Mkasa Wangu wa Kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Mwl. Nyerere, Dar es Salaam Mwaka 2006 Sehemu ya Pili
Sasa hapo ikawa nimelipata jingine. Kumbe wauza
unga hawakamatwi hadi amri itoke juu. Sasa kama amri haikutoka ndiyo muuza unga
atapita aingize sumu zake mitaani? Hili likazidi kunidhihirishia kuwa kukamatwa
kwangu hakukuwa na uhusiano wowote na vita dhidi ya mihadarati bali ni vita vile
vile vikongwe dhidi ya Uislam.
Nikawa pale usiku kucha. Sasa
wakati niko pale wakidhani nimelala. Wakawa wenyewe kwa wenyewe wanazungumza kuhusu hii ‘operation’ neno
walilotumia ni kuwa 'leo tume-dial wrong number.' Wakawa wanasema, “Huyu bwana
mbona hakuelekea kama muuza unga tena huyu mtu bwana kasoma kweli kweli” Wanadhani
mie nimelala kumbe ni macho nawasikiliza. (Vipi utalala katikati ya
michongoma?). We umeona jinsi alivyokuwa akijibu na kuchambua mambo.” Hilo
ndilo likawa gumzo lao wakinisifia kwa ufasaha na mantiki lakini wakizungumza
kwa sauti ya chini kabisa. Hapa ikanidhuhirikia kuwa hawa vijana walikuwa
wanatimiza wajibu wao wa kazi tu lakini kiini khasa cha kukamatwa kwangu
hawakuwa wanakifahamu.
Walionikamata walikuwa vijana
kama wanne na wote walijitambulisha kwa majina ya Kiislam. Nilijua ni waongo
kwa kuwa Muislam anonekana katika uso na katika matumizi ya lugha. Lakini yule
mchezaji wa Simba ni Muislam na yeye ndiye aliekuwa mkubwa pale akiongoza ile
shughuli yote tena kwa kujidai na kujifaharisha sana. Kisa kile kile cha mtumwa
anelimishwa na yule anefanya kazi za ndani nyumbani kwa bwana. Ila kitu kimoja lazima nikiri. Wale vijana walikaa na
mimi kwa wema na hawakunibughudhi hata kidogo. Hata nilipokuwa nakwenda msalani
kijana alienisindikiza alinitaka radhi akasema, ”Nakusindikiza kwa sababu ni
sheria lakini sisi tunakustahi kwa hiyo utuwie radhi kwa kukufuta hadi msalani.”
Asubuhi wakubwa wakaja kazini
lakini hakuna alienikabili. Walikuwa wakinichungulia kutoka mlangoni kama simba
ndani ya kizimba kwenye zoo, nami nikawa najifanya siwaoni. Ndipo akaja mkubwa
mmoja tena akaniita kwa jina langu na kwa heshima na bashasha sana, "Bwana
Mohamed tuwie radhi sana pamekuwa na makosa kidogo tuwie radhi sasa hivi
tutakuruhusu uende nyumbani. ” Akatoka nje akawa akipiga simu. Kisha akarudi
ndani akaamrisha nibebewe mizigo yangu na gari la polisi linirudishe nyumbani. Kistaarabu
kabisa nikakataa gari ile huku nikifanya maskhara kuwa naogopa gari ya polisi
asijepiga simu akasema mrudisheni huyo mtuhumiwa. Ofisi nzima ikacheka. Hapo
ndipo wale wakamataji wangu wa usiku wakabeba mizigo yangu nami nafuata nyuma
tunatoka nje ya uwanja.
Kilichobaki sasa ni kueleza sababu ya mimi
kukamatwa. Mwaka wa 2006 Chuo Kikuu cha Ibadan, Nigeria kilifanya kongamano la
kimataifa hapo chuoni kwao kuzungumza kuhusu Ugaidi katika Afrika ya Mashariki
na Maendeleo (Conference on Islam, Terrorism
and African Development). Mimi ninlitoa mada iliyokuwa na anuani hii: Terrorism in East Africa the
Tanzanian Experience. Katika mada hii nilijikita mahsusi katika kuisema Marekani kwa
udhalimu wao duniani. Nikaeleza kuwa huo udhalimu wao ndiyo unaopelekea wao
kuchukiwa dunia nzima. Hapa ningependa kufahamisha kuwa mkutano huu wafadhili
wakubwa walikuwa Iran na Marekani. Saudi Arabia ilikataa kuchangia mkutano ule.
Wakati nasema maneno haya ya kuwakanyanga wenyewe Waamerika wapo hapo
mkutanoni.
Baada ya
kuwalani Waamerika sasa nikaigeukia serikali ya Tanzania na kuishutumu
vikali kwa kupitisha Sheria ya Ugaidi. Hapa nikaeleza kuwa Waamerika wasione
kuwa Tanzania imepitisha sheria hiyo ya ugaidi kwa haraka kwa sababu Tanzania
ina tatizo na ugaidi. Nikaeleza kuwa sheria hiyo imepitishwa kwa sababu Bunge
la Tanzania limehodhiwa na Kanisa na kupitishwa kwa sheria hiyo hakuna uhusiano
wowote na ugaidi ila Wakristo wamepata fursa ya bure ya kupambana na Uislam
wakitumia serikali ya Marekani kama upawa wao wa kuopolea chinyango ya moto
kwenye chungu kinachotokota. Nikauchekesha mkutano kwa kuwaambia kuwa
Wamarekani wamefanywa wajinga na Kanisa kwa kuchonganishwa na Waislam wa
Tanzania ambao hawana ugomvi nao asilani. Baada ya kusema hayo nikahitimisha
kwa kueleza nguvu ya Waislam Tanzania, kwanza kwa wingi wao na kisha kwa
historia yao iliyotukuka iliyodumu takriban miaka mia wakipambana na ukoloni wa
Wajerumani kwa silaha (1905 - 1907), kisha ukoloni wa Waingereza (1929 1961) na
kuhitimisha kwa kuleta uhuru na kuanzia 1961 hadi sasa wanapambana na nguvu ya
kanisa katika kupiga vita Uislam.
Kufikia hapa ukumbi ukawa umepata joto. Wanigeria
wamesimama kutaka niwaeleze vipi Waislam watakuwa wamepigania uhuru kisha wako
wengi nchini wanaruhusu wao kufanywa raia daraja la pili. Wakashangazwa kuwa hata
historia ya mashujaa Waislam waliopigana Maji Maji na kunyongwa na wakoloni na
mashujaa walipigania uhuru wa Tanganyika hawatajwi katika historia ya ukombozi.
Nilitoa majibu kadri Allah alivyoniwezesha. Nakumbuka kitu kimoja walichosema
wale ndugu zetu Wahausa. Walisema hali hiyo iliyoko kwenu haiwezekani kutokea
Nigeria kwa kuwa hiyo itakuwa na sawa na kutangaza vita. Kisha wakanihakikishia
kuwa sheria hiyo ya ugaidi haitapitishwa Nigeria hata siku moja.
Wapashaji habari wangu wakajanieleza baadae ni hili
hitimisho langu ndilo lililosababisha Wamarekani kuleta taarifa Dar es Salaam kutaka
taarifa zangu za “ugaidi” ikawa sasa sababu imeptikana ya mimi kushughulikiwa
na vyombo vya dola. Ndipo ikatengenezwa hadithi ya kuku na ng’ombe dume
(cock and bull story) kuwa Mohamed Said ni Mzungu wa Unga kwa hiyo akamatwe.
Mkasa huu ulinifika miaka sita iliyopita lakini
hadi leo kovu la mkasa ule limebaki katika pasi yangu. Sielewi pasi yangu
inaonyesha nini inapotiwa katika compyuta baada ya mkasa huu kwani kama mara
tatu husimamishwa kwa muda nakuombwa nitoe maelezo ya ziada kuhusu niendako
kila nisafiripo nje ya Tanzania. Nimeshuhudia hali hii Uwanja wa Ndege
Amsterdam na Detroit, Marekani. Berlin, Ujerumani niliambiwa mzigo wangu
umepotea lakini hata kabla sijatoka
uwanjani nikatafutwa na kukabidhiwa
mzigo wangu na kwa hili sikuwa peke yangu nilikuwa na mwenzangu, jamaa wa
Kiarabu kutoka Misri. Sijui kama mizigo yetu ilikuwa imebakishwa nyuma kwa
upekuzi zaidi. Amsterdam, Uholanzi baada ya kupita sehemu zote muhimu za
upekuzi wakati naelekea kituo cha mwisho niingie kwenye ndege inayoelekea
Detroit, Marekani nikachopolewa kutoka kwenye mstari na nikawekwa pembeni peke
yangu kwa usaili wa ziada. New York kadi yangu ya benki ilikataa kutoa fedha
kwa siku nzima hadi siku ya pili. Nilikujafahamishwa baadae kuwa “system”
ilikuwa inanichunguza kwanza. Ilikuwa siku ya pili baada ya kuonana na maofisa
wa benki ndipo kadi yangu ikaanza kutoa fedha. Geneva, Uswisi kadi yangu
ilikataa kutoa fedha katika mgahawa. Sikujua kama ni yale yale au haya yalikuwa
mengine. Lakini pasi hii afisa wa uhamiaji wa Tanzania alipoiingiza kwenye
compyuta yake alimwita mwenzake kuja kutazama kisha wakawa wanacheka. Waliona
nini kwenye pasi yangu Allah ndiye ajuaye.
Mwisho
25th February 2008
Nini kilisababisha mimi kukamatwa uwanja wa ndege kisha kuachiwa asubuhi yake bila kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kusafirisha madawa ya kulevya?
Ni kweli kuwa walikuwa na taarifa zangu za kufanya biashara hiyo?
Jibu ni kuwa haiwezi kuwa kweli na sababu ni kuwa nafahamika vyema.
Kwa nini walinikamata?
Jibu ni kuwa walikuwa na taarifa za mada niliyotoa Chuo Kikuu Cha Ibadan mwaka uliopita na maneno niliyosema kuhusu serikali ya Tanzania kuwa inatawaliwa na Kanisa Katoliki na jinsi nilivyoishutumu Marekani kwa uonevu wake duniani.
Maneno haya niliyasema mbele ya maofisa balozi wetu kutola Ubalozini Lagos na mbele ya Waamerika wenyewe ambao walikuwa pale pembeni na dawati lao makhususi wakifuatilia mijadala.
Waamerika walileta taarifa Dar es Salaam wa kutaka kunijua vyema.
Waamerika walinipa lebo ya ''terrorist sympathiser.''
Lebo hii naivaa kila niendako.
Wataalamu wameniambia kuwa lebo yangu si mbaya sana kwani inaniruhusu kusafiri.
Hakika lebo yangu si mbaya kwani mwaka 2011 Waamerika walinialika na nikafanya mhadhara Chuo Kikuu Cha Iowa, Iowa City na Chuo Kikuu Cha Northwestern, Evanston Chicago.
Kama wasemavyo wenyewe Waamerika hawana urafiki wa kuduu wala uadui wa kudumu.
Muhimu kwao ni maslahi yao.
Hakika lebo yangu si mbaya kwani mwaka 2011 Waamerika walinialika na nikafanya mhadhara Chuo Kikuu Cha Iowa, Iowa City na Chuo Kikuu Cha Northwestern, Evanston Chicago.
Kama wasemavyo wenyewe Waamerika hawana urafiki wa kuduu wala uadui wa kudumu.
Muhimu kwao ni maslahi yao.
Ushahidi wa haya nimeueleza hapo juu.
Katika hali kama hizi ndipo mimi nikashutumiwa kwa kuwa muuza madawa ya kulevya.
Sheikh Juma Kheri anashutumiwa kwa kufadhili magaidi kwa kuwa analipa mishahara walimu wa madras ya kijijini kwake.
Sheikh Chambuso anakabiliwa na kesi ya ''Kushawishi mauaji'' kwa kuwa alikuwa anatoa msaada kwa Waislam waliopigwa risasi katika ''operesheni ya kupambana na Al Shabab'' wa Madina na alikuwa anawatafutia watoto ambao wazee wao walishambuliwa na nyumba kutiwa moto msaada, watoto ambao tunaelezwa wameokolewa kutoka katika mafunzo ya ugaidi. Wanaficha ukweli kuwa hawa watoto walikuwa wanasomeshwa Qur'an na wengi wao wamehifadhi kuanzia juzuu moja hadi ishirini na kupita.
Tunaelezwa kuwa watoto hawa sasa wanafanyiwa mipango wasirejee tena katika mafunzo ya kigaidi.
Waislam amkeni.
Katika hali kama hizi ndipo mimi nikashutumiwa kwa kuwa muuza madawa ya kulevya.
Sheikh Juma Kheri anashutumiwa kwa kufadhili magaidi kwa kuwa analipa mishahara walimu wa madras ya kijijini kwake.
Sheikh Chambuso anakabiliwa na kesi ya ''Kushawishi mauaji'' kwa kuwa alikuwa anatoa msaada kwa Waislam waliopigwa risasi katika ''operesheni ya kupambana na Al Shabab'' wa Madina na alikuwa anawatafutia watoto ambao wazee wao walishambuliwa na nyumba kutiwa moto msaada, watoto ambao tunaelezwa wameokolewa kutoka katika mafunzo ya ugaidi. Wanaficha ukweli kuwa hawa watoto walikuwa wanasomeshwa Qur'an na wengi wao wamehifadhi kuanzia juzuu moja hadi ishirini na kupita.
Tunaelezwa kuwa watoto hawa sasa wanafanyiwa mipango wasirejee tena katika mafunzo ya kigaidi.
Waislam amkeni.
![]() |
| Sheikh Chambuso Rajab Ramadhani Chambuso |
| Mwandishi akiwa Capitol Hill Washington, DC |

No comments:
Post a Comment