Friday 18 August 2017

KUTOKA JF: TAHARUKI - NYERERE KALISHWA SUMU 1950s


Bi. Mgaya Nyang'ombe







Yericko,
Kwa kuwa umependa kumbukumbu hizi za nyumbani kwetu Gerezani basi
nataka nikupe kisa kilicholeta taharuki kubwa ambayo naelezwa haijapata
kutokea katika historia ya TANU na Nyerere labda hadi Baba wa Taifa
anaaga dunia.

Siku za mwanzo za TANU viongozi wake walikuwa wakiwa na jambo zito
la kujadili walikuwa wakikutana nyumbani kwa Abdul Sykes Mtaa wa
Stanley na Sikukuu.

Walikuwa wakimaliza shughuli basi inakuwa chakula na vinywaji kujipongeza.
Siku hiyo baada ya kikao wakala chakula cha mchana.

Baada ya kula ghafla Nyerere akaanza kulalamika kuwa tumbo linamkata.
Nyerere akawa anajipindua huku na huku kwa maumivu.

Siku zote TANU walikuwa wakiishi chini ya hofu ya Nyerere kudhuriwa na
maadui wa TANU lakini katika chakula kile cha nyumbani kwake hapakuwa
na hofu kwani chakula chake kilikuwa kinatoka Kariakoo na kwa watu maalum
ambao Market Master, Abdul Sykes akiwafahamu na Mzee Mshume na ndiye
akikinunua, mpelekaji wa chakula hicho kwa Mama Maria alikuwa dereva wa
TANU, Said Kamtawa maarufu kwa jina Said TANU.

Nyerere kalala kwenye kochi anaugulia na taharuki ikazuka na minong'ono
haikuweza kukwepeka.

Nyerere kalishwa sumu!
Sumu Nyerere alishwe nyumbani kwa Abdul Sykes?
Uani jikoni walikuwa mama yake Nyerere Bi. Mgaya, Mama Maria, mama
yake Abdul Sykes Bi. Mruguru bint Mussa, 
mkewe Abdul Sykes, Mama
Daisy
.

Bi. Mgaya 
hakuweza kustahamili alipoona wanaume ingia toka kule ndani.

Aliposikia kuwa Nyerere anaumwa baada ya kula chakula kitu cha kwanza
kilichomjia ni kuwa mwanae kalishwa sumu akawa sasa mikono kichwani
analia na kutembea ua mzima.

Bi. Mgaya anasema Kizanaki na anachanganya na Kiswahili.
Ikawa patashika kumtuliza.

Wote waliokula chakula kile walikuwa salama na hawa ni watu waliokuwa
wakijuana vizuri na wakiaminiana mwisho wa imani.

Nani anaweza kupenya nyumbani kwa Abdul akampa sumu Nyerere?
Nani?

Mama Daisy ndiye alikua akinihadithia alipomaliza aliinamisha kichwa
akasema, ''Mwanangu MohamedAbdul na Nyerere wametoka mbali
sana na walikuwa zaidi ya ndugu.''

Iko siku nitakileta hapa kisa cha sanduku la fedha la Abdul Sykes.


Kushoto: Dossa Aziz, Julius Nyerere, Abdul Sykes na Lawi Sijaona

No comments: