Kushoto: Owera, Ombok (Kenya), Mahmoud Al Hakim (Sudan), Charles Mwambenja, Mohamed Said, Khalifa Mkwizu na Mwanyika (Tanzania) Escola Nacional De Aeronatica Mozambique Monday Juliy 30 1990 |
Sasa tukiwa hapo Manzini ndipo tulipofahamiana na hawa wenzetu ambao sote tulikuwa tunakwenda kwenye kozi moja. Mwanyika alikuwa afisa wa ngazi ya juu wizarani ambayo ndiyo ilikuwa wizara ambayo Bandari tulikuwa chini yake na Mwaya yeye alikuwa mwalimu akisomesha hapo chuoni. Wakati tunasubiri ndege irejee kutuchukua nilitoa radio yangu aina ya Philips siku hizo maarufu kwa jina la ‘’World Receiver.’’ Radio hizi zilikuwa na ‘’band’’ kama 12 hivi na ikisemekana ilikuwa na uwezo wa kukamata stesheni za radio dunia nzima. Radio hii nilikuwa nikiipenda sana na hazikuwa nyingi nchini maana siku zile nchi yetu kidogo mambo ya kuagiza vitu vya kielektroniki ilikuwa shida. Radio hii nilinunua Port Said Misri mwaka wa 1988 ambako nilikuwa nimekwenda kozi nyingine katika mambo ya ufanisi wa bandari. Kozi hii ilifanyika Alexandria na nakumbuka wenyeji wetu walituambia tusinunue chochote hapo kwani bei ni juu tusubiri watatupeleka Port Said ambayo ni, ‘’Free Port,’’ tutanunua vitu kwa bei nafuu.
Basi nikaitoa hii radio yangu kutoka katika mkoba wake mweusi mzuri nikaiweka katika FM nikaanza kutafuta stesheni. Stesheni ya kwanza kuipata nakumbuka ilikuwa Radio Transvaal kutoka Afrika Kusini. Nilishtuka kidogo kwa kuwa wakati ule Tanzania na Afrika Kusini walikuwa maadui wakubwa kwa ajili ya siasa za kibaguzi za Makaburu. Mimi kama Mtanzania yoyote sikutaka kujihusisha na chochote na Afrika Kusini na kubwa zaidi kulikuwa na ‘’embargo,’’dhidi ya nchi hiyo. Radio yangu kukamata stesheni ya Kikaburu kisaikolojia ilinistua kidogo. Lakini kilichonistaajabisha zaidi ni pale nilipomsikia mtangazaji akizungumza ki-Afrikaans anasema neno, ‘’Nat King Cole.’’ Nilitulia tuli kusikiliza na hapo ikaingia sauti ya Nat King Cole ambae ni katika waimbaji niwapendao sana hadi leo.
Nikashangaa zaidi kuwa hawa Makaburu juu ya ubaguzi wao wa mtu mweusi bado nao wanapenda kusikiliza muziki wa watu weusi. Sikujua kuwa makubwa yalikuwa yananisubiri Msumbiji kuhusu uhusiano wa Afrika Kusini na nchi za Kiafika zilizokuwa majirani zake. Ingawa tulikuwa tunaaminishwa kuwa Mozambique haina uhusiano wowote na Afrika Kusini nilishangaa kukuta bidhaa nyingi katika maduka ya Maputo ni vitu vinavyoagizwa kutoka huko. Nilikuwa nanunua, ‘’Johannesburg Star,’’ gazeti linalochapwa Afrika Kusini katika mitaa ya Maputo na Shopping Malls zote za Maputo zilikuwa zimefurika vitu kutoka Afrika Kusini. Nakumbuka nimekwenda bank na, ‘’Thomas Cooke Travellers Cheque,’’ badala ya kupewa dola za Kimarekani nikapewa Rand za Afrika Kusini.
Lakini hayo si makubwa katika yaliyonishangaza kama vitendo vya mapenzi vya watu wa Msumbiji kwa Watanzania na heshima waliyokuwa wakitupa. Nilikishuhudia vitendo hivi kwa macho yangu mwenyewe mara tu tulipotua Maputo na kuanza mchakato wa ‘’Passport Control,’’ na ‘’Customs.’’ Ghafla nimewaona vijana kama wawili hivi wameingia ndani ya sehemu maarufu kwa jina la ‘’Arrivals,’’ wanaomba pasi zetu wakijitambulisha kuwa wao wametoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Msumbiji na wamekuja kutupokea. Vijana hawa wakawa wanatupitisha kwa haraka haraka kugonga pasi bila kujali wasafiri wengine waliokuwa mbele ya mstari. Ghafla tumekuwa watu mshuhuri VIP hatutakiwi kupanga foleni. Mimi binafsi nilikuwa nimepigwa na butwaa sikutegemea kitu kama hiki ingawa sikuwa mgeni wa taadhima mfano wa hii. Niliwahi kupewa taadhima kama hiyo Uwanja wa Ndege wa Khartoum nilipokwenda kozi ya uongozi mwaka 1989. Nilipitishwa VIP mizigo yangu ikashughulikiwa pamoja na kugongwa pasi na kupewa, ‘’visa,’’ hapo uwanjani. Lakini hii ya Maputo kupewa taadhima hii kundi letu la watu wa kawaida sikuweza kuielewa kwa haraka. Walijuaje kama sisi tunaingia leo Maputo na Royal Swazi? Nani kawaamrisha waje watupokee kwa taadhima ile nk. nk.
Tatizo lilitokea tulipofika, ‘’Customs.’’ Afisa wa ‘’Customs,’’ kaniamuru nifungue sanduku langu kwani mimi nilikuwa mbele ya wenzangu wote na mwenyeji wetu kasimama kati yangu na huyo mtu wa ‘’Customs.’’ Walikuwa wanazungumza Kireno na kutokana na zile sauti zilivyokuwa zinapanda nikajua kuna tatizo na kuna mabishano makali. Majibizano haya yalikwenda kama dakika tatu hivi na foleni imesimama haisogei. Msumbiji wenye kusema Kiswahili wengi. Msafiri mmoja aliyekuwa nyuma yangu akaniambia kuwa wanabishana kuhusu sanduku langu. Huyo mwenyeji wako anamwambia mtu wa, ‘’Customs,’’ kuwa nyinyi ni wageni wa serikali kwa hiyo msibughudhiwe kwa kufungua masanduku yenu lakini yeye anakataa anasema lazima akague mizigo yote. Nikashangaa kuwa sisi tumeshakuwa wageni wa serikali ya FRELIMO. Mimi kusikia vile sikupoteza muda nikapita mbele na kufungua sanduku langu likakaguliwa na nikapita na wenzangu waliokuwa nyuma yangu wakafanya hivyo sote tukapita.
Mapito 1990 |
Nimeleta utangulizi huu mrefu kiasi ili kuonyesha mshtuko wangu niliopata baada ya kusoma katika magazeti, kutazama katika TV na kusoma katika mitandao ya kijamii ushenzi wanaofanyiwa Watanzania Msumbiji, kupigwa, kufungwa na wanawake wao kunajisiwa. Sikuweza kuamini kile nilichokuwa nasoma. Swali nililojiuliza ni kuwa, ‘’Kimetokea nini?’’ Hayo yaliyokuwa yanatokea Msumbiji haikuwa picha wala kumbukumbu yangu ya Msumbiji kama nilivyoikuta mwaka wa 1990.
Tukiwa pale Cardoso Yvonne Chaka Chaka mwimbaji maarufu kutoka Afrika Kusini akaingia pale hotelini na bendi yake. Tukapata taarifa kuwa atafanya onyesho Machava Stadium. Uwanja ulifurika na mistari ya kukata tiketi nje ya uwanja ilikuwa mirefu. Onyesho lilikuwa linaanza saa moja usiku. Kitu kimoja kilichonistaajabisha ni ile nidhamu ya watu kupanga foleni bila kusukumana wala kusimamiwa na askari na bila ya zogo lolote. Lakini kubwa zaidi ni pale niliposhuhudia wasichana wadogo wakiuza vitu kama maji, soda, sigara na vitu vingine huku wakipita katikati ya makundi ya wanaume na hakuna aliyethubutu hata kumgusa au kumtania. Hii kwangu mimi ilikuwa nidhamu ya hali ya juu kabisa kwa kuwa nawafahamu watu wetu huwaje katika hali kama hiyo.
Onyesho lilipoanza Chaka Chaka alianza kwa nyimbo zake ambazo zilikuwa maarufu kipindi kile. Sikuwa najua kama watu wa Msumbiji wanapenda kucheza muziki kiasi kile. Uwanja ulilipuka na watu wakawa wanacheza pale walipo na wengine katika uwanja na dansi ikichezwa kwa nidhamu. Mwenyewe Chaka Chaka ni hodari sana wa kucheza dansi. Siku zile alikuwa msichana mdogo kembamba, karefu. Alimkaribisha mtoto mmoja aliyekuwa akicheza chini ya jukwaa akamwita apande jukwaani na muziki ukaanza. Ilikuwa burudani ya namna yake. Kale katoto kalikuwa hodari hapana mchezo. Niliwauliza wenyeji wangu imekuwaje watu wa Msumbiji wamekuwa na nidhamu ya hali ya juu ya kiasi kile kuwa hata katika burudani hakuna vurugu hata kidogo. Jibu nililopewa ni kuwa hiyo ni sababu ya vita vya ukombozi. Nikaambiwa kuwa FRELIMO iliwafunza wananchi wote nidhamu bila ya kujali kama alikuwa mstari wa mbele mpiganaji msituni au raia wa kawaida.
Mwandishi na Yvonne Chaka Chaka Arusha
Miaka
mingi baadae nilikutana na Yvonne Chaka Chaka Arusha wakati huo alikuwa
Ambassador wa, ‘’Roll Back Malaria,’’ tulikutana Arusha katika mpango wa
vyandarua mimi nikwakilisha Bandari ya Tanga ambayo ndiyo ilikuwa ikitumika
kusafirisha vyandarua hivyo nje ya Tanzania na pia kuingiza malighafi ya
kutengeneza vyandarua hivyo. Nilipiga stori nyingi sana na yeye na nilimshangaza
nilipomtajia kaka yangu ambae yeye anamfahamu vizuri kwa kuwa mumewe na kaka
yangu wote ni madaktari na wakijuana katika shughuli zao Cape Town ambako kaka
yangu alikuwa akifanyakazi. Nikamkumbusha kuhusu ile, ‘’show,’’ ya Machava
Stadium 1990 aliikumbuka. Nikamuuliza imekuwaje amekuwa mnene kiasi kile.
Alicheka akanambia neno moja, ‘’Nimeolewa na nina watoto.’’
Tulikaa Maputo kwa majuma matano kamili. Iko siku nilikwenda kupata chakula cha mchana hoteli moja maarufu katikati ya jiji la Maputo. Mwenzangu mmoja alinisifia hoteli ile akanambia kuwa wana chakula kizuri na wao kitoweo chao ni samaki tu wa kila aina. Kitu ambacho hakunieleza ni kuwa hoteli hiyo hawauzi vinywaji baridi ila pombe tu. Basi nikapiga oda ya chakula changu na niliposema nipatiwe Coke, nikajibiwa kuwa hapo hawana vinywaji baridi. Ikawa nile chakula bila kinywaji cha kushushia. Katika ile meza nilikaa na kijana mmoja akaniuliza kama sinywi pombe. Akaniuliza ninakotoka.
Nilimfahamina kuwa natoka Tanzania. Yule kijana akanyanyuka kutoka kwenye meza yake akanambia anakwenda kunitafutia soda. Haukupita muda akarejea na chupa ya Coke. Mazungumzo yakaanza kwa yeye kunambia kuwa mimi ni nduguye wa damu kwa kuwa Watanzania wengi wamekufa katika ardhi ya Msumbuji wakipigana bega kwa bega na FRELIMO ili kuwatoa ndugu zao katika minyororo ya Wareno na makaburi yao yapo Msumbiji. Alizungumza mengi na kwa hakika nilihisi yale mapenzi ya watu wa Msumbiji kwa Watanzania na heshima yao kwetu. Huyu kijana alinifahamisha kuwa anafanyakazi benki. Hii ndiyo Msumbuji niliyoikuta nilipofika huko mwaka wa 1990.
Pale Cardoso mimi na wenzangu hatukukaa sana tukajulishwa kuwa kuna hoteli nzuri inaitwa Rovuma ni ya FRELIMO na bei zake ni nafuu tena iko katikati ya mji. Cardoso ilikuwa nje ya mji kidogo. Tukahama pale tukahamia Rovuma na kwa hakika ilikuwa hoteli nzuri kwa kiasi chake ingawa haifikii Cardoso lakini tuliipenda kwa unafuu wa bei na kuwa mjini ambako jioni tuliweza kutembea kwingi nyakati za jioni kuangalia mandhari ya Maputo. Kwangu mimi binafsi nilipata nafasi ya kuzunguka kutafuta hoteli ya kistaarabu kula chakula cha jioni bila ya bugdha za ulevi na nilipata hoteli moja ya mzee wa Kingazija ambae alikuwa anasema Kiswahili vizuri kabisa. Hii ikawa kama kijiwe changu kila jioni nakwenda pale na kupiga soga na yule mzee. Nakumbuka alinifahamisha kuwa ana ujamaa wa mbali na Rais Ali Hassan Mwinyi. Yeye pia alikuwa hana jingine ila kumwaga sifa kemkem kwa jinsi Tanzania ilivyojitolea katika kupigania uhuru wa Msumbiji kwa silaha.
Ilikuwa wakati tupo hapo Maputo Rovuma Hotel ndipo Nelson Mandela akaja kutembelea Msumbiji. Hili lilikuwa jambo kubwa sana na alipangiwa kutembelea Town Hall na kuzungumza pale. Hii Town Hall iko jirani na Rovuma Hotel na ili mimi niweze kufika hotelini kwangu ilibidi nishike njia inayopita pembeni na City Hall. Siku ile mimi nikawa narejea hotelini wakati Mandela yuko City Hall. Kumbe barabara zote jirani na hapo walikuwa hawaruhusu mtu kupita akiwa kabeba chochote. Mimi nilikuwa na mkoba mdogo na ndani yake nilikuwa nimehifadhi kamera yangu. Mimi na wenzangu tukasimamishwa kufanyiwa upekuzi na askari alipoona ile kamera akanizuia akanambia siwezi kupita lakini akawaruhusu wenzangu. Hapo tunazungumza Kiingereza na mimi nikawa najitahidi kumridhisha kuwa hiyo ni kamera tu haina chochote na hoteli yangu ni ile pale usoni aniruhusu nipite. Yule askari akanikatalia katakata.
Basi mimi nikawa nawaambia wenzangu kwa Kiswahili, ‘’Huyu bwana ananizuia bila sababu sasa mimi nitakaa hapa mpaka saa ngapi?’’ Hata kabla sijajibiwa na wenzangu yule askari akanijibu kwa Kiswahili kilichonyooka kabisa, ‘’Wewe hata useme nini hapa sikupitishi.’’ Sote tukaangua kicheko na ghafla ule uhusiano wa askari na raia ukaondoka ikawa sasa tunazungunza kama mtu na rafiki yake waliopoteana siku nyingi. Gumzo likaanza. Akatuleza kuwa yeye ameishi Dar es Salaam Kurasini na anaijua Dar vizuri kabisa. Basi yule askari akanionyesha mgahawa pale pale City Hall akanambia niende nikapumzike pale hadi Mandela atakapomaliza shughuli yake pale City Hall. Hawa ndiyo watu wa Msumbiji niliobahatika kukutananao na hawakuniachia isipokuwa kumbukumbu nzuri katika fikra zangu.
Haya tulinayoshuhudia kutoka Msumbiji ni mambo ya kuhuzunisha pasi na kiasi. Huu ni msiba mkubwa kusikia kuwa hii leo Watanzania walioko Msumbiji wanafanyiwa ushenzi na wanakimbia kurudi Tanzania kujinusuru. Tabu sana kuamini lakini ndiyo ukweli wenyewe. Kitu gani kimewageuza ndugu zetu kiasi cha wao kujenga chuki kubwa kama hii? Iweje leo Watanzania wawe maadui wa wananchi wa Msumbiji? Nini kimewageuza watu wa Msumbiji? Zahir Hotel, Dar es Salaam, mgahawa huu maarufu kwa vyakula vya Kiswahili kama pilau na biriani FRELIMO wameweka kibao cha ukumbusho katika mlango wa kuingilia hapo mgahawani. FRELIMO wameandika maneno ya kujikumbusha siku zao walipokuwa wanaishi Tanzania wakapataja hapo kama sehemu waliyokuwa wakikutana kupata chakula na kwa mazungumzo. Ni nani huyo anaetaka kuichafua historia hii?

Rovuma Hotel Maputo 1990 |
No comments:
Post a Comment