Monday 15 January 2018

YERICKO NYERERE NA HISTORIA YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR YA 1964


Take time to READ
Anaandika mkulima wa bamia. #YerickoNyerere
Tusipoandika historia yetu tusilaumu tukiandikiwa, Mapinduzi ya Zanzibar 1964.

...................................................................
Taifa la Zanzibar limekulia na kudumaa katika uongo, ulaghai, ghiriba, vitisho na mauaji kwa zaidi ya nusu karne. Vizazi vimelishwa uongo wa uhalisia wa mapinduzi, Sababu za Mapinduzi na wanamapinduzi halisi wa Zanzibar bila sababu za msingi, lakini kwa maslahi ya watawala wa Zanzibar kwa msaada wa watawala wa Tanganyika leo Tanzania.

Ifahamike na kueleweka kuwa bendera ya Taifa huru la Zanzibar ilipeperushwa tarehe 12 Disemba 1963. Na huu ndio uhalisia wa uhuru wa Zanzibar nje ya mapinduzi ya John Okello na Julius Nyerere na kisha Sheikh Abeid Karume kuvishwa taji la ushindi wa mezani chini ya mkono wa Julius Nyerere.

Wanamapinduzi halisi wametupwa, hawatajwi wala kukumbukwa popote na zaidi wengi wamefutwa usoni padunia. Wamevishwa wengine taji la mapinduzi ilihali hawakujua hata kilichotokea usiku wa tarehe 12 Januari 1964. Karume huyu Abeid hakujua hata mapinduzi hayo yaliandaliweje na nini kilitokea bali aliyajua mapinduzi yao (ASP) yaliyokuwa yakiratibiwa Dar es Salaam huku Mwalimu akiwalaghai kuwa yupo nao ilihali nyuma ya pazia alikuwa kiungo muhimu wa John Okello kupitia njia ya Kipumbwi kule Tanga. Ilikuwa ni mbinu ya kijasusi na Mwalimu alifanikiwa sana, ilikuwa ni lazima atumie njia hii ili Jumuiya za kimataifa na wana ASP wasitambue kuwa ni uvamizi wa kiinchi bali mapinduzi ya wazawa.

Lakini ukweli unaanzia kwenye kundi la watu 300 waliokitwaa kisiwa cha Unguja wakiongozwa na mtu asiyekuwa maarufu kipindi hicho, aliyekuwa akiitwa John Okello, John Okello alikuwa wakala maalumu wa Tawi Maalumu (TISS ya leo) na akiishi Pemba ambako alitokea Uganda miaka michache tu. Ndani ya Zanzibar Okello alipata umaarufu kwa vijana majabali, ambao wengi katika wao walikuwa ni makuli na wachukuzi wa meli zilizoingia na kutoka bandarini Zanzibar, kundi lake hili John Okello lilikutana kwa siri. Okello aliwapa matumaini ya mabadiliko watu wake hawa, wafuasi, ambao wakifanya kazi pamoja kwa muda mrefu, mara nyingine katika mazingira ya hatari, na tayari kufuata amri za kiongozi yeyote ambaye ataweza kuwalipa. Wao walikuwa waasi wanaotafuta makazi.

Mchafuko wa kisiasa ulikuwa ukiongezeka ndani ya Zanzibar na Pemba tangu kifo cha Sultani Khalifa katika mwaka 1960. Sultani Khalifa alitawala Zanzibar kwa karibu ya miaka 50, tangu mwaka 1911. Baada ya udanganyifu mkubwa kwa majimbo ya uchaguzi na mseto katika chaguzi kuu mbili za mwaka 1961 vyama vikuu vilishindwa kujipatia wingi wa kura kwa kila kimoja.

Waingereza waliondosha majeshi yao kikiwemo kikosi maalumu cha Kiarishi ambacho kilikuwa kimewekwa karibu na uwanja wa gofu na mpaka wa mji Mkongwe mapema mwaka 1963. Wakati mfalme mpya, Jemshid akipandisha bendera ya Taifa huru la Zanzibar tarehe 12 Desemba 1963, aliadhimisha uondokaji wa Gavana wa kiingereza Zanzibar na mwisho wa ukoloni Zanzibar.

Uchaguzi mwingine uliofanyika mwishoni mwa mwaka 1963 ukiipa ush…Uchaguzi mwingine uliofanyika mwishoni mwa mwaka 1963 ukiipa ushindi mdogo wa kura Muungano wa vyama viwili ZNP na (chama cha kizalendo Zanzibar) na ZPPP (Chama cha watu wa Pemba na Unguja). A.S.P (Chama cha Afro shirazi) kilikuwa kiwe kipo katika Serikali iliyo na chini ya nusu ya wabunge kwa mtindo wa bunge la Kiingereza na Sultani, akiwa kama ni mtawala tu lakini sio mtawala mwenye maamuzi ya mwisho. Taifa hili la Zanzibar ambalo lilikuwa mwanchana kamili wa Jumuia ya madola na mwanachana mpya wa Umoja wa Mataifa lilidumu kwa siku 33 tu.

Majadiliano makali ya kisiasa na maandamano yalikuwa ni matukio ya kawaida siku hizo. makundi ya watu yaliyokuwa yakiimba na kusifu majina mbalimbali ya viongozi wa kisiasa, huku yakivuka vizuizi vya barabara vilivyokuwa vikilindwa na askari wa kiingereza. Vikundi mbalimbali vilijadiliana juu ya mambo mbali mbali; mfano Haki dhidi ya fursa, Wageni dhidi ya wenyeji wa zamani, Ubepari dhidi ya Ujamaa, Wafanyabiashara dhidi ya wamiliki ardhi, Waunguja dhidi ya Wapemba, Waasia dhidi ya pazia la nyuma la vita baridi na harakati za utaifa na kuondosha ukoloni ambazo zilikuwepo kipindi hiki ndani ya Afrika.

John Okello hakuwa na jawabu ya mambo haya nyeti, lakini alikuwa na kipawa cha kutambua kwamba vikundi hivi vinavyoshindana vinatoa nafasi nzuri kwa mtu wa harakati kama yeye Okello. Hata hivyo, watu kama mia waliojizatiti wangaliwez kutwaa vituo muhimu vya kienyeji vya habari na kambi za Polisi. Mara tu baada ya vituo vya habari na Kambi za polisi pamoja na silaha kudhibitiwa na John Okelo, Ni nani katika visiwa angeweza kumshinda? Je, wanasiasa wangeliungana na kumshutumu na kumpinga kwa vitendo vyake visivyo halali? Au kama alivyotaraji, wangeendelea kutoaminiana na kutuhumu kwamba kati yao ndio wanaomuunga mkono? Je, wasingelitaka kukubaliana na yeye, haraka kabla mwengineo hajafanya hivyo? John Okello alichezesha rafu usiku huo wa mwezi wa Januari.

Viongozi wa A.S.P walifadhaishwa na matendo ya Okello (wengi wao, walikuwa hata hawapo visiwani wakati huo). Walikimbilia haraka kuwaunga mkono waasi. Mamia ya wafuasi wa vyama walipigwa na butwaa juu ya wale ambao walikuwa na shuku ya kukata fundo hilo gumu la majadaliano ya kidemokrasia na kukimbilia moja kwa moja kwenye utawala. Hawa walitafuta njia ya kuiandaa jamii kwenda sambamba na kanuni zao. Kanuni siku hizo zilikuwa ni ghali sana kama sarafu ya Marekani. Ubinadamu ulikuwa ni kitu adimu sana. Baadhi ya viongozi wa ASP baada kuona kwamba serikali itakuwa haina udhibiti na uwezo kujilinda na kutokuwa na imani matokeo ya chaguzi huria zilizofanyika, viongozi hawalitafuta njia za haraka za kuhalalisha udhibiti yale ambayo yaliitwa sasa "Mapinduzi". Makundi ya watu wenye fujo yalikuwa huru. Sheria na amani zilikuwa hazipo katika mitaa ya Zanzibar.Walimiliki ardhi na wafanya biashara waliburutwa kutoka majumbani na madukani mwao, uporaji na mauaji yalienea mji mkongwe mzima. Kwa kweli mji wenyewe uliporwa.

Waarabu na Waasia, waliokuwa wakiunga mkono vyama vyingine waliuliwa kwa makundi. Kwa usiku mmoja maisha ya watu yasiyovika yalipotea na siku nyengine baadaye maelfu ya watu waliikimbia nchi pamoja na kila walichoweza kubeba. 

John Okello mwenyewe alijipachika cheo cha Jemedari Mkuu akishirikiana na bataliani zake zenye fujo walianzisha utawala wa vitisho ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba. John Okello alitangaza vitisho visivyo vya kawaida na ahadi ya kifo kwa wote watakaojaribu kumpinga yeye. John Okello aliamini alikuwa akipokea maelekezo /dokezo kutoka kwa Mungu na akionyesha uwezo usiokuwa wa kawaida kwa kutumia nambari, kwa mfano tarehe 13 Januari, 1964, alitangaza ujumbe ufuatao." Serikali sasa inaendeshwa na sisi ikiwa mtakuwa wakaidi na kukataa kutii amri, Nitachukua hatua kali mara 88 zaidi ya hatua ninazozichukua hivi sasa" na "Na ikiwa yeyote atashidnwa kutii amri ya kutotoka nje ya nyumba kama walivyofanya wengine.sitokuwa na njia nyengine lakini kutumia silaha nzito. Sisi, ni jeshi lenye nguvu ya 99,099,000". Vitisho vyake na uwezo wake wa kuvitekeleza viliwatia hofu raia, hasa makundi mbali mbali ya jamii zilizo ndogo. 

Tarehe 14 Januari, 1964 alitangaza maneno haya ya kufadhaisha, “Huyu hapa ni Jemedari Mkuu wa Unguja na PembaNafikiria kuelekea kijiji cha Mtendeni kukiangamiza ikiwa watu wa hapo hawatafuata amri. Baada ya dakika 40 nitawamaliza nyote hasa Wangazija", " na kwa vijana wote wa kiarabu wanaoishi Malindi; Nitapita Malindi nikiwa nimesheheni silaha ambazo mimi mwenyewe ndie nizijuazo. Nataka kuona kila mmoja abakie na chupi na kulala chini. Nataka kuwaona wao wanaimba... Baba wa Waafrika. Mungu Mbariki yeye na malengo yake na yale ya Jemedari Mkuu" Huko mjini Dar es Salaam ndani ya kipindi cha mapinduzi kulikuwa kugumu sana, hata Julius Nyerere aliingiwa na hofu ya utawala wa mkono wa chuma wa Okello (wakala wake), sasa ikaanza kusukwa mikakati ya kumpoka mamlaka aliyokuwa nayo. Okello hakuwa na chama cha siasa hivyo Mwalimu akapendekeza liundwe baraza la mapinduzi na Okello awe  mkuu wa baraza hilo ambalo ndilo litakuwa na mamlaka yote ya Zanzibar.

Okello alikubali wazo hilo ambalo kikao kilifanyikia Dar es Salaam 1/2/1964, ikakubaliwa urais apewe kiongozi wa chama cha siasa yaani Abeid Karume lakini asiwe na sauti yoyote katika Zanzibar. Baraza hilo lilijumuisha wapiganaji watiifu wa Okello ambao hawakuwa Wazanzibari asilia (Mawakala wa Tawi Maalumu leo TISS). Nao ni pamoja na Field Marshal John Okello (Mganda) na msaidizi wake, Absalom Anwi Ingen (Mjaluo kutoka Kenya). Wengine ni Saidi Washoto (Tanganyika), Mohamed Kaujore (Mmakonde wa Msumbiji) na Hamisi Darwesh (Tanganyika). Walikuwapo pia akina Abdallah Mfaranyaki (Tanganyika), Saidi Natepe (Tanganyika), Seif Bakari (Tanganyika) na Edington Kisasi (Mchaga wa Kilimanjaro-Tanganyika).

Baada ya mgawanyo huo ilikubaliwa pia Abdulahman Babu awe mkuu wa vyombo vya habari pia akiwa ni mjumbe wa baraza la mawaziri. Walikubalikubaliana kuwa tarehe 1/4/1964 warejee tena Dar e salaam kwaajili ya kumalizia mipango ya kuitawala Zanzibar. Hapo ndipo siku aliyokwenda kufutwa Okello katika ardhi ya Tanganyika na Zanzibar katika msingi na muundo wa kisiasa, viongozi na wajumbe wote wa baraza la mapinduzi walipanda ndege moja kuja Dares salaam akiwemo Mungu wa Afrika, Okello walipofika uwanja wa ndege, itifaki iligeuzwa na John Okello akaambiwa asubiri kushuka awe wa mwisho. Baada ya kushuka wajumbe wote ndani ya ndege ile, alikwenda komandoo mmoja wa Kitanganyika ambaye alikuwa mkuu wa Tawi Maalumu la Ujasusi Tanganyika Bwana Emilio Mzena, Alimwamuru Okello asalimishe silaha yake na kisha kumwamuru rubani aipaishe ndege kuelekea Nairobi. Kenyatta alimwambia Nyerere kuwa mtu huyo (Okello) sio wa Kenya hivyo ndege ikaelekezwa Uganda ambako alibwagwa na historia yake ikaishia hapo. John Gideon Okello alizaliwa 1937, katika Wilaya ya Lango nchini, Uganda na alifariki mwaka 1971 kijijini kwao Lango Uganda alikokwenda kutupwa na Julius Nyerere na Karume. Kifo chake kimeacha majonzi kwa wanamapinduzi, kwani licha ya kuwa Baba halisi wa Taifa la Zanzibar kwa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar lakini Waafro + Shiraz hawa wamemezeshwa uongo kuwa Karume ndie baba yao.

Okello kafa masikini hata msiba wake umehudhuriwa na ndugu tu bila heshima yoyote ya kiukombozi.Huku nyuma kazi ya propaganda ya kubadili ukweli kuwa uongo na uongo kuwa ukweli ilisimamiwa na Babu, alipiga propaganda kupitia radio kuwa akiyefanya mapinduzi ni Karume na ASP, hata chama chake cha UMMA Party hakukisemea tena. Wakati unyanyasaji uliposima jamii za tamaduni tofauti za Zanzibar zilikuwa zimeparaganyika. Taifa la chama kimoja lilitangazwa. Lakini bado Taifa hili likihofia uwezekano wa kufufuka upinzani kutoka kwa wapinzani waliokimbia nchi. Wateka mapinduzi hawa baadaye walijihakikishia udhibiti zaidi baada ya kusaini mkataba wa muungano wa Tanganyika. 

Hii ingeruhusu maelfu ya marafiki wa kisiasa wa Tanganyika kuingilia kati upinzani wowote wa baadaye katika visiwa hivi. Askari polisi wa Zanzibar walibadilishwa kwa askari polisi kutoka Tanganyika ambao ni watiifu kwa chama na pazia la siasa za utengano ziliwakumba wazanzibari ambazo zilitakiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 20. Kwa lugha rahisi tunaweza kusema mapinduzi yalipinduliwa.

Leo hii siasa hizi za utengano hazipo tena, kumalizika kwa vita vya baridi na kuelekea kwa uchumi wa kisasa umeweza kuifungulia Zanzibar milango kwa ulimwengu wa nje. Uchaguzi wa vyama vingi ulifanyika mwaka 1995, 2000, 2010 na 2015 katika uchaguzi uliosiginwa na mamlaka za Tanganyika. Viongozi walaghai na wenye kujali hali zao siasa za wameibuka Tanzania na hii imewafanya wakimbizi waliokimbia wakati wa mapinduzi kurejea visiwani kwa jicho la tatu. Uvumilivu na amani wa watu wa aina tofauti, ambayo ni tabia ya maisha ya wazanzibari, sasa hivi unajitahidi kurejea katika mitaa ya mji Mkongwe, Katika uga huu wa kisiasa ni kuwa matakwa ya Wazanzibar katika siasa mpya bado yanafinyangwa bila sababu za msingi.

 Tutumie muda wetu kumuenzi mwanamapinduzi wetu Che Guevara wa Afrika, Field Marshal John Okello baba wa Taifa la Zanziba.

Makala hii inatoka katika kitabu cha Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi.

0715865544
0755865544

Na Yericko Nyerere

ASIYOYAJUA YERICKO NYERERE
Mohamed Said

Hicho anachoita kitabu wala hakina publisher wala mswada haukusomwa na mhariri yeyote sijuae historia ya mapinduzi ni sawa na mtu aliyejifungia chumbani kwake anaandika katika mtandao wa kijamii.

Yericko hana moja alijualo. Anachofanya ni kunakili yaliyoandikwa na wengine na kuungaunga kisha akayaleta kama fikra zake.

Hicho kichwa chake cha habari kwa haya aliyoandika ameyanakili kutoka kwangu kayabadilisha kidogo tu. Mwenye maneno hayo ambayo mimi ndipo nilipoyachukua ni Prof. Mohamed Bakari nimemsikia akiyasema kwenye kongamano Kampala mwaka wa 2003 akisema, ‘’Ikiwa sisi hatutoandika historia yetu watakuja watu kutuandikia na huenda tusipendezewe na hayo waliyoandika.’’

Prof. Mohamed Bakari ofisini kwake Fatih University Istanbul 2015
Angekuwa mjuzi kweli wa historia ya mapinduzi angemtaja kwanza Ali Mwinyi Tambwe aliyetumikia intelligence toka ukoloni hadi uhuru unapatikana 1961. Ali Mwinyi ndiye kiongozi wa Kambi ya Kipumbwi na ndiye aliyemtia Mohamed Omari Mkwawa katika njama ya mapinduzi na kumpa kazi ya kuvusha askari mamluki akifanyakazi chini ya Victor Mkello. 

Victor Mkello
Vitabu vyote vya historia ya mapinduzi hakuna mwandishi aliyelijua hili. Yeye Yericko kazi ni yake kukopi tu. Ghassany kazungumza na Victor Mkello si mara moja au mbili ilikuwa kazi ya kwenda Tanga na kurudi Muscat Mkello hakufungua kinywa chake hadi nadhani alipohisi hana siku nyingi za kuishi. Mimi nilikuwapo kwenye vikao vyote isipokuwa cha mwisho Mkello alipoamua kueleza ukweli mbele ya mkewe kikao hiki mimi nilitoka nje kuwapa faragha na kumtoa Mkello wasiwasi kwa kuwa Dr. Ghassany yeye mgeni mimi naishi na yeye mji mmoja. Yericko hana moja alijualo.
Dr. Ghassany na Mzee Mkwawa Tanga 2003.

Na Dr. Ghassany nyumbani kwake Muscat 1999 alipomfahamisha Mwandishi
mradi wa kutafiti historia ya mapinduzi ya Zanzibar ya 1964

Dr.. Ghassany na Mzee Mkwawa, Tanga 2009




No comments: