Sheikh Idriss,
Mashekh wa BAKWATA hakika wana mambo sana.Kuna kitu kinaitwa ''theatrics,'' masheikh wa BAKWATA ni mabingwa na wana medali za dhahabu. Sheikh Mkuu wa BAKWATA Shaaban Simba aliwahi kutoa medali kumpa Reginald Mengi kwa utumishi wake uliotukuka kwa Waislam. Hakika umma ulipigwa na butwaa. Umma ukajiuliza. Sheikh Shaaban Simba hajapata kumsikia Sheikh Hassan bin Amir bingwa wa tafsir ya Qur'an na bingwa wa lugha ya Kiarabu aliyeandika vitabu lukuki mpaka akapewa shahada ya heshima na Al Azhar, Cairo mwaka 1964?Ukiachia sifa yake ya kupigania uhuru wa Tanganyika nk. nk.
Umma ulijiuliza Sheikh Shaaban Simba hajamsikia Sheikh Mohamed Ayub aliyesomesha dini maisha yake yote na ana wanafunzi Afrika ya Mashariki nzima na hao wote wanafunzi wake wana vyuo wanaisomesha Qur'an? Sheikh Shaaban Simba hivi kweli hajapatapo hata siku moja kumsikia Sheikh Aboud Maalim aliyejenga misikiti chungu mzima kwa kuwahamasisha Waislam matajiri na masikini wachangie ujenzi kila mtu kwa uwezo wake alojaaliwa na Allah? Sheikh Aboud Maalim akaweza kujenga Msikiti wa Manyema, Msikiti wa Ngazija, Msikiti wa Maamur, Msikiti wa Mwinjuma Mwinyikambi na mingine tusiyoijua. Achilia mbali kuanzisha scholarship kwa vijana wa Kiislam kusoma Udaktari na Uhandisi Uturuki chini ya taasisi aliyoanzisha, Tanzania Muslim Solidarity Trust Fund.
Sheikh Shaaban Simba hawa wote hakuwaona ila kamuona Sheikh Reginald Mengi?
Kwa wasiowajua masheikh wa BAKWATA hakika wanapata tabu.
Kwa wanowajua masheikh wa BAKWATA hawashangazwi.
Wakati mwingine hakika huwa vioja na vichekesho khasa mtu unatamami kucheka lakini kinachokuzuia ni kuwa jambo lenyewe si la kuchekesha.
Kuna msemo wa Kiarabu unaosema,''Sababu ikijulikana ajabu huondoka.'' Naamini Sheikh Jongo anaujua msemo huu.
No comments:
Post a Comment