Wednesday, 1 January 2014

Ahmed Rashad Ali Bingwa wa Propaganda za Ukombozi wa Afrika Sehemu ya Tatu

Nikiwa na Abdillatif Abdallah  Humburg 2011


Nimepokea ujumbe kutoka kwa kaka yangu Ahmed Rajab akinambia kuwa katika bandiko langu la pili kuhusu Ahmed Rashad Ali wa kuzungumzwa pale alikuwa si yeye bali ni Abdilatif. 

Ahmed Rajab alisema haya baada ya kuona picha yake na Abdilatiff ambayo nilikuwa nimeitanguliza kabla ya makala ile.  

Kwa hakika ningeweza kuandika mengi kuhusu Abdilatiff. Nilimjua Abdilatif London na aliyenijulisha ni yeye Ahmed Rajab. 

Kwa ufupi nilimjibu kaka yangu kwa kumwambia kuwa iko siku In Sha Allah nitamwandika Abdilatiff. Abdilatiff ni mada nzito inayojitegemea kwani ana historia ya pekee. 

Historia hii sikuisoma. 

Historia hii kanieleza mwenyewe kwa kinywa chake nikiwa mgeni wake nyumbani kwake Humburg.

Nilimwomba Abdilatif aandike kitabu cha maisha yake.

Kutoka Kushoto: Sheikh Ali Muhsin, Mwandishi na Sheikh Badar
Muscat, Oman 1999
Sheikh Badar Aliondoka Ndani ya Meli Moja na Sultan Jamshid na Wote
Walipata Hifadhi Uingereza
Kutoka kushoto Kanyama Chiume, Kaluta Amri Abeid, Abbas Sykes (nyuma) Julius Nyerere









Katika miaka ya mwishoni ya 1950 Ali Muhsin alikwenda Cairo kujaribu kukipatia kuungwa mkono na Gamal Abdel Nassser chama chake ZNP. Kwa wakati ule Mzanzibari aliekuwa maarufu pale Cairo alikuwa Ahmed Rashad akifanya kazi na Radio Free Afrika. Nasser na Rashad walikuwa wakijuana vyema. Nasser alikuwa akimchukua Rashad kama mtaalamu wake katika masula ya Afrika. Rashad alikuwa akifanya kazi kwa karibu sana Mohamed Faik Waziri wa Mambo ya Afrika. Nkrumah alipotembelea Misri Nasser mwenyewe alimuomba Rashad  kumtayarishia habari zote kuhusu Ghan na Nkrumah. Rashad aliifanya kazi ile akishirikiana na waandishi wengine wa Kimisri. Alipokuwa Cairo Ali Muhsin alikaa kwa Rashad. Wawili hawa walisoma darasa moja Zanzibar mwaka 1928. Wakati ule shule yao ilikuwa ikijulikana kama Government School sasa inaitwa Ben Bella. Baadhi ya wanafunzi wengine katika daraza lao la mwaka wa 1928 alikuwa Juma Alley ambae baadae alikuja kuwa waziri katika serikali ya kwanza ya Zanzibar, Sheikh Abdallah Saleh Farsi baadae akajakuwa kadhi wa Zanzibar, Mohamed Said Abdullah mwandishi maarufu alieandika kitabu ‘Mzimu wa Watu wa Kale’ kitabu maarufu ambacho hakijapata mfano wake Zanzibar, Ahmed Seif Kharusi mhariri wa ‘Kiongozi’ gazeti lililokuwa limeegemea Hizbu, Mohamed Burhani Mkelle mtaalamu wa kIswahili, Said Nassor Abrawly aliekuja kuwa liwali wa Dar es Salaam. Picha iliyopigwa ya darasa hili tarehe 23 January 1928 inaonyesha watu waliokuja kuibadili historia ya Zanzibar wakati ule watoto hawa wastani wa umri wao ulikuwa haujazidi miaka kumi na mbili.

Ali Muhsina alipokwenda Cairo 1958 wakati haukuwa muafaka kwa kuwa Nasser alikuwa kashughulishwa na mambo ya serikali. Alikuwa kashikwa na mazungumzo kati ya nchi yake na Syria. Mawaziri walikuwa wakipishana kati ya Cairo na Damascus na ikawa vigumu sana kwa Faik kuweza kuwapatia Rashad na Ali Muhsin miadi ya kumwona Nassser.  Ali Muhsin alisubiri miezi mitatu kabla ya kumuona Nasser. Na ujumbe ulipowafikia kutoka kwa Faik kuwa Nasser atawaona waliambiwa kuwa mazungumzo yatachukua dakika kumi na tano. Mazungumzo kati ya Nasser na rais wa ZNP Ali Muhsin yalifanyika kwenye Kasri ya Quba. Nasser aliwapokea kwa taadhima na itifaki zote na baada ya kupiga picha watu hawa watatu yaani Nasser, Rashad na Muhsin wakaanza mazungumzo ambayo yaliyomweka Muhsin Cairo kwa miezi mitatu akimsubiri Nasser.

Wakati Rashad anaondoka Zanzibar kulikuwa hakuna vyama vya siasa. Kulikuwa na vyama vya kijamii basi. Kulikuwa na African Association kulichoasisiwa mwaka wa 1934 na mwakilishi wake katika Baraza la Kutunga Sheria alikuwa Amir Tajo. Ahmed Rashad alieleza hali ya siasa Zanzibar kwa muhtasari akitilia mkazo madhila ya Waingereza visiwani. Rashad alipomaliza kuzungumza Ali Muhsin akaeleza kwa kirefu harakati na nafasi ya vyama vya siasa ambacho chama chake kilikuwa kimojawapo. Nasser alisikiza kwa utulivu na akaahidi kuunga mkono harakati za Zanzibar kwa hali yoyote ile. Walipofika pale mazungumzo yakajikita katika elimu ya vijana wa Zanzibar. Nasser akatoa takriban scholarship hamsini kwa Zanzibar.

Wakati ule Nasser alikuwa ametoa nafasi kwa vijana wa Somaliland na kwenda kusoma Misri. Nafasi miat tatu zilikuwa kwa wavulana na sitini kwa wasichana. Rashad akamgutusha Nasser kuhusu hilo. Nasser kufuatia ombi la Rashad akatoa scholarship zisizo kikomo kwa vijana wa Zanzibar kwenda kusoma Misri na akasema haijawezekana kuwasomesha vijana wa Kenya na Uganda ambao ndiyo watakuja kuwa viongozi wa mapinduzi ya Afrika. Kufuatia maneno haya Nasser akamtwisha Ali Muhsin mzigo wa kuwatafuta vijana wa Kenya na Uganda kwenda kusoma Misri. Nasser alikuwa ameupa ujumbe wa Zanzibar dakika kumi na tano. Zilipokwisha akaingia mtumishi kumfahamisha Nasser kuwa muda ulikuwa umekwisha na alikuwa anasubiriwa kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri chumba cha pili.

Faik alikuwa kaupenyeza mkutano wa ujumbe kutoka Zanzibar na Nasser kwa dakika kumi na tano na baada ya hapo Nasser alikuwa aende kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri kama mwenyekiti. Nasser akamwambia yule afisa kuwa mkutano wa Baraza la Mawaziri usubiri kwa kuwa alikuwa ana mazungumzo muhimu na ujumbe kutoka Zanzibar. Mkutano ule uliendelea kwa dakika themanini. Ali Muhsin alipomaliza Nasser akataka amsikie Rashad anasema nini kuhusu aliyoeleza  mwenzie. Rashad akasadikisha yote aliyosema Ali Muhsin. Baada ya mkutano Nasser akasimama akageuka akafungua mlango nyuma yake na mara alikuwa chumba cha pili walichokuwa mawaziri wake akiangaliananao uso kwa uso.

Nasser kama alivyokuwa mtu wa kutimiza ahadi yake akatoa kwa Zanzibar kama alivyoiahidi Zanzibar na kiongozi wa ZNP. Lakini uchaguzi wa wanafunzi wa Ali Muhsin ulimuudhi rafiki yake Rashad. Rashad alikuwa  mtu wa kutoka Malindi. Katika uchaguzi wa 1957 Ali Muhsin mtu wa Shangani alikuja kugombea kiti Malindi. Katika chaguzi zote tatu Ali Muhsin alisimama Malindi. Hakuweza kusimama Shangani kwa kuwa kule ilikuwa milki ya Waasia na kwake yeye kusimama kule ni sawa na kifo. Watu wa Malindi wengi wao wakiwa Waafrika walimpa kiti kile bila matatizo. Lakini Ali Muhsin alipokuwa anachagua vijana kwenda kusoma Misri Waafrika hawakuwamo. Sababu ni kuwa Waafrika wasingeweza kumudu nauli ya ndege ambayo ilitakiwa ilipwe na mzazi wa mwanafunzi aliechaguliwa. Wavulana na wasichana waliochaguliwa takriban walikuwa Waarabu kutoka familia za juu. Jambo hili lilichoma nyoyo za Waafrika wengi Zanzibar. Mmoja wa wanafunzi waliopelekwa Cairo na Ali Muhsin alikuwa Mohamed Tahir ambae baadae alikujakuwa Kadhi wa Comoro.

Inasemekana Ali Muhsin hakufanya juhudi yoyote kuwapata wanafunzi kutoka Kenya na Uganda kama alivyoahidi. Rashad ambae alimsaidia Ali Muhsin kupata zile scholarship kwa ajili ya Zanzibar, Kenya na Uganda akaona amesalitiwa. Rashad yeye alijiona kama mpigania utaifa, mpigania uhuru, bingwa wa propaganda aliekuwa juu ya magomvi ya siasa yasiyokuwa na maana. Katika matangazo yake ya radio Rashad alichukua mkondo wa kuielezea Zanzibar kama nchi ambayo ilikuwa katika matatizo sawa na yale ambayo Misri ilipitia chini ya Mfalme Farouk kabla ya mapinduzi ya 1952. Rashad alikuwa akiieleza Zanzibar kama nchi iliyokuwa ikipigana kujitoa katika utawala mbovu wa kifalme uliokuwa ukitiwa nguvu na Uingereza. Kwa msimamo wake huu Rashad alikuwa amejitenga mbali kabisa na siasa za kibaguzi. Rashad kwa hiyo alifadhaika kuona kuwa hakukuwa na kijana hata mmoja wa Kiafrika katika orodha iliyopelekwa serikalini Misri kwa ajili ya kupata ufadhili na hapakuwa na wanafunzi kutoka Kenya na Uganda achilia mbali hakuna hata kijana mmoja kutoka nyumbani kwake Malindi. Hivi sasa imekuja kujulikana kuwa kukosekana kwa wanafunzinkutoka Kenya na Uganda na Tanganyika ilikuwa ni sababu ya propaganda dhidi ya Misri kama taifa la Kiarabu. Ali Muhsin alikuja kuandika katika kumbukumbu zake:

‘’Kulikuwa na tuhumu katika magazeti ya Tanganyika kuwa huu ulikuwa ni ujanja wa kuwaghilibu vijana wa Kiafrika upande wa harakati za Waarabu. Baada ya kumaliza masomo hao vijana watakuwa wanaunga mkono Waarabu na hiyo ni dhambi isiyosameheka. Huu ndio ulikuwa upuuzi ambao watu kama Francis Khamis wa Kenya walikuwa wakiandika katika magazeti. Mwandishi akahimiza serikali ya Uingereza ipige marufuku wanafunzi wa Kiafrika kusafiri kwenda Misri. Kwa urahisi kabisa serikali za Kenya na Tanganyika zikapiga marufuku mtu yeyote kutoka nchi hizo kusafiri kwenda Misri na Ugiriki kwa ajili ya masomo. Hakukuwa na alietaka kwenda Ugiriki lakini iliwekwa tu pale kama njia ya kuonyesha kuwa serikali ya kikoloni haikuwa na upendeleo.’’

Kuanzia hapa Rashad alianza kumshambulia Ali Muhsin katika matangazo yake ya kila siku kwa dharau bila ya kumtaja jina lakini kwa kupiga vijembe kuhusu mtu aliekuwa na kitone katika uso wake. Ali Muhsin alikuwa na kitone cheusi usoni na haikuwawia shida watu wa Zanzibar kutambua kuwa aliekuwa akidhamiriwa katika matangazo ya Radio Free Africa kutoka Cairo alikuwa Ali Muhsin. Kwa hakika kwa namana yoyote ile hiyo ilikuwa ni shambulio binafsi ingawa Rashad aikuwa na akida ambayo alitaka kuitetea. Shambulio dhidiya Ali Muhsin ilikuwa Shambulio dhidi ya Hizbu. Rashad alikuwa na jukwaa kueleza fikra zake ni njia ipi alidhani ndiyo sawa kufuatwa na Zanzibar katika harakati zake dhidi ya Uingereza na Sultan. Ali Muhsin na Hizbu hawakuwa na jukwaa kama hilo.

Ikaonekana njia pekee ya kupambana na Rashad ilikuwa kwa Hizbu kukabiliananae (pamoja na wapinzani wengine) katika uwanja wake huko huko Misri. Hizbu walichukua njia mbili za mashambulizi. Njia ya kwanza ilikuwa kumpeleka Abdulrahman Babu Cairo kuonana na Nasser kumwomba  ZNP kufungua ofisi nay a pili mayo ndio ilikuwa muhimu kabisa ilikuwa ni kumng’oa Rashad kutoka katika ile radio. Ali Muhsin akaenda Misri akiwa na Abdularazak Kwacha ( huyu alikuwa bingwa wa kusoma Qur’an) na hawa wawili wakaeleza malalamiko yao kwa Mohamed  Faik, Waziri wa Mambo ya Afrika katika serikali ya Nasser. Faik akamwita Rashad na akamwambia Ali Muhsin aeleze mbele ya Rashad maneno ya Hizbu dhidi ya Rashad mbele ya uso wake. Aeleze ni namna gani Rashad alikuwa anaviza mapambano ya Zanzibar kupitia matangazo yake mabaya dhidi ya Hizbu akitumia radio ambayo watu wa Misri wameitoa kwa ajili ya vyama vya ukombozi. Ali Muhsin hakuwa na la kueleza alimaliza kwa kusema kuwa Rashad alikuwa ni kachero wa Waingereza.

Serikali ya Misri ikakataa kuiruhusu ZNP kufungua ofisi Cairo. Rashad alikataa kuunga mkono wazo hilo na kuishawishi serikali ya Misri kuwakubalia ZNP ombi lao. Hizbu walikuwa na nia ya kuiambia serikali ya Misri kuwa Rashad alikuwa ni kachero wa Waingereza kw ahiyo afukuzwe Misri. Katika vita hivi kati ya Rashad upande mmoja na Ali Muhsin upande wa pili hakuna waliofaidikia katika propaganda za Rashad kutoka Cairo kama Afro-Shirazi Party na umma wa Waafrika wa Zanzibar kwa ujumla.

Mwaka 1950 Babu akaenda Cairo na azma ya kufungua ofisi ya Hizbu. Babu alidhania kwa ajili ya umaarufu wake katika siasa asingemuhitaji Rashad. Rashad alipotakwa ushauri kuhusu Hizbu kuwa na ofisi Cairo, Rashad aliiambia serikali ya Misri kuwa kwa maslahi ya muda mrefu ya watu wa Misri hilo jambo si jema kwa kuwa Hizbu kinatambulikana kama chama kinachowakilisha utukufu wa Waarabu dhidi ya Waafrika walio wengi Zanzibar. Kuirihusu Hizbu kuwa na ofisi Cairo itachukuliwa na Waafrika kama serikali ya Kiarabu ikiunga mkono utawala wa Kiarabu katika Afrika. Nasser hakuweza kupuuza ushauri wa Rashad. Hizbu hawakukubaliwa ombi lao la kufungua ofisi Misri. Babu alikuwa ameshindwa katika azma yake na akarejea Zanzibar amevunjika moyo.

Ilikuwa baadae wakati Hizbu walipomtuma Ali Sultan ndipo Rashad aliunga mkono ombi la Hizbu na wakaruhusiwa na serikali ya Misri kufungua ofisi Cairo. Rashad na Ai Sultan walikuwa ndugu na kwa kuwa damu ni nzito kuliko maji Rashad alimuunga mkono Ali Sultan. Lakini kama njia ya kuweka mizani sawa Rashad akaiambia ASP chini ya Karume nao wafungue ofisi Cairo. Lakini kitu kama hiki kilikuwan nje ya uwezo wa fikra na uoni wa viongozi wa ASP.  Viongozi wake walikuwa hawajafikia uelewa wa kuweza kuanzisha sera maslahi yao wenyewe za kuunganisha chama chao katika mshikamano na vyama vya kigeni na serikali zilizokuwa zikiunga mkono harakati za ukombozi.  



No comments: