Sunday, 5 January 2014

UDHALILISHWAJI WA WAISLAM NA VYOMBO VYA DOLA VYA TANZANIA SEHEMU YA KWANZA

UDHALILISHWAJI WA WAISLAM NA VYOMBO VYA DOLA VYA TANZANIA
Mkasa Wangu wa Kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Mwl.  Nyerere, Dar es Salaam Mwaka 2006
Mohamed Said

Mwandishi akiwa katika studio za Radio Tehran Iran  kulia kwake
ni Ahmed Rashid na kushoto Abdufatah Mussa
Wapenzi wa CUF wakienda mkutanoni wakati wa Uchaguzi Mkuu
Mwandishi na Watangazaji wa Radio Tehran
Mwandishi akiwa mkutanoni Tehran
Mwandishi akifanya mahojiano na Mtangazaji Abdufatah Mussa
Radio Tehran Iran


Mwaka 2006 Radio Tehran walipendekeza jina langu kwa Wizara ya Mambo ya Nje Iran wanialike katika hawli ya Imam Khomeni. Sababu ya kualikwa ni kuwa mara kwa mara nilikuwa nikifanya mahojiano na Radio Tehran Idhaa ya Kiswahili kuhusu siasa za Tanzania hususan wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 na ikatokea kuwa yale mahojiano yangu yakawa yanapendwa na wasikizaji wa Afrika ya Mashariki na Kati na sehemu za Emirati. Nilikwenda Iran na waalikwa  walikuwa kutoka dunia nzima na wa kila aina, waandishi, wahadhiri wa vyuo vikuu, wasomi wa kawaida, mawaziri wa serikali kutoka nchi tofauti na watu wengine wengi. Msafara wetu wa wageni kwenda mahali ulikuwa ni msururu wa mabasi zaidi ya kumi yakisindikizwa na kimulimuli cha polisi. Kutoka Tanzania nilikuwapo mimi pamoja na waandishi kutoka Daily News na Kituo Cha TV cha Channel Ten. Nikiwa Tehran niliingia studio za Radio Tehran Idhaa ya Kiswahili na tukafanya mahojiano na mtangazaji wao mashuuri Abdulfataa Mussa na wenzake na vilevile kurekodi vipindi vingi kuhusu hali ya Waislam Tanzania.

Mambo yalianza wakati sasa narudi Dar es Salaam na ndege ya Emirates iliyokuwa inatua usiku. Inaelekea maofisa wa pasi pale uwanjani walikuwa na taarifa zangu mapema na walikuwa wakinisubiri kwa hamu kubwa kwani nilipotoa pasi yangu kwa afisa wa pasi hapo ndipo shughuli za kunishughulikia zilipoaanza. Mimi sikuwa na hili wala lile. Nikawa namuona yule dada aliyekuwa kwenye kile kizimba akikukurika na pasi yangu akiitia katika mashine na kuitoa mara kadhaa. Fikra iliyonijia kwa haraka ilikuwa mashine ni mbovu na harakati zile zilikuwa ni kurekebisha mitambo. Kumbe sivyo wahusika nadhani walikuwa wanahakikisha kuwa mimi ndiyo huyo waliokuwa wakimwinda na kumsubiri na sasa kapatikana, kaingia mwenyewe kwenye mtego na kanasa. Yule afisa wa pasi akanambia nikae pembeni natakiwa kwa mahojiano na watu wa usalama. Hofu haikuwa imeniingia kwa kuwa nilikuwa natambua kuwa harakati dhidi ya ugaidi zilikuwa zimepamba moto na labda nilitakiwa kwa mahojiano mafupi kutaka kujua nyendo zangu. Sikujua wala kutarajia kuwa mshtuko mkubwa ulikuwa unanisubiri.

Nilichukuliwa hadi kwenye chumba kimoja na hapo niliwakuta maofisa wa usalama watatu wakanikaribisha kwa taadhima kisha wakanambia kuwa niko chini ya ulinzi kwa kuwa zimewafikia taarifa zangu kuwa mimi nasafirisha mihadarati. Mpaka hapa sikuwa na hofu bado ilinijia picha kuwa yawezekana wamefananisha majina. Niliwaambia huenda Mohamed Said muuza madawa ya kulevya siyo mimi niliye mbele yao. Wakaniambia kwa kujiamini kabisa kuwa taarifa zao ni madhubuti muuza unga ni mimi na wamekuwa wakinifuatilia siku nyingi.  Hapo ndipo walipotoa pasi yangu na kuniomba niitambue kama hiyo pasi ni yangu au la. Niliwajibu kuwa hakika hiyo ndiyo pasi yangu khasa. Wakaniamuru sasa tutoke twende nikachukue mizigo yangu ili wafanye upekuzi wa mihadarati katika mizigo niliyotokanayo Tehran. Hapo ndipo nilipojuwa kuwa niko katika lindi kubwa la matatizo na ubongo wangu ukaanza kufanya kazi kwa haraka huku nikisoma dua kumuomba Allah ulinzi wake kwani kwa hakika nilijua kama ni njama zimekamilika na leo imefika siku yangu. Nikajiuliza itakuwaje watakapotoa madawa kwenye mizigo yangu. Nikaanza kufikiri vichwa vya habari vya magazeti yatakavyopambwa na habari zangu. Ikanijia yakini kuwa watu wa usalama wameniwekea madawa ya kulevya katika mizigo yangu ili waniangamize na maadui zangu wapumzike na shari yangu.

Nilimgeukia yule ofisa mkuu aliyekuwa ananihoji nikamwambia kuwa sitokubali kugusa mizigo yangu bila kuwapo mashahidi isijekuwa mizigo yangu ishawekewa hayo madawa ya kulevya kwani nilikotoka Tehran mizigo ilikuwa imekaguliwa na ilikuwa salama. Hoja yangu kubwa kwao ilikuwa kupata uhakika kutoka kwao kuwa wananijua vizuri kiasi cha kuthibitisha kuwa kweli mie ni msafirishaji wa madawa ya kulevya. Jibu nililopewa ni kuwa wao wanafanya kazi kutokana na taarifa zilizowafikia. Wakasema, “Sisi tunazo taarifa zako kamili kuwa wewe ni msafirisha madawa ya kulevya.” Nikawauiza,“Baada ya kupata taarifa hizo zangu nyie mmechunguza kutafuta ukweli?” Wakasema, “Ndiyo maana leo tumekukamata.” Nikawaambia, “Si kweli kama kwa sababu mie nafahamika Dar es Salaam takriban kwingi maana ndio nilikozaliwa na kukulia. Hapo Kariakoo ukiwaambia watu kuwa Mohamed ni “Mzungu wa Unga” kila mtu atacheka maana huo kwao ndugu zangu ni mzaha mbaya.” Walitaka kujua nilkwenda kufanya nini Iran. Niliwaambia nilialikwa na serikali ya huko kuhudhuria mkutano. Wakataka kujua vipi nilipata mwaliko. Nikawajibu kuwa hilo swali sina jibu labda waiulize serikali ya Iran. Nikawaeleza kuwa mbona siku zote napita hapo uwanjani nikenda sehemu tofauti duniani kwa mialiko na kutoa mada sijakamatwa kimezidi nini katika hii safari ya Iran? Niliwaeleza kuwa miezi michache  iliyopita nilikuwa Chuo Kikuu Cha Ibadan kwa mwaliko tena mkutano umefadhiliwa na serikali ya Marekani na wamenipa na tiketi toka Dar  es Salaam hadi Lagos na kuniweka hoteli na kunilipa fedha.  “Mbona hamkunikamata wakati ule?” Nikafungua mlango mwingine nikawaambia, “Nakuapieni nyie msingethubutu kumkamata Mkristo anaetoka Vatican mkutanoni. Lakini kwa kuwa mie ni Muislam sina wa kunitetea. Nchi hii nani atakuuliza kwa kumnyanyasa Muislam?” Walishtuka na wakawa wanyonge sana wakasema si kweli kuwa naponzwa na dini yangu.

Baada ya kukurukakara nyingi na mabishano makubwa kuhusu mie kukubali kufanyiwa upekuzi wa mizigo yangu alikuja binti mmoja katika wao na yeye akanihakikishia kuwa wao ni serikali na sio wahuni. Hawathubutu kuniwekea dawa katika mizigo yangu hivyo akanisihi sana kwa upole nikubali ili wajitoe wasiwasi na wataniachia endapo hakuna kitu. Niliomba apatikane shahidi wa kushuhudia mizigo yangu kabla ya kufanyiwa upekuzi lakini hakuna mtu aliyekubali kuchukua dhima ile katika maofisa waliokuwa kazini pale uwanja wa ndege usiku ule. Upekuzi ukafanyika hadi mwilini. Hakuna kitu. Wakanipela katika choo maalum cha kutolea madawa kwa njia ya haja kubwa. Nikakataa kujisaidia pale. Ilikuwa ndio mara yangu ya kwanza kuona choo kama kile. Choo chenyewe ni cha aluminium. Tofauti na vyoo vya pale ambavyo siku zote ni vichafu, hiki kilikuwa kisafi sana kiasi mtu unaweza hata kutengewa chakula na akala bila ya kuhisi kinyaa.

Nilitegemea wataweka ahadi yao kuwa ikiwa hawatakuta madawa ya kulevya katika mizigo yangu watanirejeshea uhuru wangu wataniachia niende nyumbani. Haikuwa hivyo. Wakanirudisha ofisini kwao. Sasa wakaacha madawa ya kulevya wakahamia katika vitabu na “audio cassette” nilizokuwa nimepewa kama zawadi kule Tehran wakaniluliza kwa nini naingiza vitu vile khasa kanda za Khomeni na vitabu vyake nchini. Nikawauliza, “Kwani kanda na vitabu vya Khomeni haviruhusiwi kuingizwa Tanzania? Maana mimi hata nyumbani kwangu hii leo mkifika nina vitabu vya Khomeni na wanafalsafa wengine kama Karl Marx ambao nimesomeshwa pale Chuo Kikuu Cha Dar  es Salaam. Sasa hapo ikaja kejeli. “Ala wewe mtu wa Kariakoo lakini umefika hadi Chuo Kikuu!” Sikujibu kitu. Awali waliponitia mbarani waliniuliza kwetu na  nikawaeleza kuwa nimezaliwa Kariakoo.

Hawakunipa jibu kuhusu kuingiza vitabu na cassette za Khomeni. Ikawa sasa kama vile wameishiwa maswali. Nikaona kuwa sasa ni zamu yangu nami kuwapiga maswali. Yule aliekuwa akinihoji nikamwambia, “Mimi wewe nakufahamu vizuri sana kwa sababu ukicheza mpira Simba Sports Club na mie ni mpenzi wa club hiyo toka utoto wangu wakati huo ikiitwa Sunderland na mmoja wa baba zangu alikuwa mchezaji marufu wa club hiyo katika miaka ya 1950 akafiikia hadi kucheza Kombe la Gossage.” Nilihisi amepata mfadhaiko kidogo akanambia,“Unanifananisha yule aliekuwa akicheza Simba ni ndugu yangu.” Alikuwa anasema uongo lakini mie nikamkubalia. Hapo nikajua kuwa nishampata sasa hana nguvu tena ya kuuliza maswali. Kusema uongo ni dalili ya kujihami. Nikamrushia kombora lingine, “Sasa tuhuma za madawa ya kulevya zimekwisha tuko katika kwa nini naingiza  vitabu vya Khomeni nchini?” Akanijibu kinyonge, “Tumeridhika huna madawa.”  Kufika hapa tukawa tumemaliza  mahojiano.

Wakati huo sasa ni usiku wa manane na nishapeleka SMS kwa sahib yangu mmoja bingwa wa mambo ya mtandao wa kompyuta kumjulisha kuwa nimekamatwa uwanja wa ndege kwa tuhuma za uongo za kuvusha mihadarati na yeye ile kuipata tu ule ujumbe wangu akaifahamisha dunia kuwa nimekamatwa uwanja wa ndege nikitokea mkutanoni Iran na nimebambikiziwa tuhuma za kuingiza nchini mihadarati. Waliponitia mbaroni tu walinionya kuhusu kutumia simu yangu ya mkononi lakini bahati nzuri hawakuninya’ganya. Aliyenipa onyo hili alikuwa mkuu wa kituo cha polisi cha uwanja wa ndege. Huyu rafiki yangu akawa kanisaidia sana maana hadi kumekucha wapenzi wangu wote ndani na nje ya nchi pamoja na vyombo vya habari vinavyonifahamu walikuwa na taarifa za kukamatwa kwangu. (Kwa kipindi takriban miaka ishirini nyuma kwa nyakati fofauti nimekuwa nifanya mahojiano na radio zote muhimu kama, BBC, VOA, Sauti ya Ujerumani, Sauti ya Iran nk.). 

Nikawaomba wale watu wa Usalama waniachie basi nende zangu kulala nyumbani nirudi hapo kesho asubuhi kwa kuwa sikuwa nimebeba madawa ya kulevya. Wakaniambia, “Itabidi tukulaze hapa hadi asubuhi wakubwa wetu watupe amri ya kukuachia. Maana amri ya kukukamata wewe imetoka juu.” 


Mwandishi Akiwa KAtika Studio za Radio Iran Tehran
Idhaa ya Kiswahili

No comments: