Zanzibar 1950s |
Gazeti la Afrika Kwetu lilichapa makala haya katika toleo lake la tarehe 12 Oktoba 1961 na kwa hakika ni mahojiano mahakamani kati ya Wakili Talati na Karume. Katika mahojiano yale Karume aliweza kueleza hali halisi ya siasa kama ilivyokuwa wakati ule kati ya chama chake ASP na ZNP ambacho Karume alikitambulisha kwa jina la Hizbu. Ndani ya makala hii yapo mafunzo mengi kwa atakae kujifunza kutoka katika historia.
''Rais wa Afro-Shiraz Mheshimiwa Abeid A. Karume ametoa ushahidi wake mbele ya Halmashauri ya Uchunguzi. Siku ya Jumamosi tarehe 7/9/1961 asubuhi wakili wa ASP Bw. K.S. Talati alimuuliza Bwana Abeid Karume kuwa wewe ni kiongozi wa ASP? Alijibu naam. Tena alimuuliza kuwa wewe ni raia wa nchi hii? Baada ya kujibu hapo alimuuliza tena kuwa wewe ulikuwa mwanachama tangu wakati gani, akajibu mimi nilikuwa mwanachama katika chama cha African Association, akamuuliza tangu kuanza kwa chama hicho? Aliitikia na halafu akasema tangu nilikuwa Hon. Secretary mpaka nikapata u-president. Aliulizwa hiki chama cha Afro-Shiraz kilianza lini? Alijibu kilianza mwaka 1956 mwezi wa February, hapo wakili alimuuliza tena ilikuwaje.
Hapa kiongozi alieleza kwa makini na kuwafahamisha wachunguzi matokeo ya awali na kufika kikomo hiki Bw. Karume alisema kama kama sisi tulianza chama cha siasa katika mwaka huo na kuwa wote pamoja, ilipokuja Common Roll Election ndipo tulipochanganyika na kuunda chama cha siasa. Baada ya kufanya chama hiki tukapiga kura na kuwashinda Hizbu kwa ushahidi wote, baada ya kupata tukaona ndipo vitimbi namna kwa namna, kushinda kwetu ndiko kulikotuletea kupata ubaya na kuonekana wabaya wakubwa.
Hapo alihojiwa tena na aeleze sababu ya kufanya maduka katika mji, alisema kuwa sababu ya kufanya maduka, maduka haya ni ya cooperative , walijikusanya watu 100 kila duka na kufanya michango kwa ajili ya kuanzisha maduka na yakawa kwa wingi sababu maduka hayo huwa na kitu baada ya mwaka watu kupata wale wenye ushirika. Akaulizwa hamkufanya sababu ya kupinga akajibu sio kweli.
Wakili Bwana Talati akamuuliza habari kuhusu motokaa sababu ya kutia alama, alijibu kuwa Afro-Shirazi hawana motokaa, hizi motokaa ni za matajiri na wanafanya hivyo kwa maslahi yao wenyewe sio watu wa katika chama cha ASP.
Tena alimuuliza sababu ya kufukuzwa watu katika mashamba, alisema kuwa mambo hayo yalitoka kwa viongozi wa Hizbu, ndio wenye mashamba na Wamanga walipoona wakuu wao wanafanya hivyo na wao walikaa wote kwa sauti moja kuwafukuza watu katika mashamba. Watu hao walikaa wote kwa muda wa miaka mingi lakini tangu kushindwa katika uchaguzi huo ndipo yalipotokea mambo kama haya.
Wakili alimuuliza kuwa kabla ya kutokea uchaguzi yalikuwapo mambo ya kuwafukuza watu mashambani? Alijibu hayakutokea kabisa, hapo aliambiwa eleza: Akasema kuwa katika mfukuzano huo walifanya Register Cards zao kila mtu asiye ni mwanachama wa Hizbu hana haki ya kulima katika mashamba ya Mwarabu yeyote na ya Mmanga, wakaweka shabaha hiyo kwa sababu ya kupata memba tena kila aliyekuwa mwanachama wa ASP ni lazima atolewe katika mashamba na kung’olewa vitu vyao na kukata migomba hata mimi nikaona jambo baya sana nikaenda kwa Bwana Senior Commissioner kumueleza mambo haya na yakaendelea kwa nguvu kabisa ikafanywa ni lazima kila mtu anaetolewa katika mashamba ni wajibu apate haki ya malipo ya vile vitu vyake. Wapo waliolipwa na wengine hawakulipwa kabisa. Tena wakili alimuuliza katika hawa waliotolewa katika mashamba walikuwa watu wa Bara? Alijibu: katika hawa wengi ni watu wa Unguja ni raia wa Bw.Seyyid kidogo sana ambao ni watu wa Bara.
Alihojiwa habari ya ZNP kuchukua bendera, alijibu jambo hili sisi tulilipinga sana hatukupendelea kabisa bendera ya mfalme kuchezewa katika chama cha siasa. Sababu ya hawa Hizbu kufanya hivi wanawadanganya watu kuwa chama cha Hizbu ni chama cha mfalme nae hayumo katika mambo ya siasa, hata yalipozidi tukaona ni lazima kupeleka maombi yetu kwa Bwana Balozi, hapo tuliitwa na kuambiwa vyama vyote vitatu na kutia sahihi lakini Hizbu walishikilia hapohapo hawakusikia na wakaendelea hata baada ya kwisha uchaguzi huu wa June Mosi wakawa hawaweki tena bendera katika motokaa zao na kufanya fujo kama ile.
Tena aliulizwa na wakili: YOU walikuwa na Band? Akasema kuwa hawa wakisikia kama Mfalme anakwenda mahali fulani, hutoka na Band yao wakawa wanamsalim na baada ya kuondoka wakatumia propaganda ili watu wasadikishwe na kuamini kuwa hiki ni chama cha Mfalme, na mfalme hayumo kabisa.
Akaulizwa mambo yahusuyo mikutano: Naye alisema kuwa katika mikutano mingi mimi sikupata kwenda ila nilifika nafsi yangu katika mkutano mmoja tu wa Ng’ambo ambao siku hiyo nilimsikia Abdulrahman Mohamed Babu, Ahmed Seif na Sh. Ali Muhsin. Wa kwanza alisema Hizbu wote kuweni imara kwa sababu Manjo amekaa kwa kutaka kututawalia nasi hatutaki kutawaliwa na watu wa Bara Wanyamwezi na Wandengereko.
Babu akawauliza mnakubali kutawaliwa na watu wa Bara? Watu waliohudhuria hapo walijibu kuwa hatutaki, basi tufanye kila tuwezalo lazima tuchukue serikali yetu wala msiogope tena. Ahmed Seif alisema kwa sauti kubwa kuwa sisi sote tusimame kiwanaume wala msifanye dharau, tufanye kama tuwezavyo lazima tuchukue serikali au tumwage damu? Mnasemaje? Wanachama wa Hizbu waliitikia kwa nguvu na halafu akawauliza tena mara tatu, hata aliposimama kiongozi mkuu aliyatilia nguvu maneno ya Ahmed Seif. Akaulizwa katika hotuba zako zote uliwahi kutamka jambo kama hili? Alijibu kuwa ni jambo la hatari kwa Binadamu yoyote mwenye kujua ni vibaya kusema maneno kama haya, mimi siwezi kusema maneno kama haya, wala hayatanitoka.''
Jina la gazeti: Afrika Kwetu
Toleo: Na 48
Tarehe: 12 Octoba 1961
Ukurasa wa 4.
Bei kwa toleo: Senti 25
Bei kwa mwaka: Sh 12 kwa Unguja mjini na Sh 17 kwingineko
Mhariri mkuu: M. A. Reihan Mzigua
Msimamizi wa gazeti: Ramadhan I. Sadalla
TANBIHI: Kwa hisani ya ukurasa wetu wa Tulikotoka ni Mbali
No comments:
Post a Comment