Askari wa Miguu wa Burma, 1942 (The Burma Infantry)
![]() |
Kulia Abdulwahid Sykes na mdogo wake Ally Sykes wakiwa katika kikosi cha Burma Infantry 1942 |
Utangulizi
Nimehamasishwa na kipindi cha Al Jazeera ‘’The Burma Boys,’’ kuhusu askari kutoka Afrika ambao walipigana katika King’s African Rifles (KAR) katika misitu ya Burma dhidi ya Wajapani wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1938 – 1945). Kipindi hiki kimeeleza historia ya askari kutoka Ghana na Nigeria. Nimeona niweke hapa yale ambayo marehemu Ally Sykes alinieleza kuhusu askari waliotoka Tanganyika kwenda kupigana Burma yeye na kaka yake wakiwa miongoni mwa
askari hao.
Abdulwahid
- jina limaanishalo 'Mtumishi wa Allah, Mmoja na Aliye Pweke alikuwa mjukuu wa
Sykes Mbuwane, shujaa aliyetoka mbali na kupoteza maisha yake Tanganyika,
akipigana katika jeshi la Wajerumani. Shuleni Abdulwahid alikuwa daima anaogoza
katika darasa lake. Alipomaliza masomo yake ya msingi katika Al Jamiatul Muslim
School alichaguliwa kuingia shule ya serikali (Dar es Salaam Government School)
ambako alifundishwa na Mwalimu Mdachi Shariff. Shariff alikuwa rais wa
Tanganyika Territory African Civil Service Association (TTACSA). Abdulwahid
alimaliza darasa la kumi na kufanya mtihani wa kuingia Makerere College ambao
aliongoza. Serikali ya kikoloni, kutokana na msimamo wa siasa wa baba yake,
ilimfanyia khiyana asiingie Makerere kwa kisingizio kwamba alikuwa na umri
mdogo. Wakati huo Abdulwahid alikuwa na umri wa miaka kumi na saba. Ingawa
Waingereza waliuonaumrihuu mdogo kuendelea na masomo katika Makerere, lakini
Waingereza waliuona kamautoshao kumwandikisha kwenda kupigana vita kama askari
katika Kingís African Rifles (KAR)!
Mwaka
wa 1941 Abdulwahid, bila ya khiyari yake aliandikishwa katika jeshi la KAR
kwenda kupigana katika Vita Vya Pili vya Dunia vilivyokuwa vinaendelea Ulaya na
sehemu nyingine za dunia. Hili lilikuwa pigo kubwa kwa Kleist. Mwanaye alikuwa
bado yupo katika orodha ya wanafunzi waliokuwa wakitaraji kuingia Makerere College
huko Uganda. Kleist alikuwa na matumaini makubwa kwa mwanae. Kuchukuliwa kwa
Abdulwahid kwenda vitani kulikatisha ndoto yake kabisa. Kleist hakuwa na
uhakika kama mwanae angenusurika au angerudi jina tu. Mwaka 1933 Kleist
aliandika usia ambamo ulionyesha mapenzi aliyokuwa nayo kwa watoto wake.
Aliwaambia katika usia ule kuwa ilikuwa ni mapenzi yake, Mwenyezi Mungu
akijaalia, kuwasomesha hadi kufikia kiwango cha juu kabisa, Makerere ama Ulaya. Ikitokea atafariki kabla
ya kutekeleza azma hii, aliwataka waitimize nia yake hii wao wenyewe kwa
kusaidiana. Kleist hakuwa mtu wa maneno matupu. Alihakikisha anawaachia watoto
wake mali ya kutosha ili kukamilisha haja hiyo. Usia huu uliposomwa baada ya
kufa kwake mwaka 1949, hali ya siasa nchini Tanganyika ilikuwa ikibadilika kwa
haraka - na vivyo hivyo majaliwa ya Abdulwahid na nduguze.
Askari
wa zamani waliopigana katika jeshi la Wajerumani dhidi ya Waingereza katika
ardhi ya Tanganyika wakati wa Vita Kuu vya Kwanza vya Dunia kati ya mwaka
1914-1918 walimuunga mkono Hitler, ingawa si wazi wazi kwa kuwa kufanya hivyo
kungekuwa usaliti na uhaini dhidi ya Himaya ya Waingereza. Hata hivyo
hilohalikumzuia Schneider Plantan, askari wa Kijerumani wa Vita Kuu vya Kwanza
vya Dunia, kutembea huku na kule katika mitaa ya Dar es Salaam akiwachochea
watu wasimuunge mkono Winston Churchill katika vita vyake dhidi ya Adolf
Hitler. Schneider alikamatwa na kuwekwa kizuizini huko Mwanza, na hakufunguliwa
hadi mwisho wa vita mwaka 1945. Wengi wa askari hawa,waliokuwa katika jeshi la
Wajerumani katika Vita Kuu ya Pili walikuwa wamepitisha umri wa katikati. Hivi
Vita vikuu viwili vilikuwa vimetengana kwa miaka ishirini na nne tu. Askari
hawa wa zamani walikuwa na kumbumbu za kile walichokiona kuwa utawala wa haki
na uadilifu wa "Wadachi", Kama Wajerumani walivyokuwa wakiitwa na
wazee hao wakongwe wa Vita ya Kwanza ya Dunia. Lakini Kleist hakukubaliana na
mtazamo huu. Alikuwa na fikra zake mwenyewe za haki na uadilifu. Alikuwa
anavipinga vita hivyo kwa sababu yeye aliifahamu vyema hatma ya vita vile kwa
Waafrika wa Tanganyika. Alijua
iwangeendelea kutawaliwa tu ingawa safari hii huenda akaja mtawala mwingine.
Baada
ya Abdulwahid kupelekwa vitani na Waingereza, pigo jingine lilifuatia. Ally
alitoroka nyumbani akaenda kwenye kambi ya jeshi la Waingereza na kujitolea
kuwa askari wa KAR Ally akiwa na umri wa miaka kumi na tu. Kituo cha
kuandikisha askari kilikuwa Kilwa Road. Ally alitoroka kwa sababu alijua wazazi
wake wasingemruhusu kujiunga na jeshi.
Alimuonea gere kaka yake kwa kuwa mbali na nyumbani akiwa huru, tena
mwenye kujitegemea, na kuwa na maamuzi yake mwenyewe mbali na amri za baba yao.
Kleist alikuwa mkali sana. Aliitawala
nyumba yake kama kambi ya jeshi. Hakuwa mtu wa kupenda mchezo ama upuuzi. Ally
alikuwa chini ya umri uliotakiwa kuajiriwa vitani. Kleist alidhania serikali
ingetilia maanani umri mdogo wa Ally na hivyo kutompokea katika KAR. Lakini
maadam Ally alikuwa amejitolea kwa khiari yake mwenyewe, Waingereza walimpokea
kwa mikono miwili. Kama kaka yake, Ally alipelekwa Kabete kwa mafunzo ya
kijeshi ili kwenda kupigana Burma.
Ally
alipojiunga na KAR Abdulwahid alikuwa tayari ameondoka kwenda Nairobi, Kenya
kupata mafunzo ya kijeshi kama askari wa miguu. Ally alipowasili Kabete kwa
mafunzo, Abdulwahid alikuwa tayari ameondoka kwenda Ceylon (Sri Lanka) baada ya
kupewa likizo ya kurudi nyumbani kuaga wazazi wake. Kleist alisafiri kwenda
Nairobi kuonana na Ally kabla ya kuondoka kwake kwenda Ceylon, lakini alizuiwa
kuingia kambini kumuaga mwanae. Misiba miwili ilikuwa imemsibu Kleist alikuwa
na watoto wawili vitani wakimpigania adui wake wa zamani, Mwingereza. Kleist
hakuwa na ndugu wengine wa damu mbali ya watoto wake watatu. Alijaribu
kuwasiliana na ndugu zake nchini Msumbiji lakini bila mafanikio. Kleist
alihangaishwa na mawazo. Vipi ikiwa hawa
wanawe wawili watafariki... fikra hiyo ilikuwa nzito. Kleist na mkewe Bibi
Mruguru Mussa walibakia na kijana mmoja tu Abbas kuwafariji.
Bibi
Mruguru, tofauti na mume wake hakuweza kuwa na subira na kuzuia uchungu wake
moyoni. Alikuwa ameolewa na Kleist alipokuwa na umri wa miaka kumi na tatu tu
na alimzaa mwanae wa kwanza Abdulwahid akiwa na umri wa miaka kumi na tano.
Kwake yeye, wanae kwenda vitani kulimaanisha kifo. Taarifa zilikuwa
zikipokelewa mjini Dar es Salaam kila siku toka ng'ambo Kuhusu askari waliokuwa
wakipoteza maisha katika mapambano. Bibi Mruguru aliwaona watoto wake kama
tayari wameshaaga dunia. Hakuweza kula au kulala na alilia karibu wakati wote,
wakati mwingine akijitupa chini kwa uchungu. Majirani na marafiki walimfariji
kwa kumuambia: '’Bi Mluguru acha kulia usiwachurie watoto kwani watoto wangali
hai na kuwalilia ilikuwa ni sawasawa na kuwachimvia.’’ Kwa woga wa watoto wao
kupelekwa vitani, baadhi ya wazazi waliwaficha watoto wao wakubwa uani na
kuwakataza kutoka nje. Kwa mila za watu wa pwani uani ni mahali pa wanawake.
Wanaume hawakai huko, kwao wao ni barazani.
Kleist alistahamili kimya kimya na alikuwa akifanya shughuli zake kama
kwamba hakuna jambo lolote lililotokea. Kleist alikuwa mtu jasiri na ilikuwa
nadra kudhihirisha hisia zake. Kila asubuhi Bibi Mruguru alikwenda kwenye kituo
cha kuandikisha askari pale Kilwa Road kuulizia habari za wanae.
Abdulwahid
na Ally walikwenda ng’ambo kutumika chini ya Military Labour Service. Kikosi
hiki kilianzishwa Julai 1940 wakati Italia, chini ya Mussolini, ilipojiunga na
vita upande wa Wajerumani. Madhumuni ya kikosi hiki ilikuwa kusaidia majeshi ya
washirika kwa kuwaingiza raia katika vita,
kuwafundisha mbinu za vita na kuwekwa chini ya nidhamu ya jeshi. Askari
hawa kutoka uraiani walipewa kila kitu sawa na askari wa KAR kuanzia posho,
mahali pa kulala, tiba, malipo ya uzeeni na malipo endapo ulemavu au kifo
vitatokea. Kambi ya kuwafunza ilijengwa Kabete karibu na Nairobi kwa ajili ya
mafunzo ya awali. Mshahara kamili ulikuwa shilingi kumi na mbili kwa mwezi,
posho ya kila siku pamoja na sare. Cheo kikubwa kwa Waafrika kilikuwa sajini,
koplo na koplo lansi. Hawa walikuwa wakilipwa mishahara zaidi ya askari wa kawaida.
Askari
waliondoka na meli kuelekea vitani kupitia Kilindini, Mombasa. Meli hizo
zilisindikizwa na Jeshi la Wanamaji wa Uingereza (Royal Navy) ili kuzilinda na
mashambulizi kutoka nyambizi hatari za Wajapani. Waafrika walikuwa wa kwanza
kupelekwa Ceylon kwa mafunzo ya vita vya msituni kuunda lile jeshi lililokuja
kuwa maarufu la askari wa miguu la Burma (Burma Infantry). Jeshi hili ndilo
lililokuja kupigana na Wajapani. Jeshi hili la askari wa miguu liliundwa na
Waafrika kutoka nchi nyingi. Lilikuwa na
Waafrika toka Northern Rhodesia (Zambia), Southern Rhodesia (Zimbabwe), Belgian
Congo (Zaire), Nigeria, Gold Coast (Ghana), Kenya, Uganda na Tanganyika. Baadhi
ya askari hawa waliwahi kupigana Abyssinia, (Ethiopia) na Somaliland (Somalia)
ambako Waingereza na Makaburu wa Afrika ya Kusini walipambana na Wataliani.
Kutokana na kampeni iliyofanikiwa ya kikosi hiki nchini Abyssinia, ilionekana
kuwa ni muhimu kuunda kikosi kama hiki kwa haraka. Hii ndiyo ilikuwa sababu ya serikali kutoa
wito kutaka watu wa kujitolea kujiunga na KAR. Hawa Waafrika waliojitolea
katika vita hivi walileta taathira kubwa na kusababisha ushindi wa Waingereza
katika vita ile.
Mwaka
wa 1943 Ally aliondoka bandari ya Mombasa katika msafara wa meli ukielekea
Ceylon huku wakisindikizwa na wanamaji wa Kiingereza. Meli aliyopanda Ally
ilikuwa ya abiria ambayo katika siku za amani ilikusudiwa iwachukue Wazungu tu
wakati wa likizo. Chombo hicho hakikusudiwa kuwa na abiria Waafrika sembuse
askari weusi. Chombo kile hakikuundwa kuwachukua abiria hata Wazungu mafukara.
Ilikuwa meli ya anasa kwa ajili ya Wazungu matajiri. Wakati meli ile inafanya
safari zake za kawaida wakati wa amani Mwafrika ambae kwa bahati angekuwa ndani
yake angekuwa mtumishi wa kuwahudumia abiria wazungu. Kazi yake ingekuwa kuwapelekea
vinywaji, kuwasubiri mabwana wa
Kiingereza na wake zao wakila chakula cha jioni huku wakimulikwa na miangaza ya
mishumaa. Waafrika hawa kazi zao nyingine labda ingekuwa kufagia na kusugua
sakafu, kutandika vitanda na kusafisha vyoo. Lakini sasa Uingereza ilikuwa
ikipigana vita vikali dhidi ya adui wenye nguvu, Ujerumani, Japan na Italia.
Uingereza kuendelea kuwepo kama taifa kulikuwa hatarini, achilia mbali
kunusurika kwa makoloni yake yaliyotawanyika duniani kote. Haikuwa katika hali
ya kuangalia nani bwana na nani mtwana. Ikiwa ile meli ya abiria iliweza
kuwachukua waungwana wa Kiingereza kwenda Carribean kwa likizo kustarehe chini
ya vivuli vya minazi, basi ingeweza vilevile kuwachukua Waafrika kwenda vitani
kufa kwa ajili ya Mfalme.
Wakati
msafara wa Ally ulipokuwa baharini kuelekea Colombo, moja ya meli ilipigwa
kombora na nyambizi ya Wajapani. Chombo hicho kilizama na kuwaua askari wote
pamoja na maafisa wao Wazungu. Askari mmoja tu kutoka Tanga aliyekuwa
akijulikana kama Magembe ndiye aliyenusurika.
Askari kwenye meli zingine hawakujulishwa juu ya msiba huu hadi walipowasili
Colombo. Maafisa Wazungu walidhani kuwa kama Waafrika wangejulishwa kuhusu
msiba ule wakiwa bado katika bahari wangetaharuki na kuvunjika moyo. Licha yA Waafrika kujitoa muhanga, Wazungu
waliwabagua askari weusi. Waafrika walipachikwa jina la ëmilitary labourí
(vibarua wa kijeshi), wakati ambapo Wazungu kutoka Marekani na New Zealand
walitambulika kama ëalliesí (washirika) ingawa wote walikuwa wanapigana vita
moja chini ya amri moja..
Waafrika
kwa kupewa nembo kama hizo walihisi kudhalilishwa na kujiona kuwa wao kazi yao
kubwa ilikuwa kutafuta ushindi kutokana na nguvu za misuli yao; akili zao
hazikuwa na nafasi katika vita vile. Wao walikuwa ni sawa na zana isiyokuwa na
fikra, zana ya kutumiwa kukamilisha kazi ngumu. Askari Waafrika waliitwa
natives yaani wenyeji. Hao wenyeji
vilevile walibaguliwa kati ya wenyeji wasemao-Kiingereza na
wasiosema-Kiingereza. Mshahara wa askari wa Kiingereza ulikuwa wa juu zaidi
kuliko wa Mwafrika katika cheo kilekile. Chakula kilitolewa kulingana na taifa
la askari. Kulikuwa na chakula cha Mzungu, Muasia na Mwafrika, cha Mwafrika
kikiwa ndicho hafifu kuliko vyote. Askari Mwingereza alipewa kile kilichokuwa
kikijulikana kama, ‘’family allotment allowance,’’ ili aweze kuikimu familia
yake huko kwao. Hakukuwa na ruzuku kama hiyo kwa Waafrika. Waafrika walipewa
mvinyo kama sehemu ya chakula chao wakati ambapo wazungu walipewa brandi, wiski
na bia. Ilikuwa tu pale Waafrika walipoanza kuingia katika mapambano na
Wajapani ndipo chakula kikawa sawa kwa wote bila kujali rangi au utaifa wa
askari. Chakula hiki kwa lugha ya jeshi kilijulikana kama ‘’K’’ ration nacho
kilikuwa kikidondoshwa toka juu angani na ndege za Kiingereza (British Royal
Air Force).
Gazeti
la jeshi lililokuwa likijulikana kama Second Enchelon, lililokuwa likichapwa
kila wiki na kusambazwa katika kambi za majeshi ya washirika, lilichapisha jina
na nambari ya Ally kwa makosa likidai alikuwa miongoni mwa wale waliokufa
baharini. Ally alipofika kwenye kambi ya Kurnegala, nje kidogo ya Colombo,
Abdulwahid alikuwa amekaa hapo katika kikosi cha Service Corps kwa zaidi ya
mwaka mmoja. Kikosi chake kilikuwa kikishughulikia usafirishaji na mawasiliano.
Abdulwahid alikuwa anasema lugha zote mbili- Kiingereza na Kiarabu- vizuri
sana; kwa sababu hii alipandishwa cheo kutoka koplo hadi kuwa sergeant.
Abdulwahid alipata habari ya ‘’kifo,’’
cha mdogo wake katika gazeti hilo la jeshi na kumpelekea habari hizo za
kuhuzunisha baba yake. Ilikuwa pale tu Ally alipowasili Kurnegala na kuzungumza
na Abdulwahid kwa simu ndipo ilipotambulikana kuwa alikuwa yu hai. Ally
anakumbuka ilikuwa jioni alipowasili kwenye kambi hiyo. Amri ya kutotembea
usiku tayari ilikuwa imeshaanza kuzingatiwa. Saa hizo hakuna askari aliyeruhusiwa
kuwa nje ya kambi. Abdulwahid alikuwa katika kambi nyingine karibu na hiyo
aliyofikia ndugu yake. Habari zilipomfikia kuwa mdogo wake amewasili, alipata
shauku ya kumuona ndugu yake. Abdulwahid alichukua gari na kutoka kambini bila
ya dereva na hali amri ya kutotembea usiku ingalipo. Wakati ule Abdulwahid
alikuwa amepandishwa cheo na kuwa "Quarter Master Sergeant" na sheria
za kambi hazikumzuia yeye kutoka nje ya kambi wakati wa usiku. Ingawaje kwa
kawaida alikuwa na dereva wa kumuendesha, Abdulwahid aliamua kuendesha mwenyewe
jeep yake kwenda kumwona mdogo wake na kupata habari kutoka nyumbani. Majaaliwa ya binadamu yalivyo hayatabiriki,
kwani dereva aliyekuwa akimuendesha Abdulwahid Burma,alikuja kushika nafasi
ya juu katika Jeshi la Ulinzi la Watu wa
Tanzania.
Ally,
kama askari asemaye Kiingereza, alikuwa chini ya kikosi kilichojulikana kama
Education Corps. Kazi yake ilikuwa kuwafundisha Wazungu Kiswahili ili waweze
kuwaamrisha Waafrika hasa wale watokao Afrika ya Mashariki. Vilevile
aliwafundisha kusoma na kuandika Waafrika ambao hawakupata bahati ya kupitia
shule Kadhalika aliwafundisha jinsi ya kusoma ramani ili waweze kumudu kujua
njia ndani ya misitu ile ya Burma ambayo ilikuwa inababaisha sana kwa mtu
asiyekuwa na maarifa ya porini. Ingawa askari kutoka Afrika walikuwa muhimu
katika vita vile kama ilivyokwishaelezwa bado walidharauliwa na askari wenzao
kutoka Ulaya na kwingineko. Jambo hili liliwafanya askari kutoka Afrika
wajitazame upya.
Wakiwa
pale Kurnegala, askari Waafrika walipata mafunzo ya kupigana msituni kwa miezi
minne na kisha wakaondoka kwenda Burma kupitia Trincomalee. Kutoka hapo
wakielekea Chittagong. Wakati wote huo wakiwa katika msafara walisindikizwa na
British Royal Navy, meli zao zikienda polepole kwa tahadhari, zikipita njia
ambayo walihisi ni shwari kutokana na mashambulizi ya Wajapani. Ilikuwa hapo
Chitagong ambapo askari walipata kwa
mara ya kwanza kuonja kile kilichokuwa kikiwangoja. Kulikuwa na kitambo cha
takribani kilometa kumi baina ya bandari na kambi. Barabara ilikuwa mbaya na
ilikuwa imejaa matope ambayo yalifika kina cha kifundo cha miguu kutokana na
mvua kubwa za monsoon. Kambi ilikuwa
chafu kwa matope yaliyotapakaa kila mahali. Askari ilibidi abebe mzigo wake
mzito wa vifaa na zana, bunduki na risasi. Vilevile ilibidi wachimbe mahandaki
siku hiyo hiyo kwa ajili yao wenyewe na kwa maafisa wao Wazungu. Kambi iiliwapa
picha kamili ya kilichokuwa kikiwasubiri hata kabla hawajasikia milio ya bunduki za Wajapani.
Baada
ya kufika Chitagong walikaa hapo kwa siku chache kisha wakasafirishwa kwenda
Imphal, Burma, kwa malori ya Jeshi la India. Imphal ina umuhimu mkubwa kwa
askari wa Burma waliotoka Tanganyika. Ilikuwa ni hapa, siku ya mkesha wa
Krismas mwaka 1945, ambapo Abdulwahid na askari wengine, pamoja na mdogo wake
Ally na James Mkande, walifanya makubaliano ya kuunda chama cha siasa kudai
uhuru wa Tanganyika mara tu watakaporudi nyumbani baada ya vita. Imphal ilikuwa
ndiyo "command centre "ya askari wa Burma. Ilikuwa ukanda wa
hatari ambapo Wajapani walikuwa
wakipigana hasa na Waingereza. Askari wengi kutoka Afrika waliuawa Burma
wakimtumikia Mfalme ili jua lisitue katika Dola ya Waingereza. Watanganyika
wengi walipotezea maisha yao huko wakipigania kuiokoa Dola ya Waingereza chini
ya Mfalme George. Kulikuwa na mwimbo wa kuisifu dola ya Mwingereza uliokuwa
ukiimbwa hasa mashuleni, baadhi ya maneno yake yakiwa haya:
"Dola
ya Mwingereza,
Imetuletea
uhuru,
Tunamsifu
Baba Marehemu Kingi Joji".
Ilikuwa
ni pale Anfal ambapo, huku vita vinafikia ukingoni, Abdulwahid na askari wenzake wa Burma walikaa
kitako kutafakari mambo yaliyowasibu katika vita na kuufikiria mustakbal wa
Tanganyika. Iliamuliwa kuwa askari wa Burma kutoka Tanganyika waliokuwa
batalioni ya sita wawe ndio chanzo cha
chama cha siasa kupigania uhuru wa Tanganyika kwa kuuhamasisha umma. Wote waliafiki wazo hilo. Jina
lililochaguliwa kukitambulisha chama hicho lilikuwa Tanganyika African National
Union (TANU). Ally Sykes anamkumbuka Abdulwahid kiliandika jina la chama hicho
kilichokusudiwa ndani ya shajara yake. Hawa askari wa Burma walikuwa wakifahamu
vyema kuwa tayari huko nyumbani kulikuwapo na African Association, chama
ambacho kilikuwa kikipigania haki za Waafrika. Abdulwahid alitarajiwa afahamu hili
zaidi ya wenzake kwa sababu baba yake
ndiye aliyekianzisha chama hicho akiwa katibu wake wa kwanza. Lakini
suala la jinsi wangelivyokiunganisha chama hicho kipya cha TANU na kile cha African Association ili kudai
uhuru, halikujadiliwa.
Abdulwahid
alilitumikia jeshi nchini Kenya, Ceylon, India na Burma. Hata kabla hajafikisha umri wa miaka ishirini
na mmoja alikuwa amekwishapanda cheo na kufikia Regimental Sergeant Major. Hiki
kilikuwa ndio cheo cha juu kabisa ambacho Mwafrika aliruhusiwa kukifikia. Cheo
kingine cha juu ambacho kiliwekewa Mwafrika kilikuwa kile cha Kapteni ambacho
Waingereza walimtunukia Kabaka Edward Mutesa wa Buganda na Chifu Adam Sapi
Mkwawa wa Wahehe. Lakini Kabaka Mutesa na Chifu Adam Sapi Mkwawa walitunukiwa vyeo hivi kwa sababu ya nyadhifa
zao kama machifu, wakati Abdulwahid alizipata tepe zake kwa sababu ya ujasiri
wake, kipaji chake cha uongozi na umaridadi wake. Vilevile Abdulwahid alivishwa
nishani kadhaa, baadhi yake Burma Star na ile ya War Medal.
Baada
ya Vita Vya Pili kumalizika, Wazungu waliruhusiwa kuondoka uwanja wa mapambano
kurudi makwao kabla ya Waafrika, huku ikidaiwa kuwa wao walikuwa wakihitajika
haraka sana huko Ulaya kwa ajili ya ujenzi wa nchi zao zilizoteketea kwa ajili
ya vita. Vikosi vya Waafrika vilipewa ruhusa mwisho. Askari wa KAR kutoka
Tanganyika walikusanywa katika kambi moja iliyokuwa ikijulikana kama Kalieni,
nje ya Bombay, kwa ajili ya safari ya kurudi nyumbani. Walipokuwa Kalieni
Abdulwahid alikutana na rafiki yake toka nyumbani, Ahmed Rashad Ali,
Mzanzibari. Ahmed Rashad alikuwa mcheza kandanda mashuhuri na alikwenda India
kwa masomo. Tutakutana na Ahmed Rashad hapo baadaye tutakapojadili harakati za
kudai uhuru huko Zanzibar. Askari kutoka Tanganyika walikuwa na maroli ya juu
walipokuwa baharini wakirudi nyumbani; kitu pekee kilichotawala mazungumzo yao
kilikuwa ni jinsi wangevyoweza kuwaondoa Waingereza kutoka ardhi ya Tanganyika.
No comments:
Post a Comment