Tuesday, 19 July 2016

TAAZIA SHEIKH KHAMIS SAID MSINDIKAJI WA MWISHO WA MLANGO WA WANAZUONI WA ZAMA ZAKE



Photo
Sheikh Khamis Said


Sheikh Khamisi ameufunga mlango wa wanazuoni wakubwa wa rika lake, ni mwanazuoni mkubwa ambae hakupenda makuu na wala hakua msemaji na hakua Sheikh wa kujitokeza katika hafla zisizo na ulazima na hata akitokea hatozungumza chochote, na ndio sababu wengi hawakumfaham Sheikh huyu yeye alichagua kusomesha zaidi, na ametoa wanazuoni wengi ni Sheikh aliejipamba zaidi na uchamungu. Innalillahi wainna ilayhi raajiun.

Huyo ni katika masheikh wa mwanzo kusoma nje ya nchi baada ya kusoma Kilwa baadae Zanzibar miaka ya hamsini na ndio Sheikh wa kina  Sheikh Twaha Bane na wengine wengi tu, ni sheikh wa mfano kwani alijikita na mambo ya elimu na biashara waalimu wa madrasa zake ni wanafunzi wake na anawalipa mwenyewe. Sheikh Khamis Said alikuwa na Madras kubwa Mtoni kwa Aziz Ali.

Sheikh Khamis ni mmoja wa wanafunzi wakubwa wa Gofu Zanzibar na alikuwa swahibu mkubwa wa Marhum Sheikh Nurdin Hussein Shadhilly.

Photo

SALAMU ZA RAMBI RAMBI YA SHEIKH KHAMIS SAID KHALFAN KUTOKA KALAMU EDUCATION FOUNDATION

Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un (إِنَّا للهِ وَإِنَّـا إِلَيْهِ رَاجِعونَ)  Sura Al-Baqara, aya 156.

Sheikh Khamis Said Khalfan amefariki mchana wa saa tisa mchana leo Shawaaal 14, 1437H sawa na 19 July, 2016 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Sheikh Said mmoja wa watu wenye elimu kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki alisifika sana katika elimu na uchamungu.

Sheikh alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu (Blood Pressure) ambapo alipelekwa Hospitali Shree Hindu Mandal na baadae kuhamishiwa Hospital ya Muhimbili.

Sheikh alikwenda Zanzibar kusoma kwa Sheikh Suleiman Alawi na Alhabib Ali Badawi. Pia amesoma kwa Alhabib Omar bin Sumeit huko huko Zanzibar.Alisoma kwa muda wa miaka 21. Miongoni mwa aliosoma nao huko alikuwa ni Sheikh Abdallah Ayoub kwa miaka minane.

Mwaka 1967 aliruhusiwa kurudi Dar es Salaam. Aliporudi hakuanzisha kusomesha na alianza ziara ya kutembelea Madrasa Kadhaa nchini.

Alienda Madrasa Ya Shamsia (Tamta) na kukaa kwa Sheikh Muhammad Ayoub kwa siku Tisa. Kisha alikwenda Arusha na Lamu. Ziara hiyo ilikuwa ni mwaka 1967 na 1968.

Mwaka 1969 alianzisha Madrasatul Ihyaa iliyopo mtoni kwa Azizi ali jijini Dar es Salaam. Alianza kwa kusomeshea msikitini.

Mwaka 1970 ndipo alipopata jengo la madrasa na alianzisha Boarding ya Madarsa.

Madrasa hiyo ikaendelea na kupata matawi kadhaa ikiwemo Kilwa Kisiwani na Kilwa Masoko na sehemu kadhaa nchini.

Kalamu Education Foundation Imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Madrassa za Sheikh Khamis hasa ile ya Kilwa ambapo kushiriana nayo Mwaka 2014 Kalamu ilifanikiwa kuwapeleka vijana wanane wa Madrassa Lyhaa Nchini Sudan katika Chuo International University of Africa kusomea kozi mbali mbali zikiwemo za Sayansi, Sheria na Dini.

Sheikh Khamis kushiriki kikamilifu katika mapokezi ya Imam Qasim Ibn Ali Khan alipozuru Madrassa zake Kilwa Kisiwani na Kilwa Masoko.

Mwenyezi Mungu amsamehe makosa yake na alifanye kaburi lake kuwa moja ya Mabustani ya peponi.


No comments: