Thursday, 26 May 2016

FORGOTTEN FACTS ABOUT THE UNION - OTHMAN OTHMAN


Ndugu Salim,
Ni juu ya wasomi, hasa wanahistoria wakisaidiwa na mashuhuda wa matukeo, kuinusuru historia isipotoshwe au kupindwa kwa maslahi yoyote yale ya kisiasa. Tuwe chonjo, angalau sisi mashuhuda tuliobaki bado hai. Mwenyezi Mungu Atupe umri mrefu wenye afya.

Ndani ya PAFMECA  ( Pan-African Freedom Movement for East and Central Africa), mshikamo wa Vuguvugu za vyama vyote vya kupigania huru katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, kulikuwemo pia ndani yake vyama vya ASP na Hizbu ( Nationalist) vya Zanzibar. Kwa hivyo mimi napata taabu kufahamu kwamba PAFMECA hiyohiyo na tena wakati huohuo iwe ni taasisi ilioowanisha mpango wa kufikiwa mapatano baina ya TANU na ASP ambayo moja katika ibara za mapatano hayo ilitaja kwamba "Mwishowe, kupatikana uhuru wa Tanganyika na Zanzibar kutapelekea nchi mbili hizo kuungana pamoja kuwa Jamhuri ya Kiafrika." Napata taabu kukumbuka kwamba PAFMECA iliiunga mkono ajenda ya aina hiyo, japokuwa  viongozi wake waliungana na zile hisia za kutaka Afrika nzima ilioungana katika miaka inayofuata.

Kweli PAFMECA ilijaribu mara kadhaa kuwa mpatanishi ( kwa kuwatuma Dr. Hastings Kamuzu Banda wa Malawi- wakati huo ikiwa katika Shirikisho la Rodesia/Kaskazini na Kusini na Nyasaland- na pia Bibi Titi Mohammed wa TANU ) katika mvutano uliokuweko Zanzibar wakati huo baina ya ASP na Hizbu. Vyama  hivyo vyote viwili vilitambuliwa sawasawa na PAFMECA kuwa ni vya kizalendo vyenye kupinga ukoloni wa Kiingereza Visiwani. Japokuwa natambua kwamba baadae ilikuja kujulikana kwamba kulikuweko baadhi ya viongozi wa PAFMECA walioelemea zaidi, bila ya kuonesha hadharani,upande wa ASP, huenda kama unavyosema kupinga tu uzalendo wa Kiarabu ulioambatanishwa pia na Rais Gamal Abdel Nasser wa Misri.Hiyo hati ya TANU unayoitaja yawezekana yalikuwa tu maono ya baadhi ya wana TANU  wa wakati huo na ambayo wanachama wengi, hata viongozi, wa ASP walikuwa hawana habari nayo.

Juni 1959 nilikuwa miezi minne kabla ya kufikia umri wa miaka 12. Licha ya utoto wangu nilikuwa mfuatilizi wa karibu sana  wa mikutano ya hadhara ya ASP na Hizbu hapo Raha leo na karibu na Malindi huko Zanzibar. Licha ya hayo nilifaidika kwa kuzaliwa katika "nyumba ya kisiasa" ambapo siasa ilikuwa inazungumzwa kwa masaa 24 kila siku, kama chakula chetu, na ndani ya nyumba hiyo wanafamilia wakiwa na mitizamo tafauti ya kisiasa miongoni mwao. Ila Baba, Mungu Amrehemu, aliniambia "fuatiliza na soma siasa na vitimbi vyake, lakini katu usithubutu kuwa mwanasiasa- huo ni mchezo mchafu." Nimeifuata kauli yake hiyo, sijamsaliti na sijajuta.

Othman

(Othman writing to Salim)

No comments: