Friday 30 May 2014

KUTOKA JF: MAREHEMU HASSAN UPEKA (TANU INTELLIGENCE 1956) NA UANDISHI WA HISTORIA YA TANU

Sideeq,
Kleist Sykes katika ''memoir'' zake alizoandika katika miaka ya 1940 kabla ya kifo chake 1949 akieleza kwa nini African Asscoation ilikuwa wamejazana Waislam anasema kuwa Wakristo walikuwa wakikatazwa kanisani kujihusisha na siasa. (Anaetaka habari hizi asome: Daisy Sykes Buruku, ‘The Townsman: Kleist Sykes,’ in Illife (ed) Modern Tanzanians, Nairobi, 1973, pp. 95-114. Vilevile kuna ''seminar paper'' ya Sykes Buruku, ''The Life of Kleist Sykes,'' bahati mabaya sina citation yake lakini inapatikana Maktaba ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, East Africana, ''The Life of Kleist Sykes.'') Kazi hizi zote Daisy kazifanya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam akiwa mwanafunzi wa John Illife.

Wakati jopo la wanahistoria wa TANU kutoka Kivukoni wanaandika historia ya TANU Hassan Upeka aliwapa ''notes,'' zake alizokusanya katika mahojiano na Abdul Sykes kuhusu TANU. Jopo lilizikataa zile ''notes,'' kwa kumwambia Upeka kuwa historia ile haina uhusiano wowote na Abdul Sykes. Ukweli ni kuwa Upeka alikuwa pale ofisi ya TANU toka mwaka wa 1956 na file lake la kuajiriwa ni na. 1. Upeka alijiunga na TANU Intelligence alipomaliza darasa la 10 Tabora mwaka 1956.

Mimi alikuwa mzungumzaji wangu sana na iko siku alinialika ofisini kwake Mtaa wa Mvita kwa mazungumzo rasmi kuhusu historia ya TANU. Upeka ndiye aliyeniambia kuwa Abdul aliacha katikati kuandika historia ya TANU baada ya kutokubaliana na Nyerere kuhusu asili ya TANU na siasa katika Tanganyika. Dk. Kleruu aliukamilisha baada ya kufanya mabadiliko na mswada ule ulikaa TANU muda mrefu hadi ulipokuja kuibiwa na ''fulani,'' akenda uchapa kwa jina lake. Kitabu hiki hakina tofauti kubwa na kitabu cha historia ya TANU cha Kivukoni College. Vijana wengi wa Dar es Salaam wakimuogopa Upeka ila mimi. (Jamaa watasema najikweza, lakini huo ndiyo ukweli na tulifika mahali tukawa tunapigiana simu mimi niko Tanga na tukiitana ''kaka,'' mimi mdogo kwake akiniita ''kaka'' na mimi ni kaka yangu kwa umri). Wakimuogopa Upeka kwa ile historia yake ya nyuma ya kutisha katika Intelligence.

Upeka amefariki kama miaka minne iliyopita nyumbani kwake Mwananyamala. Hivi natafuta picha za maziko yako nikipata nitazileta hapa In Shaa Allah. Katika watu wa CCM waliohudhuria maziko alikuwa Mzee Kingunge Ngombale Mwiru peke yake.


Waombolezaji Katika Maziko ya Hassan Upeka Nyumbani Kwake Mwananyamala

No comments: