Msomaji,
Fatilia ukurasa huu In Sha Allah tunatengeneza kipindi maalum cha historia ya mapinduzi.kutokana na vyanzo ambavyo kwa muda mrefu havikunukuliwa kwa sababu moja au nyingine...
![]() |
Mwandishi Akiwa na Sheikh Ali Muhsin Barwan Kushoto na Sheikh Badr Kulia Mascut, Oman 1999 |
Mwandishi akiwa pwani ya Kipumbwi, Tanga 2003 Picha imepigwa na Dk. Harith Ghassany |
Dk. Harith Ghassany Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani akiwa Kipumbwi wakati wa utafiti wa historia ya mapinduzi ya Zanzibar Picha imepigwa na Mwandishi |
![]() |
Siku Nyerere Alipomuadhiri Hanga Viwanja Vya Mnazi Mmoja Mbele ya Kibarua Bar Nyuma ya Ukumbi wa Arnatouglo Hanga Alitolewa Jela Ukonga Kuletwa Pale Makhsusi kwa Shughuli Hiyo Baada ya Siku Hii Hanga Hakuoenekana Tena |
Dk. Harith Ghassany na Mwandishi Wakiwa Sauti ya Amerika, Washington DC 2011 |
Mohamed Omari Mkwawa Akishikilia Nakala ya Kitabu ''Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru'' Kilichoandikwa na Dk Harith Ghassany
Mohamed Omari Mkwawa (Tindo)
mwanamapinduzi aliyesahauliwa, mwamasishaji, mpelelezi, mtekelezaji mipango
ya upigaji kura Zanzibar 1963, mwanamapinduzi Zanzibar 1964, askari wa msituni wa Afro Shirazi Party,
mvushaji askari mamluki wa Kimakonde na makabila mengineo kwenda Zanzibar
kupiga kura na kushiriki katika mapinduzi akiwa amekishika kitabu Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!
Utangulizi
Kwa kipindi kirefu historia ya mapinduzi
ya Zanzibar ilikuwa ni ile historia rasmi ambayo imeathiri historia nyingi
Afrika. Viongozi wa Afrika wanapenda ile historia itakayowakweza na kuwaonyesha
wao katika mwanga wa kupendeza. Vinginevyo historia hiyo haitakiwi.
Wazalendo wenyewe hawakuwa na hamu ya kuandika historia hii na watu wa nje
walioandika historia ya mapinduzi ya Zanzibar hawakupata kuifanyia haki
historia ya Zanzibar labda kwa ugeni wao na kwa kuyaamini maelezo yaliyokuwa
“wazi” kwa wakati ule, mfano mkubwa ukiwa ni kule kuamini kuwa mapinduzi ya
Zanzibar yalipangwa na makomredi wa Umma Party.
Hapajakuwapo
udanganyifu mkubwa katika uandishi na utafiti kama huu. Dkt Ghassany amekiweka
chano uwanjani bila kawa. Akizungumza na Abdushakur Aboud wa Sauti ya Amerika
Dkt Ghassany amesema kuwa historia ya Zanzibar ni historia ya kujijuwa maisha
yake akiwa mjukuu wa babu wa mababu Muomani na mabibi wa Kimanyema na Kimwera–
mchanganyiko wa damu ya Kiarabu na Kiafrika. Hii kwa hakika ndiyo historia ya
wananchi wa Zanzibar. Ni tabu sana kumpata huyo Muarabu Zanzibar kila umuonae
Muarabu basi ana mjomba na shangazi Mwafrika. Maadui wa Zanzibar wakiweka mkazo
katika ubaguzi wa rangi na kuwafitinisha Wazanzibari. Ukweli huu ndiyo chanzo
cha matatizo yote yaliyoikumba Zanzibar toka vyama vya siasa vilipoanza katika
miaka 1950 na matatizo yaliyosababisha mauaji ya mwisho yakiwa mwaka 2001.
Mohamed
Omari Mkwawa
Mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa
vyama vyingi Tanzania nilibahatika kufuatana na mgombea urais wa CUF Prof. Ibrahim
Haruna Lipumba katika kampeni za uchaguzi katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Prof. Lipumba alifanya mkutano mkubwa sana Tangamano kiasi cha kuishtua CCM.
Baada ya mkutano ule Prof. Lipumba na ujumbe wake walialikwa nyumbani kwa mama
mmoja akijulikana kama Mama Ummie (sasa ni marehemu) ambako walifanyiwa dhifa
kubwa. Kote tukipita mitaa ya Tanga msafara wetu ulikuwa ukishangiliwa kwa
nguvu sana. CUF ilikuwa imeingia Tanga kwa kishindo kikubwa.
Mimi kazi yangu ilikuwa kuangalia
niliyokuwanayaona na kupiga picha. Kwa hakika nilikuwa nikishuhudia historia
ikijiandika. Historia ambayo ilikuwa imeshahibiana sana na ile ya wakati wa
kudai uhuru wa Tanganyika katika miaka 1950. Lakini ninalotaka kusema si hili
bali ni picha ambayo niliipiga ndani ya nyumba ya Mama Ummie. Picha hii ilikuwa
inamuonyesha mzee mmoja wa makamo aliyevaa fulana ya CUF mbele ikiwa na picha
ya Prof. Lipumba. Mzee huyu alikuwa amekaa nyuma ya Prof. Lipumba. Kwa wakati
ule picha hii haikuwa na maana yoyote kwangu na hata nilipokuwa naitazama mara
kwa mara sura yake si iliyokuwa inanivutia bali ile fulana ya CUF aliyovaa
ambayo ilikuwa na picha ya rafiki yangu Prof. Lipumba.
Kushoto: Mzee Mohamed Omari Mkwawa Juma Duni na Prof.
Lipumba Tanga 1995
Mungu ana mipango yake. Mihangaiko ya
kutafuta riziki yakanihamishia Tanga na nikawa karibu sana na baadhi ya
viongozi wa CUF na wanachama wake. Sasa
hapa ndipo nilipokujakuonana uso kwa uso na mzee yule kwenye picha yangu
niliyoipiga hata kwa wakati ule ilikuwa miaka mingi iliyopita. Jina la huyu
mzee wangu ni Mohamed Omar Mkwawa.
Ilikuwa katika barza yetu ya kawaida ya kunywa kahawa na kula pweza huku tukijadili
historia ya Tanzania ambako siku moja Mzee Mkwawa alinambia, “Mohamed nataka
nikuambie kitu. Unajua mimi nimehusika sana katika mapinduzi ya Zanzibar?”
Nilimuangalia Mzee Mkwawa kwa makini.
Fikra yangu ya utafiti na uandishi ishashtuka haipo tena usingizini. Mzee
Mkwawa aliendelea, “Mimi ndiye niliyekuwa nikiwavusha Wamakonde kutoka Kipumbwi
kwenda Zanzibar kuipigia kura ASP na wakati wa mapinduzi mie ndiye niliyewavusha
Wamakonde kwenda kuipindua serikali ya Jamshid.” Sasa moyo wangu ukaanza
kudunda kwa nguvu. Naisemesha nafsi yangu, “Huyu mzee anajua uzito wa maneno
haya?” Tuishie hapa. Kuanzia siku ile nikawa sasa namtazama Mzee Mkwawa kwa jicho
jingine na heshima yangu kwake ikawa imepanda maradufu. Nilikuwa nimeshatambua
kuwa Mzee Mohamed Omari Mkwawa alikuwa mmoja wa wanahistoria waliosahaulika
katika historia ya Tanganyika na Zanzibar. Juu ya hayo nilishangazwa na kitu
kimoja. Iweje leo huyu mwanamapinduzi wa ASP ambae Abeid Amani Karume alimpa
jina la “Tindo” kwa ujasiri wake amekuwa mstari wa mbele CUF chama ambacho
kinanasibishwa na Hizbu hasimu mkubwa wa ASP?
![]()
Dr
Harith Ghassany
Nilikutana na Dr Harith Ghassany mwaka
1999 nyumbani kwake Maskati, Oman. Naikumbuka siku ile kama jana vile. Kanipeleka
kwake mwenyeji wangu Farouk Abdulla lakini kabla ya kunipeleka nilikuwa nimeshalisikia
jina lake mara nyingi sana pale Maskati kila nikikutana na jamaa wenye asili ya
Tanzania jina lake litaibuka. Katika fikra yangu ikanijia kuwa Dkt Ghassany
atakuwa ni mtu mzima. Sielewe kwa nini nilipata picha hii. Tulipopiga hodi na
akatokea Dkt Ghassany kuja kutufungulia mlango nikapata mshangao mkubwa.
Aliyekuwa mbele yangu alikuwa ni kijana
mdogo sana tofauti na nilivyodhani. Kwa njia ya utani hata kabla sijatoa
salamu. Nikamgeukia Farouk nikasema, ”Ah! Dkt Ghassany, Dkt Ghassany, Dkt
mwenyewe ndiye huyu?” Mila na tamaduni za watu wa pwani wakikutana hazipishani.
Maskhara ni dalili ya mapenzi. Dkt Ghassany pale pale alipokea yale maskhara na
akajibu, ”Bwana wangu we wanakutisha
bure kwani we ulidhani litakuwa jitu kubwa?” Urafiki na udugu wetu umedumu hadi
leo na ndipo katika mazungumzo aliponifahamisha kuwa anataka kuandika historia ya
kweli ya mapinduzi ya Zanzibar. Hapo ndipo nilipomjuvya kuhusu Mzee Mkwawa na nikamuomba
aje Tanga amuhoji.
Kitu kimoja mashuhuri kwa mashujaa wa
harakati za siasa katika Tanzania ni kuwa takriban wote wana hali ngumu sana za
maisha. Sikujua vyema hali ya Mzee Mkwawa hadi nilipofika nyumbani kwake na Dkt
Ghassany. Utu uzima na udhaifu wa maisha ulikuwa umempiga barabara.
Nilimjulisha Dkt Ghassany kwa Mzee Mkwawa na kuwaacha waendelee na maongezi yao.
Niliporudi mchana kumchukua Dkt Ghassany rafiki yangu alinambia nimuache nije
jioni kumfuata. Niliporudi jioni nilimkuta Dkt Ghassany amechoka na uso umesawijika.
Tukiwa ndani ya gari yangu tunaondoka
nikamuuliza kulikoni. Dkt Ghassany akanambia maneno ambayo hadi leo yamebaki
kichwani mwangu, ”Mohamed ufunguo wa kitabu changu anao Mzee Mkwakwa na kama
nisingeonana nae utafiti wangu wote wa kabla ungelikuwa hauna maana yoyote.”
Dkt Ghassany alikuwa amechukuliwa na Mzee
Mkwawa katika safari ya zaidi ya nusu karne. Mzee Mkwawa akimshika mkono kwanza
kumpeleka Pemba ambako akiwa kijana wa kiasi cha miaka 25 akifanya kazi ya
uashi. Huo ndio ulikuwa wakati wa siasa za ASP na Hizbu zimepamba moto. Mzee
Mkwawa alikuwa mmoja wa wachezaji wa ngoma ile hata kama alikuwa anatoka
Tanganyika. Dkt Harith akavushwa na kuletwa pwani ya Kipumbwi na Sakura ambako
Mzee Mkwawa alikuwa akisimamia kambi ya
mafunzo iliyokuwa msituni ya wakata mkonge wengi wao wakiwa Wamakonde, kambi
ambayo ilitoa askari waliotumika kuipindua serikali ya Mohamed Shamte 12 Aprili
1964.
![]()
Wakata Mkonge Katika Mashamba ya Mkonge Maarufu
Wakijulikana Kama Manamba
Dkt Ghassany hakuwa amejitayarisha kwa
haya. Alishangwazwa na uwezo wa kumbukumbu wa Mzee Mkwawa, akitaja majina na
mahali na akirudia mazungumzo neno kwa neno kati yake na maofisa wa serikali ya
Tanganyika kutoka vyombo vya usalama waliomtia katika operesheni maalum ya
kuipindua Zanzibar kutoka Tanganyika. Majina ya Abdulla Kassim Hanga, Jumanne
Abdallah, Ali Mwinyi Tambwe, Victor Mkello, Oscar Kambona na wengine yakawa
yanadondoka moja baada ya lingine. Taarifa hizi ndizo zilizommaliza Dkt
Ghassany na kumsawajisha uso.
Mimi binafsi nilipigwa na butwaa. Nilibaini
kama alivyobaini Dkt Ghassany kuwa Mzee Mkwawa alikuwa hazina na tulikuwa tumevumbua
mgodi wa dhahabu. Kazi yetu sasa ilikuwa kuchimba tu. Kumekuwa na uvumi kwa
miaka mingi katika duru za wanasiasa wapya na wa zamani na katika wanafunzi wa
historia ya Tanzania na Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Ali Mwinyi Tambwe alihusika
sana katika kupinduliwa kwa serikali ya Zanzibar lakini hakuna aliyejuwa ni kwa
kiwango gani na alihusika vipi. Lakini zito ni kuwa yeye mwenyewe akiudhika
sana mtu akimuuliza habari zile. Kwa nini ilikuwa hivyo? Kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru cha Dkt
Ghassany kilikuja kutoa majibu. Hakuna binadamu apendae historia yake ihusishwe
na mauaji na dhulma na kufutwa kwa nchi yake.
Kwa kipindi cha takriban miaka saba Dkt
Ghassany alikuwa akija Tanga kwa mahojiano na Mzee Mkwawa na katika kipindi
hicho Mzee Mkwawa alitupeleka Kipumbwi na Sakura na kutuonyesha sehemu zile
ambazo walikuwa na kambi na wakifanya mazoezi ya kivita na matumizi ya silaha. Mkahawa
ambao wale wakata mkonge walikuwa wakila chakula cha usiku kabla ya kuvushwa
kwa vyombo vya bahari kwenda Unguja bado upo hadi leo ingawa kwa sasa kijumba
kile hakitumiki tena kama mkawaha. Endapo itakuja siku serikali ya Zanzibar
itataka kuhifadhi historia ya Mapinduzi ya Zanzibar bila shaka moja ya vitu
vitakavyokuwa katika makumbusho ni picha ya hicho kibanda.
Victor
Mkello
Victor Mkello Akiwa Nyumbani Kwake Nguvumali Tanga
Akiwa Katika Kitanda Chake cha Mauti
Napenda kukiri kuwa sikupata kushiriki
kama msikilizaji wa mahojiano wakati wa utafiti wa Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru.
Kazi yangu kubwa sana ilikuwa kufungua milango na kumwendesha daktari. Kwa
ufupi kazi yangu ilikuwa kumwekea mwandishi mazingira mazuri ili kazi yake iwe
nyepesi. Kwa hakika ilikuwa kazi ambayo na mimi vilevile nilisoma, kujifunza
mengi na kupata faida kubwa. Katika haya nakumbuka sakata la kumtafuta Victor
Mkello. Leo si wengi wanaomjua Victor Mkello au hata kupata kusikia jina lake
likitajwa. Lakini kwa sisi tuliokuwa wadogo tukiwa shule katika miaka ya 1960
Mkello alikuwa hapungia katika magazeti ya Ngurumo
na Mwafrika. Mzee Mkwawa ndiye
aliyetusaidia kumtafuta alipo. Victor Mkello ndiyo aliyekuwa ”Amiri Jeshi Mkuu”
wa lile jeshi la Wamakonde lililokuwa na makao yake makuu katika mashamba ya
mkonge ya Sakura na Kipumbwi. Bila ya kupata kauli ya Mkello kitabu kisingeweza
kuandikika.
Ilichukua muda kuweza kumpata. Kwanza
tulikwenda Muheza ambako ndiko kwao. Huko tukaambiwa kuwa hakuwapo hapo bali
kwa muda mrefu alikuwa Tanga. Mwishowe tulimkuta nyumbani kwake Nguvu Mali.
Mkello alikuwa katika kitanda cha mauti. Kisukari kilikuwa kikimla kiwiliwili
chake. Hakuwa anaweza kunyanyuka kitandani wala kukaa. Kwa hakika alikuwa
anasikitisha. Huyu hakuwa Victor Mkello niliyekuwa namsoma katika magazeti wala
yule ambae Mzee Mkwawa alikuwa akituelezea. Mtu mjanja aliepambana na Magiriki
wamiliki wa mashamba ya mkonge akitetea haki za Waafrika katika miaka ya 1960.
Huyu kwa kweli hakuwa yule Victor Mkello aliyekuwa akisaidiana na TANU na
Mwalimu Julius Nyerere kupigania uhuru wa Tanganyika. Hiki mbele yetu kilikuwa
kivuli chake. Hapakuwa na wasiwasi wowote Victor Mkello alikuwa akisubiri
malaika wa mauti amtembelee na yeye hilo alikuwa akilijua fika.
Victor Mkello na Mzee Mkwawa
wanamapinduzi waliofutwa katika historia walitazamana na wakasalimiana kama
vile hakuwapata kujuana. Jicho la Mkello lilikwenda kwa Dkt Ghassany kisha
likaangukia kwangu kisha likarudi kwa mwanamapinduzi mwenzake Mzee Mkwawa.
Baada ya utambulisho uliofanywa na Mzee Mkwawa nilihisi woga na wasiwasi kwenye
sura ya Victor Mkello. Hakuwa anaamini kuwa Dkt Ghassany katoka Maskati kwa
ajili ya utafiti wa historia na hili lilijidhihirisha alipofunua kinywa
kuzungumza. Victor Mkello alikuwa na hisia kuwa alifuatwa kukamatwa kwa vifo
vya Waarabu vilivyotokea Zanzibar wakati wa mapinduzi ili apelekwe Mahakama ya
Kimataifa. Baadae Dkt Ghassany alinifahamisha kuwa jinsi Waingereza
walivyomueleza katika taarifa zao za siri ambazo yeye alizisoma London
zimeafikiana kabisa na jinsi alivyomuona pale. Waingereza walimsifia Mkello kwa
kusema kuwa alikuwa bingwa wa kuteleza kama samaki ndani ya maji.
Kufupisha maelezo. Ilichukua karibu miaka
mitatu kwa Victor Mkello kukubali kuzungumza kuhusu mapinduzi ya Zanzibar. Dkt
Ghassany akienda Maskati na kurudi Tanga na kila akienda kwa Victor Mkello,
Mkello hakuwa tayari kueleza kile alichokijua kuhusu mapinduzi ya Zanzibar.
Kila nilipokwenda na Dkt Ghassany kumuona Mkello hali yake ilikuwa inazidi
kudidimia. Sasa alikuwa kakatwa mguu mmoja kwa ajili ya kisukari. Ilikuwa
katika hali ile katika siku zake za mwisho ndipo siku moja alipomwambia Dkt
Ghassany aje siku ya pili na yeye atazungumza na angependa azungumze mbele ya
mkewe ili amkumbushe pale atakapokuwa kasahau kitu.
Hapa ndipo ilipo moja ya sehemu tamu
kabisa ya kitabu hiki Kwaheri Ukoloni
Kwaheri Uhuru. Victor Mkello Amiri Jeshi Mkuu wa Mamluki wa Kimakonde
alizungumza. Mimi sikushiriki katika mazungumzo yale nilijiweka pembeni ili
Mkello azungumze na Dkt Ghassany kwa utulivu. Nilikuwa nimeegesha gari yangu
karibu ya msikiti jirani ya nyumba ya Mkello nikimsubiri daktari akamilishe
upasuaje mgonjwa apate nafuu. Mwendo wa Dkt Ghassany wa kudunda alipokuwa ananijia
pale nilipoegesha gari ulidhihirisha furaha yake.
Haukupita muda mrefu baada ya mazungumzo
yale na Dkt Ghassany, Victor Mkello akaaga dunia kimya kimya. Hakuna mtu aliyejua
kifo chake kama ilivyokuwa vifo vingi vya mashujaa waliopigania uhuru wa Tanganyika.
Hakuna hata gazeti moja lililotoa taazia yake wala hotuba hazikusomwa kaburini
kwake. Mkello aliondoka katika historia ya Tanzania kimya kama jinsi mamluki
wake walivyokuwa wakiingia Zanzibar kimya kimya usiku mkuu na kwa siri, mapanga yao makali ya kukata
mkonge yakiwa chini ya nguo zao za ndani yakisubiri kuivamia Zanzibar na kuua
watu wasio na hatia. Kazi hii kwao haikuhitaji mafunzo kwani mafunzo walikuwanayo muda mrefu katika kazi
yao ya kukata mkonge katika mashamba ya mkonge ya Tanga. Pigo moja lilitosha
kuangusha chini jani zito la mkonge seuze kiungo cha binadamu.
Kwaheri
Ukoloni Kwaheri Uhuru ni
kitabu kilichoandikwa kwa staili ya pekee wahusika wenyewe wa matokeo katika
mapinduzi kujitolea kueleza kile kilichotokea katika mapinduzi, kabla na baada
yake. Kuanzia mipango ya kuangusha serikali ya Zanzibar hadi katika kuwaua wale
waliokujakushukiwa kuwa ni maadui wa mapinduzi hadi kufikia hata kuweka wazi
jinsi walivyoshiriki katika mengi ya kusikitisha kupelekea hata msomaji
kujiuliza kwa nini hawa watu baada ya miaka yote hiyo kupita wameamua kueleza
yote hayo. Vipi Abdallah Kassim Hanga, Othman Shariff, Mdungi Ussi, Jaha Ubwa,
Abdulaziz Twala na wengineo walivyouliwa, nani alitoa amri ya mauaji, nani
aliwauwa na katika mazingira gani. Kifo cha Karume mwenyewe kwa mtutu wa
bunduki hakikuwekewa pazia na chanzo cha kuamuliwa kuwa auawe ni tofauti ya
kilichozoeleka kuelezwa. Karume hakuuawa na ”wapinga mapinduzi” kama ilivyozoeleka
kuelezwa katika historia rasmi.
Kwa kumaliza
tusubiri mapitio ya kitabu hiki na ni wazi kuwa wasomaji watapata mengi ya
kuelimisha na kuhuisha. Tunategemea wasomi wa somo la historia watakaopitia
kitabu hiki watatufanyia hisani kubwa kwa kuwaleta katika picha wahusika wakuu
wa mapinduzi – Mwalimu Julius Nyerere – fundi mkuu mwenye kishindo kikubwa
lakini hakisikiki, mkono wake wa chuma hauonekani, uso wake nyuma ya pazia, Abdallah
Kassim Hanga – kiongozi hasa na mpangaji wa mapinduzi, Victor Mkello – mtumishi
wa Hanga na Nyerere bila ya yeye
mwenyewe kujua kati ya hao wawili nani aliyekuwa bingwa kumshinda mwenzake
katika mchezo mchafu wa siasa ya kuiuwa Zanzibar na Wazanzibari na wengineo.
Lakini
juu ya hayo yote mipango hii ilikuwa ni ya akina Nyerere, Hanga na Mkello
pekee? Dkt Ghassany anaeleza nini kuhusu mkono wa Waingereza, Algeria, Misri,
Wachina, Warusi, Marekani na Mayahudi? Nini kilichowasukuma hao wote katika
mapinduzi ya Zanzibar? Nini kilimsukuma Nyerere, kuwapindua Waislam
walioupigania Uhuru wa Tanganyika na baadae kuwapinduwa Waislam walioupigania
Uhuru wa Zanzibar na kuendelea kuwadhibiti hata baada ya kuipindua Zanzibar?
Nini kilichowasukuma Waingereza na Wamerekani kuachia mapinduzi yafanyike?
Lakini kubwa zaidi kipi kilichowasukuma Wayahudi kuingia na kusaidia mapinduzi,
ni ile chuki yao ya asili dhidi ya Waarabu au kulikuwa na jengine ambalo
liliwatia khofu? Na kwanini kitabu kiitwe Kwaheri
Ukoloni Kwaheri Uhuru: Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia? Kitabu kina majibu
ya haya maswali mengine ambayo bado hayajaulizwa na chemchemu mpya za utafiti.
Dkt
Ghassany anastahili pongezi kubwa sana kwa kuinusuru historia ya mapinduzi ya
Zanzibar na kuwaamsha Wazanzibari na Watanganyika toka lepe zito la usingizi
ili wajitambue na wamjue adui yao. Anastahiki pongezi kubwa zaidi si kwa
kukiandika kitabu cha Kwaheri Ukoloni,
Kwaheri Uhuru bali kwa kutumia mrengo usiokuwa na mrengo. Huna pa kumuweka
Dkt Ghassany na baada ya kumaliza kukisoma kitabu ukaridhika napo. Kama
utafikiria kuwa kitabu ni cha CUF basi baada ya kusoma mpaka mwisho utavunjika
moyo. Kama utamtumbukiza ndani ya CCM basi ataelea. La kama unataka upae nje ya
masunduku na mapakacha basi utamuona katulia ndani ya uhuisho wa umoja wa
Zanzibar na Tanganyika Mpya – Tanzania Mpya.
Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru ni
ngoma nzito ambayo watu wameanza kuicheza hata mdundo haujaanza kupigwa! Tayari
imeshaingia katika rikodi za Hansard za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tayari imeshasikika katika Sauti ya Marekani. Tayari daktari anafuatilia kwa
karibu ukweli wa Maridhiano na kuwa kwa mara nyengine tena ukweli wake
umeshaanza kupotoshwa na waroho na tayari historia mpya na kubwa zaidi hata
kuliko ile ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 imeshaanza kuvurugwa.
Watengenezaji
wa filamu Hollywood wana mtindo wa kumaliza senema zao za matokeo ya kweli kwa
kueleza katika maandishi yale yaliyowafika wahusika wa kisa kilichotengenezwa
hiyo senema. Huonyesha majina na mwisho wa hao wahusika, kama wahai, wako wapi,
wamekufa na kama wamekufa ni kwa kuuliwa au kwa amri ya Mungu nk. Katika Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru majina ya
wahusika machache ambayo yametajwa katika makala haya yako kama hivi:
17 Ramadhani 1431
28
August 2010
|
No comments:
Post a Comment