Abdulkarim Omar Mtiro (Cisco) |
Maskini
kaka yangu "Cisco" umetangulia mbele ya haki.
Huyu
kwangu mimi ni baba maana marehemu mzee wangu Abdallah Salim Matimbwa alikuwa ni
mmoja wanaosoma katika darsa ya marehemu Sheikh Omar Mtiro hapa Mtaa wa Kipata
nyumba no. 1 ambae ni baba yake Abdulkarim Mtiro maarufu kwa jina la, ''Cisco.''
Hii
nyumba no. 1 Mtaa wa Kipata na Msimbazi na Congo ndimo alimozaliwa Cisco.
Nyumba yetu ni no. 2 kwa hiyo nyumba zetu
zikitazamana miaka nenda miaka rudi na wazee wakifahamiana vyema kabisa.
Mwezi
kama huu wa Ramadhani enzi hizo chano kiko barazani kwa Sheikh Omar Mtiro, uji unapikwa kwetu na mama yangu na futari zote zinapelekwa kwa
Bibi bint Seif (mama yake mzazi Cisco).
Dar es Salaam hii ya miaka ile ya 1950 wakati sisi tunazaliwa leo haipo tena.
Kwa
daraja hiyo niliyoizungumza hapo juu, ya baba yangu Mzee Abdallah bin Salim
Matimbwa kuwa mwanafunzi wa Sheikh Omari bin Mtiro, kwa nidhamu ya Kiislamu
Sheikh Mtiro anakuwa babu yangu na Abdulkarim Mtiro, mwanae anakuwa baba yangu
kwa maana yeye anamwita baba yangu kaka yake ki daraja.
Kwa
umri aliokuwanao baba yangu anamzaa Abdulkarim pasi na shaka yoyote lakini ada ni ada Abdulkarim alibaki kuwa mdogo wake na kwangu baba.
Dada
yangu wa kwanza Bi. Hidaya bint Abdallah Salim watoto wake kina marehemu
Shaaban Juma Semlangwa Assistant Commissioner of Police (ACP) na dada yake Bi Mwanahawa Juma ndiyo walikuwa
mchezo mmoja na Balozi Cisco katika utoto wao.
Hivyo
nimeondokewa na baba yangu, kaka yangu, mzaliwa mwenzangu mtaani Kipata (sasa Mtaa wa Kleist Sykes) na kiongozi
wangu katika nyanja mbalimbali.
Mwenyezi
Mungu amuondolee adhabu ya kaburi na amsamehe makosa yake.
Aiweke
roho yake mahala pema peponi.
Amin.
No comments:
Post a Comment