Abubakar
Mohamed Saleh Tambaza 1959 - 2012
Ukitaka kumjua Abubakar itabidi
kwanza uanze na wazee wake. Ukoo wa Tambaza historia yao Dar es Salaam
inakwenda zaidi ya miaka mia moja na zaidi na hii ni historia ambayo inaweza
ikaelezwa na wao wenyewe kwa kukuonyesha yale yalioachwa na wazee wao kuanzia
Kariakoo, Kisutu sasa sehemu ya Mtaa wa Bibi Titi, Upanga na Mabibo ambako kwa
sasa ndiyo yalipo makaburi yao. Ukianzia eneo la Upanga hodhi yote ile ilikuwa
mali yao. Makaburi yao mengine ya wazee wao yapo Upanga ambapo sasa umejengwa
Msikiti wa Maamur. Lakini kubwa ni jinsi wao wenyewe wanavyoweza kuhadithia kwa
njia ya ajabu sana habari za wazee wao hao kwa uhakika kabisa hadi kuishia kwa
Bwana Abdallah aliyekuwa Jumbe wakati wa ukoloni wa Waingereza. Msikiti wa
Kisutu maarufu kama Msikiti wa Mwinyi Kheri Akida ambao ulijengwa na Sheikh
Mwinyikheri Akida katika miaka ya mwisho ya 1800, ni msikiti wao na hadi sasa
uko chini ya uongozi wao. Huyu Sheikh Mwinyikheri Akida ni katika mababu zake Abuu.
Kwa uhakika kabisa ni babu wa babake Abuu Marehemu Mzee Mohammed Saleh Abdallah
Tambaza.
Historia ina kawaida ya
kujirudia. Sheikh Mwinyikheri Akida aliishi Kisutu ambayo ni sehemu ya mwanzo
ya makazi Dar es Salaam. Sheikh Mwinyikheri Akida alikuwa katika masheikh
wakubwa wa wakati wake na alikuwa na sifa kubwa ya ucha Mungu. Sheikh
Mwinyikheri Akida alipofariki miaka ya mwanzo ya 1900, Dar es Salaam ilitaka
kumpa maziko makubwa sana. Abuu kama
babu yake, ambae kati yao wametenganishwa na zaidi ya miaka mia moja maziko
yake yamefuata nyayo zile zile. Dar es Salaam kama ilivyotoka kumzika babu yake
mkuu miaka mia iliyopita iliamka kwa kishindo kuja kumzika mwana mji Abubakar
Mohamed Saleh, kijana wa Kariakoo, mtu mwema na karim, aliyependa kusaidia
aliyemjua na asjiyemjua, msheshi, mtu wa maskhara na aliyejikurubisha kwa kila
mtu kwa mapenzi na bashasha bila kujali hali yake.
Dar es Salaam huwa ina kawaida ya kulala usingizi ikawa
huisikii kabisa na wakati mwingine ukasema haipo. Lakini Dar es Salaam hiyo
hiyo ghafla huzinduka ikaamka kwa kishindo kikubwa na kwa hakika kila mtu
akashtuka akasema, “Ala kumbe Mzizima na watu wake bado ipo.” Hali hii hutokea
kwa ghafla na bila taarifa pale Dar es Salaam inapompoteza mtu wake. Hapo ndipo
utaijua kuwa Dar es Salaam ingalipo na ina watu wake. Achana na maneno kuwa Dar
es Salaam hii ya sasa ati haina mwenyewe. Hakuna mali isiyokuwa na mmiliki
wake. Utaijua Dar es Salaam ina wenyewe mmoja wa watoto wa Dar es Salaam
anapokutwa na fardhi (mauti). Maziko ya Abubakar Mohamed Saleh wa Tambaza,
hayajapata kuonekana. Dar es Salaam ina historia ya maziko ya watu wake. Kumbukumbu za mazishi katika historia ya Dar es
Salaam zinaonyesha kuwa mazishi ya kwanza makubwa yalikuwa ya Sheikh Idrissa
bin Saad. Sheikh Idris alifariki mwanzoni mwa miaka ya 1950 na alizikwa ndani
ya msikiti wake Mtaa wa Narung'ombe, Kariakoo. Jeneza lilitoka nyumbani kwake
na nyumba yake ikitazamana na msikiti wake lakini ilikuwa kazi kubwa
kulifikisha jeneza msikitini jinsi umma ulivyokuwa umejaa. Mkanyagano juu ya
mkanyagano. Maziko makubwa mengine yalikuwa ya Sheikh Kaluta Amri Abeid
aliekuwa Waziri wa Sheria katika Serikali ya Awamu ya Kwanza. Sheikh Amri Abeid
alifia Ujerumani mwaka 1963 na maiti yake ilirudishwa nchini na kuzikwa katika
makaburi ya Chang'ombe. Yakafuatia mazishi ya Abdulwahid Sykes mwaka 1968 ambae
alizikwa makaburi ya Kisutu. Maziko ya Abdulwahid Sykes yaliacha historia.
Ilikuwa nani ni nani katika Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza Nyerere
alionekana akitembea kwa miguu nyuma ya jeneza kutoka nyumbani kwa mama yake
Abdu Mtaa wa Lindi kuja Msikiti wa Kitumbini.
Baada ya hapo yakaja mazishi ya Sheikh Kassim bin Juma mwaka 1993. Umma
uliojitoleza kuja kumzika Sheikh Kassim ulitisha.
Dar es Salaam ina historia ya
kuwaenzi watu wake maarufu. Sheikh Idrissa alikuwa Khalifa wa Tarika
Askariyya aliyoianzisha yeye mwenyewe. Tarika hii ina murid wengi
kutoka sehemu za Rufiji na Kilwa. Sheikh Amri Abeid alikuwa katika kundi la
Waislam wa mwanzo kushika madaraka ya juu serikalini. Abdulwahid alifahamika zaidi
kwanza kutoka kwa sifa aliyokuwa nayo baba yake katika jamii wakati wa ukoloni
wa Wajerumani hadi kuingia kwa Waingereza. Lakini kubwa kwa Abdulwahid ni kuwa
alikuwa mwanasiasa kijana, muasisi wa TANU na watu wa Dar es Salaam walimjua kama
mtu aliyemkaribisha Nyerere mjini na kumwingiza katika harakati za siasa.
Sheikh Kassim Juma jinsi vyovyote ingevyotokea, Allah alimpa kipaji cha ajabu
akifika mahali hata kama palikuwa pamepooza basi patachangamka. Katika siku za mwisho za uhai wake alitofautiana
vibaya sana na serikali. Hii ilimpelekea yeye kukamatwa na kutupwa gerezani na
baadae akafa huku kesi yake ikiwa bado ipo mahakamani.
Wote hawa walikuwa na michango
yao kwa mji wa Dar es Salaam ingawa kwa viwango tofauti, na watu hawa walipokufa
watu wa Dar es Salaam walitoka kuja kuwapa heshima zao walizostahili kama
viongozi na mashujaa wa taifa hili. Mazishi ya watu hawa wote waliokuwa na
majina makubwa ya kutajika katika vyombo vya habari na wakialikwa katika hafla
kubwa kubwa za kitaifa hao wote mazishi yao hayakufikia maziko ya Abubakar
Tambaza hata kwa mbali. Yapo maziko mengine makubwa lakini hatuwezi kuyataja
yote mathalan maziko ya Rubani wa Ndege za Kivita, Said Karama, maziko ya Mzee
Maneno Kilongora, maziko ya hivi karibuni ya baba yetu mrehemu Mzee Kitwana Dau
na mengine mengi. Sasa iweje Abuu kijana wa Kariakoo, mtu wa kawaida kabisa,
mtu ambae sura yake haikupata hata kutokea katika gazeti wala runinga, apewe
maziko makubwa kupita watu hao wote waliokuwa maarufu na wenye majina ya
kutajika? Iweje leo Abuu anasomewa visomo leo Msikiti wa Makonde, kesho Msikiti
wa Mtoro, nk. Nani huyu Abubakar Tambaza kiasi awe mpenzi wa kila mtu wa kila
msikiti?
Lazima nikiri kuwa nilishtuka
nilipofungua gazeti la “Mwananchi” na kukuta picha ya Abuu na chini yake ipo
taazia iliyoandikwa na Dk. Ramadhani Dau. Haukupita muda napokea ujumbe a simu
kuwa ipo taazia nyingine ya Abuu katika “Uhuru” na “Jambo Leo” zote zimeandikwa
na Dk. Dau na amenunua ukurusa mzima kuomboleza kifo cha rafiki yake. Kwa
hakika nilipigwa na butwaa. Mimi Abuu ni mdogo wangu kwa maana halisi ya neno
lenyewe. Kaka yake Abuu, Abdallah Mohamed Tambaza ni rafiki yangu toka utoto na
tulisoma sote St. Joseph’s Convent katikati ya miaka 1960 na hadi leo ni rafiki
yangu kipenzi. Isitoshe wazee wetu wakijuana. Taazia zile tatu zote zimetoka
siku moja tena kwa kurasa ya kulipiwa na ukurusa mzima kwangu mimi kitu hicho
kilikuwa jambo geni. Sijapata kuona kitu kama hiki kabla. Kitendo cha Dk. Dau
kumlilia rafiki yake kwa namna ile kilinidhihirishia mapenzi ya hali ya juu
kati ya watu hawa wawili. Dau aikuwapo hospitali Hindu Mandal wakati rafiki
yake yuko katika sakarat maut na bila
shaka ninavyomjua Dau pale alipokuwa kwa hakika kabisa Yasin ilikuwa ikimtoka. Watu waliokuwa wakipendana na wakajahitimishana
namana hii ni wa kuliliwa ngoa. Fikra zangu zilirudi nyuma mara ya mwisho mimi
na Abuu tulipokuwa ofisini kwa Dk. Dau. Baada ya maskhara yao kama kawaida Dau
aliagiza na mara sote wawili tukaletewa zawadi za NSSF katika mifuko maridadi. Mimi
kama mwandishi kila niwapo huwa na zana zangu za kazi. Niliwaomba niwapige
picha na nikawapiga picha pamoja, ndugu wapenzi marafiki wawili. Haukunijia
hata kidogo kwa wakati ule kuwa picha ile itakujakuwa kumbukumbu kubwa ya
majonzi.
Msomaji wangu ungepata bahati ya
kuwakuta watu hawa wawili katika barza wanazungumza wewe usingelitia lako
ungekaa kimya usikize. Mimi nikifanya hivyo kila nilipokuwanao pamoja. Kwanza
ngoja nikufahamishe kitu. Ikiwa unataka kukisikia Kiswahili cha pwani kwa
lafidhi yake halisi ilikuwa umsikize Abuu akizungumza. Mimi kwa vijana wa leo
sijapata kumsikia kijana aliye na ulimi aliokuwanao Abuu. Hilo moja. Sasa
ngoja nirudi kwa sahib wake Dau. Dk. Dau
ana ulimi kama aliokuwanao Abuu lakini hakumshinda na hili naweza kulieleza.
Ingawa wote wamekulia katika mazingira sawa ya mjini na kukisema Kiswahili kwa
lafidhi ya pwani iliyonogeshwa kwa wao kusoma Qur’an iliyonyoosha matamshi yao,
Dk. Dau kwa kiasi kidogo sana kaathirika na kule kusoma Kizungu sana. Matamshi
ya Dk. Dau hayatoki na ile ladha
unayoisikia kwa Abuu. Sasa wanapopambana katika baraza ilikuwa raha na
wote wana barza huwa kimya wakiwasikia wanavyopashana. Raha ilikuwa katika
ujuzi wa lugha na pili katika kule kupeana maneno. Dau atamuambia Abuu huku
akicheka sana, “Abuu leo sheikh nimekuwa sina maana, ushasahau nilivyokuwa
nakuvusha barabara Morogoro Road tunakwenda shule...” Barza itaangua kicheko.
Abuu atarudisha mapigo sasa kawageukia wasikizaji, “Jamani hebu semeni wenyewe
huyu kwa ukubwa gani aliokuwanao kiasi yeye anivushe mie barabara. Mimi siwezi
kuwa mwizi wa fadhila kama yeye leo kasahau kama kuwa mimi ndiye nilkuwa nikiwatisha
watoto wa Kihindi shule wasimpige...” Hapo vicheko vinaongozeka. Hapo pembeni
yuko mzee wetu mkubwa wa barza na mwenyekiti wa kudumu, Mzee Kissinger, Mohamed
Khalil, Jamil Hizam (Denis Law), Panji (mdogo wake Abuu) na jamaa wengine
dhumna inakwenda lakini watu wameshikilia mbavu kwa kicheko. Mzee Kissinger ni
kamusi inayotembea kuhusu historia ya Dar es Salaam na watu wake. Jamil Hizam
alikuwa mcheza kandanda hodari katika miaka ya 1960 hadi 1970 ndiyo watoto wa
mwanzo kutoka Dar es Salaam kucheza timu ya taifa ya vijana Tanzania. Jamil katika ujana
wake akimuhusudu Denis Law mchezaji wa Uingereza na jina akalipata la shujaa
wake. Dau na Abuu wanatazamana kila mmoja anasubiri mashambulizi. Abuu kama
vile namuona kaegemea ukuta, kofia yake kaibenjua kwa mbele. Dk. Dau na yeye
yuko katika darzi yake na kofia kaiweka upande kwa mvao maarufu wa watu wa
Mafia.
Hawa ndiyo marafiki wawili ndugu
waliopendana na wakaonyesha mapenzi yao kwa dhati ya nafsi zao na kwa vitendo.
Dk. Dau mkurugenzi wa shirika kubwa, alipata kuwa mhadhiri Chuo Kikuu Cha Dar
es Salaam amekaa barazani kwa rafiki yake Abubakar, Kariakoo Mtaa wa Kongo
kamfuata kumjulia hali. Kwake yeye Abuu ni yule yule Abuu rafiki yake, cheo
chake cha ukurugenzi na kisomo chake hakikuathiri hata chembe uhusiano wao.
Wangapi leo wanayaweza haya. Tunayo mifano mingi ya baadhi ya jamaa zetu
wakiingia katika nafasi basi husahau rafiki zao wa zamani na kuwanyanyapaa wakajishughulisha
na hao ambao wao huwaona ndiyo “stahili” zao kwa kuwa ni “wakubwa” kama wao.
Wakawa wao ni watu wa Gymkhana Club na mahoteli makubwa ya fahari.
Katika taazia ya Dk. Dau, Dau
amesema Abuu alikuwa na uradi aliodumu nao hadi anakufa nao ni kuandaa chakula
asubuhi na jioni kuwakirimu watu. Neno “uradi” alotumia Dau ni neno zito sana
na kwa hakika kalitia mahali pake ingawa si kwa kawaida kwa neno hilo kutumika
hivyo. Wengi tumezoea neno “uradi” kuwa dua asomayo mja khasa katika kumuhimidi
mola wake. Dk. Dau katufahamisha kuwa uradi wa Abuu ulikuwa kutoa sadaka ya
chakula asubuhi na jioni. Hakika mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Uradi huu
umenikumbusha baba yake mkubwa Abuu, Bwana Yahya Saleh. Mzee Yahya akikaa Mtaa wa
Kariakoo na Sikukuu na ilikuwa ada ya akina Tambaza watoto na wazee wao kuswali Ijumaa msikitini
kwao, Msikiti wa Mwinyikheri Akida na baada ya sala wote kuongozana hadi
nyumbani kwa Mzee Yahya kwa chakula cha mchana. Kama vile ni jana fikra zangu
zinanirudisha nyuma. Namuona Mzee Yahya Saleh, mdogo wake Mohamed Saleh, Bwana
Mwinyimadi, wametangulia mbele nyuma wanafuatia watoto wao, Abdallah Mohamed
Saleh, Saleh Yahya, Abubakar, Mahdi (sasa ni sheikh) na sisi wengine ingawa si
akina Tambaza lakini katika ule wali haulizwi mtu ni wa nani unakaa jamvini
unanawa unakula. Dua inasomwa kisha mnatawanyika. Uradi huu uliendelea pale
Kariakoo nyumbani kwa Mzee Yahya Saleh hata baada ya kifo chake. Niliposoma
kuwa Abuu yeye kenda mbele zaidi ya wazee wake kwa ukarimu kuwa yeye kutoa
chakula ni uradi wake wa kila siku na kubwa zaidi ulezi wa mayatima,
nilishukuru. Abuu aliwachukua watoto wa mitaani akawatia katika timu ya mpira
Bom Bom. Watoto hawa kwa kiasi kikubwa walipata malezi na maadili mema. Timu
hii ni ya watoto wadogo ni maarufu sana Kariakoo. Ikutoshe tu katika watoto
hawa wawili hivi sasa ni wachezaji katika Club ya Simba. Hii leo vijana hawa si
watoto wa mtaani tena vijana wanaoendesha maisha yao na kutoa mchango katika
taifa. Vilevile kwa miaka kadhaa alikuwa akiliendesha kombe lake la kila mwaka
la Tambaza Cup. Mashidano haya yamekuwa maarufu na limetoa msisimko wa pekee
kwa vijana wa Kariakoo.
Kwa hakika wasifu wa Abubakar
Mohamed Tambaza ni mrefu na siwezi kuumaliza katika siku moja. Abubakar alikuwa
mwanasiasa, mwanamichezo mpenzi wa wa Sunderland. NImelitumia neno hili
“Sunderland” kwa makusudi sasa ni Simba Sports Club. Abuu na rafiki zake akina Mshike,
Matimbwa wengineo hufurahi sana ukiwanasibisha na Sunderland kwa kuwa
unawakumbusha mbali. Baba yake Abuu Mzee Mohamed Saleh alikuwa mchezaji wa
Sunderland katika ujana wake kasha akaja kuwa kiongozi wa Simba katika miaka ya
1970 akwa Mtunza Fedha. Baba yake mkubwa Bwana Yahya alipata kuwa Mbunge wa Dar
es Salaam mkwaka wa 1970 hadi 1975 wakati huo haijagawiwa. Mzee Yahya Saleh
alimwangusha Balozi Tatu Nuru (sasa marehemu). Mzee Yahya Saleh alikuwa
mmoja wa wanachama shupavu wa TANU Tawi la Mvita wakati wa kudai uhuru wa
Tanganyika. Tawi hili lilikuwa Mtaa wa Mvita Dar es Salaam Kaskazini chini ya
uongozi wa Mtoro Kibwana kama mwenyekiti na Sheikh Hadair Mwinyimvua kama
katibu. Ilipofika mwaka wa 1957 Yahya Saleh akachaguliwa kuwa mwenyekiti wake.
Lakini asili ya tawi hili lilianzia Kisutu kasha likahamia Mtaa wa Mvita. Mtoto
wa Sheikh Haidar Mwinyimvua ndiye imam hivi sasa wa Msikiti wa Mwinyikheri
Akida. Inasemekana katika Tanganyika nzima hapakuwa na tawi la TANU lililokuwa
na nguvu kama tawi hili. Abuu alikujafuata nyayo hizi hizi za wazee wake katika
siasa. Alitoa mchango wake katika tawi lake la Jangwani kwa kadri ya uwezo wake
akiwa Mwenyekiti Serikali ya Mtaa CCM Kata ya Mtambani B Mtaa wa Kongo kwa
vipindi vitatu mfululizo. Vilevile Abuu
alikuwa Mwenyekiti CCM Tawi la Jangwani ambalo limejumuisha hata Makao Makuu ya
CCM Ofisi Ndogo Mtaa wa Lumumba. Tawi hili la la Jangwani hii leo unaweza
kulifananisha na tawi lile la Mvita wakati wa kudai uhuru. Vilevile alikuwa
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Ilala. Hii ni kamati kubwa sana katika
CCM.
Naambiwa kwenye mazishi yake
waheshimiwa wote walikuwapo wakipigana vikumbo. Mbele ya nyumba yao Mtaa wa
Congo No. 1. Kilipokuwa kinara palijaa wanawake ikabidi wanaume wasogee mbele
mitaa ya jirani. Hili si jambo la kawaida kwa kuwa kisomo sasa kitasommwa kwa
mbali na nyumba ya msiba. Wanasema Dar es Salaam haijapata kushuhudia wanawake
wengi kiasi kile katika msiba. Uani kwenye nyumba ya shughuli walijazana
wanawake wa kila umri. Sheikh Zuberi alikpokwenda uani kuwafariji alipewa sifa
ya Abuu kuwa alikuwa kimbilio lao kila walipokuwa na matatizo na aliwasaidia na
kuwawekea heshima zao. Uani kulikuwa vilio na kwiki. Mtaa wa Kongo na mitaa ya
jirani ilikuwa haipitiki. Kila utakapoingilia, iwe umeingia kwa Mtaa wa Twiga,
au Nyati, Matumbi au kutokea Mtaa wa Msimbazi au Swahili kuingia mitaa ya
jirani kama Rufiji ilibidi uishie huko huko haikuwezekana kuifikia nyumba ya
shughuli. Sala ya jeneza haikuweza kuswaliwa msikitini kwa kuwa hapakuwa na msikiti
ambao ungeliweza kuchukua umati ule wa Waislam waliokuwa pale. Ilibidi sala ile
iswaliwe palepale nyumbani kwao mbele ya uwanja wao. Haya yalipataikana kuonekana mara moja tu
katika historia ya Dar es Salaam. Kwanza ilikuwa katika maziko ya Prof. Malima
na pili maziko ya Abubakar. Msafara wa kuelekea shambani kwao Mabibo
ulisindikizwa na askari wa Usalama Barabarani vinginevyo ingelikuwa shida
kuupitisha umma ule wa magari Barabara ya Morogoro hadi Port Accees Road na
kuingia Mabibo
Mkono wangu wa pole uende kwa
mama yetu Biti Selemani Nyaubuguyu ambae kila siku akimtia machoni Abuu. Huyu
Bi Mkubwa mimi ni mama yangu. Siku moja nilifika pale nyumbani baada ya miaka
mingi na katika mazungumzo akanambia, “Mimi nikimfahamu mama yako pale Kipata.
Mimi nilipoolewa na baba yenu nilikuwa nakaa kwa Mama Nambaya.” Mama yangu kafa
1956 na huyu Mama Nambaya alikuwa shoga ya mama yangu. Hadi miaka ya 1970
nilikuwa nikipita kumwamkia Mama Nambaya na alikuwa akifurahi sana na wakati
mwingine akinihadithia habari zangu kuwa mama yangu alikuwa akitaka kwenda
sokoni alikuwa akiniacha kwake hadi arejee. Mwanae Shabaka alibaki kama kaka
yangu mkubwa hadi alipofariki kiasi miaka mitatu iliyopita. Mkono wangu wa pole
umfikie Dk Dau. Hapa sitasema mengi. Nampa pole kaka yake Abubakar rafiki
yangu, Abdallah Mohamed Saleh wa Tambaza. Hakika tumeondokewa na Dar es Salaam
ina haki ya kuwa mkiwa. Mola atupe sote moyo wa subira. Tunamuomba Allah
amsamehe Abubakar madhambi yake na amjazie pale palipopungua na amlipe pepo.
Amin.
Mohamed Said
15 January 2012
No comments:
Post a Comment