wake. (Amri Kweyamba alidumu katika kazi hiyo hata baada ya uhuru lakini sasa akiitumikia serikali ya TANU na Nyerere siyo ile ya Gavana Edward Twining). Pale Kipata ndipo Ally Sykes alipokuwa ameficha mashine ya kudurufu  ambayo alikuwa akichapa makala za siri (Waingereza wakiziita za uchochezi) kuhamasisha Waafrika dhidi ya ukoloni. Shajara za Abdulwahid Sykes za kipindi hiki (1950 - 1954) ameziandika kwa hati mkato na inasikitisha kuwa hadi leo akina Sykes hawajataka kuzitoa kwa watafiti zisomwe kwa faida ya historia ya nchi yetu na kizazi kijacho.

Wazee wengi wa Dar es Salaam na wengi wao weshatangulia mbele ya haki wanafahamu fika kuwa kama unataka kumpa sifa mtu mmoja kwa kuanzisha TANU basi hatakuwa Nyerere sifa hiyo ni ya marehemu Abdulwahid Sykes ambae katika uongozi wake kuanzia 1950 hadi 1953 ndipo aliposhughulikia katiba ya TANU na kuleta mbinu mpya ya kupambana na Waingereza kiasi cha kuwa baada ya majalada ya Kiingereza kule London kuwekwa wazi (baada ya kupita miaka 50) taarifa za siri za kikachero za Special Branch zinaonyesha kuwa Abdulwahid walimchukulia kama mtu ”hatari.” Alikuwa hatari kwa kuwa ndani ya TAA katika miaka ya mwanzo ya 1950 Abdulwahid akiwa ndiye rais TAA ilikuwa na uhusiano na harakati za Mau Mau chini ya akina Kenyatta na Bildad Kaggia huko Kenya na Kenneth Kaunda toka Northern Rhodesia. Itoshe tu kusema mwaka 1950 Abdulwahid Sykes alifanya mkutano wa siri na viongozi wa KAU Nairobi wakiwemo Kenyatta mwenyewe, Kaggia, Kungu Karumba na wengine nia ikiwa ni kuunganisha nguvu za Tanganyika na Kenya katika kuupiga vita ukoloni. Kisa cha Ally Sykes na Kenneth Kaunda ni kisa kingine cha kusisimua sana. Baada ya kuwasiliana na Kaunda mwaka 1953 na Kaunda kumwalika Ally Sykes na Dennis Phombeah katika mkutano wa wanaharakati wa ukombozi kusini ya Afrika uliokuwa ufanyike Lusaka Ally Sykes na Dennis Phombeah waliishia mbaroni mjini Salisbury Southern Rhodesia. Hizi ndizo zilikuwa harakati za TAA pale Makao Makuu na hawa ndiyo walikuwa viongozi walokuja iasisi TANU.

Niongeze kidogo kwa kusema kuwa na hili suala la katiba ya TANU wala si kitu cha kukipigia sana kelele kwani walichofanya viongozi wa TAA ilikuwa kunakili katiba ya Convention Peoples Party (CPP) chama alichokianzisha Kwame Nkrumah. Mahali palipoandikwa CPP viongozi wa TAA waliweka TANU. Kwa hakika kama kuna kitu cha kujivunia katika maandiko yaliowahi kuandikwa na TAA basi ni ile memorandum ya TAA Political Subcommittee iliyotayarishwa mwaka 1950 na uongozi wa TAA na kusainiwa na viongozi hawa wafuatao: Abdulwahid Sykes, Sheikh Hassan bin Amir kama Mufti wa Tanganyika na Zanzibar; Dr Vedasto Kyaruzi, Hamza Mwapachu, Said Chaurembo,  John Rupia na Stephen Mhando. Waraka huu ndiyo Nyerere alikwendanao Umoja wa Mataifa mwezi Machi mwaka wa 1955 na kuusoma mbele ya Baraza la Udhamini. Hiki ndicho kitu cha kuringia na kujivunia si hiyo katiba ya TANU waliyonyambua toka kwa Nkrumah. Inasemekana hatima iliyoikumba ile kazi ya historia iliyoandikwa na Abdulwahid Sykes kuibiwa pale Makao Makuu ya TANU imeikumba na nyaraka hii muhimu ya kihistoria iliyotayarishwa mwaka 1950 na viongozi wa TAA. Haishangazi leo ukisikia baadhi ya viongozi wakiikashifu TAA wakinadi kinywa kipana na bila ya soni ati TAA hakikuwa chama cha siasa bali kilikuwa chama cha starehe.

Mzee Bogohe anasema jina la TANU kalitoa yeye na anataka atambulike kwa hilo, sawa. Wangapi leo wanajua kuwa kadi za TANU za kwanza 1000 alizitengeneza Ally Sykes na akazilipia kutoka mfukoni kwake binafsi? Wangapi leo wanajua kuwa kadi ya Nyerere ya TANU ni namba 1 na imetiwa saini na Ally Sykes? Wangapi wanajua kadi namba 2 ya TANU  ni ya Ally Sykes mwenyewe na namba 3 ni ya kaka yake Abdulwahid Sykes? Vipi kaka mtu apate kadi namba 3 na mdogo namba 2 ikiwa utamaduni wa Kiafirika na adabu zetu ni kumtanguliza mkubwa mbele? Majibu yapo na ndiyo yanayokoleza utamu wa historia ya kweli ya TANU. Kinyume cha hapo utapambana na historia ya kubuni na kitu cha kubuni au kisichokuwa na ithibati siku zote huwezi kukitegemea kujenga hoja thabiti.

Hapa si mahali pale kuyaeleza yote hayo. Bwana Ally Sykes yu hai na wanahistoria waende wakamhoji watapata faida kubwa. Sasa na tujiulize, lipi kubwa. Kutoa jina la TANU au kukianzisha chama chenyewe cha TANU? Historia imeshuhudia kuwa hadi anaingia kaburini marehemu Abdulwahid Sykes hakupata kukumbusha kuwa TANU chanzo chake ni baba yake au kuwa yeye ndiye aliyemweka Nyerere katika uongozi wa TAA na mwishowe TANU. Msisitizo ni kuwa hadi marehemu Abdulwahid Sykes anaingia kaburini 1968 hakupata kujinasibu kwa kuanzisha TANU wala kusema kuwa alikuwa yeye ndiye aliyempa Nyerere nafasi ya uongozi kwanza katika TAA 1953 na kisha 1954 katika TANU. Abdulwahid Sykes kwa waliomjua wanasena alikuwa mtu muungwana sana. Juu ya hayo yote alofanya ukiondoa kuwa alikuwa kati ya wafadhili wanne wa awali wa TANU wengineo wakiwa mdogo wake, Ally, John Rupia na Dossa Aziz hawa wote wametolewa katika kumbukumbu za historia ya TANU. Ukikisoma kitabu cha historia ya TANU kilichoandikwa na Kivukoni College hili utaliona dhahiri.

Tumalize kisa chetu. Yapo makosa kidogo katika simulizi ya Mzee Bogohe bila shaka ni kwa sababu ya miaka mingi kupita. Mzee Bogohe anasema kuwa Mhasibu Mkuu wa kwanza wa TANU alikuwa Julius Mwasanyangi. Ukweli ni kuwa mweka hazina wa kwanza wa TANU alikuwa Iddi Faizi Mafongo aliyekuwa mhasibu vilevile wa Al Jamiatul Islamiyya. Iddi Faizi Mafongo ndiye aliyekuwa na jukumu la kukusanya fedha za safari ya Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa mwezi Machi 1955. Katika nafasi yake ya kuwa mweka hazina wa vyama hivyo viwili Iddi Faizi alitoa fedha katika hazina ya za Al Jamiatul Islamiyya na kuzitia katika mfuko wa TANU ili kufanikisha safari ile. Iddi Faizi ana historia nzuri sana na ni jukumu lao sasa wanahistoria kuzitafuta habari zake. Iddi Faizi, Sheikh Suleiman Takadir na Nyerere ndio waliotembea Jimbo la Mashariki mwaka 1958 kuwahamasisha wana -TANU wasisuse kuingia katika Uchaguzi wa Kura Tatu.

Iwe itakavyokuwa nyaraka za historia zinaonyesha kuwa alotoa jina la TANU alikuwa marehemu Abdulwahid Sykes na jina hilo alilitoa Kalieni Camp India mkesha wa Christmas mwaka 1945 akiwa askari wa 6 Batallion, Burma Infantry katika King’s African Rifles (KAR) wakati wa Vita Kuu ya Pili. Kalieni Camp ndipo askari wa KAR walipokuwa wamekusanywa wakisubiri kurudishwa makwao baada ya kumalizika vita. Ukienda katika shajara yake ya mwaka huo taarifa hizi utazikuta. Juu haya hilo haliondoi ukweli kuwa huenda na Mzee Bogohe na yeye vilevile alikuwa na wazo la kuanzisha chama cha siasa hata kama si kile cha  TANU. Ala kuli hali muhimu ni kwa wanahistoria kuwatafuta wazee hawa na kupokea hazina ambayo si muda mrefu itatoweka.Wangapi leo wanajua kuwa ni Hamza Mwapachu na Abdulwahid Sykes ndiyo waliomsukuma Nyerere katika ulingo wa siasa? Au wangapi wanajua historia ya madaktari watano – Dr. Vedasto Kyaruzi, Dr Joseph Mutahangarwa, Dr Wlibard Mwanjisi, Dr Michael Lugazia na Dr Luciano Tsere na mchango wao katika kusukuma mbele harakati za TAA  kati ya 1948  – 1950?

Kwa kumaliza napenda kumuuliza msomaji wangu kuwa je, haishangazi kuwa historia ya kutukuka kama hii ya wazalendo na mashujaa wetu leo imetupwa na haipewi thamani? Kama inashangaza je, haiwi vyema tukajiuliza kwa  nini imekuwa hivi? Ni nini viongozi wetu wanachokiogopa katika kuwaenzi mashujaa wa uhuru wa Tanganyika? Je ndiyo tuchukulie kuwa Tanzania ni nchi isiyokuwa na mashujaa wake? Wasomaji hamkubaliani nami kuwa kuna haja kubwa sana ya kuandika upya historia ya uhuru wa Tanganyika na kuwaenzi wale wote waliotoa mchango katika vita vya uhuru? Kwa kumaliza makala haya namshukuru Mzee Lameck Bogohe kwa kufunua kinywa na kutueleza yale anayoyajua katika kuanzishwa kwa TANU na kuonyesha kidole kwa yale ambayo ameyaona yanapotosha historia hiyo. Nitafurahi sana Insha Allah kama watajitokeza wengine na kuandika wanayoyajua kuhusu mashujaa wetu wa uhuru ambazo habari zao hazijulikani na wengi. Je hapana haja ya kuiuliza CCM hivi hadi lini wataiacha historia yao inapotoshwa na kupotea?

Mohamed Said
8th Julai 2010
mohamedsaidsalum@yahoo.com

Ukipenda kusoma zaidi ingia:

http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-historia/543213-tumkumbuke-muasisi-wa-tanu-lameck-bugohe.html

No comments: