Friday, 15 January 2016

RASHID MFAUME KAWAWA KATIKA HISTORIA YA UHURU WA TANGANYIKA


MAPITIO YA KITABU SIMBA WA VITA KATIKA HISTORIA YA TANZANIA RASHIDI MFAUME KAWAWA

Na Mohamed Said

Kwa mara ya kwanza Tanzania ilishuhudia kuandikwa kwa historia ya mmoja wa viongozi wakuu wake kupitia kitabu “Simba wa Vita Katika Historia ya Tanzania Rashidi Mfaume Kawawa” kilichoandikwa na Dk. John M. J. Magotti. Sidhani kama katika historia ya Tanzania kuna kumbukumbu ya kuandikwa kwa kitabu kinachohusu maisha ya kingozi yoyote achilia mbali kufanyika kwa sherehe ya kukizindua kitabu hicho Ikulu ikiongozwa na rais mwenyewe.  Kwa hakika sherehe ilifana sana na tukakisubiri kwa hamu kitabu madukani ili tupate kunufaika na kumbukumbu za Mzee Kawawa.

Msomaji anaweza kukisoma kitabu chote chenye kurasa 127 kwa muda wa saa moja akawa kakimaliza chote na atakapokiweka chini akawa hakubakia na chochote cha maana katika fikra yake. Kwa nini iwe msomaji asibaki na kumbukumbu yoyote ya kiongozi mkubwa kama Mzee Kawawa mtu aliyeshuhudia kwa macho yake mwenyewe harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika na si hivyo tu yeye mwenyewe ni mmoja wa wale waliopigania uhuru wa Tanganyika na kushika nyadhifa kubwa za uongozi chini ya Mwalimu Julius Nyerere. Kwa kawaida vitabu vya maisha ya viongozi hasa wapigania uhuru huwa vina mambo mengi  sana ambayo kwa muda mrefu huwa siri, hayafahamiki hadi hapo kitabu kitakapoandikwa ama kwa mkono wake kiongozi mwenyewe au kuandikwa na muandishi. Mifano ipo mingi. Kitabu kama “Mahatma Gandhi” klichoandikwa na Robert Payne au “Long Walk to Freedom” alichoandika Nelson Mandela mwenyewe au “Seeds of Freedom” alichoandika Bildad Kaggia hakika unapomaliza kusoma vitabu hivi lazima urudi nyuma kufungua kurasa hapa na pale kuzisoma upya zile sehemu zinasosisimua.

Huwezi kupata haya katika kitabu cha Mzee Kawawa. Huwezi kuyapata haya kwa kuwa mwandishi hakuandika kitu. Hakuandika kitu si kama Mzee Kawawa hana historia ya kusisimua na kuwa hana mengi ambayo wengi hawayajui katika maisha yake, nadhani mwandishi hakuwezakuja na jipya labda kwa sababu hakufanya utafiti wa kutosha kuweza kuandika kitabu kinachomuhusu simba wa vita aneunguruma. Kuna msemo wa Kiswahili usemao “Aungurumapo simba mcheza ni nani?” Kwa hakika simba wa vita hakuunguruma kabisa katika kitabu hiki. Sijui lawama zielekezwe wapi.

Mimi simjui Mzee Rashidi Kawawa kwa kiwango cha kusema naweza kunyanyua kalamu na kufanya pitio la kitabu kilichoandikwa kuhusu yeye. Nathubutu kuandika kuhusu kitabu chake kutokana na kumjua kwangu mimi nikiwa kama mwandishi na mtafiti ambae katika kutafiti kwangu nimekutana na jina la Mzee Kawawa hapa na pale katika nyaraka zilizo katika hifadhi ya ukoo wa akina Sykes. Nitatumia uzoefu wangu huu kueleza yale niliyoyaona katika nyaraka hizi na ninayojua kuhusu Mzee Kawawa na kufanya tathmini kwa yale niliyoyasoma katika kitabu cha Magotti.

Miaka kama ishirini iliyopita nikiwa kijana mdogo nilipata hamu ya kuandika historia ya kudai uhuru wa Tanganyika. Sikuona mtu wa kumuendea isipokuwa Ally Sykes. Nilipomueleza kuwa nia yangu ni kuandika kitabu kuhusu marehemu kaka yake Abdulwahid Sykes (1924- 1968) Ally Sykes alinambia kuwa atanipa nyaraka zake zote nizipitie kisha ndiyo nakaenae chini kwa mahojiano ya ana kwa ana. Katika nyaraka alizonikabidhi ndani yake nilikuta barua ya mkono aliyoandika Rashid Kawawa mwaka 1952 kutoka Bukoba akimletea Ally Sykes aliekuwa Dar es Salaam. Barua hii ya Mzee Kawawa kwa Ally Sykes ilikuwa ikimfahamisha Ally Sykes hali ya siasa Kanda ya Ziwa. Hii barua hadi leo ipo katika nyaraka za akina Sykes. Nilipokaa na Ally Sykes kutaka maelezo ya barua ile aliyoandikiwa na Kawawa, Ally Sykes alinipa kisa hiki:

Mwaka 1951 nilichaguliwa kuwa katibu mkuu wa Tanganyika African Government Servants Association (TAGSA). Chama hiki kiliundwa mwaka wa 1927 kwa lengo la kuendeleza maelewano mazuri baina ya serikali ya Malkia na sisi watumishi Waafrika. Rashid Kawawa alikuwa mwana kamati. Mimi nilichaguliwa pamoja na Thomas Marealle kama rais wa TAGSA. Katiba ya TAGSA iliamuru uchaguzi wa kila mwaka, na mimin nilirudishwa madarakani kama katibu mara nne hadi Oktoba, 1954 nilipojiuzulu baada ya kuhamishwa kwenda Korogwe kamaadhabu kwa kuwa miongoni mwa wale wanachama 17 waliounda TANU. Watu kadhaa walishika urais. Stephen Mhando na Dr Wilbard Mwanjisi wote hao waliwahi kuchaguliwa kuwa marais wa TAGSA. Miongoni mwa wanachama watendaji wa TAGSA walikuwa Dr Michael Lugazia na Rashid Kawawa ambao alichaguliwa kuwa katibu baada ya mimi kujiuzulu. Kupitia TAGSA, Kawawa alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Tanganyika Federation of Labour (TFL).

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulipokuja kuzuru Tanganyika Agosti, 1951 kwa mara ya tatu, vyama vyote viwili, TAA na TAGSA, viliwakilisha malalamiko kwa ujumbe huo. TAGSA iliwakilisha malalamiko yake kuhusu ubaguzi katika utumishi serikalini kwa mujibu wa kupanga mishahara kufuatana na rangi ya ngozi. Mshahara wa Mwafrika ulikuwa wa chini zaidi kuliko ule aliokuwa akipokea Mzungu au Muasia kwa kazi hiyo hiyo. Kwa mfano Mwandishi wa hati mkato Mzungu alikuwa akipata mshahara mkubwa kuliko Mwafrika aliyekuwa na shahada au digrii kutoka chuo Kikuu cha Makerere. TAGSA vilevile tulilalamika kuhusu kuajiri makarani wa kutoka India na hali walikuwepo Waafrika kutoka Afrika ya Mashariki na Nyasaland ambao wangeweza kujaza nafasi hizo kwa urahisi.

Vyama vyetu hivi viwili TAA na TAGSA viliwakilisha malalamiko haya tukifahamu fika kwamba Uingereza ilikuwa ikiitawala Tanganyikachini ya vifungu nambari 76 na 77 vya Umoja wa Mataifa ambavyo viliwekwa ili kuendeleza maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya nchi zilizokuwa chini ya udhamini. Kama mdhamini Uingereza ilitakiwa kuhimiza na kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa kwa wote bila kubagua kwa misingi yajinsia, lugha au dini. Lakini Uingereza ilikuwa ikipuuza vifungu hivi bila aibu. TAGSA tuliwakilisha malalamiko haya ili Umoja wa Mataifa ujue matatizo halisi ya ukoloni nchini Tanganyika.

Mimi nikiwa katibu wa TAGSA nilifuatilia serikalini masuala yaliyoainishwa ndani ya malalamiko yetu. Suala lililokuwa likituhangaisha sanawakati ule ilikuwa uajiri wa Wahindi kutoka India, jambo ambalo niliieleza serikali halikuwa na faida, maadam kulikuwako na Waafrika ndani ya nchi ambao wangeweza kujaza nafasi zile. Jambo hili lilikuwa likisababisha manugíuniko makubwa miongoni mwa Waafrika. Hakuna majibu maridhawa yaliyopatikana kutoka kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa. Barua tulizoandika serikalini juu ya masuala hayo zilipuzwa na Chief Secretary, Bruce Hutt. Katika kufuatilia malalamiko haya, Niliandika barua moja kali sana na kwa mara ya kwanza bila kutafuna maneno niliuliza uhalali wa Waingereza kututawala Waafrika wa Tanganyika. Nillimwambia Katibu Mkuu kuwa kwa kuwa serikali imeshindwa kupata ufumbuzi kwa matatizo ya Waafrika, Uingereza lazima ijitoe Tanganyikana Umoja wa Mataifa utawale Tanganyika. Barua hiyo ilimkasirisha Katibu Mkuu na siku chache baadaye nilipokea barua kutoka serikalini iliyokuwa imejaa vitisho, dharau, stihizai na makemeo. Nikajibiwa kuwa hakuwa na suala la Umoja wa Mataifa kutekeleza utawala wa moja kwa moja Tanganyika.

Dkt Mwanjisi alikuwa amegusa suala nyeti sanakwa kuzungumzia matatizo ya ubaguzi wa rangi uliokuwa ukitukabili Waafrika wa . Kawawa, kama mjumbe wa kamati, akaniandikia barua akanitahadharisha nisichapishe ile hotuba ya Dkt Mwanjisi katika jarida la TAGSA bila idhini ya kamati ya utendaji. Kufuatia majibishano haya kati ya TAGSA na serikali, Dkt Mwanjisi kama alivyofanyiwa Dk Kyaruzi kabla yake, akahamishwa kutoka hospitali ya Sewa Haji mjini Dar es Salaamhadi Kingolwira Prison Hospitalkaribu na Morogoro. Kawawa na yeye akapewa uhamisho kwenda Bukoba na mimi nikapewa uhamisho kwenda Mtwara. Dk Mwanjisi na Kawawa walikubali uhamisho wao na wakaondoka Dar es Salaam. Mimi nilikataa uhamisho na nikabakia Dar es Salaam kupinga uhamisho wangu.

Alipokuwa Bukoba ndipo Kawawa akamwandikia Ally Sykes barua ile ya mwaka 1952 akimweleza hali ya siasa kamaalivyoikuta Kanda ya Ziwa. Huyu ndiye Kawawa niliyemjua mimi kupitia nyaraka na mahojiano na Ally Sykes. Kwa kweli inasikitisha kuwa Dk Magotti hakupata fursa ya kuziangalia nyaraka hizi muhimu sana katika siyo historia ya Kawawa bali katika historia ya kuundwa kwa TANU na kudai uhuru wa Tanganyika. Endapo angepata nafasi ya kuziona hizi nyaraka zingempelekea katika kuwajua wazalendo wengine waliotajwa mle ndani kama Dk. Kyaruzi, Dk. Wilbard Mwanjisi ambao Kawawa alikuwanao katika harakati za TAGSA. Katika majina hayo angeweza kudodosa mengi kutoka kwa Mzee Kawawa na hivyo kuandika yale ambayo hayafahamiki kwa wengi. Hii imgekifanya kitabu kiwe cha maana.

Mathalan Kawawa angeeleza mtafaruku kati ya Mwalimu Nyerere na Dk. Mwanjisi nini chanzo chake na nini ikajakuwa matokeo yake. Halikadhalika angempa fursa Mzee Kawawa kumuhadithia mchango wa Dk. Michael Lugazia katika kuasisi kwa TANU hasa kipindi kile cha 1953 wakati TAA ilipokuwa inatayarisha rasimu ya katiba ya TANU. Kwa ufupi ni kuwa Dk Lugazi alikuwa akijaribu kuamsha ari ya TAA Bukoba ari iliyokufa kutokana na kufungwa kwa kiongozi wa TAA Bukoba Ali Migeyo. Kisa cha Ali Migeyo ni moja ya visa vinavyosikitisha sana katika historia ya Tanganyika kwani aliwekwa kizuizini na Mwalimu Nyerere kama alivyofungwa na Waingereza. Haiwezekani kuwa Kawawa asiwe na habari na kile kilichopelekea mpigania uhuru hodari kama Ali Migeyo aishie jela tena wakati nchi ikiwa huru. Migeyo alifungwa na wakoloni kwa kuwahamasisha Watanganyika kudai uhuru labda Mzee Kawawa angeulizwa angeeleza ni nini kilitokea wakaamua kumfunga Migeyo kama walivyomfunga Waingereza.

Kitabu kimegusia kazi alofanya Kawawa kama mtumishi wa serikali ya kikoloni katika kambi za raia wa Kenyawalioshukukiwa kuwa ni Mau Mau.  Katika hawa wafungwa walikuwawepo wananchama wa TANU ingawa hawa walikuwa Wakenya. Maarufu katika hawa alikuwa Dome Okochi Budohi (ambae kadi yake ya TANU ilikuwa na 6) na Patrick Aoko. Budohi alicheza senema pamoja na Kawawa iliyoitwa “Wageni Wema.” Kawawa na Budohi walikuwa wakifahamiana vizuri sana kwa sababu wote walikuwa wasanii. Budohi alikuwa mmojawapo katika bendi ya vijana wa mjini iliyojulikana kama Skylarks. Bendi hii baadaye ilibadilisha jina na kuitwa Blackbirds. Matangazo ya radio yalipoanza Tanganyika, Blackbirds midundo ya Blackbirds ilikuwa haikosekani kusikika radioni katika Sauti ya Dar es Salaam. Kawawa kama walivyo vijama wote wa Dar es Salaam wa wakati ule alikuwa mmmoja wa wapenzi wa bendi hii na alikuwa hakosekani Ukumbi wa Arnatouglo bendi hii ikitumbuiza katika ile miaka ya 1950. Ilikuwa katika ule upigaji muziki wa Budohi ndipo alipoungana na Kawawa katika kutengenezwa kwa senama hiyo ya “Wageni Wema” ambayo mwandishi kaitaja lakini aliishia hapo tu.

Budohi na Aoko ni kati ya wafungwa wa Mau Mau waliokuwa Handeni ambako Kawawa alikuwa na jukumu la kuwaangalia. Budohi ndiyo alikuwa mtu wa kati baina ya TAA na KAU na kuanzia hali ya hatari ilipotangazwa Kenya mwaka 1952 Budohi na Aoko wakawa katika jicho kali la makachero. Makachero hawa Waafrika wanafahamika na wengine walikuja kufanya kazi hiyohiyo katika Tanganyikahuru.  Hiki ndicho kipindi ambacho Kaimu Rais wa TAA na Katibu wa TAA Abdulwahid Sykes alipokutana na Kenyatta Nairobi. Wakati Wakenya hawa wanafungwa Tanganyika, viongozi wa KAU akina Bildad Kaggia, Jomo Kenyatta, Kun’gu Karumba, Achieng Oneko, Paul Ngei na Fred Kubai walikuwa wamekamatwa Kenya. Kawawa ni mmoja kati ya viongozi hawa na ingependeza sana kama kupitia kwake tungeelezwa jinsi KAU na TAA ilivyokuwa ikishirikiana kwani haiwezekani kuwa Budohi na Kawawa uswahiba wao ukaishia kwenye kucheza senema tu.

Wanaharakati wote walishtushwa na kutiwa mbaroni kwa Budohi na Aoko. Haiwezekani kuwa iwe Mzee Kawawa kasahau matukio haya muhimu. Budohi na Aoko walikuwa wamefungwa minyororo walipokuwa katika selo pale Kituo cha Kati cha Polisi kwa sasa jumba hiloliko kituo cha mabasi kinachojulikana kama“station.”  Waliwekwa pale kwa miezi sita muda wote wakiwa na minyororo miguuni. Waliwekwa pale kwa miezi sita wakihojiwa kabla hawajapelekwa Handeni walipomkuta Kawawa. Hivi ndivyo vitu ambavyo kwa hakika vingeongeza ladha ya kitabu cha Mzee Kawawa endapo mwandishi angechukua muda kutafiti na kuzungumza na watu waliokuwa katika harakati wakati ule ambao bado wa hai kama Ally Sykes na mdogo wake Balozi Abbas Sykes na wengine wengi ambao walikuwepo wakati ule kama Mzee Chipaka.

Katika migomo ya wakati wa kudai uhuru hakuna mgomo uliofanikiwa na kuvuta hisia za wananchi kamamgomo wa reli wa mwaka 1960 uliodumu kwa siku 62. Ukiachia kutajwa tu kama sehemu ya historia undani wake na jinsi mipango yake ilivyokwenda na nafasi ya viongozi wa Tanganyika Railway African Union (TRAU) walivyopata misaada kutoka nchi za Mashariki hivi havijawekwa wazi. Si treni, meli wala mabasi ya railway yaliyotembea kwa mieizi mitatu. Mipango ya mgomo huu ilifanyika Tabora ambako ndiko palikuwa na karakana kuu ya reli na hapo ndipo palipokuwa makao makuu ya viongozi wa TRAU, Salum Abdallah mwenyekiti na Kassanga Tumbo katibu. Kawawa ana mengi katika kadhia hii kwa kuwa yeye wakati ule ndiye alikuwa Katibu Mkuu wa TFL. Inasemekana mgomo huu miezi michache kabla Tanganyika haijapata uhuru ndiyo ilikuwa kama zinduo kwa Mwalimu Nyerere kutambua kuwa hakuwa peke yake na sauti kwa wananchi. Walikuwapo viongozi wengine pembeni yake ambao nao wakipiga wananchi wanacheza. Ilimdhihirikia kuwa huko mbeleni wanakokwenda ipo siku atapambana na viongozi hawa. Hivyo ndivyo ilivyotokea.

Inasemekana Mwalimu Nyerere akimtumia Kawawa alianza mipango kabambe ya kujitayarisha hilolisitokee. Hii ilikuwa nukta muhimu sanakwani haukupita muda baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 viongozi hawa wa vyama vya wafanyakazi wakajikuta wamewekwa kizuizini. Wasomaji wangependa kujua Kawawa alijihisi vipi wakati viongozi wenzake wa vyama vya wafanyakazi aliofanya nao kazi wakati wa kudai uhuru wakishirikiana na TANU kama Victor Mkello, Paul Pamba, Abdallah Mwamba, Hassan Khupe, Salum Abdallah na wengine wengi walipokamatwa mwaka wa 1964 na kuwekwa kizuizini kwa amri ya Mwalimu Nyerere. Maelezo ya Mzee Kawawa katika mambo haya yangetia mwanga katika yale mengi yasiyofahamika katika historia ya Tanzania.

Waislam wangependa sanakujua hisia za Kawawa kama muumini alihisi vipi wakati makachero walipomvamia mzalendo aliyepigania uhuru wa Tanganyika Mufti wa TanganyikaSheikh Hassan bin Amir usiku wa manane na kumrudisha Zanzibar na kuwekewa masharti kuwa hana ruhusa kurejea Tanzania Bara. Nilitegemea kusoma sakata zima la kukamatwa kwa Sheikh Hassan bin Amir na kuvunjwa kwa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) jumuia ya Waislam iliyokuwa ikipanga kujenga Chuo Kikuu Dar es Salaam.

Nilitegemea halikadhalika kusoma mchango wa Mzee Kawawa katika kuunda Bakwata. Mengi yamesemwa kuhusu hujuma hii kwa Waislam moja wapo ni kuwa EAMWS ilivunjwa kwa shinikizo la Kanisa Katoliki likimtumia Mwalimu Nyerere. Hili si jambo la siri tena tafiti mbalimbali zimefanywa na vitabu kuandikwa na waandishi kutoka nje ya Tanzania kuhusu tatizo hili la kujitokeza udini mapema baada ya uhuru kupatikana. Kwa kuwa Kawawa alikuwa pamoja na Mwalimu Nyerere na alishiriki katika kuunda Bakwata wananchi hasa Waislam wangenufaika kusoma hisia zake wakati maamuzi hayo yanapitishwa na serikali. Kwa hakika kuna maamuzi mengi sanaambayo Kawawa alishiriki yaliwaumiza sanaWaislam katika juhudi zao za kujitafutia elimu. Waislam wangependa sana kujua ni kipi kilikuwa kinamsukuma kufanya vile.

Kwa yeyote atakaepata bahati ya kusoma kitabu cha maisha ya Mzee Kawawa ni wazi hatakuta jipya ambalo hakuwa akilijua kabla. Kwa ajili hii basi mlango bado uko wazi kwa watafiti wengine kuandika kitabu kuhusu Rashidi Mfaume Kawawa kwani maisha ya Mzee Kawawa bado hayajaandikwa. Hata hivyo tumpongeze mwandishi kwa kazi hii kwani ni baada ya yeye kutuandikia kitabu ndipo nasi tumepata nguvu ya kunyanyua kalamu zetu na kusema.

3rd January 2010

No comments: