Shajara ya Mwana Mzizima
KUVUNJIKA KWA JUMUIYA EAC NA ATHARI
ZAKE – IV
Na Alhaji Abdallah Tambaza
Raia Mwema Aprili 9-10, 2018 |
MPENDWA msomaji, wiki ya jana katika
mfululizo wa makala hizi kuhusu kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki
(EAC) ya zamani, tuliona namna ilivyovunjwa kikatili na walioimiliki, na namna
ambavyo kwa sasa wanakwenda mbio kutaka kuirudisha tena lakini hiyo ni kama
vile ‘maji yakimwagika hayazoleki tena’.
Tumeona pia katika makala iliyopita,
namna serikali yetu ilivyofanya makusudi kuchakachua (walinyofoa) articles
1,2,6,13,16,17,18) kutoka kwenye ripoti
ya mgawo wa zilizokuwa mali na madeni ya jumuiya ile iliyotayarishwa na
Professa wa Ki-Swiss, Victor Umbritch, iliyojulikana kama East African
Community Mediation Agreement 1984. Ripoti ile iliridhiwa na Bunge la Tanzania
na kufanywa sheria ya nchi iliyoitwa East African Community Mediation Agreement
Act No 2. 1987.
Professa Umbritch, alikabidhi
mwenyewe ripoti ile kwa kila aliyekuwa rais wa nchi yake wakati ule, akiwamo
Milton Obote wa Uganda, Daniel Arap Moi wa Kenya na Mwalimu Julius Nyerere wa
Tanzania, aliyepokea ripoti hiyo pale nyumbani kwake Msasani, mbele ya viongozi
waandamizi wa serikali na waandishi wa habari.
Kufikia hatua ile— na kama tutakavyokuja kuona huko
mbele— Professa Umbritch alishapata habari kwamba serikali, kupitia Benki Kuu
ya Tanzania, ilikuwa imeshapokea fedha kutoka kwa Kampuni ya Crown Agents ya
U.K, iliyokuwa inatunza fedha za Akiba ya Uzeeni za Watumishi (Workers
Provident Fund) kwa niaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Fedha ile ni ya wafanyakazi wenyewe iliyotokana na
makato kwenye mishahara yao ya kila mwezi— nje ya mgawo wa mali na madeni ya
EAC kama ilivyoainishwa ndani ya Umbritch Report.
Sasa wakati akikabidhi ripoti yake, Umbritch
alimwambia Mwalimu kwamba, katu; fedha ile haikuwa msaada kutoka kwa Malkia wa
Uingereza kwenda kwa serikali husika; na hivyo ilitakiwa haraka serikali hizo ziwape
walengwa fedha zao. Umbritch alisema:
“Justice delayed by officials is justice doubly denied”
(Haki yeyote ile inayocheleweshwa upatikanaji wake na
viongozi, basi huwa ni haki iliyominywa maradufu.) Tafsiri na msisitizo ni wa
kwangu mwandishi. Kwa taarifa zaidi tembelea: http://go.worldbank.org/049WTNH500.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mramba kwenye Bunge, fedha
ile Tanzania iliitumia kwa kupigania vita na Uganda. Sasa badala ya kukubali na
kusema hayo mapema, walificha ukweli huo na kutoa maneno mengi ya kashfa na
vitisho hasa kutoka kwa aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, John Malecela
ambaye alikataa katakata kwamba fedha hiyo ya Provident Fund imepokewa na
badala yake akaonya ‘kuanzia siku ile yeyote atakayemsumbua kwa madai hayo
atapambana naye.’
Waswahili husema ‘nguvu ya mtu haipotei bure’. Siku
moja, sasa akiwa mbunge wa kawaida wa Bunge la Tanzania, aliyepata kuwa Waziri
Mkuu na Waziri wa Fedha Cleopa Msuya, alisimama Bungeni na kuliambia Bunge
kwamba ni kweli Serikali ilipokea fedha hiyo mali ya wazee wa EAC kutoka Crown
Agents ya Uingereza na ikazitumia wakati yeye akiwa Waziri wa Fedha. Hivyo
haoni ni kwa nini wasilipwe fedha yao!
Taarifa zilizopo zinasema, Serikali
ilielekezwa pale ikishapokea fedha ile, iendelee kuiwekeza, ili watu kila watapostaafu
wawe wanalipwa fedha yao. Hilo likawa gumu kwao kulifanya maana tayari
walishawagomea watu wao kuwapa ajira endelevu kwenye yale mashirika mapya
yaliyoundwa—Kenya na Uganda waliwaajiri watu wao kwa ajira mwendelezo
(continuous employment).
Fedha ile waliitumia wanavyojua wenyewe—
Kifisadifisadi— sijui kwa kupigania vita au kununulia chakula kutoka nje, maana
wakati huo nchi ilikuwa inapita kwenye kipindi kigumu kwa kila hali. Hakuna
hata serikali moja inayofanya hivyo duniani hata iwe ya kidhalimu vipi; kuwadhulumu
kimachomacho watu wako mwenyewe ndiyo iweje!
Wazee masikini wakawa hawana jinsi.
Hawajui nani wamwendee kwenye kadhia hii kwani serikali yao yenyewe ndio
inayofanya dhuluma hii. Hivyo basi, baada ya tamko la Msuya, zikaanza harakati
za kufungua kesi ya madai mahakamani. Kesi ambayo mpaka sasa imeweka rekodi ya
kuwa ndiyo iliyochukua muda mrefu kuliko zote katika historia ya taifa hili
tokea tujitawale—miaka 41 sasa na bado!
Kesi Na 50/2000 ikafunguliwa ili
kuomba mahakama ikubali serikali kushitakiwa. Kwa kawaida huwezi kuishitaki
serikali kama mwenyewe hataki kushitakiwa na wewe. Kibali kilitoka takriban
miaka 5 baadaye (2005) kwa mbinde kweli kweli.
Kesi Na 95/2005 ikaanza kusikilizwa
mbele ya Mahakama Kuu mbele ya Jaji Urio. Hapo pakapatikana kitu ushindi kwa
wastaafu kilichojulikana kama ‘Deed of Settlement’ (makubaliano ya kumaliza
kesi nje ya Mahakama) pamoja na ‘Decree’ (makubaliano ya utekelezaji wake hayo
makubaliano.)
Ile ‘decree’ ilikuwa na vipengele
tisa (9) vya malipo ambavyo serikali iliridhia itavilipa, lakini basi kwanza
kesi iwe imefutwa mahakamani, ambako ilikuwa na hofu kwamba ingeshindwa vibaya
na hivyo kutakiwa kulipa fedha nyingi zaidi.
Kwa ‘ujanjaujanja’, na uzoefu wake wa
masuala haya, kwenye ile ‘deed’ ikaweka kipengele namba nane (8) ambacho
walijua watakuja kukitumia kufanya dhuluma ya malipo yale. Kipengele hicho
kilitamka kwamba ‘mara malipo yatakapokuwa yamefanyika basi wadai watakuwa
hawana haki tena ya kudai kitu kingine chochote kutoka kwa mdaiwa’.
Kama kawaida yake, kimya kimya,
Serikali ikatengeneza malipo yale tofauti na makubaliano. Ukokotoaji sasa
ukabadilika ukafuata sheria na taratibu za ki-Tanzania na siyo kwa mujibu wa
mikataba ya kazi ya walengwa. Thamani ya pesa haikutiliwa maanani ingawa wakati
ule ilikuwa imepita miaka 30 baada ya wao kupokea mzigo wa fedha na mambo kama
hayo.
Msomaji, kumbuka kwamba kabla
hawajafanya udanganyifu huu, wataalamu wale wasomi kule serikalini, waliondosha
vipengele vyote kwenye ‘Umbritch Report’ vinavyozungumzia habari ya thamani ya
fedha (Real Value) wakati wa kufanya malipo.
Hapo pakazuka sintofahamu kubwa kati
ya wazee na serikali yao. Serikali bila aibu wala huruma inalipa fedha ya mwaka
1977 kwa wakati huu! Duh! Ikawa ngumu. Lakini wao wameshika mpini wazee
wameshika makali, ukikosea tu watakuchanja na kisu! Utu kwao ukawa haupo tena
wakawa kama mbogo waliojeruhiwa:
“… hawa wazee wasumbufu… tayari
tumeshawalipa bilioni 117 sasa wanataka nini tena na wenyewe wameweka saini
kwamba hawatarudi tena mahakamani…”
Basi wakawa wanairudiarudia hiyo
bilioni 117 kila kukicha bila ya kuelezea nani wamempa nini na kwa ukokotoaji
upi. Ikawa kama malipo yale labda tumewauzia nazi au korosho vile na kupatana
bei iwe bilioni 117. Ripoti ya Msimamizi wa Mirathi Mzee Umbritch, pamoja na
kwamba ni sheria ya nchi sasa, hawataki hata kuitaja!
Watu wa ajabu sana hawa! Msomaji hebu
wewe chelewesha kulipa kodi ya TRA, ARDHI, au Majengo na iwe imepita miaka 10
hivi hujailipa serikali uone kiama chako.
Watakupiga mafaini kibao na pengine
nyumba yako waipige mnada au mali zako nyingine wazipige bei. Huwa hawasikii
chochote. Ukiwauliza kwa nini inakuwa hivyo wanakwambia wewe umechelewesha
malipo hivyo thamani imepotea sasa lazima ulipe zaidi tena na ‘penalty‘.
Sasa kama hivyo ndivyo, kwa nini
inawalipa wazee wale masikini fedha yao ambayo wamekaa nayo— tena makusudi— kwa
miaka yote hiyo bila kuzingatia thamani ya sasa ikoje? Hivi tuseme lile jumba
zuri la Makao Makuu ya EAC pale Arusha, walilorithi na kulifanya AICC, wanakodisha
mikutano pale kwa bei ya mwaka 1977? Na je, wakiamua kesho kuliuza kwa mtu –
maana hawakawii kufanya hivyo— watamuuzia mnunuzi kwa fedha ya mwaka 1977 au
mwaka huu?
Ni bahati mbaya sana hata mahakama
zetu ambazo zinatakiwa ziwe zinazingatia haki wakati wa kusikiliza na kutoa
maamuzi huwa zinapindisha waziwazi maamuzi yake, linapokuja suala la
kutokukubaliana na serikali. Sujui huwa wanapigiwa simu au inakuwaje; maana
utashangaa kumkuta jaji anatoa maamuzi tofauti na sheria ya kazi yake
inavyomtaka. Kwenye sakata hili la madai ya wazee wa EAC tumeshuhudia ‘mauzauza’
mengi mno mahakamani.
Ni ajabu kwelikweli, kwamba watu wa
nchi hii wamekuwa wakilichukulia jambo hili kama ni ‘mchezo mchezo’ wa sinema
hivi ya maigizo. Wanajifanya wamesahau kwamba ni kweli, ilikuwapo Jumuiya ile
ya Afrika Mashariki iliyoajiri watu takriban 30,000 elfu hivi hapa kwetu kwenye
mashirika yake mbalimbali.
Ni kweli pia, jumuiya ile ilikuwa na
mali zinazohamishika na zisizohamishika kama Jumba la AICC pale Arusha, madege
na mabehewa ya treni pamoja na meli; Ni kweli pia, wenye kuimiliki waliipiga
mawe na mashoka wakaivunja na hivyo ikafa pale June 1977.
Na ni kweli pia, baada ya kifo chake
palichaguliwa msimamizi wa mirathi kutoka nchi tofauti ili pasiwe na upendeleo
na kudhulumiana, agawe mali na alipe madeni. Mali zikagawiwa na nyinyi
Watanzania mkapata sehemu yenu vitu chungu nzima mkafurahi na msiulize vimetoka
wapi.
Sasa cha ajabu leo wazee wanalalamika
kwamba walikuwa sehemu ya mirathi ile na kwamba fedha yao serikali inayo, nyote
mnashangaa, mnabeza na kucheka:
“… Hivi vizee vinahangaika vinadai nini,
waangalie wengine hata kutembea hawawezi …teh! …teh! …teh! Haa…haa…hee!”
Basi tumeambulia maneno kama
hayo tu; hawakujitokeza asilan, wananchi wenzetu wakatusaidia kuipigia serikali
kelele itende haki irudishe amana ya watu. Wabunge nao kule Dodoma wakawa
wanasimama kidete kuinusuru serikali ya chama chao ikawa ‘wanazungukazunguka’
na viti vyao vyekundu, na tai za hariri zinazomeremeta wakipigapiga meza na
kushangilia; ‘weshalipwa hao bilioni 117’.
Aliyepata kuwa Jaji Mkuu
wakati fulani, ambaye pia ana cheo cha Uchungaji hivi kwenye kanisa lake la
Ki-Anglikana, damu ya kiuchungaji ikamchemka. Aliliita lile faili kubwa la
ubabaishaji la kesi ya Ex-EAC akateua na majaji wengine sita hivi wakalipitia
na kukumbana na ‘madudu kibao’.
Hii ilitokea pale wazee
walipoamua kulala barabarani na kufunga Barabara ya Kivukoni isitumike mpaka
kieleweke. Uamuzi wa Jaji yule msomi ukawa kwamba, pamoja na mambo mengine
mengi, Jaji aliyesikiliza kesi (Jaji Utamwa), ‘atemwe’ na ateuliwe jaji
mwingine aje kutoa Hati ya Kukazia Hukumu na kuiamrisha serikali ilipe kwa
mujibu wa makubaliano ya ile ‘Decree na Deed of Settlement’.
Hapa akateuliwa Jaji Dk
Fauz, ambaye aliisikiliza upya kesi ile badala ya kutoa Hati ya Kukazia Hukumu
kama alivyoamrishwa na jopo lile kubwa lenye majaji 7 tena wa Mahakama ya
Rufaa, na ndani yake akiwamo JM (CJ).
Jaji Fauz alipomaliza
kusikiliza ile kesi, akasoma hukumu yake ndefu akasema haoni sababu ya kutoa
Hati kwa sababu haoni mahala popote ilipoelekezwa kwamba malipo yale yafanyike
kwa kuzingatia thamani ya fedha. Hivyo fedha waliyolipa serikali ni nyingi
kuliko stahili ya wazee.
Msomaji, hapa sasa ndiyo ile
dhuluma iliyofanyika inapodhihirika wazi, kwani nyaraka aliyokuwa akiitumia
Jaji Fauz kutolea hukumu yake (East African Community Mediation Agreement Act 2
ya 1987) ni ile iliyobemendwa na kunyofolewa zile sehemu zinazoonyesha malipo
yazingatie thamani ya dollar (articles 1, 2,6,13,16,17,18)—‘Justice denied by
officials is Justice doubly denied’, Umbritch alipata kumwambia Mwalimu Nyerere
pale Msasani siku aliyokabidhi ripoti yake.
Kesi ikatua Mahakama ya
Rufaa na huko nako hali ikawa ni ile ile ya ‘figisufigisu’. Kila unapokwenda
unamkuta serikali (mdaiwa) keshatangulia huko. Hapa ikasikilizwa ile rufaa na
majaji 5, wawili kati yao walikuwa ni walewale waliokuwamo kwenye jopo lile la Jaji
Ramadhani lilomuengua Jaji Utamwa na kuamrisha ateuliwe Jaji mwengine na afanye
kama walivyoelekeza wao.
Mmoja wa wale majaji
waliokuwa na Jaji Ramadhani, hapa ghafla alibadilika na kufokafoka kwa nguvu
kwamba, “hapa sisi mnataka tufanye nini wakati serikali imelipa 15% riba wakati
nyinyi mlikuwa mnaomba riba ya 7%.”
Bwana mkubwa yule msomi,
akashindwa kuona na pia kutofautisha tofauti ya ukokotoaji unapoweka 15% riba
ya asilimia ya kawaida (15% simple interest) na 7% riba ya asilimia ya
malimbikizo (7% compound interest).
Kesi ikaishia hapo kwa rufaa
ile kutupiliwa mbali na huo ukawa ndio mwanzo wa wazee wale kuanza kuaga dunia
mmoja mmoja mpaka sasa wakiwa wamebaki wachache kuliko idadi ya warithi ambao
wanawakilisha baba zako, mama zao au bibi na babu kwenye kuendeleza madai—Inna
lillah Waina Ilayhi Rajuun!
simu: 0715808864
No comments:
Post a Comment