Sunday 19 November 2017

IPI TOFAUTI KATI YA MAUAJI YA EAST TIMOR NA MYANMAR?

Utangulizi
Zitto Kabwe Mbunge wa Kigoma Mjini na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo ni kijana hodari mwenye kujua kuchagua maneno yake vyema. Hapo chini ameandika masikitiko yake kuhusu Tanzania kukataa kupiga kura kulaani mauaji ya Waislam Myanmar. Katika maandishi yake neno, ''Waislam,'' halipo. Lakini dunia nzima inajua kuwa wanaouliwa Myanmar ni Waislam si suala la kuuliwa ''wananchi.'' 

Iwe itakavyokuwa Zitto Kabwe kaeleza masikitiko yake ili Watanzania wajue nini kimetokea. Kwa sera ya Tanzania kuhusu msimamo wake wa kusimamia haki duniani kote kitendo haya ni mabadiliko makubwa sana katika msimamo huo uliowafikisha Watanzania kupigana Msumbiji bega kwa bega na Frelimo na kutoa misaada kote kulikokuwa na dhulma sawa na kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliposema, ''Tunataka kuwasha mwenge uangaze kote na kuleta matumaini kule watu walikokata tamaa.''

Hii sera mpya ya kushindwa kulaani mauaji ya Waislam wanaouliwa Myanmar huenda hii ikawa ni sera mpya ambayo kwa sasa ndiyo inaongoza Tanzania na uhusiano wake na mataifa mengine. Ndiyo kusema kuwa sasa Tanzania haijali tena dhulma bali inaongozwa na maslahi yake mengine ambayo kwa bahati mbaya kwa sasa hayajakuwa bayana. 

Tanzania ilianza na kurejesha uhusiano na Israel uliovunjwa na Baba wa Taifa mwenyewe nusu karne iliyopita. 

Leo Tanzania imeridhia kutopiga kura kwenye mauaji ya kimbari ya Waislam wa Mynmar. 

Wachunguzi wa siasa wanasubiri kutazama nini lingine litafuatia. Labda hilo litatoa mwanga zaidi kuonyesha nchi yetu imesimama upande gani na kwa nini. 

Swali la kujiuliza ni hili: Ingekuwa ni kura ya East Timor na wanaouliwa ni Wakatoliki Tanzania ingekaa pembeni ikaacha kupiga kura?

Jibu unalo wewe ndugu msomaji wangu.







Unaweza kusoma historia ya Tanganyika na Palestine hapo chini:
http://www.mohammedsaid.com/2017/06/baada-ya-kuondoka-baba-wa-taifa.html

Tanzania yalaumiwa vikali kwa kutopigia kura azimio la UN la kutetea Waislamu wa Myanmar


http://parstoday.com/sw/news/africa-i36555-

Tanzania_yalaumiwa_vikali_kwa_kutopigia_kura_azimio_la_un_la_kutetea_waislamu_wa_Myanmar
Mbunge mashuhuri katika bunge la Tanzania ameikosoa vikali serikali ya nchi hiyo kwa hatua yake ya kutopigia kura azimio la Umoja wa Mataifa linalotaka serikali ya Myanmar ikomeshe operesheni za kijeshi zinazolenga kukandamiza jamii ya wachache ya Waislamu Warohingya nchini humo.

Siku ya Alkhamisi iliyopita Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayohusika na haki za binadamu ilipitisha rasimu ya azimio linaloitaka serikali ya Myanmar ikomeshe operesheni za kijeshi ambazo "zimesababisha ukiukaji ulioratibiwa na uvunjaji wa haki za binadamu" za Waislamu Warohingya wanaoishi katika jimbo la Rakhine.

Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 135 zilizounga mkono, nchi 10 zililipinga na nyengine 26 ziliamua kutopiga kura, Tanzania ikiwa moja ya nchi hizo.

Zitto Kabwe akiamkiana na Rais John Magufuli (aliyevaa miwani) 


Akiandika katika ukurasa wake wa kijamii wa Facebook, Zitto Kabwe ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, amesema: "Juzi Umoja wa Mataifa kulikuwa na kura ya Azimio la kulaani vitendo vya unyama dhidi ya watu wa kabila la Rohingya huko Myanmar. Nchi yetu haikupiga kura (abstained). Ni kitendo cha aibu sana Tanzania kushindwa kulaani vitendo vya namna hii".

Msimamo huo wa Tanzania umetafsiriwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kidini wa nchi hiyo kama kielelezo cha kubadilika sera za serikali ya sasa ya Dar es Salaam katika suala la kutetea haki na uadilifu duniani.


Balozi wa Tanzania Israel Job Masima akikabidhi hati zake za utambulisho kwa Rais wa utawala huo wa Kizayuni Reuven Rivlin

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni serikali ya Tanzania ilianzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel. Na hii ni katika hali ambayo msimamo wa huko nyuma wa Tanzania tangu enzi za uongozi wa Rais wa kwanza wa nchi hiyo hayati Mwalimu wa Julius Nyerere ulikuwa ni wa kutetea harakati za ukombozi za wananchi wa Palestina katika kukabiliana na dhulma na ukaliaji mabavu wa ardhi zao unaofanywa na utawala haramu wa Israel.../

No comments: