UKWELI: AKINA BIBI TITI HAWAKUZUKA KATIKA UONGOZI TANU—II
Na Alhaji Abdallah Tambaza
|
Bi. Titi Mohamed wakati wa kuoigania uhuru wa Tanganyika katika miaka ya 1950 |
KATIKA safu hii Jumatatu iliyopita
tulimwangalia mwanasiasa mashuhuri wa kike hapa nchini na Afrika Mashariki kwa
ujumla, Bibi Titi Mohammed, na mchango wake mkubwa sana alioutoa katika
kuwakomboa, sio wanawake peke yao, bali watu wote wa eneo hili la Afrika
Mashariki kutoka kwenye unyonge wa kutawaliwa.
Tuliona ni kwa kiasi gani mama yule
aliweza kuchanganyika na wanaume wa shoka kama kina hayati Mwalimu Nyerere,
Zuberi Mtemvu, Oscar Salathiel Kambona, John Rupia na wengineo wengi katika
mapambano yale mazito ya kuung’oa utawala dhalimu wa Malkia Elizabeth wa Uingereza.
Katika safu hii juma hili, tunamrudia
tena mama yetu yule, ambaye kama lilivyo jina lake, tuliinyonya ‘nyonyo’ ya
titi lake wake ule wa shida, na leo tuko ‘huru huria’, tukijifanyia wenyewe
mambo yetu tutakavyo.
Ingawa wakati mwengine haturidhiki na
namna ya mambo yanavyoenda nchini mwetu, lakini— potelea mbali— kamwe, tusitamani
ya Mkoloni yajirudie hapa. Ukoloni ni hadithi nyingine kabisa, kwani wahenga
walisema: “Afadhali ya zimwi likujualo halikuli likakwisha!”
Sasa basi, katika sehemu hii ya pili
na ya mwisho katika simulizi za Bibi Titi, tutaangalia ni nini kilimsibu mpaka
akakosana vibaya sana na wenziwe katika chama cha TANU; kupoteza ubunge na
uwaziri; kufukuzwa kama mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU; na kupigwa
marufuku kwa asasi ya Kiislamu ya East African Muslim Welfare Society (EAMWS)
ambayo yeye alikuwa kiongozi wake mwandamizi hapa Tanzania.
Nikiwa kijana mdogo sana jijini kwetu
hapo siku hizo za kudai Uhuru, kwenye miaka ya mwisho ya 50s, nilikuwa
nikimwona bibi yule pale ofisi za TANU Makao Makuu, akiwa na viongozi wenzake
wakiwa wamesimama nje ya ‘kajumba kao kadogo ka TANU ka vyumba sita tu, kalikojengwa
kwa miti na kukandikwa udongo’. Wakati ule nilikuwa mwanafunzi pale Shule ya
Msingi Mnazi Mmoja, mkabala na ofisi hiyo.
Lakini pia, nilikuwa nikimwona mitaani
kwetu; mtaa wa Sikukuu na Udowe ambako alikuwa akija kumtembelea binti yake
peke, Halima, aliyekuwa ameolewa hapo na kijana mcheza soka maarufu wakati huo
Mzee Iddi Hamisi. Mzee Iddi, alikuwa mpachika mabao wa klabu ya Cosmopolitan ya
Dar es Salaam, wakati ule klabu hiyo ilipokuwa inawika na kuwa na hadhi kama
vile Simba au Yanga kwa sasa. Kwa kweli ilikuwa ndio klabu ya kwanza kupata
tiketi ya kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya Afrika kwenye miaka ya 60s,
lakini ikakwama kutokana na fedha.
Lakini sikumfaidi hasa bibi Titi
mpaka pale nilipokuwa nikichukuliwa— mimi na ndugu zangu— tukiwa na babetu au
mametu, kwenda kwenye mikutano ile ya uamsho na siasa, ambayo Titi alikuwa
mzungumzaji mkubwa akianza; halafu Mheshimiwa (Nyerere) anamaliza.
Kwa zama zile, miongoni mwa Waafrika,
mtu aliyepaswa au kustahili kuitwa mheshimiwa, alikuwa ni Nyerere peke yake.
Neno hilo ‘mheshimiwa’ hakuitwa Gavana, DC wala PC. Ukisema mheshimiwa, hiyo
peke yake ilitosha kuwa wewe ulikuwa unaamanisha kipenzi chao Nyerere kutoka
Butiama, aliyewashangaza wengi kwa uwezo wake wa kujieleza na kujenga hoja,
ambaye kwa wakati huo, pamoja na sauti yake nyororo na nyembamba, alikuwa
akipata taabu sana kutamka neno Watanganyika, ila mpaka kwa kulivuta kidogo:
‘‘Wataaa-nganyika wenzangu, Uhuruu na
Umoja; Uhuruu na Kazi; Uhuruu na Maendeleo,” hiyo ni moja ya kaulimbiu kuu za
wakati huo.
Ni ukweli uliowazi kwamba watu kama
akina Bibi Titi hawakuzuka tu na kuwa viongozi katika Chama cha TANU. Watu wa
namna ile; wenye vipaji vya namna ile;
majasiri namna ile huwa wametengenezwa. Hufundwa majumbani, hupikwa na wazazi
wao wakaiva na kuwa tayari kupambana na lolote lijalo.
Titi mama yetu ni mmoja wao.
Alizaliwa mwaka 1926 na mara alipofikia umri wa miaka 13 (kwa maana ya ‘kuvunja
ungo’), tayari alipewa mume. Hiyo maana yake ni kwamba alikuwa tayari amefundwa
na wazazi wake mapema kuja kuyakabili maisha na changamoto zake zijazo.
Titi, akiwa bado kwenye umri mdogo
kabisa aliweza kuaminiwa kuongoza katika uimbaji kwenye shughuli za kimila na
harusi kwa kutumia sauti yake nyororo, maneno yenye bashasha na vipaji vingi
vingine ambavyo alivionyesha tokea mapema.
Shneidder Plantan, ndiye
aliyemwingiza Titi na mumewe katika siasa, baada ya kuwa amependekezwa na
wanawake wenziwe waliomjua uwezo wake kutoka katika vikundi mbalimbali vya
harakati za kinamama na mambo kama hayo. Kadi ya mumewe ni namba 15 na ya kwake
ilikuwa 16.
Mwaka 1957, pale kwenye viwanja vya
Mnazi Mmoja, mbele ya mgeni kutoka chama cha Labour cha Uingereza, alipewa
nafasi kuhutubia mkutano wa TANU wakati Nyerere akiwa Butiama mapumzikoni kwa
mamake. Enzi zile kulikuwa na fikra potofu kwamba mwanamke ni mtu wa kukaa
nyumbani tu na kulea watoto. Kwamba kazi kama zile za siasa hawaziwezi hata
kidogo.
Kwa kujiamini na huku akiwaonyoshea
kidole wanaume, aliwaambia wanawake wenzake:
“…Mnawaona
hawa! Basi wafanye watakavyofanya hawa, pamoja na hao wengine wote wanaotisha
duniani, wametoka katika matumbo ya wanawake na waliishi humo miezi tisa… kila
mmoja wao kanyonya ziwa la mamake miaka miwili… sasa tujitokeze wasitushinde
hawa!
“… wanawake
amkeni, tokeni majumbani tuje tupambane pamoja na wanaume mpaka uhuru upatikane
msiogope …msiogope… msiogope
“…kutawaliwa
siyo kuzuri ndugu zangu, hili ni letu sote si la wanaume peke yao, njooni kina
dada, njooni kina mama na vikongwe pia!” aliunguruma Titi huku kelele za
nderemo, hoihoi na vigelegele vikihanikiza uwanjani pale.
Kwa mara ya kwanza nyimbo zile
mashuhuri za kwenye harusi na sherehe nyingine alianza kuwaimbisha wanawake
wenzake na kuwatia hamasa isiyo na kifani:
“Hongera
mwanangu wee hongera, nami nihongere wee hongera! x 2
Mama usungu
mama usungu! x 2 Oieh!
Oieh! Linauma
mno wee oieh!
Linauma mno
eh! Oieh linauma mno!’’
Kutoka hapo siku hiyo, Bibi Titi
ikawa ndio habari ya mjini na sifa zake zikazagaa kila pembe ya ukanda huu wa
Afrika Mashariki. Wanawake makundi kwa makundi wakawa wamejitokeza na
kukikubali chama na harakati zake. Majumbani, kwenye misiba, harusini kote ikawa
ndio mazungumzo … Titi…Titi…Titi!
Wapigania uhuru wa Kenya wa wakati
huo, akiwamo Tom Mboya, Jaramogi Oginga Odinga (baba wa Odinga wa sasa),
walipopata habari wakaleta maombi Titi aende kwao kuwasaidia kushawishi
serikali ya Mngereza kumtoa kifungoni Mzee Jomo Kenyatta (babake Rais Kenyatta
wa sasa), kwa kosa la uhaini wa kudai kujitawala.
Titi, alitia fora kwenye mikutano
yake kule Mombasa, Kisumu, Machakos na Nairobi. Titi, alisimama majukwani kule
Kenya akiwa amevalia ‘mini skirts’ zake maridadi kabisa (picha zipo mitandaoni
na kwenye vitabu mbalimbali), akilia kwa uchungu kumpigania Kenyatta awe huru
na wanawake waje wajae kwenye harakati.
Haukupita muda mrefu, miaka kadhaa
baadaye, Mzee Jomo Kenyatta aliachiwa huru kule Kenya na haraka haraka akaja
Tanganyika na kuhutubia maelfu ya watu, akiwemo mwandishi huyu, pale kwenye
viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.
Kenyatta akiwa amevalia suruali yake
ya corduroy rangi ya udongo (maarufu khaki Kenya siku zile) na koti kubwa la
kijivujivu, alipeperusha juu usinga wake mweusi na kutumia muda mwingi
kumshukuru Bibi Titi kwa kazi aliyowafanyia Wakenya.
Kwenye mkutano ule, ndipo Nyerere
alipotamka kwamba yuko tayari kuahirisha uhuru wa Tanganyika, ambao tayari
ulikuwa umeshajulikana, ili tusubiri Kenya nao wapate wa kwao na hapo nchi hizi
ziungane kuwa moja na Kenyatta awe ndio rais wake. Ni tamko zito sana hilo,
ambalo bila shaka yeyote, lilitokana na kazi ya Mama Titi. Uhuru uchelewe na
urais apewe mtu mwengine! Leo isingewezekana. Si unaona Zanzibar; Karume kataka
mwenyewe Muungano haraka kwa kuogopa kupinduliwa, leo inaonekana kalazimishwa
na Nyerere.
Baada ya Uhuru kupatikana, Titi
alipata ubunge jimbo la Rufiji, na akachaguliwa kuwa Waziri Mdogo wa Wizara ya
Utamaduni na Maendeleo. Alikuwa pia mweyekiti wa mwanzo wa UWT na kiongozi
mwanadamizi wa East African Muslim Welfare Society (tawi la Tanganyika), pamoja
na mjumbe wa Maulid Committee (kamati ndogo ya kuandaa Maulid kila mwaka).
Mwenyekiti hapo akiwa waziri mwenzake Tewa Said Tewa (Mbunge wa Kisarawe) na
Chifu bdallah Said Fundikira aliyepata kuwa Waziri wa Sheria akawa Katibu.
Timu hiyo, kwa kushirikiana na
wajumbe wengine wa EAMWS hapa nchini walifanya mambo makubwa sana katika
kuendeleza Uislamu na Waislamu; na kwa kiasi fulani walifanikiwa katika kutaka
kupunguza pengo lililopo kielimu baina ya Waislamu na watu wa dini nyengine.
Kufumba na kufumbua, waliweza kupata
kiwanja kikubwa pale Chang’ombe karibu na Uwanja wa Taifa kwa ajili ya ujenzi
wa Chuo Kikuu cha kwanza Tanganyika, kabla hata kile cha Mlimani hakijaanza.
Pamoja na kumwalika Nyerere kuja
kuweka jiwe la msingi, Nyerere na serikali anayoingoza, hakupendezwa na jambo
lile. Mipango ikafanywa, si tu kuusimamisha mradi ule uliokuwa unafadhiliwa na
Rais wa Misri wakati huo, Gamal Abdel Nasser, bali kuivunja kabisa taasisi ile ya
EAMWS na kuwaundia Waislamu baraza jengine.
EAMWS, lilikuwa na nguvu kubwa sana
kwa kila hali, maana ndani yake lilijumuisha madhehebi zote za dini ya Kiislamu
wakiwamo Waismailia, Mabohora, Waithnasheri, Mashia, Ibadhi na Ahmadia. Patron
wake alikuwa ni H.H. Aga Khan likiwa na madhumuni ya kusaidia na kuendeleza
Uislamu.
Mwalimu na wenzake katika TANU,
pamoja na kukataa ubaguzi kwa kukubali kuwapokea na kuwapigia kura Wahindi
kwenye mpango wa ‘kura tatu’, kwenye hili la Uislamu— Wahindi wakaonekana Wahindi—
hawakutakiwa wasaidie Waislamu wenzao na hapo ikavunjwa EAMWS kwa amri ya
Serikali na likaundwa BAKWATA la Waafrika watupu (Sunni tu). Sasa hivi
Waismailia, Mabohora, Waithnasheria wako kivyaovyao. Iko wapi hapo ‘Wabil
muuminuna ikhwana’ (Waislamu wenzangu ndio ndugu zangu).
Titi alipoteza kiti chake cha ubunge
Rufiji kwa mtu aliyekuwa si maarufu hata kidogo. Tewa naye alipoteza Kisarawe
na alipelekwa kuwa Balozi wa Tanzania kule China. Alhaji Chifu Abdallah Said
Fundikira, akapelekwa Nairobi, Kenya kuwa Mwenyekiti wa ‘marehemu’ Shirika la
Ndege la Jumuiya Afrika Mashariki (EAAC)—liliuawa kikatili Juni 30,1977.
Ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya
TANU, hayati Bibi Titi alipambana na kuwagaragaza wanasiasa wakongwe kwa hoja
nzito pale mjadala wa kuivunja EAMWS ulipokuwa unajadiliwa na halmashauri hiyo.
(Rejea kitabu Maisha na Nyakati, Abdulwahid Sykes cha Mohammed Said, uk 363, Seleman Kitundu (Kamisaa wa Chama Jeshini) na Rajab
Diwani (Kamanda wa Vijana), walivyomshambulia Bibi Titi).
Bibi Titi mwenyewe, miaka 30 baada ya
kuangushwa kwake kisiasa, ameliambia gazeti la Rai kwamba kuanguka kwake
kisiasa kulisababishwa na kule kumpinga Nyerere kwenye Halmashauri Kuu ya TANU,
wakati Nyerere alipokuwa anatafuta kuungwa mkono na Waislamu ndani ya chama kwa
kuivunja EAMWS. (Angalia Rai, Desemba 29,1994). Angalia vilevile Said, uk 336, Pambano
kati ya Nyerere, Titi na Tewa 1968.
Mnamo mwaka 1968, Bibi Titi
alikamatwa pamoja na mwanasiasa mwengine aliyepata kuwa Waziri wa Kazi na
kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi nchini Michael Kamaliza, kwamba
walishirikiana na wanajeshi wengine wane wakitaka kumuua na kuipindua serikali
ya Nyerere. Titi na wenzake walitiwa hatiani katika kesi iliyochukuwa siku 120
kusikilizwa; na hivyo kufungwa jela maisha.
Waswahili wana msemo usemao; tenda
wema nenda zako. Habari za kukamatwa na kufungwa jela kwa Bibi Titi
ziliwashitua na kuwasikitisha mno watu wa Kenya; na hasa wanawake ambao
walikuwa wana deni kwake.
Mwanamama mmoja, mwanasiasa
machachari nchini Kenya, alivuka mpaka na kumfuata Nyerere Butiama, alikokuwa
amepumzika baada ya kuomba wakutane huko mbele ya mamake Mwalimu, Mama Mgaya.
Baada ya mapokezi na maamkizi, mama
yule alimkabili Nyerere uso kwa uso na kumwambia kuwa alichofanya ni kukosa
fadhila kwa Bibi Titi, ambaye amewafanyia makubwa watu wa Afrika Mashariki ujanani
kwake.
‘’Utakuwa ni wizi wa fadhila na
kukosa utu kama wewe Nyerere utaendelea kumfunga jela Bibi Titi kwa yote
aliyokufanyia wewe, nchi yako na wapenda haki na usawa wote wa upande huu wa
dunia
“Tafadhali sana nakuomba nimetumwa
kwako nikiwakilisha watu wa Kenya na wanawake wa nchi hizi mbili umwachie huru
Bibi Titi, kama yeye alivyopambana na Wazungu mpaka Kenyatta wa kwetu (Kenya)
akatoka jela,’’ Alimaliza mama yule akarudi kwao Kenya.
Akiwa ofisini kwake Kenya tayari ameshasahau; siku moja akapata
habari kwamba kuna mgeni kutoka Tanzania anataka kumwona. Akaagiza apitishwe.
Alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje John Samuel Malecela akiwa na ujumbe
kutoka kwa Mwalimu: “Nimetumwa nije nikupe habari njema kwamba Nyerere tayari
ameshamwacha huru Bibi Titi,”alisema Waziri Malecela.
Mama alijibu, “Kamwambie Nyerere
kwamba kwa niaba ya wanawake wa Kenya na watu wa Afrika Mashariki, ninasema
ahsante sana, kwa uungwana wake,”alimaliza
Hivyo ndivyo alivyofungwa na kufunguliwa
mama yetu aliyerejea tena kuishi maisha ya chini kabisa ya kawaida kule Temeke,
Mtaa wa Ngarambe, maana nyumba zake mbili za kisasa pale Upanga alizokuwa
akimiliki wakati wa enzi zake za uongozi zilitaifishwa na Azimio la Arusha.
Aliwekwa chini ya ulinzi fulani hivi (semi house arrest), maana kutwa alikuwa akikaa
nje barazani kwake akiiuza mafuta ya taa kwa kupimia watu rejareja na siku
zikawa zinasogea mbele. Rais Mwinyi alipokuja madarakani alimrejeshea mama yule
zile nyumba zake mbili pale Upanga, na habari zinasema akapewa na senti mbili
tatu kujiendesha maisha yake yaliyobaki.
Tunamwomba Mola ailaze mahala pema peponi
roho ya mama yetu huyu—Ameen! Ameen!
0715808864
No comments:
Post a Comment