Wednesday 10 January 2018

YALIYOJITOKEZA SIKU CHACHE KABLA YA MAPINDUZI NA HAMZAH RIJAL





Kulikuwa na ukumbi ukiitwa ZANZINET nilikuwa mwanachama wa ukumbi huo ambao ulikusanya Wazanzibari waliokuwepo Zanzibar na waliokuwa nje ya Zanzibar, humo watu wakijadili maudhui mbalimbali yawe ya Dini, Kisiasa, Jamii na mengineo. Kulikuwa a wachangiaji mahiri kina Al Marhoum Ali Baucha, Dr. Amour, Houd Houd na wengineo. Mie Pangu Pakavu nilikuwemo humo na nikichangia baadhi ya nyakati.

Mwaka wa 2009 Dr. Amour aliandika kutoka tarehe 11 hadi 12 January 1964 alioyakumbuka na mie nikaona niseme yangu lakini kwa jazanda nyengineo, nimeyagundua leo katika pekura zangu huku na kule.

ASALAMA ALAYKUM!

Utangulizi

Nilipoandika Nakumbuka Miaka 45 iliyopita fikra ilinijia pale nilipokuwa nimekaa bure sina la kufanya sina wakuzungumza naye na kitabu nilichokuwa nakiosma cha Baraka Obama The Audacity of Hope nishakimaliza, basi hapo afkar zikawa zinazunguka magenzi yangu yanakumbuka nyuma ikiwa huku nishatembelea maeneo mbalimbali ambayo wakati mzee alipokuwa hai tukipita na kuwatembelea marafiki na hata wale aliokuwa akiwadai.

Niliyoandika yalikuwa ni juu ya mimi na wakati huo wala sijataka kuandika yale ambayo yalikuwa ni mengi mno yaliokizunguka kitandawili kizima cha Mapinduzi kwani hayo yanaandikwa kila kukicha kwa kila aina ya kalamu, nikimaanisha vile muandishi apendavyo kuandika juu ya suala hili.

Bahati Dr. Amour ameleta yale ambayo anayakumbuka kuelekea January 12, 1964. Dr. Amour kenda mbali mno kwa zile kumbukumbu na mie kanielimisha mengi katika uandishi wake, kwani siku zote hutakiwa tuwe tumo kwenye kujifunza “Elimu kuanzia kwenye kitanda cha mbeleko hadi uingiapo kaburini,” hutakiwa tuwe tunaendelea kujifunza na kusoma isiwe yale ya Rabi wa Kiyahudi aliposema maneno haya katika mwaka wa 1949:

Wasilamu Hawasomi;

Wakisoma hawafahamu;

Wakifahamu Hawatekelezi.

Hayo ni matusi tena yenye kuamsha hisia (Kutoachangamoto) tuwe sio hivyo huyo Mwanakharashi alivyosema.

Dr. Amour anazitaja Jezi ambazo Malindi wakivaa miaka ya 40 hadi 70 ambazo kwasasa zinavaliwa na Team ya Premiership ya Uiengereza Stoke City. Wenyewe Malindi wakizita Bakora, wakizivaa hizo hatoki mtu, mie nilipojiunga na Malindi na kuchezea First Division katika mwaka wa 1970 tukizivaa hizo lakini sio kwa kila mchezo na hakika tukizivaa alikuwa hatoki mtu. Katika michezo ya kawaida sare tuliyokuwa tukiivaa ni ya kijani na mikononi na ukosini ilikuwa na rangi ya njano na sare nyengine ilikuwa ya buluu ya bahari.

Nakumbuka mchezo mmoja tukicheza na Abaluhya ya Kenya baadaye ikaja kuitwa Leopards akiwemo Angana mchezaji mahiri ambaye kwasasa namfananisha na Michael Essein wa Ghana na Chelsea huyu ingekuwa anaishi nyakati hizi basi pakuchezea kunakomnasibu ni Real Madrid, AC Milan au Man Utd.

Leopards ilikuwa haifungiki na sisi tulipocheza nao watu wakiamini kuwa tutalala tena sio chini ya mabao 5, hatutoka chini ya mabao hayo, lakini mwalimu wetu Al-Marhum Seif Rashid alitufundisha mbinu za kuweza kukabiliana na team hiyo kubwa na tukaweza kuwazuia. Marehemu Seif Rashid alikuwa hodari kwa kupanga mbinu.

List yetu siku hiyo ilikuwa 1. Amiri 2. Hamza Zubeir/Abdalla Mwanya 3. Ali Fereji 4. Mzee Boti 5. Mustapha Kassim 6. Mohammed Magram 7. Mohammed Issa 8. Mansab Abubakar 9. Seif Mohd (Tornado) 10. Ahmeid Baba 11. Farouk. Tulivaa bakora ndani ya dakika 15 Ali Fereji alifanya kama anarejesha Mpira kwa Amiri, asiurejeshe halafu akaurejesha bila ya kutizama hapo tena Angana akaufumania mpira na kuweka bao. Baada ya bao hilo Mpira ulipelekwa Center na alianza Seif Tornado akampasia Baba, Baba akampa Mansab, hapo tena Mansab akapiga krosi ikamkuta Mohd Issa akakimbia nao sehemu ya Winga ya kulia akamimina krosi iliyomkuta Tornado na hapo Tornado akapiga mkwaju wa hali ya juuu na bao kusawazisha hapo hapo baada ya kufungwa, mchezo ulimalizikia 1-1 yaliofikiriwa hayajawa.

Bakora ikivaliwa ilikuwa hatoki mtu, kutoka zama za kina Kassim bin Mussa, Saidi Nyanya, Issa Juma, Boti Senior, Ramadhan Saleh, Khalid Keis, Mohd Kassim, Seif Rashid, Zaghalouli, kina Abdimout, Ahmed Ajmy, Mzee Boti, Saad, Bahbeish, Murtaza, hadi kina Mansab, Muniri beki papua niliyokuja kumrithi, Mohd Issa, Mohd Magram na Omar Magram na Hamza. Bakora ikivaliwa huwa hutoki.

Dr. Amour saa nyengine mtu akikumbuka hulia, sawa na Marehemu Bwamkubwa Bata Shoes alipokuwa anatajiwa Marehemu Islanders, alikuwa hastahamili huangua kilio, akimkumbuka Babu Ahmada, Taimuri, Marehemu Shioni Mzee, Mamdad, Marehemu Shebe na Clarinet yake na wengineo, na mie kwa kweli nasema Dr. Amour umeniliza kuitaja Bakora aaahhh, aaaah, aaaaaaah.

Kwa Dr. Omar Juma ambaye ambaye namletea nakumbuka zama hizo ambazo nilikwenda kupumzika Pemba skuli zimefungwa yeye alikuwa katika wanafunzi wa mwanzo wa Syd Abdalla Secondary School, akiwa na kina Dr. Ali Tarab, Miskir, mwenzao Head Prefect wakimwita Father, Nasim ambaye anakuja kuolewa na Dr. Jaffar Tejani, Dr. Omar ikiwa jina nimepopoa nirekebishe na wengi wengineo.

Dr. Omar amekuja na Wajiwaji ambayo ameona kwa upana na kwa upande wake. Palipokuwa na palipo lazima kuwe na mabadiliko, sawa namti huanzia mbegu ukaja mche na kisha ukaja mti na kisiki na mzizi wake, lakini vipi huo mti unapokua hakika unakua kupitia njia mbalimbali hapo ndipo pakujiuliza. Mti wenye kushughulikiwa hukuwa haraka na kutoa matawi na matunda mazuri makubwa-makubwa, naule uwachiwao na ukuwe bila kushughulikiwa basi usitegemee kupata matunda mazuri na hata mara nyengine hufikia kufa, sasa kwa mantiki hiyo ndio nililokuwa nalizungumzia kwa kuwa nipo nyuma ya pazia nakuuzunguka mbuyu au nuite kama mzee wangu alioita Mbuu siko wazi.

Hood hood anauliza verejee ikawa bakora nikaita mchapo au upupu nikauita muwasho? Hood hood ameyataka mambo yawekwe ben ben lakini mie nimekuwa nikitambaa sijapiga chubwi itategemea wengineo ambao wanaweza wakazamia kwa kupiga chubwi lakini isiyokuwa “Aaaah, Chubwi, Ndani? Aaaah, Chubwi, Ndani? Katumbukia aaah, katumbukia aaaah, Aaaaah Chubwi Ndani, Aaaah Chubwi Ndani.”

Ya Jana

“Mla Mla Leo, Mla Jana Kalani, Muulize Jirani,” Wala sio uwongo lakini wengine wanasema “Mla Mla Jana, Mla Leo Hajala Kitu,” kwani wengine huona “Mla Jana ni Mithili ya Chungu aliona Ganda la Mua la Jana ni Kivuno.” Watrib wa Malindi wameimba “Ganda la Mua la Jana Chungu kaona kivuno, aaah, kwa Mbwembwe na Kujivuna........”  Sasa Jee ni Jana au leo?

Naiwe itavyokuwa kwenye kula na kwenye jana kuna raha zake na wale ambao ukiwapeleka jana hustaladha koliko ukawaweka kwenye leo, yaani ukiwapeleka zamani wao huona ndiko na ukiwaweka sasa huwachafua na kukirihika khasa wakaazi wa Zimbabwe au kuleeee.

Jana ni Jana na Leo ni Leo iwe itavyokuwa, Jana ikipotea ikaja leo huwa haiji tena lakini ipi jana na ipi leo? Vyote hivi hukimbia na kutoweka na kuja kama leo na jana lakini sio leo iliyopita na jana iliyopita (You can’t turn the clock back-V. I. Lenin.)

Jana asubuhi, jana ilikuwa Ijumamosi nilielekea Marikiti kujinunlia mahitaji yangu ya wiki na huku afkar za miaka 45 iliyopita inanizonga baada yakusoma mails za wenzangu kuhusu hili. Napita soko la Mboga nakutana na Mzee Abdalla Habeish huyu mzee ni hazina mie nikikutana nae hupenda kumuuliza yaliopita nayeye huwa simchoyo na hakosi kunitupia chochote kile.

Kama kawaida yangu nilimtupia suala juu ya miaka 45 iliyopita kuanzia 10 December 1963 hadi January 12 1964 anakumbuka nini? Alinijibu kuwa anakumbuka mengi lakini yanataka wasaa nikae naye kuzungumza ikiwa wakati huo anaelekea kazini Masomo Bookshop. Juu ya hayo akanambia bora nikupe moja nalo “Tarehe 4 January 1964, napita Vikokotoni nakuta Umma wa watu nilipoingia kati kuyasafi mambo niliambiwa Ofisi za Umma Party zilifungwa rasmi siku hiyo.” Alisitia hapo na mie kuanza kujiuliza mengi, kwanini zilifungwa? Wao hao Umma Pary idadi yao ilikuwa haizidi watu 3,000 wakitisha kitu gani? Nikawa najiambia kuwa kulikuwa kunanukia kitu ambacho kilijificha mficho wa mbuni, ingawa kitu hicho kilikuwa kimejificha lakini kilikuwa kipo wazi.

Angalia kila mtu alikuwa na dhana kuwa kuna kitu kitatokea kwanini kikawachwa kitokee? Labda kilikuwa kimeandikwa kitoke kwayo kulikuwa hakuna nguvu ya kukizuwia. Au matokeo yaliokuwa yakingojewa yalikuwa maridhawa, Dr. Harith yuwasemaje?

Bwana Ali ni mzee rafiki wa familia yangu na kaja kuwa rafiki yangu mkubwa nazungumza naye sana na huyu mzee bingwa wa kukisarifu Kiswahili basi aliniambia kuwa kwenye tarehe 10 January 1964 alipita kwenye moja ya Makao ya ASP hapo Kijangwani akamsalim Mzee Faraji ambaye alikuwa rafiki yake, jawabu ya Mzee Faraji badala yakuitikia salamu alimjibu “Siku zenu zinahesabika, mtakiona,” Bwana Ali alimjibu “Mashudu,” hii inanijia kama al-Marhum Ali Muhsin alivyosema kwenye kumbukumbu za BBC za miaka 50 iliyopita alipoulizwa kuwa jamaa watazuia Uhuru usiwe-ndivyo wasemavyo, jawabu yake ilikuwa “Labda wanaota,” hapa mie kunanipa mtihani, aaah kwanini kulikuwa na dharau? Doto ni doto lakini ndoto huja zikawa ni yaliootwa yakawa ni kweli.

Nikiendelea na Bwan Ali aliniambia kuwa kila akikutana na Mzee Faraji akimkariria kwa uhakika kuwa wakati wao umekwsiha na watakiona.

Mzee wangu Zubeir Rijal akipenda kuweka kumbukumbu juzi katika kuchungulia moja yaFile naikuta barua ya mwanafunzi wake Dr. Zamil Suleiman  Al-Alawy amabye akimtaka mzee awe Referee wake na mzee kishampelekea hiyo barua na Dr. Zamil anamjibu natoa sehemu ya barua hiyo nayo ambayo ameiweka kwa kumbukumbu:

Dear Mr Rijal,

Thank you very much for your letter and the letter of recommendation in 6 copies. I do hope that the authorities concerned with Common Wealth Scholarship will not suspect your extravagancy in praising me. Believe me I do not possess even half the qualities mentioned in your letter of recommendation.     

I think I am not quite sure that the political tension in Zanzibar is over and things run smoothly. But to be frank, I do not know that people of Zanzibar will accept the new form of government as mentioned in your letter to me without any opposition.

You’re faithfully
Zamil Suleiman Al-Alawy

Dr. Zamil yupo Ulaya na khofu inamjia hapa nikitandawili kikubwa nataka nikionana naye nikenda Mrima au akija Unguja nijadiliane naye Dr. Zamil nimuulize juu ya hisia hizo alizokuwa nazo zilitokea wapi?

Nazungumza na Maalim M. Maalim ananiambia kuwa kwenye mwezi wa December kueleka January 1964 kulikuwa kumegubikwa juu ya kitu cha khatari kitatokea, vipi na lini hawakujua. Marehemu Nabwa moja ya makala yake alikwenda kwa undani juu ya Mapinduzi yalivyokwenda labda aambiwa Virus 99 apekue pekue atafute makala ya Nabwa juu ya Mapinduzi tuipate kuisoma hapo tena ndipo Hood hood alipopatafuta atapadasa.

Najiuliza na kujiuliza Inspector Aboud Saidi kipi kilichompelekea amwambie mzee wangu kuwa tukisikia fujo tuondoke Vitongoje tuje mjini? Kulikuwa na jambo ambalo lilikuwa ndani ya nafsi za watu lakini hakuna aliyofahamu kuwa ni jambo gani na mwisho jambo lilikuwa nalo ni MAPINDUZI Tarehe 12 January 1964.

Nakuachia hapo nitaendelea na kumbukumbu hizi kila akili itavyokuwa inanipeleka ndani ya kitandawili hichi kilichojificha hadi leo na kila mweledi kuelezea vyake.

Nakumbuka Miaka 45 Iliyopita.
Ngaridjo Onana
Ben Rijal

No comments: