TAAZIA: BURIANI
NDUGU NA RAFIKI YANGU MPENZI
MUUNGWANA
KLEIST…
(27
June, 1950 – 24 November, 2017)
![]() |
Kleist Abdulwahid Sykes |
Usiku wa Jumanne tarehe 23 nimeona katika ukurasa wa
FB wa kaka kaka yangu Prof. Charles Mgone kuwa yuko Glasgow, Scotland akaandika
kuwa anafurahi kurudi tena katika mji huo. Nami nikaandika kumwambia kuwa
amenikumbusha Dumbarton Road mtaa ambao yeye akiishi na mimi nikienda
kumtembelea katika miaka ya mwanzoni ya 1990 kwanza nikitokea Dar es Salaam na
baadae nikitokea Cardiff, Wales. Asubuhi yake nikapokea ujumbe mfupi kutoka
kwake ukisema, ‘’Nasikitika kuwa sintokuwapo kumsindikiza ndugu na rafiki yangu
katika safari yake ya mwisho.’’ Jina la aliyefariki hakuliandika bila shaka
akiamini kuwa taarifa tayari ninazo. Nikashtuka kwani ujumbe huu ulikuwa
ukinitaarifu msiba na haraka nikarejesha ujumbe kumuuliza nani kafariki? Mimi
ndiyo kwanza nilikuwa nimeamka na kuwasha simu yangu. Jua lilikuwa limeshapanda
pakubwa. Hata sekunde tatu hazikupita taarifa nyingi zikawa zinaingia kwa
kufukuzana katika simu zikitoa taarifa ya kifo cha Kleist na taarifa ya kwanza
ilikuwa kutoka Saigon Club.
Imesadifu kifo cha Kleist ikutane na kumbukumbu zangu
za Glasgow ambako takriban miaka 30 iliyopita kila nilipokuwa hapo Dumbarton Road
kwa labda ule upweke wa Ulaya tulikuwa tukikumbushana habari za utoto wetu Dar
es Salaam Mtaa wa Kipata tulipozaliwa na Charles mara kwa mara atanihadithia
habari zake za udogoni na Kleist. Hawa walikuwa marafiki toka utoto na mama zao
walikuwa mashoga. Charles alimtangulia Kleist kwa mwaka mmoja. Charles kazaliwa
1949 na Kleist 1950. Charles alikuwa akinihadithia mchezo aliokuwa akicheza na
Kleist kwenye bomba la maji lililokuwa Mtaa wa Kipata na Swahili pembeni ya
nyumba ya Mama Kilindi. Miaka ile ya 1950 si kila nyumba ilikuwa na maji ndani
na haya mabomba yalikuwa kila mtaa kwa ajili ya watu kuteka maji.
Taarifa ya kifo cha Kleist haraka ilinirudisha nyuma
katika historia hii ya Dar es Salaam ya Tanganyika ya miaka 1950 wakati sisi
tunazaliwa wazee wetu ndiyo walikuwa wanaanza harakati za wazi za kupambana na
Waingereza kuidai Tanganyika. Baba yake Kleist, Abdulwahid Sykes katika mwaka
wa 1950 ndiye alikuwa Katibu na Kaimu rais wa Tanganyika African Association
(TAA). Siku hizo wakiishi Mtaa wa Stanley na Sikukuu katika nyumba ya kupendeza
katika hali za wakati ule, nyumba iliyoezekwa bati ina maji na umeme na nyumba
ambayo si ya mtindo wa vyumba sita bali numba yenye veranda na vyumba vya
kulala na ua mkubwa na vyoo vyenye mabomba ya mvua ya kuogea. Nyumba nyingi
wakati ule zilikuwa za makuti na zilizoezekwa kwa madebe na kujengwa kwa
udongo, fito na kutomelewa kwa chokaa na sementi. Hii ndiyo Dar es Salaam
ambayo Kleist alikuwa kazaliwa pamoja na wengi ambao niliwaona pale mazikoni
walipokuja kumsindikiza ndugu yao katika safari yake ya mwisho.
Bomba la maji la Kipata lilikuwa pembeni ya nyumba ya
Mama Kilindi mumewe Mzee Hassan bin Khamis kabila Mnubi ambae kivazi chake siku
zote kilikuwa ni kanzu koti na tarbush. Mzee Hassan alikuwa akifanya biashara
Soko la Kariakoo ambako baba yake Kleist alikuwa ndiyo Market Master yaani Mkuu
wa Soko. Watu mfano wa Mzee Hassan diyo walikuja kununua kadi za kwanza za TANU
pale sokoni wakiuziwa na Abdul Sykes na ndiyo watu wa mwanzo kumtia machoni
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka wa 1952 akiwa na Abdul Sykes katika
mitaa ya Gerezani au pale Sokoni Kariakoo. Makaburi ya Kisutu wakati tunamzika Kleist,
nilimuona kasimama Amani, mjukuu wa Mama Kilindi na Mzee Hassan bin Khamis.
Amani hakumuwahi Kleist katika mitaa ya Gerezani akicheza jirani ya kwao kwenye
bomba la maji kwani yeye ni uzawa wa miaka ya 1970, lakini siku hii Gerezani na
Dar es Salaam yote kwa ujumla ilitoka kuja kumzika mwana wa mji kindakindaki
kuanzia babu, bibi na baba. Makaburini niliwaona pia wajukuu wa Hassan
Machakaomo. Huyu Machakaomo ni katika kizazi cha kwanza cha Wazulu. Mzee wa
Kizulu Machakaomo aliingia Tanganyika akiwa askari mamluki kama alivyoingia
babu yake mkuu Kleist, Sykes Mbuwane miaka ya mwishoni 1800 wakiwa wamebeba mikuki
na ngao mikononi. Ukoo wa Machakaomo hadi leo hawa bado wanaishi Kipata.
Kleist wazee wengi waliokuwa wanamfahamu baba yake
wanasema alishabihina sana na baba yake kwa tabia na hulka hususan katika
uungwana na ukarimu. Nilipatapo kumsikia Mzee Kitwana Kondo akisema, ‘’Abdul
alikuwa mtu muugwana sana.’’ Sifa hii ya ungwana aliitoa pia Mhariri wa Africa
Events (London) Mohamed Mlamali Adam katika utangulizi wa makala niliyoandika mwaka
wa 1988 ambamo nilimtaja Abdul Sykes. Katika utangulizi wake Mlamali alimwita
Abdul Sykes, ‘’…the sweet Abdul Sykes…’’ kwa tafsiri nyepesi ni sawa na kusema,
‘’Muungwana Abdul Sykes.’’ Hivi ndivyo ilivyokuwa tabu sana Kleist kukikwepa
kivuli cha baba yake lau kama katika uhai wake Kleist aliweza kujijengea haiba
na historia yake mwenyewe nje ya haiba na historia ya baba na babu yake ambao
wote walitoa mchango mkubwa katika kukita misingi ya Tanganyika kujikomboa
kutoka minyororo ya ukoloni wa Waingereza. Juu ya juhudi zake za kusimama na
miguu yake mwenyewe miwili siku zote kivuli cha historia ya baba na babu yake
ilimwandama Kleist na kumuelemea sana.
Ingekuwa labda si kwa udugu waliokuwanao wazee wetu na
pengine pamoja na mapenzi yangu ya kupenda kusoma kuandika na kuvutiwa na stori
yoyote ya kusisimua nisingepata hamu ya kuandika maisha ya Abdulwahid Sykes. Historia
ya ukoo wa Sykes dhidi ya ukoloni na juhudi yao kaika kuwaunganisha Waafrika ni
kisa cha kuvutia. Hii ilikuwa historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika na
Kleist akijua mengi katika historia hii na vipi asijue ilhali Baba wa Taifa
alipokelewa Dar es Salaam na kutiwa katika uongozi wa TAA na TANU kwa juhudi za
baba yake? Historia hii ya kusisimua ilinisogeza karibu zaidi na Kleist kiasi
cha sasa kufunika ule urafiki na udugu wetu wa asili ulioanza na babu zetu hadi
sasa kutufikia sisi wajukuu, historia ambayo sasa imetimiza karne moja.
Kleist alikuwa na kisa cha kueleza cha historia hii
ambayo kwa sababu zisizoweza kufahamika ilikuwa inatoweka taratibu, lakini
alikuwa hana msikilizaji wala mtu anaetaka kuijua. Nilipotokea mimi kama
muulizaji maswali na msikilizaji kifua cha Kleist na moyo wake vyote
vilifunguka na kuanza kueleza mambo ambayo kwangu yalikuwa kama vile nimekaa
kwenye kiti cha Empire Cinema naangaalia filamu nzuri mfano wa ‘’Hercules in
the Land of Cyclopes,’’ filamu iliyotusisimua watoto wote wa wakati ule. Siku
moja mdogo wake Kleist marehemu Omari alinambia, ‘’Mohamed dada Daisy ameandika
kitabu kuhusu babu kitafute ukisome.’’ Ikasadifu kuwa nilikuwa nakwenda Arusha
na nilipokuwa nimemaliza shughuli zangu nikaingia Maktaba ya Taifa, Arusha na
hapo nikakikuta kitabu kilichohaririwa na John Iliffe, ‘’Modern Tanzanians,’’
na ndani nikamkuta Daisy kamwandika babu yake ‘’The Townsman: Kleist Sykes,’’
yaani, ‘’Mwanamji: Kleist Sykes. Kuanza kusoma utangulizi tu nikawa nimeshatoka
katika karne ya 20 hii, dada yangu Daisy amenipeleka karne ya 19 niko
Mozambique, Mhambane katika kijiji cha Kwa Likunyi nipo na Mjerumani Herman von
Wissman anawapakia askari mamluki wa Kizulu katika manowari bandari ya Laurenco
Marquis (leo Maputo) anawaleta Pangani kuja kupigana na Abushiri bin Salim na
Chief Mkwawa. Katika askari hawa mamluki wa Kizulu waliokuwa wanakuja
Tanganyika alikuwapo babu yake mkuu Kleist, Sykes Mbuwane na nduguye kipofu Ally
Katini.
Nilibakia na maswali mengi sana nayatafutia majibu.
Nilifahamu fika kuwa huyu aliyeandika maisha ya Kleist katika mji wa Dar es
Salaam ya 1900 hakuwa Daisy Sykes. Hii ni kalamu ya mtu mwingine kabisa. Siku
hizo Kleist yuko Geneva anafanya kazi United High Commission for Refugees
(UNHCR). Maswali yangu yakawa yanamsubiri Kleist. Nyumba ya Kleist ilikuwa
inaangalia shule yake aliyosoma, Aga Khan School. Kiasi Kleist asome shule hiyo
maana baba yake alikuwa kwa miaka mingi wakati wa uhai wake mjumbe katika Aga
Khan Education Committee. Kleist alikuwa naamini akifurahi sana kuzungumza na
mimi kuhusu historia ya ukoo wao. ‘’Sheikh Mohamed ngoja nikuletee kinywaji
chako.’’ Kleist alikuwa akijua kuwa mimi ni mpenzi wa muziki wa jazz kama yeye
basi hapo ataniwekea santuri baada ya santuri ya muziki wa wapigaji maarufu
kutoka maktaba yake, muziki ukija kwa sauti ya chini sana.
![]() |
Bushiri bin Salim Al Harith |
Tulikuwa kama vile tuna ratiba yetu maalum
tunayoifuata. Ilikuwa kwanza lazima tubadilishane ‘’notes,’’ kuhusu baba zetu
na maisha yao walipokuwa vijana mitaa ya Gerezani. Hapo tukicheka sana na
kuwarehemu wazee wetu. Baba yangu katika umri mdogo sana alikuwa na wake wawili
na baba yake Kleist pia alikuwa na wake wawili. Basi tutatia yetu huku
tunacheka na kushangaa maisha ya wazee wetu na hawa wakijiona kuwa wao walikuwa
watu wa kisasa kwa wakati wao. Wazee wetu wote walikuwa ‘’sharp dressers’’ na
wapenzi wakubwa wa muziki. Baadhi ya mambo naona na sisi watoto waliturithisha
na yameathiri sana mtindo w maisha yetu.
Tukimaliza hapa ndipo tutaingia katika mazungumzo
mazito. Nitakuwa na maswali ya kumuuliza Kleist kuhusu historia ya baba yake na
ukombozi wa Tanganyika kupitia TAA na kisha TANU. Ghafla ile hali ya vicheko
itatoweka na Kleist anabadilika anazungumza kwa kuchunga sana ulimi wake
akichagua maneno na hali ya simanzi nyepesi itatanda. Kleist alinifahamisha kuwa katika vitu ambayo
yeye vimemstaajabisha sana ni kuwa Iliffe akimtegemea sana Daisy katika kupata
taarifa za African Association kuasisiwa kwake na mambo mengine na Daisy
akimuuliza baba yake lakini kitu cha kustaajabisha ni kuwa Iliffe hakutaka
kukutana na Abdul Sykes kupata historia ile moja kwa moja. Wakati ule Daisy
alikuwa mwanafunzi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam akiwa mmoja wa wasichana
wachache wa Kariakoo kupata elimu ya juu. Namna hii ikawa nakusanya ‘’notes,’’katika
mazungumzo yangu na Kleist na nilihisi kama vile Kleist alikuwa kama mtu
aliyekuwa anahitaji, ‘’therapy,’’ ya aina fulani kupunguza joto katika nafsi
yake. Alikuwa ni mtu ambae alitaka sana mchango wa baba yake utambuliwe katika
kuunda TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika. Kwa miaka mingi haya ndiyo yakawa
maisha yetu mimi na Kleist. Mimi nikijichukua kama mwanafunzi na Kleist ndiyo
mwalimu wangu.
Mimi na Kleist tukawa sasa tuna maisha yetu
tumejizingirisha sisi wawili tu tuko nje ya lile duru letu la kawaida la
marafiki zetu wengine kama marehemu Yusuf Zialor, Wendo Mwapachu, Abdallah
Tambaza, Abdul Mtemvu kwa kuwataja wachache na ikawa kama chama cha wachawi.
Huingii hadi nawe uwe mwanga. Hii ikawa ‘’Exclusive Club,’’ yaani chama
makhsusi cha watu wawili tu. Miaka ilivyokuwa ikipita nami ndivyo nilivyokuwa
nafaidika na kuzidi kuchota elimu ile kutola kwa Kleist. Akienda Geneva na akija
Dar es Salaam tunakutana kama ada yetu na mazungumzo yanaendelea. Lakini Kleist
hakuwa mtu wa kusukumwa aharakishe. Kila kitu kilikuwa kikienda kwa kasi aliyokuwa
akiitaka yeye. Alipatapo kuniambia mwanzo kabisa nilipomwambia kuwa nataka
kuandika kitabu cha baba yake, ‘’Mohamed haya mambo yanataka subira na wewe
ujue lipi la kusema na lipi la kuacha kusemwa.’’ Maneno haya aliyoniambia
Kleist yalikuwa sawasawa na maneno ambayo Daisy aliambiwa na mwalimu wake wa
historia, John Iliffe mwaka wa 1968 alipotaka kuandika historia ya baba yake.
Sababu ya haya ni kuwa tayari palishazuka sintofahamu chinichini katika
historia ya TANU.
Siku moja nikamwambia Kleist maneno aliyonieleza Dossa
Aziz nyumbani kwake Mlandizi Nilimwambia Kleist, ‘’Mzee Dossa kaniambia kuwa
TANU ilitaka kuandika historia ya TANU miaka ya mwanzoni ya uhuru.’’ Kleist
akanijibu kuwa hiyo ni kweli na yeye alikuwa akienda pale Ofisi ya TANU akitoka
shule kwenda nyumbani wakati baba yake na Dr. Wilbert Klerruu wakiandika
historia ile. Kwa huzuni Kleist akanieleza kuwa kazi ule haikuweza kukamilika
licha ya kuwa baba yake alikuja na nyaraka zote za TAA na TANU. Kleist
hakunambia kwa nini ile kazi iliishia njiani. Miaka mingi ya mazungumzo na
Kleist nilijua wapi nisimame. Akitumia lugha ya kiungwana Kleist alikuwa
akinambia kuwa TANU ilikuwa inaikataa historia ya baba yake katika uhuru wa
Tanganyika. Jambo hili lilichoma sana moyo wa Kleist. Nilijua hapa ni mahali pa
kusimama nirejee wakati mwingine kwa mazungumzo. Mambo haya yalinifikirisha
sana.
Mwaka wa 1988 katika kukumbuka ya miaka 20 baada ya kifo
cha Abdul Sykes, Ally Sykes alinunua nafasi katika Daily News na Uhuru ili
kuchapa kumbukumbu ya kifo cha kaka yake. Usiku Kleist akapokea simu kutoka kwa Reginald
Mhango wa Daily News akimwomba radhi kuwa ingawa wamelipia tangazo la
kumbukumbu ya baba yake lakini yeye hawezi kuidhinisha ichapwe hadi atakapopata
ruhusa kutoka Makao Makuu ya CCM Dodoma kwa sababu maisha ya baba yake yamegusa
historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika. Kleist alisoma na Mhango Aga Khan
School kwa hiyo wakijuana vizuri. Kleist alimwambia Reginald kuwa hayo ndiyo
yalikuwa maisha ya baba yake na hana namna ya kuweza kubadili historia hiyo. Kleist
akamshauri Mhango aende kwenye gazeti la Sunday News la tarehe 20 October 1968
atakuta taazia ya baba yake iliyoandikwa na Mhariri wa Tanganyika Standard
Brendon Grimshaw inayoeleza hayo yaliyopelekwa
Daily News. Kumbukumbu zile zilichapwa na
Daily News na Uhuru lakini uhariri uliopitishwa uliondoa utamu wote wa
kumbukumbu ile. Lile ambalo lililokusudiwa halikupatikana.
Inawezekana huu mtiririko wa dharau kwa baba yake
ndiyo uliomfanya Kleist anipe moja ya labda siri kubwa katika historia ya uhuru
wa Tanganyika. Ilikuwa mkakati aloweka baba yake na Hamza Mwapachu katika
kuunda TANU toka mwaka wa 1950. Hiyo ndiyo siku aliponitajia jina la Earle Seaton.
Mimi nilikuwa nikimjua Seaton kijuujuu tu. ‘’Earle Seaton alikuwa rafiki ya
baba yangu,’’ Kleist alianza. ‘’Seaton alikuwa anatoka Bermuda. Seaton alikuwa
mwanasheria Moshi. Seaton akimsukuma baba aondoke Tanganyika aende kusoma
Amerika baada ya kujua kuwa baba alikosa kwenda Makerere College 1942 kwa kuwa
Waingereza walimtia katika jeshi lao, King’s African Rifles (KAR) kwenda Burma
katika Vita Kuu ya Pili.’’ Mkakati huu wa Abdul Sykes na Hamza Mwapachu pamoja
na Stephen Mhando na Dr, Vedasto Kyaruzi na Dossa Aziz ndiyo uliomwingiza Seaton
katika siasa za Tanganyika kupitia TAA Political Subcommittee. Seaton akawa
mshauri mkuu wa TAA na akaisaidia TAA katika kutayarisha mapendekezo ya katiba
yaliyoitishwa na Gavana Edward Twining mwaka wa 1949. Kleist akanambia kuwa
hotuba ya Nyerere UNO ilitoka katika mapendekezo haya ambayo pia yalijadiliwa
katika mkutano wa kuasisi TANU 1954. Sasa
nikawa namwangalia Kleist kwa jicho jingine. Huyu anaezungumza na mimi hakuwa
Kleist kwani ilinidhihirikia kuwa haya hayakuwa maneno yake Kleist, huyu ni
baba yake anazungumza na mimi kutoka kaburini. Kleist alikuwa mtu wa subira kubwa sana. Yote
haya akiyajua na akikaa kimya wakati baadhi ya watu ndani ya TANU baada ya
uhuru kupatikana 1961 wakawa akiifanyia dhihaka TAA na kukipa chama kile kila
aina ya majina ya kebehi kuwa hapakuwa na siasa katika TAA bali starehe nk. nk.
Kleist sasa akawa moja ya funguo katika uandishi wa maisha ya baba yake na
historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika.
![]() |
Kushoto mbele Kleist Sykes na mwanae Abbas Sykes Waliosimama kulia ni Abdul Sykes katika sare ya King's African Rifles (KAR) na Ally Sykes, 1942 |
Earle Seaton na Julius Nyerere |
Ndiyo siku moja Kleist akaniangushia bomu nusura
likatishe maisha yangu. Akanionyesha shajara (diary) za baba yake akaniambia,
‘’Hizi shajara siwezi kuzitoa humu ndani nikakupa kwani zina na mengi sana
kuhusu historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika na sijaweza kuzisoma zote kwa
kuwa baadhi zimeandikwa katika hati mkato.’’ Kleist akanambia kuwa amesoma nini
baba yake aliandika siku alipozaliwa tarehe 27 June, 1950. Kleist akacheka
akanambia, ‘’Baba aliniita, ‘’Prince.’’ Hakika baba yake hakukosea kumvika taji
mwanae kwani Kleist alikuwa na sudi ya kupendeka. Alipokuwa UNHCR Lusaka,
Zambia naambiwa Thabo Mbeki alikuwa akitembea na ufunguo mmoja wa nyumba ya
Kleist ili aweze kuingia wakati hata kama yeye hayupo. Huu ndiyo ulikuwa wakati
ule wa mapambano ya ANC na makaburu wa Afrika Kusini yamepamba moto.
Halikadhalika mmoja wa mawaziri wakuu wa Mozambique
alipata kumuomba Kleist arejee ‘’nyumbani,’’ Msumbiji ampe kazi. Ilikuwa wakati
yupo na UNHCR, Lusaka basi siku moja katika mazungumzo na Waziri Mkuu huyu mjini
Maputo, Kleist akamueleza kuwa yeye asili yake ni Msumbiji, Kleist akanambia
Waziri Mkuu akashtuka sana Kleist alipompa historia ya ukoo wake. Waziri Mkuu
akamwambia, ‘’Kleist tuko huru sasa rudi nyumbani nikupe kazi.’’ Kleist anasema
huyu bwana alidhamiria khasa kuwa arudi ‘’nyumbani,’’ ampe kazi waijenge pamoja
Msumbiji. Kleist alikuwa na mengi na si rahisi kuyaeleza yote.
Siku chache kabla hajafariki Kleist alikuwa alinipigia
simu akaniahidi kunipa nyaraka mbili.
Moja ilikuwa ''Admission Letter,'' ya 1953 ya baba yake kutoka Princeton
University na nyingine barua pia ya 1953 kutoka kwa Earle Seaton. Ndani ya
barua ile Seaton alimwambia Abdul Sykes kuwa asiache kufika UNO kufuatilia
mijadala ya Mandate Territories atakapokuwa Princeton, New Jersey. Akaniambia pia alikuwa anataka niende kwake akanionyeshe
picha za ufunguzi wa Petrol Station ya baba yake iliyokuwa Ilala mkabala na
Ilala Boma. Petrol Station hii ilikuwa chanzo cha fedha nyingi ambazo baba yake
alizitoa kwa TANU wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.
Namuomba Allah
amsamehe ndugu yetu Kleist Abdulwahid Sykes madhambi yake na ampe kitabu chake
kwa mkono wa kulia.
Amin.
No comments:
Post a Comment