Hemed Seif |
Timu ya Taifa 1960s Kushoto Kwenda Kulia: Hemed Seif, Mbwana Abushiri, Awadh Matesa, (sina jina lake), John Limo, Mathias Kissa, Abdallah Aziz, (sina jina), Miraji, (sina jina) Chaki |
Waliosimama wa Kwanza Kutoka Kulia Hemed Seif |
Hemed Akida Seif |
Kushoto Kwenda Kulia: John Limo, Mbwana Abushiri, Hemed Seif na Salehe Zimbwe |
Kushoto ni Marehemu Salim Kajembe na Kulia ni Hemed Seif |
Zimenifikia taarifa hivi punde kutoka Tanga za kifo cha Hemed
Akida Seif. Hemed Seif amefariki jana baada ya kuugua kipindi kifupi
akalazwa hospitali kasha akatoka. Hemed Seif amezikwa leo asubuhi, Jumapili
tarehe 13 Aprili 2014 sawasawa na tarehe 12 Mfungo Tisa 1435 na kazikwa kwenye
makaburi ya familia yao Magaoni Tanga ambako ndiko alikozaliwa na kuishi maisha
yake yote. Huenda leo pakawepo wengi ambao hawamjui Hemed Seif ni nani.
Hemed Seif alikuwa mchezaji mpira maarufu katika miaka ya 1960 na
siku zote akivaa jezi na. 10. Hapakuwahi kutokea mchezaji akamnyang'anya jezi
hiyo wakati yeye alipokuwa bado anacheza. Jezi namba 10 ilikuwa imegongewa
misumari mgongoni kwake. Hemed Seif alikuwamo katika ile timu ya taifa
iliyochukua Kikombe cha Gossage mara mbili mfululizo mwaka 1964 na 1965 chini
ya kocha Myugloslavia, Celebic.
Sifa kubwa ya Hemed Seif ilikuwa ni kufunga magoli kutoka mbali,
yaani nje ya kumi na nane au nje ya ''box,'' kwa mashuti mazito na hapa ndipo
palipokuwa na ''uchawi'' wake. Hemed Seif alikuwa mwembamba mrefu na anapokuwa
uwanjani ikiwa humjui, picha itakayokujia ni kuwa ni mchezaji ambae mabeki
watamzoa kwa vibuyu kirahisi na kumwangusha chini kwa wembamba wake. Lakini
haikuwa hivyo kwani ingawa alikuwa mwembamba Hemed Seif alikuwa na kasi na
ujanja wa kuwatoka mabeki kirahisi. Zaidi ya hayo miguu ya Hemed Seif ilikuwa
ikibeba mabomu na mizinga mizito.
Free-kick'' zote pamoja na ''penalty'' iwe katika timu yake ya
Tanganyika Planting Company (TPC) kutoka Moshi au Timu ya Taifa alikuwa
anaachiwa Hemed Seif kupiga na kwa hakika mara nyingi sana nyavu ilikuwa lazima
zitikisike. Hemed Seif alikuwa mtaalam wa magoli. Mikwaju yake ilikuwa
gumzo kwa timu pinzani na magolikipa wote wa Afrika ya Mashariki wakati
akicheza katika mashindano makubwa ya wakati huo ya Taifa Cup na Kombe la
Gossage. Kombe ambalo likishindaniwa na nchi zote za Afrika ya Mashariki,
Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar. Hemed Seif katika timu ya taifa alikuwa
akicheza na ‘’Director’’ Mbwana Abushiri kuliani kwake na John Limo akiwa mbele
katikati ‘’centre forward,’’ au ‘’half back’’ wa kulia. Wingi wa kulia akiwa
Sembwana na kushoto Abdallah Juma Aziz.
Nakumbuaka kama jana vile jinsi tulivyokuwa tukilisubiri basi la
TPC liingie uwanjani na sisi watoto tukimbilie kuwaangalie wachezaji nyota wa
zama zile kama Hemed Seif mwenyewe na kaka yake Marshed Seif, Mbwana
''Director'' Abushiri, Sembwana, John Limo, Awadh Maseta, Ishaka Mzee, Dracula,
Emil Benadicto Kondo, Shariff Salim, Hospitali, Okoth ambae alikuwa golikipa wa
timu ya taifa Kenya kasha akaja kucheza TPC. Enzi zile takriban timu nzima ya
TPC ilikuwa ikichaguliwa katika timu ya taifa. Wachezaji hawa mimi nimewafaidi
sana katikia utoto wangu wakija kucheza Ilala Stadium katika miaka ya 1960
katikati.
Lakini kabla ya hapo niliwaona akina Hemed Seif wakati nikiishi na
wazee wangu Moshi. Niliwaona wachezaji hawa wakicheza timu ya TPC ikija Moshi,
King George Memorial Stadium, Lukaranga kuja kupambana na timu kama Kahe au Tanganyika
Coffee Curing Company (TCCC) timu ambazo ndizo zilizokuwa zikishiriki katika
ligi Moshi mjini. Kahe ndiyo timu angalau ikijitahidi kutoa upinzani mkali kwa
TPC lakini bila mafanikio. Kahe ilikuwa timu ya wafanyakazi katika shamba la
mkonge la Kahe na walikuwa na wachezaji vijana wa Kijaluo kutoka Kenya.
Wachezaji hawa wa Kahe walikuwa wakitegemea nguvu zao zaidi ya
ujuzi wa mpira. Hapo ndipo palipokuwa na raha kuangalia mpira wa TPC na Kahe
wakati nguvu zilipogeuzwa zikawa kichekesho wakati wachezaji wa TPC wakigonga
pasi kuanzia nyuma hadi mbele kisha ikapigwa ''back pass na Mbwana wakati
mwingine kwa kisigino na Hemed Seif kama vile simba aliyekuwa akisubiri mawindo
akapokea pasi bila kutuliza na ghafla nyavu zinacheza.
Mwaka 2000 nilikwenda kufanya kozi Nairobi na mmoja wa walimu
wangu alikuwa mchezaji wa timu wa zamani wa timu ya taifa Kenya Mohamed
Abdilkadir. Alipojua natokea Tanga akaniuliza kama namjua Hemed Seif.
Nilipomweleza kuwa Hemed Sief nikonae barazani kila siku na tunafanya kazi
pamoja bandarini alifurahi sana ndipo akanipa kisa chake kuhusu Hemed Seif.
Alinambia kuwa yeye katika miaka ya 1960 alikuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha
Nairobi na alikuwa akicheza timu ya taifa ya Kenya akiwa katika safu ya ulinzi
kama ''half back.'' Anasema siku ilipojuliikana kuwa Kenya watakutana na
Tanzania, kocha na wachezaji wenzake walimuonya kuwa awe makini sana na Hemed
Seif, amwangalie sana asimuachie hata kidogo kwani ni mfungaji mabao hatari mno.
Mohamed Abdilkadir anasema ikawa sasa kwake ni vitisho wenzake wakimtisha
kwa kumpigia makelele, ''Mohamed, Hemed Seif huyo nyuma yako...'' Basi katika
mazoezi ikawa ni vicheko na vitisho kwake kuhusu Hemed Seif na mashuti yake.
Maelezo haya yakanitia hamu nikamuuliza nini kilitokea Nairobi City Stadium
siku ya mechi ya Kenya na Tanzania. Mohamed Abdilkadir alitingisha kichwa
akasema,''Bwana ilikuwa kazi. Mimi nilimpania Hemed Seif. Sikuwa nabanduka
nyuma yake. Nilikuwa kama kivuli chake, kila anapokwenda niko mgongoni kwake...wapi
bwana. Kama walivyonitahadharisha wenzangu kitambo...Hemed Seif alifunga bao
kama kawaida yake. Nikakumbuka maneno ya wachezaji wenzangu kuwa Hemed Seif
hatoki uwanjani bila ya kutingisha nyavu.'' Hemed Seif alikuwamo katika timu ya Tanzania ilipocheza na timu kali ya daraja la kwanza kutoka Uingereza, West Bromwhich Albion ilipokuja nchini na kucheza na timu ya Tanzania Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru). Kama kawaida Hemed Seif aliwatoka mabeki wa West Bromwhich na kufunga goli. Picha yake ilitoka kwenye ''Tanganyika Standard'' ikimuonyesha Hemed Seif akifunga bao hilo. Huyu ndiye Hemed Seif aliyekuwa msakata kabumbu maarufu.
Hemed Seif alistaafu kazi Tanzania Ports Authority (TPA) Tanga
kiasi cha kama miaka kumi iliyopita na tofauti na wenzake wengi aliochezanae
mpira wakati mmoja, Hemed alikuwa na maisha mepesi ya kupendeza na alikuwa
akicheza mpira na utu uzima wake kila alipopata nafasi. Mmoja wa marafiki zake
na mwanabaraza nilipompigia simu kumpa mkono wa pole akanambia kuwa,’’Hemed
Seif siku zote alikuwa mwanamichezo hadi umauti ulipomfika.’’ Nilikuwa
nikimtania Hemed Seif kuhusu gari zake nzuri za kupendeza alizokuwa akiendesha
pale mjini. Yeye alikuwa siku zote akinipa jibu kuwa, ''Ah! Sheikh Mohamed
watoto hao wananiletea.''
Nyakati za jioni Hemed Seif alikuwa anapenda kukaa kwenye baraza
yao ya ''watoto wa mji,'' akina Said Bembea, Saleh Makubeli na nduguye Athmani
Makubeli, Salim Mohamed Kajembe, Mzee Ali ''Ma-White,'' ambao wote ukimtoa Said Bembea wameshatangulia mbele ya haki.
Baraza hii ilikuwa kwenye kituo cha kuuza mafuta cha Agip karibu sana na
Mkwakwani Stadium ambapo hadi leo napakumbuka maana palikuwa na chai nzuri sana
jioni ambayo nikisimama kusalimia wanabaraza watanilazimisha kunywa angalau
kikombe kimoja kabla sijashika hamsini zangu. Kituo hiki cha mafuta kilikuwa
kikimilikiwa na marehemu Saleh Makubeli. Baraza hii ya Hemed Seif na wenzake
ilikuwa baraza ya manufaa ikipigwa adhana wote wananyanyuka kwenda msikiti wa
jirani maarufu Msikiti wa Maalim Jumbe kwenda kusali. Hemed Seif alikuwa mtu wa
ibada na ukiangalia picha yake na Salim Kajembe utaiona sijda yake jinsi
ilivyomuenea usoni.
Allah amsamehe sahib yangu na kaka yangu dhambi zake na amweke
mahali pema peponi.
Amin.
Kushoto Kewnda Kulia: Kitwana Manara, Rashid Seif Hemed Seif, Abdallah Luo |
Waliosimama wa Kwanza Kushoto: Hemed Seif |
1 comment:
Allah amsamehe dhambi zake kaka yetu, amrehemu na amuingize peponi Amin.
Post a Comment