Friday, 30 May 2014

KUTOKA JF: SHEIKH HASSAN BIN AMIR ALIVYOIONGOZA TANU KUWA CHAMA CHA KISEKULA

1.    Re: Tanganyika(TANU) imetoka mbali waasisi wake wengi wao wametangulia mbele ya haki
 By Noel 2014 View Post
MimiQuote siikatai hii historia. But naomba nikuulize, Hivi ni kweli mipango ya hawa
wazee ni kuifanya Tanganyika kuwa Nchi ya kiislamu?



Kushoto Kwenda Kulia: Mufti Sheikh Hassan bin Amir Julus Nyerere,
Abdallah Chaurembo, Rashid Kawawa na Tewa Said Tewa

Noel
Wazee wetu hawakuwa wajinga. Walijua mbinu zote za wakoloni katika kuwagawa watu wa Tanganyika. Tatizo ni kuwa historia ya kweli wengu hawaijui. Nyerere alianza kupata upinzani ndani ya TAA alipochukua uongozi ile mwaka 1953 na chama kikaelekea kufa. Kamati ya Utendaji ikawa wajumbe hawahudhurii vikao. Hili kanieleza Dossa kwa kirefu na mimi nimelieleza katika kitabu cha  Sykes. Ilipofika mwaka 1955 TANU ndiyo inataka kusimama yakatokea tena mengine ya kumpiga vita Nyerere kwa kisingizio cha kutomwamini  kwa Ukristo wake. Sasa hapa ndipo Sheikh Hassan bin Amir akaitisha mkutano Mtaa wa Pemba tena kikao cha usiku kuja kujadili tatizo hili. Mmoja wa masheikh waliohudhuria mkutano ule alikuwa Sheikh Nurdin Hussein.


Sheikh Nurdin Hussein

Hao wote waliokuwa wakileta chokochoko hizi walizileta katika misingi ya dini. Sheikh Hassan bin Amir alijua wazi kuwa wakikosea hapa kupiga vita udini basi wakaloni watakuwa wamapeta bakora ya kuwapigia wananchi kwani wao watatumia kigezo cha dini kuleta fitna baina ya Waislam na Wakristo kama walivyofanya India na Pakistan. Wazee wetu wakiyajua yote haya. Ndipo Sheikh Hassan bin Amir alipoweka msimamo wa TANU kuwa ni chama cha kisekula na yoyote atakaemnyanyapaa Mkristo adhabuyake ni ''kutoswa,'' yaani kufukuzwa chama.(Habari hizi zipo mtu akizitaka anaweza kuzisoma katika makala ya  Rajab Diwani''TANU Ilipambana na Misukosuko Mingi' UHURU 3rd July, 1974).


Ikawa kuanzia pale Bantu Group ya akina Yusuf Bakis ikawa moja ya kazi yake kubwa ni kupiga vita viashiria vyovyote vile vya Uislam katika TANU kiasi hata ukisalimia mathalan,''Asalaam Aleikum,'' jibu ambalo utakalopata siyo mwitiko wa ''Waleikum Salaam,'' kama ilivyo sheria bali utajibiwa, ''Ahlan tabu.'' Siku ya pili hurudii tena utasalimia, ''Uhuru,'' na jibu litakuja, ''Uhuru.'' Haya yote nimeeleza kwa kirefu sana katika kitabu cha Sykes kwa hiyo ukweli ni kuwa hapakuwa na msukomo wowote wa kutaka ati kuifanya Tanganyika nchi ya Kiislam. Ndiyo maana mwaka 1958 Sheikh Suleiman Takadir alifukuzwa TANU pale alipohoji nafasi ya Waislam katika Tangayika huru na kuleta hali ya ugomvi baina yake na Nyerere.

Mifano iko mingi lakini hii nadhani inatosheleza kuuweka huu ukweli wazi hapa jamvini. Ndiyo maana hata All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT) pale ilipoanzishwa na kina Ramadhani Mashado Plantan haikuungwa  mkono na Waislam. Wakati mwingine hujiuliza hivi kwa nini Nyerere aliiogopa historia hii ilahali mie naiona ndiyo iliyokuwa inajenga utaifa wa Tanganyika? Historia hii ikawa imefutwa kabisa kiasi leo ukiyataja majina haya ya  wazee wetu akina WildCard wanashtuka na kutishika sana.

No comments: