Mwandishi akimkabidhi Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi kitabu cha Maisha ya Abdul Sykes, Ukumbi wa Korea Dar es Salaam |
Kauli ya Rais Mstaafu Mzee Hassan Mwinyi kuwa kama isingekuwa katiba ya
Tanzania kuweka kikomo cha rais kutawala kwa si zaidi ya awamu mbili basi Rais
Magufuli ingefaa atawale labda maisha kutokana na kazi yake nzuri kwa taifa
hili. Kauli hii imezua mjadala mkubwa kutoka kwa wananchi. Wako wanaopinga na
halikadhalika wako pia wanaounga mkono. Mapenzi hakika humtia mtu upofo na
ikamnyang’anya akili na uwezo wa kufikiri.
Nataka wasomaji wangu nikurudisheni miaka mingi nyuma wakati Tanganyika inapigania uhuru wake na kiongozi wa mapambano haya alikuwa Julius Kambarage Nyerere. Ilikuwa mwaka wa 1957 na Nyerere alikuwa kijana mdogo wa miaka 35. Naomba mkisome kisa hiki hapi chini kama nilivyokiandika katika kitabu cha Abdul Sykes:
Nataka wasomaji wangu nikurudisheni miaka mingi nyuma wakati Tanganyika inapigania uhuru wake na kiongozi wa mapambano haya alikuwa Julius Kambarage Nyerere. Ilikuwa mwaka wa 1957 na Nyerere alikuwa kijana mdogo wa miaka 35. Naomba mkisome kisa hiki hapi chini kama nilivyokiandika katika kitabu cha Abdul Sykes:
''Ilikuwa katika taarab iliyoandaliwa kusheherekea kufunguliwa kwa
tawi la TANU Dar es Salaam ya Kaskazini katika mtaa wa Mvita, nyumba namba 10,
tarehe 10 Agosti, 1957, ulimi wa Sheikh Takadir ukateleza, akamuita Nyerere
‘’Mtume,’’ Tawi la TANU Dar es Salaam ya Kaskazini lilikuja kuwa lenye nguvu
sana kuliko yote na tawi likawa na mafanikio labda kupita matawi yote katika
Tanganyika. Mwenyekiti wake alikuwa Mtoro Kibwana na mweka hazina Haidar
Mwinyimvua, ambae baadae aliingia Kamati Kuu ya TANU ya Taifa. Kwenye hafla
ile, katika kumtambulisha Nyerere na kummiminia sifa, Sheikh Takadir bila
kufikiri aliwaambia wasikilizaji wake kuwa, ‘’Nyerere ni Mtume wa Afrika.’’
Kama kauli ile ingetolewa siku nyingine yoyote ile, huenda tamko hilo
lisingezua kishindo, na huenda lingepita bila kuwa na taathira yeyote mbaya.
Lakini ufunguzi wa tawi la TANU la Mvita katika siku hiyo tarehe 10 Agosti,
1957 ilikuwa siku maalum kwa wakazi wa Dar es Salaam.
Kushoto Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadiri, Clement Mtamila na Titi Mohamed Nyuma ya Nyerere Mama Maria Nyerere, Rajab Diwani na John Rupia |
Kwanza, Dar es Salaam ilijitokeza kushuhudia
kuhama kwa mwimbaji stadi, Nuru binti Sudi, kutoka Al-Watan na kujiunga na
wapinzani wao Egyptian. Hivi vilikuwa vikundi viwili vya taarab vikishindana
mjini Dar es Salaam. Siku hiyo Nuru alikuwa anaimba pamoja na kikundi chake
kipya kwa mara ya kwanza na mashabiki wake walikuwa wamekuja kumwona bingwa wao
akiimba katika hafla ya TANU. Halikadhalika mashabiki wa Egyptian walikuwa
wamekuja vile vile kushangilia na kuwazomea washindani wao kwa kumchukua bingwa wao.
Kulikuwa na sababu nyingine kwa watu kushangilia. Katika kuhama huko kutoka
Al-Watan na kuingia Egyptian, Nuru alikuwa ameweka msimamo wa kisiasa. Nuru
alikuwa na damu mchanganyiko. Baba yake alikuwa Mwarabu na mama yake alikuwa
Mwafrika. Kabla ya kutoka Al-Watan na kuingia Egyptian alikuwa
mwanachama wa Coronation ambacho kilikuwa chama cha akina-mama wenye asili ya
Kiarabu. Kwa hiyo ilichukuliwa kwamba, maadam Egyptian ilihusiana na Waafrika,
kwa kitendo kile cha kuhama Al-Watan, Nuru alikuwa ameasi na kurudi kwa ndugu
zake, yaani Waafrika. Amerudi kwenye asili yake, kwenye tumbo la
mama yake aliyemzaa. Hivi ndivyo mambo yalivyokuwa siku zile, kila jambo
lilipewa tafsiri ya kisiasa. Wakati huo UTP ilikuwa tayari imeshanzishwa na
Egyptian ilikuwa imetunga nyimbo maalum kwa ajili ya hafla hiyo ambayo Nuru
aliimba kuidhihaki UTP. Sehemu ya mashairi yake yalikuwa yanasema hivi:
‘’Ma-UTP wana majambo, TANU wanaichukia.’’
Chief David Kidaha Makwaia |
Pili, ili kuadhimisha kufunguliwa kwa tawi
la TANU Mvita, TANU iliwaalika wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria, wengi wao
machifu, ili kushuhudia sherehe hiyo. Miongoni mwao walikuwa Chifu David Kidaha
Makwaia, Humbi Ziota, Chief Msabila Lugusha, Mwami Theresa Ntare na wengine wengi.
Vilevile walikuwepo watu wengine mashuhuri kama Hamis Mfaranyaki ambae ndiye
alikuwa kiongozi wa Wangoni mjini Dar es Salaam, Paul Bomani, Said Chaurembo,
kaka yake Sheikh Abdallah Chaurembo na watu maarufu wengine wengi. Pamoja na
watu wote hawa mashuhuri kuhudhuria, huu ulikuwa usiku adhimu kwa TANU.
Hapakuwa na shaka yoyote kuwa chochote kitakachosemwa katika hafla kama hiyo
kitakuwa na athari kwa watu. Ilikuwa katika hafla hii ndipo siku ulimi wa
Sheikh Takadir ukateleza akampa utume Nyerere.’’
Upepo ukabadilika baada ya mwaka mmoja tu
katika joto la siasa lililoanzishwa na Uchaguzi wa Kura Tatu wa mwaka wa 1958
pale Nyerere alipoonekana kuwaleta watu katika TANU ambao walisimama katika
uchaguzi ule kwa tiketi ya TANU ili kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. Wengi katika hawa hawakuwa wamenyanyukia na TANU. Sheikh Takadiri uso na macho akamtuhumu Nyerere kwa tuhuma nzito na ya kutisha
jambo ambalo TANU yenyewe ilionya mapema kabisa kuwa lisiletwe hata kwa mbali
katika TANU nalo lilikuwa suala la Waislam. Vumbi zito lilifumuka kwa wanachama
wa TANU kukiacha chama na kuunda kwanza African National Congress (ANC) ya
Zuberi Mtemvu na kisha All National Union of Tanganyika (AMNUT) ya Mashado Plantan na
wenzake. ‘’Utume.’’ wa Nyerere ulikuwa umetiwa dosari na mwenyewe aliyempa cheo
hicho Sheikh Takadiri.
Zuberi Mtemvu Rais wa African National Congress (ANC) |
Lakini vita hivi havikuishia hapo. Mwaka
wa 1963 Nyerere akalivunja Baraza la Wazee wa TANU, baraza ambalo wajumbe wake
wote zaidi ya 200 walikuwa Waislamu watupu na sababu iliyotolewa ni kuwa
lilikuwa likichanganya, ‘’dini na siasa.’’ Huu pia haukuwa mwisho wa vumbi lile
zito. Mwaka wa 1968, Nyerere akapiga marufuku East African Muslim Welfare
Society (EAMWS) chama cha ustawishaji Uislam. Ilisadifu kuwa wakati haya
yanatokea Sheikh Takadir hakuwepo kushuhudia mabadiliko haya ya ‘’Mtume,’’ wa
Afrika. Baada ya kufukuzwa TANU na kupigwa pande na ndugu zake Sheikh Takadir
hakuchukua muda akafa.
Sifa kubwa ya binadamu ni kukosa uwezo wa kujua
ghaibu. Inawezekana Mzee Mwinyi kama alivyokuwa Sheikh Takadir kashindwa kutafakari
ule ukweli kuwa binadamu ni kigeugeu na nyoyo za binadamu hugeuka. Aliye mwema
leo ndiyo huyo mbaya wa kesho. Tuna mengi ya kujifunza katika historia ya nchi
yetu. Sheikh Takadir alimpa Nyerere sifa ya utume, Mzee Mwinyi yeye angependa
kumpa Magufuli urais wa maisha.
No comments:
Post a Comment