Thursday, 29 September 2016

NYARAKA ZA SYKES KATIKA KAVAZI LA MWALIMU NYERERE


Nyaraka kutoka  kwa  Kavazi la Mwalimu Nyerere ikionesha nyaraka kutoka jalada za Ally Sykes
Angalia uongozi wa TAA 1953 pamoja na Mwalimu Nyerere yuko Abdulwahid Sykes, Dome Budohi,
John Rupia, Dossa Aziz na Ally Sykes

Kushoto: Dossa Aziz, Julius Nyerere, Abdulwahid Sykes na Lawi Sijaona 
Arnautoglo Hall 1957

Kulia: Zuberi Mtemvu, Julius Nyerere na John Rupia
Waliosimama nyuma ni Bantu Group wa pili kulia waliosimama ni Ali Msham
picha hii ilipigwa nyumbani kwake Magoeni Mapipa ambako alifungua tawi TANU, 1955
...Ally Sykes alimniruhusu nisome majalada yake binafsi, barua zake, shajara na kumbukumbu nyinginezo za ukoo wa Sykes. Ally Sykes alinifahamisha kuwa kumbukumbu hizi zilikuwa ndani ya sefu ambayo haikupatwa kufunguliwa kwa zaidi ya miaka therathini. Nikiyapitia majalada yake nilishangazwa na utaratibu wa Ally Sykes wa kupanga kila kitu na kila kipande cha habari mahali pake hata kingekuwa kidogo namna gani wakati ule wa harakati. Ally Sykes ana barua ya mwaka 1954 iliyoandikwa kwa penseli toka kwa Zuberi Mtemvu kwenda kwake akimtaarifu juu ya mazungumzo aliyokuwanayo (Mtemvu) na Nyerere kuhusu yeye na TANU; stakabadhi ya hundi ya posta toka kwa Ally Sykes kwenda kwa Japhet Kirilo wakati wa Mgogoro wa Ardhi ya Wameru; nakala ya barua isiyokuwa na tarehe kutoka TAA kwenda kwa Malkia Elizabeth iliyotiwa saini na viongozi wote wa TAA: Rais Julius Nyerere, Makamu wa Rais Abdulwahid Sykes, Katibu Mkuu Dome Okochi, Naibu Katibu Dossa Aziz, Mweka Hazina John Rupia, Naibu Mweka Hazina Ally Sykes ikimpongeza Malkia kwa kutawazwa; barua ya mwaka 1952 toka kwa Rashid Mfaume Kawawa kutoka Bukoba kwenda kwa Ally Sykes ikimfahamisha juu ya hali ya siasa katika Kanda ya Ziwa; barua ya mwaka 1963 toka kwa Lady Judith Listowel, Kenneth Kaunda, Julius Nyerere, Kasela Bantu, Chifu Thomas Marealle ...orodha haina mwisho. ..


Kleist Sykes na wanae kulia pembeni yake ni Abbas, nyuma kulia ni Abdulwahid na Ally
Chief Thomas Marealle

Kulia: Abdulwahid Kleist Sykes na Ally Kleist Sykes
Burma Infantry Vita Kuu ya Pili
Baadaye nilipofnya utafiti kuhusu maisha ya baba yake, Kleist Sykes, nilikuja kufahamu kwamba tabia hii ilirithiwa kutoka kwa baba yake ambae alikuwa akiweka ndani ya jalada kila kipande cha karatasi kilichokuwa na habari iliyostahili kukumbukwa. Ni jambo la kuhuzunisha kwamba sikuweza kupewa shajara za Abdulwahid ambazo nilielezwa kwamba baadhi ziko katika hati-mkato na hadi leo hazijafasiriwa. Shajara hizi nimezioana kwa macho yangu lakini kwa kukosa idhini sikuweza kuzifungua na kuzisoma. Vilevile sikuweza kupata kumbukumbu halisi za Vita Kuu ya Kwanza zilizoandikwa na Kleist Sykes kwa mkono wake mwenyewe. Hapana shaka yoyote kwamba nyaraka hizi ni hazina zenye thamani isiyo na mfano wake. Ni matumaini yangu kwamba siku moja nchi yetu itakubali na kuthamini mchango wa Abdulwahid katika taifa la Tanzania na nyaraka hizi kama kielelezo cha harakati dhidi ya ukoloni, zitakubalika na zitawekwa chini ya hifadhi ya Nyaraka za Taifa kwa faida ya vizazi vijavyo.

Kasella Bantu

Dome Okochi Budohi
Kulia ni Dome Okochi Budohi na kushoto ni Mwandishi Ruiru,
Nairobi 1972
Familia yangu ilifahamiana na Dome Budohi, mmoja wa wanaharakati kutoka Kenya. Wakati ule wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika alikuwa akiishi Dar es Salaam. Budohi alikuwa mmoja wa wazalendo walioasisi TANU na kadi yake ya uanachama no. 6 aliyopewa Julai 1954. Mwaka 1955 alikamatwa na serikali ya kikoloni kwa tuhuma ya kuwa mmoja wa askari wa Mau Mau harakati za wazalendo takriban wengi wao wakulima wadogo waliokuwa wakipigana na ukoloni wa Waingereza nchini Kenya. Ninazo kumbukumbu nyingi za utoto nikimtembelea Budohi ndani ya selo yake Kituo Cha Kati cha Polisi. Hivi sasa jengo hilo ni Makao Makuu ya Shirika la Reli la Tanzania. 
Hili jengo mkonno wa kushoto ni Railway Station, jengo la mbele yake ndiyo
ilikuwa Central Police Station wakati wa ukoloni

Wakati huo mimi nilikuwa mtoto, si zaidi ya miaka minne hivi. Jambo la kwanza ninalokumbuka kuhusu Budohi ni kuwa kila mara tulipokwenda kumtembelea tulimkuta anasoma gazeti. Baadae Budohi alihamishiwa Kenya na aliwekwa kizuizini katika kisiwa cha Lamu. Alipofunguliwa toka kizuizini mwaka wa 1963 miezi michache kabla ya uhuru wa Kenya, Budohi alikwenda Uganda na akaajiriwa na gazeti la Uganda Argus. Hivi sasa ninaelewa kwa nini siku zile kila mara nilikuwa namkuta amezama ndani ya gazeti kila tulipokwenda kumtembelea pale rumande mjini Dar es Salaam. Niliweza kwa msaada wa rafiki yake Maxwell aliyelowea Tanganyika, kumpata Budohi mjini Nairobi mwaka 1972. Nilimtembelea mjini Nairobi wakati huo alikuwa akiishi Ruiru maili chache kutoka Nairobi mjini. Budohi alikuwa ametundika picha ya Nat King Cole sebuleni kwake. Mwaka 1974 nilimtembelea tena, safari hii katika nyumba yake ya Ngei Estate. Budohi alikuja kuwa mtu wa kwanza kabisa kunipa habari kuhusu historia ya harakati za Tanganyika dhidi ya ukoloni wa Waingereza. ...

(Kutoka Kitabu Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924 - 1968)...

Mwandishi na Mzee Maxwell 1997

No comments: