KUVUNJIKA KWA JUMUIYA EAC NA ATHARI ZAKE—II
Na Alhaji Abdallah Tambaza
Abdallah Tambaza Nairobi 1972 |
Ndugu msomaji hii ni sehemu ya pili ya makala mfululizo kutoka
kwenye Shajara ya Mwana Mzizima kuhusu KUVUNJIKA KWA JUMUIYA EAC NA ATHARI
ZAKE—I, na tukaona namna Jumuiya ile ilivyokuwa muhimu kwa nchi wanachama yaani
Kenya, Uganda na Tanzania. Katika sehemu hii ya pili, tutangalia wapi
tuliteleza mpaka leo imekuwa marehemu. Sasa enedelea….
KWENYE Shirika la Posta na Simu la iliyokuwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, lililokuwa na makao yake makuu pale Nairobi, Kenya, pamoja na
kupokea na kutawanya barua, lakini pia lilikuwa ndio shirika pekee lilohusika
na simu, iwe majumbani au maofisini; siku zile hakukuwa na kampuni za simu za
viganjani (cell phones) za TiGo, Airtel na Voda, kama ilivyo sasa.
Chuo kikubwa kabisa cha kufundisha wafanyakazi wa Posta kilikuwapo
pale Kabete, Nairobi, ambapo wafanyakazi wote wa idara mbalimbali walipata
mafunzo hapo.
Shirika Posta Afrika Mashariki, lilikuwa na idara nyingi sana
zilizokuwa zimetapakaa kila pembe ya ukanda huu na majumba ya ofisi pamoja na
ya kuishi wafanyakazi yasiyokuwa na idadi.
Wale waliokuwapo wakifanya kazi huko labda wangekuwa mashahidi,
lakini sipati picha kama lisengevunjika wakati ule, leo tungekuwa wapi kiuchumi
na kimaendeleo kwa ujumla na kwenye nchi moja moja.
Wafanyakazi walioajiriwa na Posta, waliwapita wale wa Bandari na
Reli kwa uwingi. Shirika la kwetu tulilounda badala yake ni kama vile ‘cha
mtoto tu’. Watu maelfu kwa maelfu waliokuwa wakiajiriwa kutokea shuleni kila
mwaka kupitia shirika hilo, moja kwa moja walipelekwa chuoni kule Kenya
zilikofundishwa fani zote, ikiwamo ya uhasibu pamoja na ya kibenki.
Benki ya Posta wakati huo, ilikuwa ndio kimbilio la watu wengi
katika kuhifadhi pesa za ziada, kwani ilikuwa ni muhimu miaka ile kila mtu kuwa
na kitabu cha Posta kwa ajili ya kujiwekea akiba ya fedha.
Posta, ndio iliyokuwa njia kuu ya pekee kwa kutuma pesa za haraka
kwa njia ya simu za upepo (telegrams). Hakukuwa na TiGo pesa au Airtel
Money wakati huo. Uchumi huu wote mkubwa uliopo sasa kutokana na matumizi ya
simu za viganjani na huduma zake kemkem, ungekuwa unabaki hapahapa na siyo
kuchukuliwa na kampuni hizi za kiuwekezaji kutoka nje zilizopo sasa.
Kule nchini Uganda, mjini Soroti kulikuwa na chuo kikubwa sana cha
kufundisha marubani wa ndege, si tu kwa kuja kuajiriwa na Shirika la Ndege
Afrika Mashariki peke yake, lakini pia kwenye serikali zote tatu, makampuni
binafsi na taasisi za kidini kama vile ‘Flying Doctors’ na za kubeba watalii
kwenda mbuga za wanyama.
Chuo cha Reli Afrika Mashariki, pale Nairobi South B – ni taasisi
moja kubwa sana nadhani mpaka leo hivi ipo; maana ile ilirithiwa na Wakenya
kama sisi tulivyorithi lile jumba la Makao Makuu EAC pale Arusha, tukalifanya
Jumba la Mikutano –AICC Arusha na leo kuvuna ‘mapesa’ mengi kiulaini.
Wakenya pia wamepata chuo kingine kikubwa tu cha Bandari (Bandari
College), pale Mombasa ambacho kilikuwa kinatoa, pamoja na mambo mengine,
maofisa wa masuala ya Ushuru na Forodha (Customs and Excises), pamoja na
ukadiriaji wa kodi (taxation). Mambo hayo yote huko nyuma yalikuwa yakiendeshwa
kwa pamoja. Hakukuwa na TRA, URA, wala KRA. Idara lilikuwa ni moja East African
Customs & Income Taxes Department.
Idara nyingine zilizokuwapo ni pamoja na zile za kitafiti kama
vile East African Literature Bureau; East African Malaria Institute; na East
African Industrial Research Institute kilichokuwa kikishauri namna ya kuanzisha
na kuendeleza viwanda kwa nchi za Afrika Mashariki. Unataka nini tena ukiwa na
mambo mazuri kama haya?
Kwa vile huduma hizi zimekuwa zikitolewa na Jumuiya Afrika Mashariki
kwa pamoja, ziliwaondolea mzigo mkubwa sana nchi wanachama mmoja mmoja kuweza
kuwazia namna ya kuziongoza au kuzifanya kila mtu kivyake vyake. Huduma zile
zilichukua fedha nyingi, utaalamu mkubwa na kama inavyojionyesha sasa ulikuwa
ni mzigo kwelikweli kwa nchi moja moja, maana hapa kwetu hatunalo hata moja
miongoni mwa mashirika hayo, ambalo tulilianzisha wenyewe ambalo tunaweza
kusema tumefanikisha kazi au kufanana na yale. Kila tulichokiunda, kimebakia
jina tu; maana ama shirika hilo litakuwa limeundwaundwa upya na kuvunjwa zaidi
ya mara tano, au mengine kuwa hayafani kwa ubora na kiutendaji kama yale ya
pamoja.
Kwa mfano kwenye Air Tanzania, wakati Kenya wakiwa bado na Kenya
Airways ileile waliyoiunda, sisi shirika letu— tena si kubwa kama lao— limevunjwa
na kuundwa upya zaidi ya mara 7 na kupoteza fedha nyingi sana za Walipa Kodi wa
taifa hili masikini!
Hali kadhalika kwenye Shirika la Reli nako kumepitia misukosuko
mingi isiyo na idadi. Mara hivi, mara vile; leo treni ipo kesho hakuna. Kila
siku ‘uongo’ mkubwa ni kukosekana vipuri na mabehewa. Waliletwa mpaka
Wahindi hapa wakapewa kuliendesha eti wenyewe limetushinda. Leo iko treni
Tanzania imepewa jina ‘Ya Mwakyembe’, inayokwenda Ubungo na Pugu. Wakati wa
Jumuiya ya zamani, treni kama zile zilikuwa za mizigo na mifugo tu na wala siyo
za kupakia watu na suti zao.
Kuuawa kwa iliyokuwa EAC, kumeirudisha nyuma sana kimaendeleo nchi
yetu na watu wake, maana si ajira tu zilizopotea kwa maelfu, lakini zile faida
zilizokuwapo hazipo tena. Ni ukweli usiofichika kwamba leo yapata miaka 41
tokea kufa kwa EAC bado hatujaweza kuwa na Shirika la Ndege la maana; hatuna
Shirika la Reli la maana; hatuna Shirika la Posta la maana; hatuna Shirika la
Bandari na Upakuaji mizigo la maana. Achilia mbali vyuo na taasisi zile za
kitaalamu zilikuwapo wakati ule.
Msomaji kama bado unakumbuka wakati ule wa miaka ya nyuma, nchi
yetu hii ilikuwa ikitegemea sana wataalamu wa nje waliokuwa wakijulikana kama
ma—TXs, mashirika na taasisi ya iliyokuwa EAC hayakuwa na haja ya kuwa na watu
wa namna hiyo mahala popote. Idara zote zile na mashirika yale ya kitaalamu,
yaliendeshwa kwa kutumia watu waliofundishwa kwenye vyuo vya EAC yenyewe
vilivyotapakaa kila kona ya nchi hizi.
Mwandishi huyu alikuwapo pale School of Aviation, Nairobi kwa
nyakati mbili tofauti kwa kozi ndefu ndefu—1970 na 1973— na mara zote hizo
madarasani mle kulikuwapo na watu waliotoka nchi za jirani kama Rwanda, Burundi
na Shelisheli ambao walikuwa wakisoma kwa ufadhili (scholarships); na walikuwa
wakijiona kama vile wako Ulaya pale Nairobi. Kumbe ni Kenya tu ile, iliyokuwa
ikimeremeta kwa maendeleo ikawahadaa na kuwatisha wakatishika.
Uwepo ule wa EAC wakati ule, kwa kiasi kikubwa sana ulizipa nchi
wanachama mwanya wa kushughulika na masuala mengine kwenye serikali zao. Kwa
mfano kwa Tanzania, nafikiri Mwalimu aliweza kutumia vyema nafasi ile kwa
kushughulikia zaidi mambo ya vijiji vya ujamaa, kuimarisha chama chake cha CCM
mpaka kikawa na hadhi kama vile nacho ni serikali; kwani kilitambulika kwamba
kimeshika hatamu na kiko juu ya serikali.
Faida nyingine iliyopatikana kwa Tanzania ni kwamba, kwa vile
nyenzo kuu za uchumi (economic infrastructure) ziliendeshwa kijumuiya, Mwalimu
Nyerere na wenzake walijikita zaidi katika ukombozi wa nchi za kusini mwa
Afrika kwa sababu nchi yetu ndio iliyokuwa mwenyekiti wa zile zilizoitwa
‘frontline states’. Nchi nyengine ni Zambia, Msumbiji, Angola na Botswana
huku Mwalimu akiwa ndiye mwenyekiti wao.
Mara nyingi mikutano ile ilifanyika hapa Dar, ambako pia kulikuwa
ndio Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi wa Afrika (OAU liberation Committee).
Hayati Brigadier Hashim Mbita, ndiye aliyekuwa Katibu Mkuu Mtendaji, akiwa na
hadhi ya kibalozi humu humu nchini mwake.
Sasa Msomaji, jiulize vipi kitu kizuri kama ile EAC; kitu chenye
manufaa kama yale ya ile EAC; kitu kilichowafanya watu wake wakaoleana na kuzaliana
watoto baba Mkenya na mama Mtanzania au Mganda kiruhusiwe kuaga dunia
kibwegebwege.
Imewezekana kufanya hivyo kwa sababu watu wake ‘walilewa
mafanikio’ na hivyo kuleteana jeuri na kibri kilichopitiliza kwa kudhani kwamba
hata kama wakiivunja basi wataweza kubakia salama tu kama mwanzo walivyokuwa
EAC.
Sisi Watanzania tulikuwa msitari wa mbele kwa kuwa kikwazo kwa
kila mapendekezo mapya ya kupeleka mbele Jumuiya ile, tukilalamika eti ikiwa
hivi ama vile basi Kenya ndio watakaonufaika! Basi, msimamo wetu ukawa ni
kwenda kupinga kila kipya kiletwacho kwenye vikao—“hilo ni ‘ubepari au
unyonyaji’ hatutaki”.
Wenzetu walituvumilia kwa kiasi fulani lakini ilifika mahala
wakasema basi; liwalo na liwe, huku ‘Wazungu wale uchwara’, wakisema, “Kenya
can go it alone!”
Hapa kwetu, Bwana Mkubwa naye akawa hataki katakata kukaa meza
moja na muuaji Iddi Amin—ambaye ndiye rais wa Uganda wakati huo iwe tunamtaka
au hatumtaki— aliyempindua rafiki yake kipenzi Milton Obote. Obote alipewa
hifadhi ya kisiasa hapa kwetu na ikawa anatengenezewa mazingira ya kurejeshwa
madarakani Uganda kutokea hapa.
Amin, hakufurahishwa hata kidogo na jambo hilo, hivyo wawili hao
wakawa mahasimu wakubwa wakijibizana na kutukanana ovyo tu. Watanzania
tukimwita Amin, Nduli na kwamba anakula nyama za watu na wengine anawatupa
kwenye Ziwa Victoria waliwe na mamba. Amin, naye akawa hana adabu chembe kwa
Nyerere, mpaka akafikia kusema eti, “…Nyerere kama ingekuwa manamuke mimi
angemuoa yeye…” ...teh …teh …teh. Basi tuliishia hivyo kucheka tu.
Sasa hali ikawa hivyo, matusi na vijembe kila kukicha na wakubwa
waliojulikana kama “The summit”, wakawa hawakutani hata kuidhinisha matumizi ya
pesa tu, kama Mkataba wa Ushirikiano (Treaty of Coorporation) unavyowataka.
Mwalimu ndiye aliyekuwa na jukumu la kuitisha mkutano huo kwa sababu uenyekiti
wa hiyo summit ulikuwa kwake kwa mujibu wa mzunguko.
Basi wakachokozanachokozana hivyo, Amin akidhani yeye kwa vile ni
mwanajeshi mwenye kutisha, basi Nyerere ‘atagwaya’(atatishika). Siku moja
akatishia atatupiga kwa mabomu angani kwenye miji ya Dodoma na Dar es Salaam
kama tusiposhika adabu. Siku nyengine Amin alivuka mpaka akamteka nyara
aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (RPC) wa Bukoba Hanz Poppe aliyekuwa
akiangalia hali ya mpaka, akamwua na baadaye kumburura barabara akidai ni
askari wa Kichina! Hanz Poppe alipondwapondwa midomo ili wajihi wa sura yake
uonekane Mchina hasa. Masikini, dunia ikaamini hivyo kwamba tulikuwa na askari
wa Kichina jeshini, kwa ule urafiki wetu wa siku nyingi na nchi ya China.
Amin akaingiza majeshi yake yakaikalia Bukoba kule Mutukura.
Jaafar Nimeiry, akiwa Rais wa Sudan siku hizo alikuja hapa kumwomba Nyerere
aache kupigana na Amin; wapatane yaishe. Nyerere alikataa kabisa akaweka
masharti magumu kwa kila aliyejaribu kutaka kusuluhisha ugomvi ule. Kenya nao
walipochoshwa wakatangaza kujitoa Afrika Mashariki na hapo hapo wakazuia
‘madege’ yale na mabogi ya treni kutoondoka Nairobi kuelekea kokote kule.
Tanzania nayo ikatangaza kufunga mpaka wake na Kenya na haraka
haraka ikakodisha ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kwenda Nairobi
kuwarudisha nyumbani raia wake wote waliokuwa wamekwama nchini humo na familia
zao.
Ikawa kama mchezo wa sinema vile—labda watapatana; watu wakubwa
hawa na akili zao hawawezi kuacha kitu kama hiki kijifie mbele ya macho yao.
Kwa upande wetu na Uganda, vita ikawa imepamba moto. Haishikiki,
haikamatiki; tukaanza kupata ushindi. Nyerere akawahutubia wazee huku akitamba;
‘mvua za kwanza zimemnyeshea, nguvu ya kumpiga tunayo, uwezo wa kumpiga tunao
na nia ya kumpiga tunayo!’ akawa anashangiliwa kwelikweli kwa kugombana na
‘nduguye’.
Jumuiya ile ‘takatifu’ ikakata roho namna hiyo huku wadau na
waliokuwa wafanyakazi tukasambaratishwa tusijitambue! Kama vile limbukeni,
Watanganyika tukalikimbilia lile jumba la Makao Makuu na kukaa humo
tukishangilia, ‘letu… letu… letu!!’ Kama vile watu tulioridhika kwa kupata
mjengo tu. Ndio ilivyokuwa, maana mgao ulipofanyika na msimamizi wa mirathi
walikuja kupata na vitu vingine kama mashirika na mali zake ambavyo leo vyote
wameviacha vimeteketea au wameuza kwa bei poa.
Tukutane tena juma lijalo tukapoangalia sehemu ya tatu na ya
mwisho kwenye shajara hii, itakayogusia namna mgao wa mirathi ya marehemu EAC
ya zamani ulivyofanyika, uliowaacha wazee wastaafu wakisikitia nafsi zao mpaka
leo kwa kudhulumiwa haki zao.
simu: 0715808864.
No comments:
Post a Comment