Prof. Hamza Mustafa Njozi akizindua Kamapasi ya Kigamboni, Dar es Salaam |
Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Waislam Morogoro (MUM) wakipanda mabasi kuja kwenye shsrehe ya kuweka jiwe la msingi Kampasi ya Kigamboni, Dar es Salaam |
Ulipopatikana
uhuru mwaka wa 1961 Sheikh Hassan bin Ameir aliwatangazia Waislam kuwa sasa
anapumzika na shughuli za siasa na atatia juhudi kuwatumikia Waislam wa
Tanganyika khasa katika ukombozi wa elimu kwani tayari Tanganyika ishakombolewa
kutoka makucha ya wakoloni. Sheikh Hassan bin Ameir akaanzisha Daawat Islamiyya
yeye mwenyewe akiwa Mwenyekiti na Katibu Schneider Abdillah Plantan. Wawili
hawa wote wana historia kubwa katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Schneider
alifanya juhudi kubwa sana mwaka wa 1950 kuingiza vijana katika uongozi wa juu
wa TAA, Dr. Vedasto Kyaruzi (Rais) na Abdulwahid Sykes (Katibu) na Sheikh
Hassan bin Ameir yeye mwaka huo baada ya vijana kuchukua uongozi wa TAA Abdul
Sykes alimtia kama mjumbe katika TAA
Political Subcommittee.
Baada
ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 kilichofuatia ni kuitishwa kwa Muslim
Congress ya kwanza mwaka wa 1962 na ya pili mwaka wa 1963. Muslim Congress ikaja
na mipango ya kujenga shule za msingi na sekondari Tanganyika nzima na
kumalizia na ujenzi wa Chuo Kikuu. Kazi ya ujenzi wa shule ikaanza na mwaka wa
1968 jiwe la msingi wa Chuo Kikuu likawekwa Chang’ombe na aliyeliweka alikuwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Ahmed Rashad Ali |
Ahmed
Rashad Ali wakati ule alikuwa Assistant Permanent Secretary Wizara ya Habari
ofisi yake ikiwa Askari Monument.
Ananihadithia
Mzee Rashad. Anasema sherehe ya kuweka jiwe la msingi wa Chuo Kikuu Cha Kiislam
ilikuwa kubwa haina kifani. Mabalozi wa nchi za Kiislam wanaowakilisha nchi zao
Tanzania wote walialikwa na viongozi wa East African Muslim Welfare Society
(EAMWS) ambao ndiyo walikuwa wasimamizi wa mradi ule walikuwapo wakiongozwa na
Aziz Khaki kama mwakilishi wa Aga Khan, Patron wa EAMWS. Baada ya Mwalimu
Nyerere kuweka jiwe la msingi akiwa yuko katikati ya Sheikh Hassan bin Ameir na
Tewa Said Tewa mmoja wa waasisi 17 wa TANU mwaka wa 1954, alipelekwa kuangalia
michoro ya Chuo Kikuu ikionyesha idara zote za chuo, Tewa Said akimpa maelezo
ya ziada.
Kushoto Sheikh Hassan bin Ameir akisalimiana
Julius Nyerere katikati ya ni Tewa Said Tewa siku
ya sherehe ya kuweka jiwe la msingi Chuo Kikuu
Cha Waislam
Kushoto Sheikh Hassan bin Ameir, Julius Nyerere, Sheikh Abdallah Chaurembo Rashid Kawawa na Tewa Said Tewa |
Ahmed
Rashad anasema yeye alikuwa katika ule msafara kwa ajili ya wadhifa wake akiwa
nyuma ya Mwalimu Nyerere, Sheikh Hassan bin Ameir, Tewa Said Tewa kama Rais wa (EAMWS) tawi la Tanzania. Anasema hakikuwa
kilichokuwa kinampita. Radio Tanzania walikuwapo pale na Mtangazaji alikuwa
akitangaza kila hatua ya shughuli ile. Akiwa katika hali ile alishuhudia kitu
ambacho kwa wakati ule hakukitia maanani ila baada ya mambo mengine kutokea
ndipo akazindukana. Mzee Rashad anasema aliona mtangazaji anahangaika na tape
iliyojizingira katika mashine ya kurekodi na kilichomstaajabisha ni kuwa badala
ya kusimamisha mashine na kurejesha nyuma ili tape ikae sawasawa yule kijana
akawa anatumia mikono yake kujaribu kuinasua ile tape na kwa kufanya hivyo
alikuwa anaiharibu tape yenyewe. Mzee Rashad wakati wa kupigania uhuru yeye
alikuwa mtangazaji wa Radio Free Africa Cairo, radio iliyoanzishwa na Gamal
Abdel Nasser kwa ajili ya ukombozi wa nchi za Afrka Tanganyika ikiwa moja ya
nchi hizo. Ilimdhihirikia baadae kuwa yule kijana alikuwa anafanya yale
makusudi kuharibu rekodi ya shughuli ile isibaki katika kumbukumbu katika
Maktaba ya Radio Tanzania.
Waislam
siku ile waligubikwa na furaha kubwa kwani ukoloni uliwabinya sana katika elimu
kwa takriban miaka mia. Kuwa sasa wanajenga Chuo Kikuu hili lilikuwa jambo
kubwa na la kihistoria. Chuo kilikuwa kinajengwa kwa msaada wa serikali ya
Misri na mkandarasi Al Nasr kampuni ya Kimisri iliyokuwa na ofisi zake Mtaa wa
Jamhuri ndiyo waliokuwa wamepewa kazi ya ujenzi wa chuo. Furaha hii haikudumu
wala mafundi hawakupata hata nafasi ya kuchimba msingi wa chuo. Serikali ikaipiga
marufuku EAMWS baada ya mgogoro mkubwa uliopikwa ndani na nje ya EAMWS, mgogoro
uliodumu kwa kama miezi miwili hivi. Tarehe 19 Desemba, 1968 serikali ikapiga
marufuku EAMWS na huo ndiyo ukawa mwisho wa ujenzi wa shule za msingi na
sekondari na mradi wa ujenzi wa Chuo Kikuu. Serikali ikaunda BAKWATA kushika
nafasi ya EAMWS na Sheikh Hassan bin Ameir akafukuzwa nchini.
Kuna
watu wanasema kuwa Waislam hawathamini elimu na husema maneno haya kwa kukosa
kujua historia ya Waislam na juhudi ambazo zimepitika katika kujinasua katika
tatizo hili. Wapo wanaowasimanga Waislam kwa kupewa chuo kikuu Morogoro bure na
serikali.
Bahati
mbaya hapajakuwa na majibu kueleza historia ya Chuo Kikuu kilichowekewa jiwe na
msingi mwaka wa 1968 na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere mwenyewe kwa mkono wake
huku akishuhudiwa na viongozi wakuu wa taasisi za Kiislam zilizokuwapo Tanzania
na picha za sherehe ile kuenea katika magazeti. Hapajakuwa na majibu kueleza kwa
nini chuo hakikujengwa. Kwa kuwa hakuna majibu ya kueleza kwa nini Waislam
hawakuweza kujenga chuo kile kebehi, kejeli na masimango yatakuwapo siku zote.
Tarehe 24 Machi 2018 Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha
Waislam Morogoro Profesa Hamza Njozi ameweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa
Kampas ya Kampas ya Kigamboni Dar es Salaam. Prof. Njozi ameweka jiwe hilo la
msingi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Muslim Development Fund (MDF) mheshimiwa
Abdulrahman Kinana. Jiwe la msingi limewekwa kimya kimya bila nderemo wala mialiko.
Rigal na Mwandishi katika mgahawa New York 2011 |
Mwaka wa 2011 nilikuwa New York, nikiwa njiani
kwenda Northewestern University, Evanston, Chicago nilikoalikwa na Idara ya
African History kufanya mhadhara. Mwenyeji wangu pale New York akaniambia kuwa
kuna Mmisri anafanya kazi Umoja wa Mataifa na huyu Mmisri aliwahi kufanya kazi
Ubalozi wa Misri Tanzania katika miaka ya 1960. Kitabu changu, ‘’The Life and
Times of Abdulwahid Sykes (1924 – 1968) The Untold Story of the Muslim Struggle
Against British Colonialism,’’ kilipotoka mwaka wa 1998 huyu Mmisri, jina lake
Rigal alikisoma na alikipenda sana khasa kwa kuwa kilieleza historia ya Chuo
Kikuu Cha Waislam kilichokuwa kijengwe na serikali ya Misri. Rigal yeye akiwa
ofisa katika Ubalozi wa Misri, Dar es Salaam alihusika sana na mradi ule na
alisikitika kuwa chuo kile hakikujengwa. Mwenyeji wangu alipomwambia kuwa niko
mjini alimuomba amkutanishe na mimi.
Siku ya Ijumaa baada ya kuswali sala ya Ijumaa
msikiti ulio jirani na ofisi za Umoja wa Mataifa Rigal alitualika chakula cha
mchana kwenye mgahawa si mbali na msikiti ule.
Rigal alitaka kusikia kutoka kinywani kwangu
nini khasa ilikuwa sababu ya serikali ya Nyerere kuipiga marufuku EAMWS wakati ilikuwa
na maradi muhimu wa kujenga Chuo Kikuu.
Nilimweleza kila kitu nilichokijua.
Rigal akaniuliza hali ya Waislam ikoje hivi
sasa katika elimu.
Nilimweleza.
Swali alilouliza mwanafuzi katika mhadhara uliofanyika MUM tarehe 7 Juni 2018 mzungumzaji akiwa mwandishi |
Rigal aliniuliza kama nitakuwa tayari kwenda
Misri na kufanya mihadhara kueleza uhusiano mzuri uliokuwapo kati ya Gamal
Abdel Nasser na Julius Nyerere kiasi cha Nasser kuamua kujenga Chuo Kikuu Dar
es Salaam mradi ambao kwa wakati ule ulikuwa mkubwa wa elimu Misri hawajapata
kutekeleza nje ya nchi yao.
No comments:
Post a Comment