Mkasa
Wangu wa Kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Mwl.
Nyerere, Dar es Salaam Mwaka 2006
Sehemu ya Kwanza
| Mwandishi Akiwa Katika Mkutano Tehran Iran 2007 |
Mohamed Said
Mwaka 2006 Radio Tehran walipendekeza jina langu
kwa Wizara ya Mambo ya Nje Iran wanialike katika hawli ya Imam Khomeni. Sababu
ya kualikwa ni kuwa mara kwa mara nilikuwa nikifanya mahojiano na Radio Tehran
Idhaa ya Kiswahili kuhusu siasa za Tanzania hususan wakati wa uchaguzi mkuu wa
mwaka 1995 na ikatokea kuwa yale mahojiano yangu yakawa yanapendwa na
wasikizaji wa Afrika ya Mashariki na Kati na sehemu za Emirati. Nilikwenda Iran
na waalikwa walikuwa kutoka dunia nzima
na wa kila aina, waandishi, wahadhiri wa vyuo vikuu, wasomi wa kawaida, mawaziri
wa serikali kutoka nchi tofauti na watu wengine wengi. Msafara wetu wa wageni
kwenda mahali ulikuwa ni msururu wa mabasi zaidi ya kumi yakisindikizwa na
kimulimuli cha polisi. Kutoka Tanzania nilikuwapo mimi pamoja na waandishi
kutoka Daily News na Kituo Cha TV cha Channel Ten. Nikiwa Tehran niliingia studio
za Radio Tehran Idhaa ya Kiswahili na tukafanya mahojiano na mtangazaji wao
mashuuri Abdulfataa Mussa na wenzake na vilevile kurekodi vipindi vingi kuhusu
hali ya Waislam Tanzania.
Mambo yalianza wakati sasa narudi Dar es Salaam na
ndege ya Emirates iliyokuwa inatua usiku. Inaelekea maofisa wa pasi pale
uwanjani walikuwa na taarifa zangu mapema na walikuwa wakinisubiri kwa hamu
kubwa kwani nilipotoa pasi yangu kwa afisa wa pasi hapo ndipo shughuli za
kunishughulikia zilipoaanza. Mimi sikuwa na hili wala lile. Nikawa namuona yule
dada aliyekuwa kwenye kile kizimba akikukurika na pasi yangu akiitia katika
mashine na kuitoa mara kadhaa. Fikra iliyonijia kwa haraka ilikuwa mashine ni
mbovu na harakati zile zilikuwa ni kurekebisha mitambo. Kumbe sivyo wahusika nadhani
walikuwa wanahakikisha kuwa mimi ndiyo huyo waliokuwa wakimwinda na kumsubiri na
sasa kapatikana, kaingia mwenyewe kwenye mtego na kanasa. Yule afisa wa pasi
akanambia nikae pembeni natakiwa kwa mahojiano na watu wa usalama. Hofu haikuwa
imeniingia kwa kuwa nilikuwa natambua kuwa harakati dhidi ya ugaidi zilikuwa
zimepamba moto na labda nilitakiwa kwa mahojiano mafupi kutaka kujua nyendo
zangu. Sikujua wala kutarajia kuwa mshtuko mkubwa ulikuwa unanisubiri.
Nilichukuliwa hadi kwenye chumba kimoja na hapo
niliwakuta maofisa wa usalama watatu wakanikaribisha kwa taadhima kisha
wakanambia kuwa niko chini ya ulinzi kwa kuwa zimewafikia taarifa zangu kuwa
mimi nasafirisha mihadarati. Mpaka hapa sikuwa na hofu bado ilinijia picha kuwa
yawezekana wamefananisha majina. Niliwaambia huenda Mohamed Said muuza madawa
ya kulevya siyo mimi niliye mbele yao. Wakaniambia kwa kujiamini kabisa kuwa
taarifa zao ni madhubuti muuza unga ni mimi na wamekuwa wakinifuatilia siku
nyingi. Hapo ndipo walipotoa pasi yangu
na kuniomba niitambue kama hiyo pasi ni yangu au la. Niliwajibu kuwa hakika
hiyo ndiyo pasi yangu khasa. Wakaniamuru sasa tutoke twende nikachukue mizigo
yangu ili wafanye upekuzi wa mihadarati katika mizigo niliyotokanayo Tehran.
Hapo ndipo nilipojuwa kuwa niko katika lindi kubwa la matatizo na ubongo wangu
ukaanza kufanya kazi kwa haraka huku nikosoma dua kumuomba Allah ulinzi wake
kwani kwa hakika nilijua kama ni njama zimekamilika na leo imefika siku yangu. Nikajiuliza
itakuwaje watakapotoa madawa kwenye mizigo yangu. Nikaanza kufikiri vichwa vya
habari vya magazeti yatakavyopambwa na habari zangu. Ikanijia yakini kuwa watu
wa usalama wameniwekea madawa ya kulevya katika mizigo yangu ili waniangamize
na maadui zangu wapumzike na shari yangu.
Nilimgeukia yule ofisa mkuu aliyekuwa ananihoji
nikamwambia kuwa sitokubali kugusa mizigo yangu bila kuwapo mashahidi isijekuwa
mizigo yangu ishawekewa hayo madawa ya kulevya kwani nilikotoka Tehran mizigo
ilikuwa imekaguliwa na ilikuwa salama. Hoja yangu kubwa kwao ilikuwa kupata
uhakika kutoka kwao kuwa wananijua vizuri kiasi cha kuthibitisha kuwa kweli mie
ni msafirishaji wa madawa ya kulevya. Jibu nililopewa ni kuwa wao wanafanya
kazi kutokana na taarifa zilizowafikia. Wakasema, “Sisi tunazo taarifa zako
kamili kuwa wewe ni msafirisha madawa ya kulevya.” Nikawauiza,“Baada ya
kupata taarifa hizo zangu nyie mmechunguza kutafuta ukweli?” Wakasema, “Ndiyo
maana leo tumekukamata.” Nikawaambia, “Si kweli kama kwa sababu mie nafahamika
Dar es Salaam takriban kwingi maana ndio nilikozaliwa na kukulia. Hapo Kariakoo
ukiwaambia watu kuwa Mohamed ni “Mzungu wa Unga” kila mtu atacheka maana huo
kwao ndugu zangu ni mzaha mbaya.” Walitaka kujua nilkwenda kufanya nini Iran.
Niliwaambia nilialikwa na serikali ya huko kuhudhuria mkutano. Wakataka kujua
vipi nilipata mwaliko. Nikawajibu kuwa hilo swali sina jibu labda waiulize
serikali ya Iran. Nikawaeleza kuwa mbona siku zote napita hapo uwanjani nikenda
sehemu tofauti duniani kwa mialiko na kutoa mada sijakamatwa kimezidi nini
katika hii safari ya Iran? Niliwaeleza kuwa miezi michache iliyopita nilikuwa Chuo Kikuu Cha Ibadan kwa
mwaliko tena mkutano umefadhiliwa na serikali ya Marekani na
wamenipa na tiketi toka Dar es
Salaam hadi Lagos na kuniweka hoteli na kunilipa fedha. “Mbona hamkunikamata
wakati ule?” Nikafungua mlango mwingine nikawaambia, “Nakuapieni nyie
msingethubutu kumkamata Mkristo anaetoka Vatican mkutanoni. Lakini kwa kuwa mie ni Muislam
sina wa kunitetea. Nchi hii nani atakuuliza kwa kumnyanyanyasa
Muislam?” Walishtuka na wakawa wanyonge sana wakasema si kweli kuwa naponzwa na
dini yangu.
Baada ya kukurukakara nyingi na mabishano makubwa kuhusu
mie kukubali kufanyiwa upekuzi wa mizigo yangu alikuja binti mmoja katika wao
na yeye akanihakikishia kuwa wao ni serikali na sio wahuni. Hawathubutu
kuniwekea dawa katika mizigo yangu hivyo akanisihi sana kwa upole nikubali ili
wajitoe wasiwasi na wataniachia endapo hakuna kitu. Niliomba apatikane shahidi
wa kushuhudia mizigo yangu kabla ya kufanyiwa upekuzi lakini hakuna mtu
aliyekubali kuchukua dhima ile katika maofisa waliokuwa kazini pale uwanja wa
ndege usiku ule. Upekuzi ukafanyika hadi mwilini. Hakuna kitu. Wakanipela
katika choo maalum cha kutolea madawa kwa njia ya haja kubwa. Nikakataa
kujisaidia pale. Ilikuwa ndio mara yangu ya kwanza kuona choo kama kile. Choo
chenyewe ni cha aluminium. Tofauti na vyoo vya pale ambavyo siku zote ni
vichafu, hiki kilikuwa kisafi sana kiasi mtu unaweza hata kutengewa chakula na
akala bila ya kuhisi kinyaa.
Nilitegemea wataweka ahadi yao kuwa ikiwa
hawatakuta madawa ya kulevya katika mizigo yangu watanirejeshea uhuru wangu
wataniachia niende nyumbani. Haikuwa hivyo. Wakanirudisha ofisini kwao. Sasa
wakaacha madawa ya kulevya wakahamia katika vitabu na “audio cassette”
nilzokuwa nimepewa kama zawadi kule Tehran wakaniluliza kwa nini naingiza vitu
vile khasa kanda za Khomeni na vitabu vyake nchini. Nikawauliza, “Kwani kanda
na vitabu vya Khomeni haviruhusiwi kuingizwa Tanzania? Maana mimi hata nyumbani
kwangu hii leo mkifika nina vitabu vya Khomeni na wanafalsafa wengine kama Karl
Marx ambao nimesomeshwa pale Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Sasa hapo ikaja kejeli. “Ala wewe
mtu wa Kariakoo lakini umefika hadi Chuo Kikuu!” Sikujibu kitu. Awali
waliponitia mbarani waliniuliza kwetu na
nikawaeleza kuwa nimezaliwa Kariakoo.
Hawakunipa jibu kuhusu kuingiza vitabu na cassette
za Khomeni. Ikawa sasa kama vile wameishiwa maswali. Nikaona kuwa sasa ni zamu
yangu nami kuwapiga maswali.
Yule aliekuwa akinihoji nikamwambia,
“Mimi wewe nakufahamu vizuri sana kwa sababu ukicheza mpira Simba Sports Club
na mie ni mpenzi wa club hiyo toka utoto wangu wakati huo ikiitwa
Sunderland na mmoja wa baba zangu alikuwa mchezaji marufu wa club hiyo katika miaka
ya 1950 akafiikia hadi kucheza Kombe la Gossage.” Nilihisi amepata mfadhaiko
kidogo akanambia,“Unanifananisha yule aliekuwa akicheza Simba ni ndugu yangu.” Alikuwa
anasema uongo lakini mie nikamkubalia. Hapo nikajua kuwa nishampata sasa hana
nguvu tena ya kuuliza maswali. Kusema uongo ni dalili ya kujihami. Nikamrushia
kombora lingine, “Sasa tuhuma za madawa ya kulevya zimekwisha tuko katika kwa
nini naingiza vitabu vya Khomeni nchini?” Akanijibu kinyonge, “Tumeridhika
huna madawa.” Kufika hapa tukawa tumemaliza mahojiano.
Wakati huo sasa ni usiku wa manane na nishapeleka
SMS kwa sahib yangu mmoja bingwa wa mambo ya mtandao wa kompyuta kumjulisha
kuwa nimekamatwa uwanja wa ndege kwa tuhuma za uongo za kuvusha mihadarati na
yeye ile kuipata tu ule ujumbe wangu akaifahamisha dunia kuwa nimekamatwa
uwanja wa ndege nikitokea mkutanoni Iran na nimebambikiziwa tuhuma za kuingiza
nchini mihadarati. Waliponitia mbaroni tu walinionya kuhusu kutumia simu yangu
ya mkononi lakini bahati nzuri hawakuninya’ganya. Aliyenipa onyo hili alikuwa
mkuu wa kituo cha polisi cha uwanja wa ndege. Huyu rafiki yangu akawa
kanisaidia sana maana hadi kumekucha wapenzi wangu wote ndani na nje ya nchi pamoja
na vyombo vya habari vinavyonifahamu walikuwa na taarifa za kukamatwa kwangu. (Kwa
kipindi takriban miaka ishirini nyuma kwa nyakati fofauti nimekuwa nifanya mahojiano
na radio zote muhimu kama, BBC, VOA, Sauti ya Ujerumani, Sauti ya Iran
nk.).
Nikawaomba
wale watu wa Usalama waniachie basi nende zangu kulala nyumbani nirudi hapo
kesho asubuhi kwa kuwa sikuwa nimebeba madawa ya kulevya. Wakaniambia, “Itabidi
tukulaze hapa hadi asubuhi wakubwa wetu watupe amri ya kukuachia. Maana amri ya kukukakamata wewe imetoka juu.”
In Sha Allah Itaendelea...
| Mwandishi (mmoja wa watoa mada) akiwa katika mazungumzo na mmoja wa vijana wa Kinigeria katika mkutano wa ugaidi uliofanyika Chuo Kikuu Cha Ibadan. Hisia ni kuwa huyu kijana alikuwa afisa usalama kutoka serikai ya Nigeria |
| Mwandishi Akiwa Katika Studio za Radio Tehran Iran Idhaa ya Kiswahili |
In Sha Allah Itaendelea...
1 comment:
Huu mkasa ni wa kusikitisha sana, na pale airport mambo haya yapo sana.
Nasubiria muendelezo wake.
Post a Comment