Tuesday, 26 January 2016

JECHA NA UCHAGUZI WA MAREJEO - KUTOKA MWANAHALISI

Jecha Salim Jecha

MAZINGIRA yaliopo sasa ndani ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ni mabaya zaidi ya ilivyokuwa zamani. Hayawezeshi kuupata uchaguzi huru, wa haki na utakaotosha kukidhi vigezo vya kuitwa uchaguzi mzuri.

Mazingira ambayo Mwenyekiti Jecha Salim Jecha anadhibitiwa na dola inayoshikwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho viongozi wake wakuu katika kudhihirisha kiwango cha kumdhalilisha, wanamulekeza kuchomoza kichwa na kutoa amri zinazowafurahisha.

Ni viongozi hawa waliomtuma aufute uchaguzi wa 25 Oktoba, 2015, wasijali kuonekana ni wanasiasa waliofilisika kifikra. Ndio hao baada ya kubaini alitoa uamuzi batili kisheria, walijitoa akili na kumtaka achomoze tena kichwa na kuitisha kikao Novemba mosi, 2015, akatangulia kukiri eti alikosea kisheria na kuwakosea kikazi makamishna.

Hapohapo alitaka kuwatumia kuongeza uvunjaji wa sheria baada ya kuwaomba radhi akidai alilazimika kusema uongo ili kuikinga nchi na balaa ? akawataka wamuunge mkono.

Akaungwa mkono ma makamishna watatu, wawili kutoka CCM, na mmoja kutoka chama kingine lakini ambaye anatumika kuibeba CCM. Makamishna wawili kutoka Chama cha Wananchi (CUF) wakamtenga.

Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji Abdulhakim Ameir Issa, naye akamtenga. Alimwambia wazi ?ninaamini ulipokuwa unajiandaa kufanya ulichokifanya, na mpaka unatekeleza, ulijua mimi Abdulhakim sitakuunga mkono.?

Jecha akaongeza kura yake zikawa kura 4-3 ikionesha ametimiza kilichotarajiwa na waliomtuma. Tuelewane, uamuzi wa Tume kisheria unatakiwa kufanywa baada ya majadiliano. Kilichofanyika hapo, ni sawa na mtu kununua soji kabla ya kujua ukubwa wa farasi atakaemvika.

Jecha akarudi mafichoni. Nyumba zake, ya mjini na iliyoko kijijini, kwa muda wote zikabaki zinaning?inia kufuli. Baadaye sana, nikaambiwa kuna wakati anatoka magharibi na kukutana na watu wazima wenzake kwa maongezi. Sikugundua kituo chao.

Januari 12 mwaka huu, akaibukia ?makwapani? mwa viongozi wakubwa wa kiserikali kwenye jukwaa la viongozi hao Uwanja wa Amaan, kushuhudia kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kutoka hapo akaandaa utaratibu wa kukutana na makamishna kwa ajenda anazotoka nazo alikofichwa. Hatima ya vikao vyake vya siku mbili, ni kuchomoza tena kichwa chake na kutoa tangazo jingine la kumfurahisha aliyemteua mwaka 2013, Dk. Ali Mohamed Shein, na CCM wenzake.

Jecha anatangaza tarehe ya anachoita ?uchaguzi wa marudio nchi nzima? na katika majimbo yote 54 yaliyoko Zanzibar, uchaguzi licha ya kujua fika hakuna popote unapotajwa katika Sheria ya Uchaguzi Zanzibar, Na. 11 ya mwaka 1984.

Sasa ndio ninaamini CCM wamekusudia hasa kwa mara nyengine, kuonesha kwamba hakuna yeyote ardhini wa kuwazuia kufanya uhalifu na ushetani ukiwemo wa kuzikandamiza haki za msingi za wananchi wa Unguja na Pemba.

Lakini pia, ninaamini pasina shaka kuwa anayoyafanya Jecha sasa, yanaungwa mkono na uongozi wa juu kabisa wa dola ya Jamhuri ya Muungano, ambayo mkuu wake, Dk. John Magufuli, ametoa ahadi ya kushughulikia alichoita matatizo ya Zanzibar akishirikiana na Makamu wake Mama Samia Suluhu Hassan na Dk. Shein.

Dk. Magufuli, aliyejiita mtumbua majipu, alitoa ahadi hiyo 20 Novemba, 2015, alipohutubia Bunge la 11 katika kulizindu.

Ushahidi wa msimamo wangu huu ni kuendelea kwa maamuzi yanayozidi kuvunja sheria na katiba na yanayothibitisha nguvu kubwa ya ukandamizaji haki za wananchi kuchagua viongozi wawatakao.
Wanasheria wanasema kama uamuzi wa Oktoba 28 ulikuwa batili, hakuna chochote cha kutendwa au kutendeka ili uhalalike. Ina maana moja tu ? kila linalofanywa na kundi la Jecha, ni kuzidisha tu ubatili wa uamuzi ule wa awali wa kufuta uchaguzi uliokwishafanyika.

Huu ni ukweli mchungu ambao kwa masikitiko unakejeliwa na wengi, kuanzia viongozi na wakereketwa wa CCM, mpaka watalamu wa sheria wanaosema kwa niaba ya maslahi ya chama hicho.

Angalia ilivyo hatari hapa: Jecha analindwa na walinzi wanaomtii Dk. Shein, ambaye anashikilia kuongoza serikali kwa hofu akijijua haungwi mkono na zaidi ya nusu ya wapigakura walioamua kumpa ridhaa mshindani wake mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad wa CUF.

Eti Jecha huyu bado anaitwa mwenyekiti wa Tume ambaye anaendelezwa asimamie kinachoitwa uchaguzi wa marudio ambao sasa umetajwa utakuwa mwezi wa Machi.

Angalia ilivyo hatari hapa: Eti Jecha na tume ileile ambayo viongozi wakuu wa CCM waliituhumu kuvuruga uchaguzi kwa kushirikiana na wapinzani wao, inatumika kufanya maandalizi ya uchaguzi huo wa marudio.

Ikumbukwe ni tume hii viongozi wa CCM walisema iliachia ziingizwe nchini kura bandia; ikaruhusu kura halali zilizopigwa vituoni ziokotwe mitaani; iliyoruhusu kura zizidi idadi ya wapigakura vituoni; na Tume ambayo makamishna wake walikaribia (au waligombana) kuvutana shati kila mmoja akishikilia msimamo wenye utashi wa chama alicho.

Ulimwengu unashibishwa imani kwamba tume ileile iliyovuruga uchaguzi chini ya mwenyekiti wake huyu Jecha, ndio wapewe jukumu la kuendesha uchaguzi wa marudio. Watu waaminishwe sasa kwamba Jecha na wenzake katika tume ileile bomu, wameshabadilika na kuwa malaika.

Angalia ilivyo hatari hapa: Eti Jecha yule aliyekimbia majukumu yake kuongoza Tume katika siku iliyopaswa kuwa ya kumaliza kazi muhimu ya kutangaza matokeo ya urais, Oktoba 28, 2015, na hatimaye akatumika kufurahisha rafiki zake CCM kwa kutangaza kuufuta uchaguzi, leo anaaminika kufaa kuongoza walewale makamishna aliowatelekeza Oktoba 28, wasimamie uchaguzi wa marudio.
Eti kwamba katika uchaguzi huo wa marudio utakaosimamiwa na mwenyekiti Jecha huyu ambaye tangu Oktoba 28 alibadili staili ya maisha kwa kutumikia mabwana akiwa kule walikompa hifadhi ya muda, aaminike atatendea haki wagombea wasiokuwa CCM.

Eti watu wazima wanamtuma Jecha akutane na Tume kwa ajenda alizoingia nazo kikaoni ambazo amezitoa kutoka kwa wanaomlinda huko mafichoni, na aaminike na iaminike kuwa ana akili zake timamu kwa hivyo kusiwe na shaka, atatenda tu haki kwa wagombea ambao upinzani wao dhidi ya maamuzi yake ya kibabe na kimabavu, ndio sababu hasa ya hao wanaomtuma kuamua kumkingia kifua kwa kumlinda kijeshi.

Ni kwamba kuna watu wamechoka kufikiri vizuri na sasa kuamua kwa makusudi katika mtizamo wa kudhihirisha walivyofurtu ada kwa kiburi, kubeba akili za kishetani na kutaka kuihadaa dunia kuwa wao wana busara ya kisahaba, kwamba wala hawana nia mbaya na Zanzibar. Wanaisukuma nchi ionekane ya wendawazimu.

Najua kwa hatua iliyofikiwa sasa katika kuichafua Zanzibar, dunia inajua vizuri ni nani wendawazimu, maana inashangaa wadhulumu haki ya wananchi hawataki kuamini siasa za kishirikina na kihafidhina hazina nafasi.

Hata iweje, haiwezekani. Hayapo mazingira ya kuingiza Zanzibar katika uchaguzi.

Inashangaza eti kwa yote haya, ukisema kinachoandaliwa ni machafuko, wanaodharau kutatua mgogoro wananuna na kuamuru mimi na mhariri mwenzangu tufungwe. Sitajuta kusema, na ninasema nchi hii inasokomezwa kuzimu.

Chanzo: MwanaHalisi 

No comments: