Dk.Salim Ahmed Salim |
WAZIRI Mkuu
mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, ameshangazwa na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC), kufuta uchaguzi visiwani humo.
Amesema
jumuiya za kimatifa zilishtushwa na uamuzi huo.
Salim
amesema kutokana na hali hiyo, kinachotakiwa hivi sasa ni haki
itendeke kwa kila kila upande kukaa na kutafuta suluhisho la kudumu.
“Tanzania
haijazoea migogoro ya siasa jambo ambalo si jema katika sura ya kimataifa,”
alisema.
Mwanadiplomasia
huyo wa kimataifa ametoa kauli hiyo,baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim
Jecha, kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, mwaka jana.
Siku chache
zilizopita, Jecha alitangaza kuwa uchaguzi huo unatarajiwa kurudiwa
Machi 20 mwaka huu.
Salim aliyasema
hayo alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu
nyumbani kwake, Msasani, Dar es Salaam jana.
Mwanadiplomasia
huyo wa kimataifa aliwahi kushika nafasi mbalimbali ikiwamo ya Katibu
Mkuu wa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) ambayo kwa sasa inatambulika
kama Umoja wa Afrika (AU).
Alisema
hatua ya kufutwa uchaguzi wa Zanzibar ni jambo lililowashangaza
wengi kwa kuwa uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu, huku waangalizi wa
ndani na nje wakiusifia katika ripoti zao.
“Ni hatua
ambayo imewashangaza wengi…imeibua sintofahamu kubwa katika nchi yetu kwa
sababu uchaguzi uliopita Tanzania ilipata sifa,baada ya uchaguzi kufanyika kwa
amani na utulivu. Lakini kitendo cha kufutwa kumewashangaza wengi na bado suala
hili halieleweki.
“Pia hili
jambo sidhani kama ni la mtu mmoja…sidhani kama ni la Jecha peke yake. Huu si
mustakabali mzuri kabisa, Zanzibar ni nchi ndogo, lakini ina historia kubwa
kisiasa hivyo juhudi za pamoja zifanyike kutatua mgogoro huu kwa matakwa ya
Watanzania kwa ujumla.
“Viongozi
wasisitize amani na utulivu na katika hili la Zanzibar kwa kweli haki itendeke
na waache ushabiki wa vyama iwe CCM au Upinzani, wote waweke ushabiki pembeni
na watatue mgogoro huu kwa mustakabali wa Wazanzibari na Watanzania kwa
ujumla,” alisema Dk. Salim.
Alisema
ingawa viongozi mbalimbali wamekutana na kufanya mazungumzo bila kupata
suluhu,pande zote ziendelee kukutana hadi suluhu ya pamoja ipatikane.
Salim,
alisema kuendelea kuachia hali hiyo iendelee kuna hatari ya kujenga
uhasama zaidi hivyo ni vema viongozi wafikirie zaidi masilahi ya Zanzibar.
“Nchi ipo
katika hali mbaya, migogoro iko kila pahala,Watanzania hatujazoea. Jambo hili
la Zanzibar likiendelea litazaa matatizo makubwa katika Taifa letu.
“Waliangalie
kwa uzito hata kama tarehe ya uchaguzi imetangazwa waendelee na mazungumzo,”
alisema mwadiplomasia huyo wa kimataifa.
Dk. Salim
ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alipoulizwa kama Kamati
Kuu ya chama tawala katika vikao vyake ilijadili suala la Zanzibar, alisema
limegusiwa ingawa haikuzungumzwa na ni nini kifanyike.
“…japo
sikushiriki vikao vyote hivi karibuni kwa sababu nilikuwa katika majukumu
mengine, jambo hili limezungumzwa japo halikugusiwa nini kifanyike.
“Jambo
hili, linastahili kupewa kipaumbele hata katika vikao vya Kamati ya Kuu ya CUF
(Chama cha Wananchi) na vyama vingine kwa sababu madhara yakitokea yataathiri
kila upande,” alisema.
MABANGO
Akizungumzia
kuibuka vitendo vya ubaguzi yakiwamo mabango katika
sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar,Dk. Salim alishangazwa na
hali hiyo.
Alisema
kitendo cha baadhi ya wanachama wa CCM kubeba bango lililokuwa
linaonyesha ubaguzi wa rangi wakati wa sherehe hizo, wakati suala
la ubaguzi lilimalizika tangu mwaka 1964.
Alisema
hatua hiyo, imeitia doa na ni aibu kwa Zanzibar na Tanzania.
“Nchi
imekuwa mstari wa mbele kupinga ubaguzi,nimeshangazwa sana kwa kitendo kile. Ni
jambo la kufedhehesha na lisipewe nafasi hata kidogo, ukianza kubagua
watakaoathirika wengi ni watoto wa viongozi, huu ni ujinga na
inaudhi,” alisema Dk. Salim.
Alisema
kitendo cha wanachama hao kubeba bango hilo,kinadhihirisha wazi kuwa wameishiwa
hoja kwa sababu suala la Hizbu ililikufa tangu mwaka 1964.
“Maswali ya
kujiuliza ni kwamba siku wale wanachama walipobeba yale mabango katika sherehe
za Mapinduzi kwa nini waliachiwa kufanya hivyo, viongozi waliokuwapo hawakuona?
“…kwa
sababu nchi imedumisha utu, undugu na kupambana na ubaguzi wa kila aina hili,
kitendo hiki kinasikitisha. Hata kama kuna mtu yeyote anayesema hili ni sawa
huko ndiyo kufilisika kabisa,” alisema.
AKUMBUKA YA
MWAKA 2005
Akizungumzia
jinsi alivyotuhumiwa kwa kuitwa Hizbu wakati wa mchakato wa urais mwaka 2005,
Dk. Salim alisema yalikuwa ni mambo ya kufadhaisha na yaliyojaa
uongo.
“Nilizushiwa
uongo sana na hata magazeti yakawa ‘part of the process’ (sehemu ya mchakato).
Ilikuwa ni uongo wa kupindukia…watu wanapoona unakubalika na hauna sifa yoyote
mbaya wanatafuta mambo ya uongo ili tu ‘wakudestroy’ (kukuharibu),” alisema.
No comments:
Post a Comment