Waasisi wa TANU Julai 1954 |
Tatizo halipo katika kumtaja Mwalimu Nyerere katika historia ya
TANU na harakati za uhuru.
Tatizo lipo katika kumtaja Mwalimu Nyerere peke yake na kuwaacha
wazalendo wenzake waliokuwa katika kupambana na ukoloni kwanza
kabla yake na kisha wakiwa pamoja.
Ukiwa utaielezea historia ya TANU ukidhani unaweza ukaikamilisha bila
ya kuwataja akina Sykes utakuwa umeipunja historia pakubwa sana kiasi
cha kunyofoa nusu karne ya historia ya Tanganyika.
Historia ya Abdul Sykes haikufahamika popote hadi nilipoiandika na kitabu
kuchapwa London mwaka wa 1998 na ilizua tafaruku kubwa katika duru
za ndani ya CCM na kwa baadhi ya wasomi nchini.
Hapana haja ya kurudia kwani hili hapa barzani tumelizungumza sana na
wachangiaji wengi wemetoa mawazo yao.
Mwalimu Nyerere asingeweza kufanikiwa chochote katika Dar es Salaam
ya miaka ya 1950 bila ya kuungwa mkono na wenyeji aliowakuta katika
siasa.
Mwalimu Nyerere hakuja na chama wala hakuwa na fedha za kuanzisha
chama achilia mbali kuwa na watu wa kumsikiliza.
Chama alikikuta pale New Street kikiwa na viongozi na wanachama na fedha
za kuendesha harakati zilikuwa katika mikono ya John Rupia, Dossa Aziz
na Abdul na Ally Sykes.
Hata TANU ilipoasisiwa kadi za kwanza 1000 zilichapwa na Ally Sykes kutoka
mfukoni kwake na kadi namba moja Ally Sykes alimwandikia Rais wa TANU
Julius Kambarage Nyerere, kadi na namba 2 yake mwenyewe na kadi na. 3
akamwandika kaka yake Abdulwahid Kleist Sykes nk. nk.
Si hilo tu hata usanifu wa kadi ya TANU kuweka mwenge na rangi ya kijani
ilikuwa kazi ya Ally Sykes kwa kudurufu kadi yake ya Tanganyika Legion,
askari wa zamani wa KAR waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Ukipenda kujua habari hizi kwa kirefu msome Judith Listowel, ''The Making
of Tanganyika (Chato and Windus 1965).
Gari ya kwanza ya TANU alitoa Dossa Aziz kusaidia harakati za kudai uhuru.
Abdul Sykes akaishi na Mwalimu Nyerere nyumbani kwake baada ya Mwalimu
kuacha kazi ya kusomesha.
Mzee Rupia akamtafutia Nyerere nyumba Magomeni na hapo ndipo akahama
kwa Abdul Mtaa wa Aggrey na Sikukuu kwenda kwake.
Chuo Cha Kivukoni wamejaribu kuandika historia ya TANU bila ya kuwataja
wenye TANU yao sasa shuhudia leo jinsi walivyokuwa kichekesho katika duru
za utafiti wa kisomi.
No comments:
Post a Comment