Friday, 18 November 2016

KUTOKA JF: WAPIGANIA UHURU WA KILIMANJARO


Hoshea,
Katika utafiti wa kuandika kitabu cha Abdul Sykes nadhani ushakisikia
nilibahatika kusoma barua walizokuwa wakiandikiana Ally Sykes na
Chief Marealle kati ya 1950 - 1960.

Sikukuta mahali popote pale ambapo ilielezwa chochote kuwa Chief
Marealle 
alikuwa anataka Wachagga wajitenge.


Mangi Mkuu Thomas Marealle

Halikadhalika nimefanya mahojiano na Mzee Yusuf Olotu muasisi wa
TANU na alinipa habari za machifu wa Uchagani kuhusu TANU.

Hakunieleza chochote kuwa kulikuwa na vuguvugu la kujitenga.
Hebu msome Mzee Yusuf Olotu hapo chini:

Yusuf Olotu na Wapiga Kura wa Kura Tatu Kilimanjaro

Historia ya harakati za kudai uhuru wa Tanganyika kama walivyoshiriki wananchi wa Kilimanjaro, haiwezi kamwe kukamilika bila ya kutaja jina la Yusuf Ngozi. Uchagga ilikuwa chini ya utawala wa machifu waliokuwa wakijulikana kama Mangi. Baadhi ya machifu hawa walikuwa katika Baraza la Kutunga Sheria na kwa ujumla wao walikuwa karibu na serikali ya kikoloni kuliko walivyokuwa na wananchi wanaowaongoza. Hali ya siasa Jimbo la Kaskazini ilikuwa ngumu na ya kukatisha tamaa. Wakati TANU inakabiliwa na Kura Tatu mgogoro wa ardhi ya Wameru ulikuwa umekwisha kwa wananchi kudhulumiwa haki yao. Japhet Kirilo alikuwa amerudi kutoka Umoja wa Mataifa alikopeleka madai ya Wameru mikono mitupu. Kirilo hakuwa na chochote cha kuwaonyesha Watanganyika. Ilikuwa Yusuf Ngozi ndiye aliyeweza kuifanya TANU iingie kwanza Moshi mjini kwa vishindo na kutoka hapo mjini akaieneza vijijini. Kupitia kumbukumbu za Mzee Yusuf ngozi ndipo unapokutana na historia za awali kabisa za wanasiasa maarufu waliopata majina na vyeo; na wengine kuwa mawaziri katika Tanganyika huru, kama Lucy Lameck, Enesmo Eliufoo na wengineo. Ilikuwa Yusuf Ngozi ndiye pamoja na wazalendo wengine waliifanya TANU ishinde uchaguzi wa Kura Tatu mwaka 1958. Kupitia kumbukumbu zake halikadhalika ndipo kwa huzuni kubwa utakapokutana na mashujaa waliosahaulika kama yeye mwenyewe, mashujaa wa kike na wa kiume, wazalendo kama marehemu Mama Bint Maalim, Amina Kinabo, Halima Selengia, Juma Ngoma, Melkezedek Simon, Gabrieli Malaika na wengineo. Hawa ndiyo mashujaa ambao kwa muda waliamua wasahau nguvu na utawala wa machifu wao na kujiweka chini ya TANU.

Yusuf Ngozi hakuwa na elimu, alikuwa mwananchi wa kawaida aliyethamini utu wa Mwafrika na mtu aliyechukia dhulma na fedheha ya kutawaliwa. Kilimanjaro ilikuwa inasifika kwa kuwa na Waafrika waliokuwa na elimu ya juu kabisa katika Tanganyika. Lakini wasomi hao walishughulishwa zaidi na maslahi yao binafsi. Wengi wao walikuja kujitokeza kuingia TANU mwaka 1958 katika uchaguzi wa Kura Tatu, wakati mambo ni shwari na Waingereza walikuwa wamesalimu amri. Yusuf Ngozi labda kwa kuelewa mazingira ya Kilimanjaro alianza kujenga msingi wa TANU si kwa wanaume bali kutoka kwa akina mama. Hiki ni kitu aziz sana katika historia ya uhuru. Katika historia ya TANU ni zile sehemu ambazo kulikuwa na utamaduni wa Kiswahili wa vyama vya akina mama kama hapo Moshi mjini, Dar es Salaam, Tanga, Lindi na kwingineko ndiko chama kilipata nguvu kubwa sana ya wanawake.

Joseph Kilamalando aliogopa kuitumikia TANU lakini alijiona amesalimika kuifanyia kazi United Tanganyika Party (UTP), chama cha Wazungu kilichoundwa kuipinga TANU. Kimalando alikuwa katibu wa UTP Moshi, na Mohamed ëKishikioí Badi mwenyekiti wake. Mzee Yusuf Ngozi aliwahamasisha wanawake wa Moshi chini ya Mama bint Maalim kuipiga vita UTP hadi ikafa. Wanawake wale walikuwa wakizikusanya kadi za UTP na kumpelekea Mzee Yusuf Ngozi ofisi ya TANU. Yeye kama njia ya kuwakatisha tamaa na kuwapiga vita vya kisaikolojia UTP, alikuwa akichukua marundo kwa marundo ya kadi za UTP na kumpelekea rais wake Mohamed Badi kumhakikishia kuwa wananchi walikuwa hawakitaki chama chake cha vibaraka.

Yale masharti ya Kura Tatu ya kipato, elimu na kazi ya maana kwa wapiga kura na wagombea, kwa Wachagga wengi hivyo havikuwa vikwazo kwao. Wachagga walikuwa ni watu waliokuwa na elimu na vipato vya kutosha kuwafanya sheria ile ambayo kwa sehemu kama Bagamoyo iwe kikwazo kwa wana-TANU, kwao wao iwe kitu chepesi na iwaruhusu kupiga kura. Lakini kwa bahati mbaya sana iliingia fikra kuwa masharti yale ya kupiga kura hasa kile kipengele cha kipato ilikuwa njama ya serikali ya wakoloni kutengeneza orodha ya Wachagga ili wawatoze kodi ya mapato. Wachagga wamejaaliwa kwa ujuzi wa biashara na bidii katika kilimo. Hiki kipengele cha kipato kiliwatia wana-TANU wa Uchaggani, wafugaji na wakulima wa kahawa hofu kubwa. Hulka ya kuthamini mali ilikuwa imefifilisha umuhimu mzima wa tatizo la Kura Tatu na umuhimu wa watu wa Kilimanjaro kupiga kura ili TANU ichukue viti katika Baraza la Kutunga Sheria. Tatizo la Uchagani sasa likawa ni la kipekee. Ilikuwa ni kubadilisha fikra za watu na kuwatoa hofu ya kulipa kodi kwa mali zao na kuwafanya kuona ukweli na umuhimu wa kuishinda UTP na kumngíoa Mwingereza Tanganyika. Hili lilikuwa tatizo ambalo TANU hawakukutananalo popote katika Tanganyika. Hata katika mkutano wa Tabora kujadili Kura Tatu hakuna kumbukumbu yeyote inayoonyesha kuwa kuna Waafrika watashindwa kutumia haki yao ya kupiga kura kwa kuwa na fedha nyingi. Tatizo ilikuwa ni kinyume chake. Tatizo la TANU katika majimbo mengine ilikuwa kuwafanya watu wakubaliane na masharti yale magumu ya kibaguzi katika kupiga kura ili chama kiingie katika uchaguzi.

Katika hali ya kawaida ungelitegemea watakaosimama ni wale wasomi wa Makerere kuwaeleza wananchi hali ya mambo na mwelekeo wa nchi. Katu hawakusimama. Alikuwa Yusuf Ngozi ndiye aliyetembea Kilimanjaro nzima kuwaeleza watu kuwa kama hawatajiandikisha kuipigia kura TANU na kumuunga Nyerere mkono katika vita dhidi ya Waingereza basi UTP itashinda na Waingereza wataendelea kutawala nchi hii. Sehemu nyingine alikuwa akiwafahamisha Waafrika wenye biashara ndogondogo kuwa wao vilevile wana kazi na kipato kinachokidhi masharti ya upigaji kura kwani hesabu zao za mwaka zilikuwa zinapita kile kiwango cha pauni 400. Aliikuta hali hii kwa mafundi cherahani Kahe, kijiji kidogo nje ya Moshi. Mafundi hawa walijihesabu hawana kazi ya maana wala kipato cha pauni 400 kwa mwaka. Mzee Yusuf Ngozi aliwasomesha na kuwaonyesha kuwa walikuwa na kazi ya maana na kipato cha kutosha. Aliwanasihi wasiache kujiandikisha na kuipigia kura TANU. Sehemu nyingine Yusuf Ngozi alikuwa na propaganda yake ya kutisha. Alikuwa akiwauliza wananchi kama wao walikuwa wako tayari kuishi katika nchi yenye bendera tatu.

TANU Jimbo la Kaskazini ilimsimamisha Enesmo Eliufoo kwa kiti cha Moshi na Sophia Mustapha, Arusha. Yusuf Ngozi aliifanyia kampeni TANU kwa ufanisi mkubwa na TANU iliweza kushinda kwa kura nyingi sana na wajumbe wake kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria.''

Historia ya Mzee Yusuf Olotu iko katika kitabu hicho hapo chini:
Yusuf Olotu


No comments: