PIUS MSEKWA NA HISTORIA YA KUPIGANIA UHURU WA
TANGANYIKA
Mohamed Said
| Earle Seaton na Julius Nyerere |
‘’Mwalimu Nyerere alikuwa na uwezo
mkubwa sana wa kuridhisha watu kwa nguvu ya hoja zake (power of persuasion).
Uwezo huo ndio uliomsaidia kupata mafanikio makubwa katika malengo yake ya
kisiasa. Uwezo huo unajidhihirisha katika matukio yafuatayo:
Kwanza, ni
pale alipofanikiwa kuwaridhisha kwa nguvu ya hoja zake, wanachama wa Asasi ya
Kijamii ya kupigania maslahi ya wafanyakazi wa Kiafrika katika serikali ya Kikoloni,
iliyokuwa inaitwa “Tanganyika African Association” (TAA); kuvunja chama chao
hicho na badala yake kuunda chama kipya cha siasa cha “Tanganyika African
National Union (TANU), mwezi Julai 1954, ili kiwe ni chombo cha kupigania uhuru
wa Tanganyika.’’
(Pius Msekwa Raia Mwema toleo la
446 24 Februari 2016 ‘’Siku Nyerere Alipokataa Viatu New York.’’)
Nimeona nianze na nukuu hii ili
msomaji aelewe nini Mzee Msekwa amesema pale mini nitakapoeleza historia ya
uhuru wa Tanganyika kama nilivyoelezwa na wazee wangu ambao walikuwa bega kwa bega na Mwalimu Nyerere wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika. Imekuwa sasa jambo la
kawaida sana kwa wale waliokuja kuingia TANU baadae sana kuonyesha dharau kwa
chama cha TAA ambacho ndicho TANU ilitokea. Wakati mwingine dharau hii inaweza
ikampita mtu ikiwa hana ujuzi wa kusoma katikakati ya mistari.
Angalia jinsi
Mzee Msekwa alivyoileta TAA kwa wasomaji wake. Mzee Msekwa ameiita TAA, ‘’Asasi
ya Kijamii ya kupigania maslahi ya wafanyakazi wa Kiafrika katika serikali ya
Kioloni, iliyokuwa inaitwa “Tanganyika African Association” (TAA)…'' Mzee Msekwa
anaogopa kuipa TAA haki yake kuwa kilikuwa chama cha siasa ‘’chinichini’’ kwa
sababu akifanya hivyo atashindwa hapo baadae kumvisha Mwalimu Nyerere joho
analotaka kumvisha kuwa hapakuwapo harakati za kudai uhuru wa Tanganyika hadi
pale alipotokea Nyerere mwaka wa 1952. Huu msimamo wa Mzee Msekwa ndiyo
historia iliyozoeleka na ndiyo historia rasmi ya uhuru wa Tanganyika.
Kabla sijaieleza historia ya TANU
ningependa kusema kitu kuhusu kutoka kauli ya Mzee Msekwa kuwa TAA kuwa kilikuwa chama cha, ‘’kupigania maslahi
ya wafanyakazi wa Kiafrika katika serikali ya kikoloni.’’
Hii pia si kweli.
Chama cha kupigania maslahi ya wafanyakazi wa Kiafrika kilikuwa Tanganyika
Government Servant Association (TAGSA) na viongozi wake ndiyo hao hao pia walikuwa
katika TAA wengine kwa dhahir na wengine kwa kificho. Baadhi ya viongozi hawa
ni Thomas Marealle, Ally Sykes, Dr. Wilbert Mwanjisi, Rashid Kawawa kuwataja
wachache. Hawa ndiyo walikuwa wanasiasa wa nyakazti zile.
Chama cha TAA kilikuwa kikifanya mambo mtambuka, kikishughulika na
kila ovu lililomgusa Mwafrika wa Tanganyika awe mkulima wa Meru au mfanyakazi wa serikalini.
Vuguvugu la siasa Tanganyika lilikuja na sura na mwelekeo mpya mwaka wa 1950 palitokea ‘’mapinduzi’’
Makao Makuu ya TAA New Street baada ya kuona kuwa viongozi waliokuwapo
madarakani wengi wao wakiwa watu wazima hawakuwa wanakwenda na kasi ya
mabadiliko ya siasa kama ilivyokuwa dunia nzima kwa makoloni yote ya
Muingereza wananchi kuanzisha vuguvugu la kutaka kujitawala. Waingereza walikuwa wanashughulishwa na wazalendo India na Gahana kudai nchi zao. Hapa ndipo Tanganyika nayo ikajiingiza katika vuguvugu lile la kudai uhuru. Hii katika TAA ya mwaka wa 1950 haikuwa fikra
ya Mwalimu Nyerere kwani wakati huo hakuna aliyekuwa anamjua katika harakati za
siasa za kizalendo pale New Street.
Hamza Kibwana Mwapachu na Abdulwahid Kleist Sykes
wakisaidiwa na Schneider Abdillah Plantan waliutia heka heka uongozi uliokuwapo
hadi kufikia kuitishwa uchaguzi na Mwalimu Thomas Saudt Plantan aliyekuwa rais
na Clement Mohamed Mtamila aliyekuwa katibu kuondoshwa madarakani. Dr. Vedasto
Kyaruzi akachaguliwa kuwa rais na Abdul Sykes katibu. Uchaguzi huu
ulifanyika Ukumbi wa Arnautoglo. Juhudi hizi zote zilifanywa ili uingie uongozi
mpya wa vijana wenye fikra mpya ili uweze kupambana na Waingereza watoe uhuru.
Mwalimu Nyerere hakuwapo katika harakati hizi.
Sasa tuangalie uongozi huu mpya
wa TAA ulifanya nini kuleta matumaini mapya kwa Watanganyika.
Hapa ndipo anapoingia Abdul Sykes
katika kuunda TANU. Historia ya TANU ukipenda unawea ukaianzia hapa 1950 na
Abdul Sykes na wenzake aliokuwanao katika uongozi wa TAA mashuhuri akiwa Hamza Mwapachu. Ukipenda unaweza ukaenda nyuma pia hadi
mwaka wa 1929 kwa baba yake Kleist Sykes alipoasisi African Association, Kleist akiwa katibu. Mtoto na baba yake wote wameacha nyaraka zinazoweza kueleza historia ya siasa Tanganyika kuanzia miaka ya mwanzo ya karne ya ishirini.
Ikiwa
utaanza kuitafiti TANU kuanzia mwaka wa 1929, utaikuta katika nyaraka hizo barua
aliyoandika Kleist Sykes mwaka wa 1933 kumwandikia Mzee bin Sudi aliyekuwa rais wa chama
wakati huo, akimwambia kuwa wao wameanzisha hili jambo na hao watakaokuja
baadae watalikamilisha. Barua hii inatokana na sintofahau iliyotokea katika African Association kati ya Kleist na Erika Fiah kiasi kupelekea Kleist kujiuzulu uongozi. Chama kilidorora na Mzee bin Sudi akamwandikia barua Klesit ya kumuomba arejeshe roho nyuma arudi kwenye chama. Ndipo Kleist alipomwandikia Mzee bin Sudi barua hiyo. Barua hii Kleist aliindika kwa kutanguliza maneno haya: Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema...''
Jambo alilokuwa analizungumza Kleist ilikuwa ni kuwaunganisha Waafrika kudai
nchi yao kutoka ukoloni wa Waingereza. Kwa mukhtasari huu ndiyo utangulizi wa historia
ya uhuru wa Tanganyika na kuanzishwa kwa TANU. Inawezekana sana kuwa Mzee Msekwa hakuwa anaijua historia hii ya TANU kwa undani wake na ndiyo maana akawa kanasa katika mtego wa TANU ilianzishwa na Nyerere mwaka wa 1954. Hili jambo la kuasisi TANU halikuhitaji, ‘’power
of persuasion,’’ ya Mwalimu Nyerere mwaka wa 1954 kama alivyoeleza Mzee Msekwa.
Mwaka wa 1950 TAA
iliwasilisha kwenye ‘’Constitutional Development Committee,’’ ya Gavana Edward
Twining mapendekezo yake Tanganyika itawaliwe vipi na kubwa walilotaka TAA ni
kuwe na uchaguzi kuwachagua wajumbe kwenye Baraza la Kutunga Sheria
(Legislative Council) na baada ya muda Tanganyika ipewe uhuru wake. Sera ya TAA ilikuwa ''Mtu Mmoja Kura Moja.'' Kazi hii ya
kutengeneza mapendekezo haya ilifanywa na TAA Political Sub Committee (Kamati
Ndogo ya Siasa katika TAA) iliyoundwa na uongozi mpya wa Dr. Kyaruzi na Abdul
Sykes.
Katika wajumbe wa kamati hii alikuwepo Sheikh Hassan bin Amir kama Mufti wa Tanganyika, Hamza
Mwapachu, Said Chaurembo, Steven Mhando na John Rupia. Lakini kulikuwa na mtu
aliyekuwa akiishauri kamati hii katika mbinu za sheria kukabiliana na
Waingereza kama dola iliyokabidhiwa Tanganyika iliyokuwa nchi chini ya Udhamini
wa UNO yaani Mandate Territory kwa kifungu 76 na 77 cha Mkataba wa Umoja wa
Mataifa. Huyu mtu aliyekuwa akiisaidia TAA katika kuishauri vipi iiendee suala la udhamini jina lake lilikuwa Earl Seaton. Huyu alikuwa
rafiki wa Abdu Sykes na ni Abdul ndiye aliyemuingiza katika siasa za Tanganyika.
Seaton alikuwa mwanasheria mjini Moshi na mtu kutoka Bermuda. Katika nyaraka
zake Abdul Sykes kaueleza vyema mchango wa Seaton katika kipindi hiki cha 1950
kuelekea kuasisiwa kwa TANU mwaka wa 1954. Mapendekezo haya ya TAA Political Sub Committee yalijadiliwa katika mkutano wa kuasisi TANU Julai 1954 na ndiyo iliyotengezeza hotuba aliyosoma Nyerere UNO mwaka wa 1955.
Mwaka wa 1952 Seaton alifutana na Japhet
Kirilo kwenda UNO ambako Kirilo alihutubia Kamati ya Udahamini ya UNO kuhusu dhulma za Wazungu kufuatia Mgogoro wa Ardhi ya Wameru. Abdul Sykes wakati ule akiwa Kaimu Rais na Katibu wa TAA alishirikiana
kwa karibu sana na Meru Citizens Union ya akina Sablak na Kirilo katika mgogoro huu. Seaton akiwa ndiyo wakili wao. Ili kuivunja nguvu TAA Waingereza walianza kuwaandama viongozi. Kipindi hiki Dr. Kyaruzi alihamishwa Dar
es Salaam kwenda, kwanza Kingolwira kisha Nzega kuafuatia harakati hizi za siasa
ndani ya TAA. Hamza Mwapachu alipelekwa uhamishoni kiswani Nansio.
Abdul Sykes alikuwa
katika hatihati ya kufukuzwa kazi kama Market Master Kariakoo Market. Kufuatia
haya yote serikali ya kikoloni ikatoa Government Circular No. 5 ya mwaka 1953 kupiga
marufuku wafanyakazi serikalini kujishughulisha na siasa. Sina haja ya
kumweleza msomaji kuwa TAA ilikuwa kwenye siasa na hicho kitu alichokieleza
Mzee Msekwa kuwa TAA ilikuwa asasi ya kijamii akiwa na maana ya’’welfare
society,’’kuishusha hadhi ya siasa TAA kukifanya chama kisichokuwa na malengo ya maana historia hiyo si sawa wala haina ushahidi.
Si kweli kussema kuwa Mwalimu
aliwashajiisha aliowakuta katika TAA pale Makao Makuu kukubali kuibadilisha
TAA iwe chama cha siasa TANU. Fikra ya kuanzisha chama cha TANU alikuwanayo Abdul Sykes toka alipokuwa Burma katika Vita Vya Pili vya Dunia. Historia ya TANU haiwezi
kuanza na Mwalimu Nyerere labda kwa kulazimisha iwe hivyo. Historia ya TANU ni ndefu na inatoka mbali na
inawakusanya wazalendo wengi sana ambao kwa bahati mbaya nchi imewasahau.
Kuna mengi kuhusu nani alikuwa anafikiriwa kuongoza chama cha siasa kitakapoanzishwa na majina kadhaa yalikuwa katika fikra za wazalendo hawa ambao historia imewatupa nje.
Ikipatikana nafasi In Shaallah tutawazungumza wazalendo hawa waliokusudiwa kuingoza TANU toka miaka ya mwisho 1940s na mwanzoni 1950s na hapo tutapata nafasi ya kuona ilikuwaje Mwalimu Nyerere akaingia katika uongozi.
Kilitokea nini kwa wale waliofikiriwa kuiongoza Tanganyika kama Chief David Kidaha Makwaia na Paul Bomani hawakuichukua nafasi ile.
Kilitokea nini kwa wale waliofikiriwa kuiongoza Tanganyika kama Chief David Kidaha Makwaia na Paul Bomani hawakuichukua nafasi ile.
Nimeona nitawachosha wasomaji ikiwa nitaeleza nini kilipitika katika kukitegua kitendawili wa Kura Tatu.
Mzee Msekwa kamsifia Mwalimu Nyerere katika ''power of persuasion,'' kwenye Kura Tatu Tabora mwaka wa 1958 lakini bahati mbaya labda kwa kutoijua historia ya uhuru wa Tanganyika kayaacha nje majina mengi ya watu waliopanga mkakati ule.
Mkakati uliopangwa Tanga Mwalimu Nyerere akishirikiana katika mpango ule na Sheikh Abdallah Rashid Sembe, Hamis Heri, Ng'anzi Mohamed, Amos Kisenge, Mwalim Kihere, Mustafa Shauri na Abdallah Makata.
Ikipatika nafasi In Shaallah tutakieleza pia kisa hiki.
| Kushoto: Dossa Aziz, Julius Nyerere, Abdul Sykes na Lawi Sijaona |
Msome hapo chini Mzee Msekwa:
http://www.raiamwema.co.tz/siku-mwalimu-nyerere-alipokataa-viatu-new-york
No comments:
Post a Comment