Nini kilitokea mwaka wa 1955 hadi kumfanya Father Walsh ampe chaguo Nyerere la kubaki mwalimu au aendelee na siasa?
Julius Nyerere akiwa UNO 1955 |
Baada ya Nyerere kurejea kutoka UNO, TANU ilifanya mkutano mkubwa na hayo hapo chini ndiyo yaliyotokea baada ya mkutano ule:
''Hotuba hii aliyotoa Nyerere siku ile pale
Mnazi Mmoja ambapo aliwaeleza watu
kuhusu safari yake kwenda Umoja wa Mataifa ilikuwa ndiyo mwanzo hasa wa
historia mpya ya Tanganyika. Kabla ya hapo Waafrika wa Tanganyika hawakupata
kuonyesha shauku na matumaini katika mustakbali wao. Katika viwanja vya Mnazi
Mmoja Nyerere aliwaeleza halaiki ya watu wenye furaha na waliokuwa
wakimsikiliza kwa makini kuwa miongoni mwa mataifa kumi na mbili yanayounda
Baraza la Udhamini saba kati yao yalitoa idhini kuwa muda wa utawala wa ndani
wa Tanganyika utakapowadia, Waafrika lazima wapewe nchi yao. Katika hotuba yake
Nyerere alitilia mkazo sera ya TANU kuhusu mahusiano mema baina ya Waafrika na
watu wa mataifa mengine na aliwaonya wanachama wa TANU ambao walikuwa wameanza
kuwabagua watu wa rangi tofauti kuwaambia kuwa hivyo haikuwa sawa. Alisisitiza
juu ya umoja miongoni mwa wananachi na hatimaye aliwadhihaki wasikilizaji kwa
kuwauliza ikiwa wangesubiri kwa miaka ishirini na tano kuwa huru. Halaiki hiyo
ya watu kwa pamoja ilipiga kelele, ëhapanaí. Wananachi kwa pamoja walijibu kwa
sauti kubwa wakisema walitaka uhuru kesho au kesho kutwa.
Nyerere ambaye alikuwa akiogopa kuchukua uongozi wa TANU tangu 1953 alikuwa
amefarajika sana na mshikamano huu ulioonyeshwa na wananchi. Sasa ilikuwa
dhahiri kwake kwamba rafiki yake Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz, Rupia na uongozi
mzima wa TANU pamoja na lile Baraza la Wazee lilikuwa limemsafishia njia
kuongoza harakati kwa niaba yao. Lakini Padri Walsh na Wamishionari katika
shule ya Mtakatifu Francis, Pugu, walitazama harakati hizi kwa mtazamo mwingine
kabisa. Wamishionari hawakuweza tena kumvumilia Nyerere kuwa mmoja wa walimu
katika shule yao. Hatima ile ile iliyowasibu wazalendo wengine kabla yake sasa
ilimkabili Nyerere. Aliambiwa ama abakie mtumishi mtiifu wa kanisa au ajiuzulu;
Kanisa halikuweza kukaa kimya na kumuangalia Nyerere akiwatumikia mabwana
wawili.
Nyerere alilipeleka tatizo hili kwa
Clement Mtamila, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya TANU. Mtamila aliitisha mkutano wa
kamati kuu nyumbani kwake mtaa wa Kipata na TANU ilijadili tatizo hilo.
Miongoni mwa wajumbe wa kamati ile mbali na Rupia na Kambona walikuwa Bibi Titi
Mohamed na Bibi Tatu bint Mzee. Kamati Kuu ya TANU ilimshauri Nyerere ajiuzulu.
Tafarani hii ilitokea wiki chache tu baada ya kurudi kutoka Umoja wa Mataifa
katika wiki za mwisho za mwezi Machi. Tarehe 23 Machi, 1955 Nyerere alijiuzulu
ualimu. Ilikuwa adhuhuri Nyerere alipokuja Dar es Salaam kutoka Pugu, akiwa si
mwalimu wa shule tena. Inasemekana aliposhuka tu kwenye basi alikwenda moja kwa
moja ofisini kwa Abdulwahid katika soko la Kariakoo kumpasha habari rafiki
yake. Nyerere alikaa na Abdulwahid katika nyumba yake namba 78 Mtaa wa Stanley.
Baadaye kidogo Nyerere alirudi kijijini kwake huko Musoma. John Hatch alipokuja
Dar es Salaam kwa mwaliko wa TANU Nyerere alikuwa kwao kijijini. Tutaona hapo
baadae kidogo jinsi mgeni huyu Mwingereza alivyomgutusha Schneider Abdillah
Plantan kuhusu TANU kuwashirikisha
wanawake katika harakati za kudai uhuru.''
Kulia Bi. Tatu Biti Mzee, wa tatu Julius Nyerere na wa tano ni Bi. Titi Mohamed
Picha hii ilipigwa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam siku ya kumsindikiza Nyerere
kwenda UNO
|
Hapa ndipo Nyerere alipoifikisha TANU katika uingozi wake wa miezi minane na hali ilianza moto Tanganyika nzima kiasi ya kuwa Nyerere hakuweza tena kuwatumikia mabwana wawili. Hii ndiyo iliyopelekea yeye kuandika barua hiyo hapo juu ya kujiuzulu kazi ya ualimu.
Mwandishi akifanya Kipindi Maalum: Miaka 60 ya Hotuba ya Mwalimu Nyerere UNO katika Radio Kheri akiwa na Mtangazaji Hassan Abdulla |
Mwandishi akiwa na Happy Mtamila mtoto wa Clement Mtamila alipomtembelea nyumbani kwake mwaka 2015 Happy anaishi Ulaya kwa miaka mingi |
No comments:
Post a Comment