Haukupita muda watu wakawa wamekusanyika uwanja wa ndege wa Tanga kusubiri mwili wa Sheikh Muhammad Bakari uliowasili majira ya saa nane. Tanga ilikuwa imeondokewa na msomi wake mkubwa ambae kabla ya kifo chake Sheikh Muhammad Ayub alipatapo kusema kuwa mwanafunzi wake Muhammad Bakari ni mwanazuoni.
Katika kumueleza Sheikh Muhammad Bakari Sheikh Suleiman Amrani Kilemile akizungumza kwenye msiba Dar es Salaam kabla ya mwili haujapelekwa uwanja wa ndege alisema kuwa Sheikh Muhammad Bakari kwao wao walipokuwa wanasoma kwa Sheikh Muhammad Ayub alikuwa ‘’kaka’’ na ‘’mwalimu.’’ Alimsifia Sheikh Muhammad Bakari kwa kusema kuwa alikuwa mtu wa subira ya hali ya juu wakati wa kusoma kwani wakati ule hali ilikuwa ngumu. Aliongeza na kusema kuwa Sheikh Muhammad Bakari alikuwa msomi wa sifa na alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kusoma vitabu. Akaendelea na kusema kuwa Sheikh Muhammad Bakari alikuwa na tabia ya kuweka sahihi yake kwenye kurasa ya mwisho ya kila kitabu alichomaliza kusoma.
Baada ya kifo cha Sheikh Muhammad Ayub Sheikh Muhammad Bakari alifundisha Shamsiyya kwa muda akishika nafasi ya mwalimu wake. Sheikh Muhammad Bakari aliondoka Shamsiyya na kwenda Magomeni kwenye msikiti mdogo na hapo akaendelea kusomesha chini ya taasisi yake mpya aliyoiita Shams Maarif akisaidiwa na walimu wachache waliomfuata kutoka Shamsiyya mmojawao akiwa Mwalimu Miraj na Sheikh Said Makata.
Hiki kilikuwa kipindi kigumu sana kwake na kwa wanafunzi waliomfuata kwani alijaza wanafunzi wengi katika mahali finyu. Watu wengi hawakupenda kuona hali ile lakini hawakuwa na la kufanya. Sheikh Muhammad Ayub aliendelea kusomaesha na mara kwa mara alikuwa akisema kuwa ile hali iliyokuwa ikimkabili katika kusomesha ilikuwa ni qadar ya Allah.
|
Shams Maarif ilikuwa imezingirwa kila
upande na wale waliopata nafasi ya kuingia msikitini ni wale ambao walifika
pale asubuhi na mapema. Mji wa Tanga ulijiinamia.
Maziko haya yatazungumzwa kwa
miaka mingi sana ijayo In Shaallah.
Kwa hakika haya maziko yamemueleza Sheikh
Muhammad Bakari alikuwa nani.
Maziko haya yamethibitisha kuwa silsila yake kama alivyopata kuieleza mwenyewe siku moja kuwa kapokea ilm kutoka kwa mwalimu wake Sheikh Muhammad Ayub na inakwenda nyuma hadi kufikia kwa Mtume SAW na kumalizikia kwa JIbril AS ambae alipokea kutoka kwa Allah SW.
Ningependa kumaliza kwa kusema lini kwa mara ya kwanza nilipata kulisikia jina la Sheikh Muhammad Bakari.
Ilikuwa siku moja Msikiti wa Mtoro katika miaka ya 1970. Sheikh Kassim
Juma alikuwa anamueleza Sheikh Muhammad Ayub.
Alipomaliza akaeleza maajabu aliyoyaona
kwa Sheikh Muhammad Bakari.
Wakati ule Sheikh Muhammad Bakari alikuwa bado
kijana mdogo mwanafunzi. Sheikh Kassim alisema kubwa aliloliona kwake Sheikh
Muhammad Bakari ni ahklaki njema.
Kisha Sheikh Kassim Juma akaeleza umahiri
wa Sheikh Muhammad Bakari katika ilm.
Ilipita miaka mingi hadi mimi kuja kujuana na Sheikh Muhammad
Bakari wakati huo sasa Sheikh Muhammad Bakari alikuwa tayari ni sheikh na
Mudir wa Shamsiyya chuo alichoasisi mwalimu wake Sheikh Muhammad Ayub.
No comments:
Post a Comment