Buriani ‘Kaka Kleist’
Na
Alhaji Abdallah Tambaza
![]() |
Mwandishi wa makala Abdallah Tambaza ni huyo wa kwanza kushoto, Bubby Bokhari, Kleist Sykes, Yusuf Zialror, Mohamed Said, waliochutama kushoto ni Kaisi, Wendo Mwapachu na Abdul Mtemvu, 1968 |
AWALI
ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Allah (SW) na kumtakia rehma
Mtume wetu Muhammad (SAW) kwa kuniwezesha kukaa mbele ya kompyuta na kuandika
taazia hii ngumu na nzito ya marehemu kaka yangu; ndugu yangu; sahib yangu; na
rafiki yangu kipenzi kabisa kupata kutokea, Kleist Abdulwahid Abdallah Sykes – Inna
Lillah Waina Ilayhi Rajiun.
Mwezi
Januari mwaka huu nilimwandikia rafiki yangu mwengine, SACP Mohammed Chico,
taazia nzito kama hii iliyonitoa jasho na machozi pale ilipokamilika. Sikudhani
hata kidogo kama hautapita muda mrefu nitarudi kuandika tena taazia nyengine
kwa mtu anayefanana na yeye – wote ni watu wa kwetu Dar es Salaam niliowajua
vilivyo. Wazungu wa kule Ulaya Ingereza na Marekani, wanapofikwa na msiba wa
ukubwa kama huu, husema kwamba umekuja ‘untimely’ (haukutarajiwa kwa wakati
ule, wakati sio ule na labda ungesubiri baadaye hivi). Wanasema ‘untimely’, kwa
sababu bado wasingependa kuachana na mpendwa wao kwa wakati ule; wanasema
‘untimely’ kwa sababu wanajua uchungu wa kuondokewa; na wanasema ‘untimely’ kwa
sababu kwa anayeondokewa hategemei tena kupata mbadala wake! Kwa kiasi fulani wako
sahihi, kwani yu wapi leo ‘Kaka Kleist’ mwengine? Marehemu ‘Kaka Kleist’,
alifariki dunia alfajiri ya kuamkia Jumatano, Novemba 22, mwaka huu, katika
Chumba cha Watu Wenye Kuhitaji Uangalizi Maalumu (ICU), pale katika spitali ya
Agakhan ya hapa Dar alikokuwa amelazwa jana yake.
Mara
baada ya kifo kutokea, dadake, Misky Sykes, ambaye alikesha kucha pale spitali
kufuatilia hali ya mgonjwa wake, akanipigia simu kunipa habari za msiba ule
mzito huku akilia na kuomboleza: “…Kaka Abdallah eh …nadhani Kaka Kleist
amefariki sasa hivi, naona madaktari na manesi wanahangaika pale… nafikiri
ametutoka kwani hawasemi kitu… Ooh! Ooh! Ooh!” alikatiza Misky mazungumzo na
kutoweka na kilio chake. Kleist alizikwa siku ya Alhamisi jioni katika makaburi
ya Kisutu, katika mazishi yaliyoongozwa na aliyepata kuwa Rais wa Tanzania,
Jakaya Mrisho Kikwete, Jaji Joseph Warioba na Jaji Mkuu (mstaafu) Mohammed
Chande Othman. Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein
Mwinyi, na Waziri wa Ujenzi na Miundombinu, Makame Mbarawa, ambaye ndiye aliyemwakilisha
Rais JPM. Alikuwapo pia Prof. Haruna Lipumba wa CUF, Mbunge Mussa Azzan Zungu
na Iddi Azzan zamani Mbunge pale Kinondoni, pamoja na mameya na madiwani
mbalimbali wa jiji hili la Dar es Salaam. Walikuwapo pia vijana wengi wa Dar es
Salaam wa kizamani ambao pengine wamesoma au kucheza pamoja na marehemu katika
maeneo mbalimbali ya jiji hili.Walikuwapo pia watoto wa marafiki wa Kleist
ambao waliongozana na wazee wao kuja kumsindikiza katika safari yake ya mwisho
mwana wa jiji mwenzao ambaye habari zake na ukarimu wake pengine walikuwa
wakisimuliwa na wazee wao kwenye sebule zao.
Jaji
Chande Othman, pamoja na kwamba alikuwa pale kwenye turubai lilowakinga
viongozi, sidhani kwamba moyoni mwake alikuwa akihisi kuwa pale alipo alikuwa
akihudhuria mazishi ya mtu wa kiserekali tu, kwani siku zile za utotoni kwake,
si tu alisoma pamoja na Kaka Kleist, lakini pia yeye pamoja na kakake mkubwa
Prof. Othman Chande, walikuwa kundi moja la Boys Scouts tawi la Saint Joseph’s
Convent School, Forodhani. Mohammed Chande na Kleist pia walisoma wakati mmoja
pale H.H. AgaKhan Secondary School (1964-1967).Hawa kina Chande wawili,
waliungana na vijana wengine wa pale Shule ya Mtakatifu Joseph, Forodhani
wakaunda kikundi cha vijana kilichojulikana kama The Scorpions, madhumuni yake
yakiwa ni kupendana, kusaidiana na kutembea pamoja pale inapobidi.
Scorpions
wengine waliokuwapo pale siku ile ni Hassan Ndumballo, Abdallah Mgambo, Abdul
Mtemvu, Wendo Mwapachu, Yusuf Zialor, Christopher Faraji, Kamili Mussa, Bhobby
Bokhari pamoja na mimi mwandishi wa makala haya. Nilimwona pia Mbunge Mussa
Azzan ‘Zungu’ pale makaburini. Zungu hakuwa anamwakilisha Spika Ndugai pale.
Kwa vyovyote vile alikuwapo kwa ajili ya kuwa amecheza na Kleist utotoni kwenye
mitaa ya Kariakoo na Gerezani ambako wote ndiko walikokulia. Mzee Warioba,
pamoja na nasaba yake ya Musoma, alikuwa mtu wa hapa mjini siku nyingi. Kabla
hata hajajiunga na Chuo Kikuu, pale Mlimani alikuwa akionekana akivinjari mitaa
ya New Street, Gerezani na Mission Kota, siku nyingi sana na hivyo akawa
amezoeana vilivyo na vijana wengi wa jiji hili akiwamo marehemu Kleist Sykes. Isitoshe,
mke wa Jaji Warioba ni mwenyeji wa Dar mwenye uhusiano wa karibu sana na kina
Sykes.
Mwingine
ni Mzee Kikwete. Huyu hakuwapo pale kumzika kada mwenziwe wa CCM tu. Kikwete
naye Dar es Salaam ni yake na vijana kama Kleist ni rika lake, hivyo
wakigongana hapa na pale kwenye kumbi za starehe na burudani hasa miziki ya ‘’Buggy,’’
na kwenye viwanja vya mpira. Kikwete alipotea njia kidogo akawa anapenda Yanga,
wakati Kleist ni Simba wa kutupwa. Mapema, katika nasaha zake kwa waombolezaji
mara baada ya sala ya jeneza pale Msikiti wa Maamur, Upanga, Imam Mkuu Sheikh
Issa aliwataka waumini kujiandaa na kile alichokiita ‘certainty of mortality,’
akiimaanisha kwamba kifo kimedhihiri na kwa hakika kitamfika kila mmoja; kwa hiyo
hapana budi watu kukifanyia maandalizi yake kabla. “Katika maisha yetu ni
vizuri basi watu wakakaa mbali na yale yote ambayo Allah (SW) ameyakataza na
kuyafanya kwa wingi (kuyakimbilia) yale ambayo Allah (SW) ameyaamrisha kwayo,”amesema
Sheikh Issa.
Sasa
wakati nikiyatafakari maneno yale adhimu ya msomi yule pale msikitini,
nilijihisi kama vile alikuwa akiniambia mimi au labda alikuwa akijua namna
marehemu alivyokuwa mtu wa kheri, hasa katika utoaji wa sadaka na mambo kama
hayo. Kaka Kleist, alipenda sana kusaidia wengine na wala hakusubiri kufuatwa
kwa shida ndiyo afanye hivyo. Kuna wakati unaweza kukutana naye tu iwe ofisini
au sehemu yeyote na ghafla atakurushia swali: “Vipi wewe uko vizuri mifukoni?” Kabla
hujajibu tayari atakuwa amekwishatoa pochi lake na kukuvurumushia pesa
ukafanyie jambo lolote. Kwa watu wazima na vikongwe hapo tena ndio usiseme.
Hivyo ndivyo alivyoishi katika jamii inayomzunguka na kwenye makundi ya
marafiki zake. Sasa wakati Sheikh Issa akitoa nasaha zile ikaja taswira fulani
hivi ya kwamba rafiki yangu yule, njia yake ya kuelekea kwa Mola wake ilikuwa
kwa kiasi fulani imesafishika tayari.
![]() |
Nyuma kulia ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete |
Siku
moja wakati ugonjwa umeshamtopea kwelikweli na figo hazipatikani, nilifika
kumwona pale kwake Mbezi Beach. Tulitazamana machoni na yeye akagundua kwamba
mimi nimehuzunika sana. Alinitazama na akaniambia: “Sikiliza we ‘timbwa’ wala
usihuzunike mimi tayari nimewasomesha watoto wangu wote vizuri sana …sina
kinyongo hata kama Mwenyezi Mungu atanichukua leo… niko tayari kwa
hilo,”alisema. Yale yalikuwa ni maneno mazito kuyasema mtu aliyekuwa kwenye
hali kama yake. Palepale nilijua ile ilikuwa ni kama ananiaga kiaina, kwani
tayari alikwishahisi dalili kuwa safari yake haiko mbali. Kamwe, hakuwa mtu wa
kukata tamaa kirahisi, kwani aliujua vizuri ugonjwa wa kisukari na madhara yake
ikafikia hata wakati mwengine kupendekeza tiba mwenyewe kwa madaktari wake. Katika
juhudi zake za kupambana na maradhi, marehemu kwa nyakati tofauti alikwenda
sehemu mbalimbali duniani kutafuta tiba. Juhudi za kila aina zilifanyika kupata
figo mbadala (transplants), lakini ilishindikana kwa sababu mbalimbali ikiwemo
ya umri mkubwa n.k. Na hapa napenda kumfariji shemeji yangu Stella Mallya
ambaye alijitolea sana kuhakikisha mume wake anapona kwa namna yeyote ile.
Kwa
upendo na hali ya kawaida, tulikuwa tukipenda kumwita ‘Kaka Kleist’, hata kwa
wale ambao hawakuwa wadogo zake wa damu. Sababu ni kwamba wadogo zake walikuwa
marafiki pia, na hivyo kwa kawaida huchanganyika na watu wengine kutembea na
kustarehe pamoja. Sasa, inakuja katika mazungumzo, majadiliano ya hoja au
kutaniana kwa aina yeyote, watu wengine walikuwa wakimwita Kleist kavukavu
hivihivi; wakati wadogoze (akiwamo Abraham, Ayoub, Mussa, Misky, Omar (sasa
marehemu), Adam (sasa marehemu), Ebby (sasa marehemu) ilikuwa inawashinda;
kwani kila mara ni lazima waanze na kitu ‘kaka’. Hivyo tamko ‘Kaka Kleist’ likawa
linaleta ladha fulani kulisikia; maana nduguze hawakumwita mtu mwengine yeyote
kaka zaidi ya Kleist, hata kama ni mkubwa kama huyo kaka yao. Wengine waliitwa
tu, kwa majina yao ya utani na mzaha (nicknames) kama kawaida.
Katika
miaka hiyo, mwandishi huyu, kwa marafiki zake alikuwa akipachikwa majina mengi
ya masikhara na utani kama vile ‘Nene’ au ‘Timbwa’, kutokana na wingi wa kilo
mwilini. Lakini kamwe sikusikia mtu akiniita ‘Kaka Nene’. Tamko hilo lilikuwa
ni makhsusi kwa marehemu Kleist peke yake. Sababu nyengine ya kuitwa kaka ni
kwamba, alikuwa ni mtu wa upatanishi na usuluhishi panapotokea sintofahamu
baina ya marafiki zake. Alikuwa na kipaji, uwezo na akili nyingi sana za kuweza
kuleta suluhu au ushawishi katika kujenga hoja kwenye vikao mbalimbali. Mambo
hayo ni miongoni mwa sifa zilizomfanya watu wamwite, ‘Kaka Kleist’.
Mara ya
kwanza kabisa kukutana na Kleist, ilikuwa pale kwenye Shule ya Aljamiatul-Islamiya
fi Tanganyika, mtaa wa New Street (sasa Lumumba) kwenye miaka ya 50s,
tulikopelekwa na wazee wetu kupata elimu ya dini ya Kiislamu. Hapa Kleist
alikuwa akijulikana sana maana shule haikuwa mbali na kwao. Pia waasisi wa
mwanzo wa taasisi ile pamoja na mchango mkubwa wa jengo zima ilikuwa kutoka kwa familia ya
Sykes, hasa babu Mzee Kleist Abdallah Sykes ambaye alijitolea hali na mali
kuhakikisha Uislamu na Waislamu hawaachwi nyuma. Walimu mashuhuri pale kwa siku
zile nakumbuka alikuwa Maalim Simba, Maalim Mataar, Maalim Adam Issa na Sheikh
Abdallah Iddi Chaurembo ndiye aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa taasisi ile. Palikuwepo
pia na walimu wanawake kama vile mwalimu Sakina Arab na mwalimu Tahia.
Namkumbuka huyu mwalimu Tahia kwa sababu alikuwa pia ni mke wa Mzee Juma
Mwinyimkuu rafiki mkubwa wa marehemu babangu wakicheza mpira pamoja timu ya
Morning Star iliyokuwa timu ya pili ya Sunderland wakati huo (sasa Simba).
Mwalimu Sakina yeye alikuwa ni mwanamke mmoja maarufu sana katika harakati za
wanawake hapa kwetu, kwani alifikia hadhi ya kuwa na kiti cha kudumu cha
udiwani katika Manispaa ya Dar es Salaam siku hizo za ukoloni wa Kingereza. Habari
za Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ni ndefu mno na mchango wa Mzee Sykes
pamoja na watoto wake Abdul, Ally na Abbas katika jamii ya Kiislamu na ukombozi
wa nchi hii kwa ujumla, zimeelezwa kwa kina na mwanahistoria maarufu nchini ndugu
yangu Sheikh Mohammed Said, katika kitabu chake mashuhuri, “The Life and Times
of Abdulwahid Sykes 1968 The Untold Story of the Muslim Struggle Against British
Colonialism in Tanganyika,’’ kinachosambazwa na Ibn Hazm Media Centre ya Dar es
Salaam. Ndani ya kitabu hicho, Mohammed ameuelezea mchango mkubwa wa familia ya
Sykes katika kuanzisha chama cha TAA kabla ya TANU na namna walivyoweza
kupambana na Waingereza kwa namna mbalimbali mpaka pale uhuru ukapatikana. Msomaji
ikutoshe tu kusema hata pale TANU ilipoanzishwa, akina Sykes walikuwa na kadi
namba za mwanzo mwanzo kabisa ambazo zilibuniwa na kugharimiwa na Mzee Ally
Sykes (sasa marehemu).
Rafiki
yangu, marehemu ‘Kaka Kleist, alizaliwa jijini Dar-es-Salaam miaka 68 iliyopita
akiwa mtoto wa pili kwa baba Abdulwahid na mama Mwamvua Mrisho Mashu (maarufu
mama Daisy). Watoto wengine ni dada Aisha-Daisy Buruku, ambaye alizaliwa mwanzo
kabla ya Kleist, wakafuatia Adam na Omar ambao tayari wameshatangulia mbele ya
haki. Adam alikufa yapata nusu mwaka sasa. Anao pia nduguze wa mama mwengine,
kwa sababu mzee Abdulwahid alioa mara tatu. Huku utamkuta Ebby (sasa marehemu),
Elyassar (anayeishi Canada) na wanawake Misky na Mariamu (sasa marehemu). Hakukuwa
na mtoto yoyote kutoka kwa yule mke wa tatu ambaye alikuwa naye baada ya kuwa
ameshaachana na mama Daisy na mama Ebby.
Baada
ya kupata elimu ya dini pale Aljamiatul, ‘kaka’ Kleist, kama ilivyokuwa kwa
kina Sykes wote wakati huo, alijiunga na shule ya H.H. The Aga Khan (sasa
Tambaza High School na Muhimbili primary) pale Upanga Dar es Salaam, shule ambazo
zilikuwa mahsusi kwa watoto wa jamii ya Kihindi wakati huo wa elimu ya kibaguzi
ya utawala wa Kiingereza. Kina Sykes, walipata hadhi hiyo nadra wakati huo,
kutokana na heshima kubwa iliyokuwa imepewa familia yao kwa sababu ya mchango
wa Babu Mzee Sykes katika jamii. Na kwa heshima hiyo hiyo Mzee Abdulwahid Sykes
(babake ‘kaka’ Kleist) aliingizwa katika Bodi ya Aga Khan Schools, na kwa hivyo
ikawa ni rahisi ‘ujiko’ kwa kina Sykes wote kupata elimu pale. Kaka Kleist,
alisoma pale kuanzia chekechea mpaka Form IV alipomaliza mwaka 1967. Baadaye
akachaguliwa kujiunga na Chuo cha Kilimo kule Ukiriguru, Mwanza. Kufuatia kifo
cha ghafla cha marehemu babake, mnamo mwaka 1968, kijana Kleist Sykes, ilibidi
akatize masomo yake Mwanza na kusafiri kwenda kwa babake mdogo Abbas Sykes aliyekuwa
Balozi wa Tanzania kule Canada kwa ajili ya malezi na masomo mapya.
Nakumbuka
kama vile jana, nikiwa bado kijana mdogo nilihudhuria mazishi ya mzee Abdul
pale mtaa wa Lindi, Gerezani, jijini yaliyofurika watu wengi— wengi kwelikweli—
akiwemo Mwalimu Julius Nyerere, rais wa kwanza wa taifa hili. Tofauti na marais
Kikwete, Mwinyi na Mkapa, katika uongozi wake, Mwalimu hakuhudhuria mazishini
mara kwa mara. Ukiacha mazishi haya, mazishi mengine aliyohudhuria Mwalimu ni
ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, aliyekuwa waziri wake wa Sheria na Katiba wakati
huo, aliyefia nchini Ujerumani mwanzoni mwa miaka ya 1960s na mwili kuletwa
nyumbani kwa mazishi, akiwa kiongozi wa kwanza mwandamizi kufariki akiwa
kazini. Alishiriki pia mazishi ya makamu wake wa rais Abeid Amani Karume kule
Zanzibar na yale ya waziri wake mkuu Edward Moringe Sokoine, kule Monduli Juu,
Arusha.
Katika
mazishi ya Mzee Abdul Sykes, mwandishi huyu, alimshuhudia Nyerere akiwa kwenye
majamvi pale mtaani Lindi na baadaye kulisindikiza nyuma jeneza mpaka Msikiti
wa Ijumaa, Kitumbini. Katika hali isiyo ya kawaida, Nyerere alisubiri nje mwili
uswaliwe swala ya jeneza na ulipotoka, aliusindikiza kwa miguu mpaka makaburini
Kisutu pasi na kutaka asaidiwe usafiri. Kufuatia kifo kile, serikali ya Nyerere
ilitangaza kujitwika mzigo wa kuwasomesha na kuwaangalia watoto wa marehemu
rafiki yake yule, ambaye ndiye aliyempokea katika harakati za kugombania uhuru
wetu akawa anakula na kulala kwake baada ya kuacha kazi ya ualimu Pugu ili
ajiunge na harakati za kudai uhuru.
Katika
maisha yake ya kule Canada, Kleist alihitimu shahada yake ya kwanza na ya pili (uzamili) kwenye masuala ya Ustawi wa
Jamii. Aliweza pia kupata ajira kwenye taasisi iliyojulikana kama Canadian
University Students Organisation (CUSO). Kazi kubwa za shirika hilo ni kama
lile la kule Marekani la American Peace Corps, lenye malengo na madhumuni ya
kutoa misaada ya kimaendeleo kwa nchi changa duniani. Sasa baada ya miaka kadhaa pale kazini,
nafasi ikatokea ya kuja kuwa Mkurugenzi (Director of CUSO –Tanzania). Wakati
huo Kleist alikuwa tayari ameoa kulekule Canada na kubahatika kupata mtoto wake
wa kwanza Latifa. Kwa sababu ambazo hazikuelezwa, mamake Latifa alikataa
katukatu kuongozana na mumewe kuja Tanzania, akihofia labda pengine wasingerudi
tena Canada. Kwa mapenzi ya nchi yake na nduguze, Kleist aliondoka akaja yeye
akiwa amembeba mtoto wake mdogo Latifa, wakati huo akiwa na umri takriban miaka
mitatu hivi. Kwa kweli ilikuwa ni nderemo na hoi hoi kwenye ukoo wa Sykes kwa
ujio wa Latifa. Bibi yake, marehemu mama Daisy, alishereheka sana kupata mjukuu
yule kwa mtoto wake wa kiume. Latifa alikuwa juu juu—mara Upanga, mara Temeke,
mara Mbezi Beach kwa babu Ally Sykes.
Mamake
hayati Kleist Bi. Mwamvua Mrisho Mashu, alikuwa ni mwanaharakati mkuu wa
masuala yanayohusu maendeleo ya wanawake hapa nchini. Katika uhai wake anatajwa
kwamba alikuwa ni mmoja wa waasisi wakuu wa Chama Cha Wazazi nchi (TAPA), siku
nyingi kabla uhuru wa nchi haujapatikana. Bi. Mwamvua anatajwa pia mmoja wa
watu walioshirikiana kwa karibu na kina Bibi Titi kuanzisha UWT, ambako yeye
alidumu kuwa mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi kirefu akishinda
chaguzi mbalimbali. Mama Daisy pia alikuwa Mwenyekiti wa TANU/CCM tawi la
Miburani pale Wailes, Temeke kwa miaka kadhaa. Mwandishi huyu mara nyingi
alimshuhudia Kleist akiwa na mamake wakipanga na kupangua mipango ya siasa,
hasa zile zilizomhusu Kleist, kwani Bi. Mwamvua alikuwa na hazina kubwa ya
uongozi wa nchi hii kichwani mwake kutokana na kule kuwa mke wa Mzee Abdul
Sykes. Bila shaka yeyote ile, nguvu kubwa na uwezo aliokuwanao Kleist ulitokana
na maelekezo na mafunzo kutoka nyumbani kwa mama yake baada ya kuwa babake
aliaga dunia mapema.
![]() |
Kushoto: Mama Daiy mbele kulia Bi. Titi Mohamed |
Sasa, mnamo
miaka ya 1970 mwishoni, ili kuziba ombwe la kukosekana mama wa kumlea mtoto
Latifa, Kleist aliamua kumchumbia Stella Mallya aliyekuwa akiishi jirani na
nyumbani kwake pale mbele ya Shule ya Tambaza. Mzee Mallya ambaye ndiye baba wa
bibi harusi hakuwa ameridhia kabisa binti yake kuolewa nje ya Uchagani kwao
Moshi. Baada ya tafakuri ndefu, wawili
wale, bwana na bibi harusi wakaamua kuwa ndoa lazima ifungwe ‘iwe jua iwe
mvua’, itakiwe isitakiwe. Ndoa ikafungwa kwa siri kwa DC pale Ilala na hapakuwa
na sherehe wala mialiko yeyote. Mimi nikawa ndiyo mpambe ‘best man’ wa Bwana
harusi, wakati Bi Bernadetta Majebelle akawa mpambe wa Bibi harusi. Baada ya
shughuli ile pale bomani, tuliondoka mahala pale tukaenda peke yetu maeneo
fulani kule Sea View tukajipongeza kwa vinywaji na vyakula kidogo mpaka usiku
ulipoingia tukaagana.
Siku
kadhaa baadaye, na kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo kwa binti yake, mzee
Mallya alirudi matawi ya chini akawa tayari kumpokea tena binti yake.
Aliwatembelea nyumbani pale Upanga akakaribishwa kwa vyakula na vinywaji, ambapo
mwandishi huyu alimshuhudia Mzee Mallya akiwa mwenye furaha kwelikweli baada ya
kuwa amepata ‘kinywaji moto’ na ‘kinywaji baridi’. Ndoa ile imedumu kwa miongo zaidi
ya mitatu na ikaajaliwa kupata watoto watatu ambao ni watu wazima sasa; Aisha,
Abdulwahid, Ally na Latifa akawa dada yao mkubwa.
Uzoefu,
uaminifu na utumishi uliotukuka pale CUSO, ulimpatia sifa Kleist za kuchaguliwa
kujiunga na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambapo
alifanya kazi kule Geneva, Switzerland na Zambia kama mwakilishi mkazi. Baada
ya kuwa ametumikia UNHCR muda mrefu, ‘Kaka Kleist’ alirejea nyumbani na
kujikita kwenye biashara mbalimbali ikiwemo kuanzisha kampuni yake ya kuhudumia
meli iitwayo Prevention and Indemnity (P&I), ofisi zake mpaka leo zikiwapo
pale mtaa wa Mkwepu jijini Dar es Salaam.
Kwa
kutumia uzoefu wake wa biashara, utawala na nidhamu ya kazi, na kwa ushawishi
mkubwa kutoka kwa marafiki zake wa utotoni (akina Yusuf Zialor na Wendo
Mwapachu), ambao nao ni mabingwa katika masuala ya biashara, wakaanzisha
kampuni iliyojulikana kama Business Center International (BCI) iliyokuwa na
ofisi zake pale kwenye jumba la Bushtracker kwenye makutano ya Bibi Titi na Ali
Hassan Mwinyi. Marafiki wengine waliokuwa
pamoja utotoni kwenye kundi la Scorpions ndio waliokuwa maofisa mbalimbali pale
Bushtracker. Alikuwapo dada Mariam Zialor, Abdul Mtemvu, Booby Bhokari, Hassan
Ndumballo, Abdallah Mgambo na Ramadhani Madabida. Business Center International
(BCI) ilikuwa na kampuni tanzu kadha wa kadha ikiwamo ofisi mashuhuri ya safari
za ndege ya KEARSLEY LTD pale Barabara ya Samora jijini na kiwanda kikubwa cha
uchapishaji cha PRINTFAST kule Nyerere Road.
Kwenye
jamii, Kleist alikuwa mwanachama mwandamizi wa Klabu maarufu ya Saigon ya Dar
es Salaam, kama ilivyokuwa kwa wanafamilia wengine wa ukoo wa Sykes. Michango
ya kina Sykes kwenye klabu hii haisemeki—wako mstari wa mbele kila pale
wanapohitajika.
Kila
mmoja aliwashuhudia vijana kutoka klabu ya Saigon walivyokuwa mstari wa mbele
siku ya maziko kuanzia uhudumu wa chakula kwa wageni pale nyumbani mpaka makaburini
Kisutu, kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawasawa kwenye mazishi ya mpendwa
wao. Alikuwa mwanachama pia wa klabu mashuhuri ya viongozi pale Leaders Club, iliyoko
mbele ya Klabu ya Usiku ya Bilicanas, kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Mwanachama
mwandamizi kutoka Leaders Club, Zainul Dossa, ndiye aliyeratibu shughuli zote
za mazishi ya Kleist kuanzia chakula nyumbani mpaka makaburini Kisutu
akihakikisha kila kitu kimekwenda kama kilivyopangwa.
Katika
upande wa siasa, marehemu Kaka Kleist alikuwa kada mzuri wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) akifuata nyayo za familia yake katika harakati za siasa. Alipata kuwa
mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama chake chini ya uongozi wa Jakaya
Mrisho Kikwete. Akiwa diwani wa Kata ya Kivukoni, marehemu Kleist aligombania
na kuchaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwenye miaka ya 1990,
na moja ya mafanikio makubwa ambayo amekufa akijivunia ni kuweza kutatua tatizo
la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, kwa kubuni na kusimamia mradi mkubwa
wa Usafiri wa Mabasi ya Mwendo Kasi (Dar Rapid Transit). Aliweza kuwashawisha
maofisa wa Benki ya Dunia, akiwamo rais wake, ambao awali walikuwa wamepanga
kupeleka mradi ule kwenye moja ya nchi za kule Afrika Magharibi, kubadili
mawazo na kuleta mradi ule mkubwa hapa kwetu, mradi ambao umeiweka Tanzania
katika ramani ya dunia kwa kuwa na mradi mkubwa ambao, si tu utakidhi haja,
lakini pia imekuwa ni fursa nyingine kwenye ajira na hivyo kupeleka mbele
maendeleo ya nchi kwa jumla. Wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali ulimwengu
wamekuwa wakimiminika kuja kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa kwenye hili.
Akizungumza kabla jeneza la marehemu Kleist Sykes halijaondoka nyumbani kwa
ajili ya kwenda kuzikwa, mwakilishi aliyetumwa na shirika la UDART, ambalo
ndilo linatoa huduma za mabasi ya mwendo kasi jijini, alisema daima marehemu
atakumbukwa kwa kubuni, kupanga na kukamilisha
hatua zote za utekelezaji wa miradi yote sita ya mpango mzima wa mabasi
ya mwendo kasi.“...mpaka sasa tayari phase moja tu imekamilika yaani kutoka
Kivukoni mpaka Kimara na kwamba mradi mzima una phase 6 ikiwamo Kariakoo –
Mbagala; Morocco—Tegetta; na Kariakoo—Gongo la Mboto,...pale phase zote
zitakapomalizika nchi itakuwa imepiga hatua kubwa …” amesema.
Mpaka
umauti unamfika, marehemu Kleist, alikuwa amewekeza nguvu zake kwenye biashara
ya kilimo cha mkonge kwani tayari alishanunua mashamba makubwa kule Kibaranga,
wilayani Muheza, akiongozwa kitaalamu na mtaalamu bobezi wa Kilimo cha Mkonge nchini,
Abdallah Mussa Kamili. Kwenye kazi hiyo, tayari alikuwa akishirikiana kwa
karibu na wanawe katika uendeshaji na utawala wa shughuli hiyo. Sidhani kama
kutatokea ugumu wowote, maana katika kipindi kirefu ambacho amekuwa akiugua ni
watoto haohao ndio waliokuwa wakifanya shughuli hizo. InshaAllah kwa uwezo wa
Mungu watajiunga pamoja na mama yao kumalizia pale ambapo baba amekomea.
![]() |
Sheikh Abdallah Awadh alipata kumbeba Kleist akiwa mtoto akisoma dua kwenye kaburi |
INNA LILLAH WAINA ILLAYHI
RAJIUUN
simu: 0715808864
No comments:
Post a Comment