Rate This

Na Mohammed Said
Utangulizi
Kwa kipindi kirefu historia ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa ni ile historia rasmi ambayo imeathiri historia nyingi Afrika. Viongozi wa Afrika wanapenda ile historia itakayowakweza na kuwaonyesha wao katika mwanga wa kupendeza. Vinginevyo historia hiyo haitakiwi. Wazalendo wenyewe hawakuwa na hamu ya kuandika historia hii na watu wa nje walioandika historia ya mapinduzi ya Zanzibar hawakupata kuifanyia haki historia ya Zanzibar labda kwa ugeni wao na kwa kuyaamini maelezo yaliyokuwa “wazi” kwa wakati ule, mfano mkubwa ukiwa ni kule kuamini kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yalipangwa na makomredi wa Umma Party.
Hapajakuwapo udanganyifu mkubwa katika uandishi na utafiti kama huu. Dkt Ghassany amekiweka chano uwanjani bila kawa. Akizungumza na Abdushakur Aboud wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VoA), Dkt Ghassany amesema kuwa historia ya Zanzibar ni historia ya kujijuwa maisha yake akiwa mjukuu wa babu wa mababu Muomani na mabibi wa Kimanyema na Kimwera – mchanganyiko wa damu ya Kiarabu na Kiafrika.
Hii kwa hakika ndiyo historia ya wananchi wa Zanzibar. Ni tabu sana kumpata huyo Muarabu Zanzibar, maana kila umuonae Muarabu basi ana mjomba na shangazi Mwafrika. Maadui wa Zanzibar wakiweka mkazo katika ubaguzi wa rangi na kuwafitinisha Wazanzibari. Ukweli huu ndiyo chanzo cha matatizo yote yaliyoikumba Zanzibar toka vyama vya siasa vilipoanza katika miaka 1950 na matatizo yaliyosababisha mauaji, ya mwisho yakiwa mwaka 2001.
Mohamed Omari Mkwawa
Mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vyingi Tanzania, nilibahatika kufuatana na mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, katika kampeni za uchaguzi katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga. Alipokuwa Tanga, Prof. Lipumba alifanya mkutano mkubwa sana Tangamano kiasi cha kuishtua CCM. Baada ya mkutano ule, Prof. Lipumba na ujumbe wake walialikwa nyumbani kwa mama mmoja akijulikana kama Mama Ummie (sasa ni marehemu), ambako walifanyiwa dhifa kubwa. Kote tukipita mitaa ya Tanga msafara wetu ulikuwa ukishangiliwa kwa nguvu sana. CUF ilikuwa imeingia Tanga kwa kishindo kikubwa.
Mimi kazi yangu ilikuwa kuangalia niliyokuwa nayaona na kupiga picha. Kwa hakika nilikuwa nikishuhudia historia ikijiandika. Historia ambayo ilikuwa imeshahibiana sana na ile ya wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika katika miaka 1950. Lakini ninalotaka kusema si hili, bali ni picha ambayo niliipiga ndani ya nyumba ya Mama Ummie. Picha hii ilikuwa inamuonyesha mzee mmoja wa makamo aliyevaa fulana ya CUF, mbele ikiwa na picha ya Prof. Lipumba. Mzee huyu alikuwa amekaa nyuma ya Prof. Lipumba. Kwa wakati ule picha hii haikuwa na maana yoyote kwangu, na hata nilipokuwa naitazama mara kwa mara sura yake, si iliyokuwa inanivutia bali ile fulana ya CUF aliyovaa ambayo ilikuwa na picha ya rafiki yangu, Prof. Lipumba.
Mungu ana mipango yake. Mahangaiko ya kutafuta riziki yakanihamishia Tanga na nikawa karibu sana na baadhi ya viongozi wa CUF na wanachama wake. Sasa hapa ndipo nilipokuja kuonana uso kwa uso na mzee yule kwenye picha yangu niliyoipiga hata kwa wakati ule ilikuwa miaka mingi iliyopita. Jina la mzee wangu huyu ni Mohamed Omar Mkwawa. Ilikuwa katika barza yetu ya kawaida ya kunywa kahawa na kula pweza huku tukijadili historia ya Tanzania ambako siku moja Mzee Mkwawa alinambia, “Mohamed nataka nikuambie kitu. Unajua mimi nimehusika sana katika mapinduzi ya Zanzibar?”

Kushoto: Mohamed Omari Mkwawa, Haji Duni na Prof. Ibrahim Lipumba
Nilimuangalia Mzee Mkwawa kwa makini. Fikra yangu ya utafiti na uandishi ishashtuka haipo tena usingizini. Mzee Mkwawa aliendelea, “Mimi ndiye niliyekuwa nikiwavusha Wamakonde kutoka Kipumbwi kwenda Zanzibar kuipigia kura ASP na wakati wa mapinduzi mie ndiye niliyewavusha Wamakonde kwenda kuipindua serikali ya Jamshid.” Sasa moyo wangu ukaanza kudunda kwa nguvu. Naisemesha nafsi yangu, “Huyu mzee anajua uzito wa maneno haya?” Tuishie hapa.
Kuanzia siku ile nikawa sasa namtazama Mzee Mkwawa kwa jicho jingine na heshima yangu kwake ikawa imepanda maradufu. Nilikuwa nimeshatambua kuwa Mzee Mohamed Omari Mkwawa alikuwa mmoja wa wanahistoria waliosahaulika katika historia ya Tanganyika na Zanzibar. Juu ya hayo nilishangazwa na kitu kimoja. Iweje leo huyu mwanamapinduzi wa ASP ambae Abeid Amani Karume alimpa jina la “Tindo” kwa ujasiri wake amekuwa mstari wa mbele CUF, chama ambacho kinanasibishwa na Hizbu, hasimu mkubwa wa ASP?
Dkt. Harith Ghassany

Dr. Harith Ghassany na Mwandishi, Muscat 1999
Nilikutana na Dkt. Harith Ghassany mwaka 1999 nyumbani kwake Maskati, Oman. Naikumbuka siku ile kama jana vile. Kanipeleka kwake mwenyeji wangu Farouk Abdulla, lakini kabla ya kunipeleka nilikuwa nimeshalisikia jina lake mara nyingi sana pale Maskati. Kila nikikutana na jamaa wenye asili ya Tanzania, jina lake litaibuka. Katika fikra yangu ikanijia kuwa Dkt Ghassany atakuwa ni mtu mzima. Sielewi kwa nini nilipata picha hii. Tulipopiga hodi na akatokea Dkt. Ghassany kuja kutufungulia mlango nikapata mshangao mkubwa.
Aliyekuwa mbele yangu alikuwa ni kijana mdogo sana tofauti na nilivyodhani. Kwa njia ya utani hata kabla sijatoa salamu. Nikamgeukia Farouk nikasema, “Ah! Dkt. Ghassany, Dkt. Ghassany, Dokta mwenyewe ndiye huyu?” Mila na tamaduni za watu wa pwani wakikutana hazipishani. Maskhara ni dalili ya mapenzi. Dkt Ghassany pale pale alipokea yale maskhara na akajibu, “Bwana wangu we, wanakutisha bure kwani we ulidhani litakuwa jitu kubwa?”
Urafiki na udugu wetu umedumu hadi leo na ndipo katika mazungumzo aliponifahamisha kuwa anataka kuandika historia ya kweli ya mapinduzi ya Zanzibar. Hapo ndipo nilipomjuvya kuhusu Mzee Mkwawa na nikamuomba aje Tanga amuhoji.
Kitu kimoja mashuhuri kwa mashujaa wa harakati za siasa katika Tanzania ni kuwa takriban wote wana hali ngumu sana za maisha. Sikujua vyema hali ya Mzee Mkwawa hadi nilipofika nyumbani kwake na Dkt. Ghassany. Utu uzima na udhaifu wa maisha ulikuwa umempiga barabara. Nilimjulisha Dkt. Ghassany kwa Mzee Mkwawa na kuwaacha waendelee na maongezi yao. Niliporudi mchana kumchukua Dkt. Ghassany, rafiki yangu alinambia nimuache nije jioni kumfuata. Niliporudi jioni nilimkuta Dkt. Ghassany amechoka na uso umesawijika.
Tukiwa ndani ya gari yangu tunaondoka nikamuuliza kulikoni. Dkt. Ghassany akanambia maneno ambayo hadi leo yamebaki kichwani mwangu, “Mohamed, ufunguo wa kitabu changu anao Mzee Mkwakwa na kama nisingeonana nae utafiti wangu wote wa kabla ungelikuwa hauna maana yoyote.”
Dkt. Ghassany alikuwa amechukuliwa na Mzee Mkwawa katika safari ya zaidi ya nusu karne. Mzee Mkwawa akimshika mkono kwanza kumpeleka Pemba ambako akiwa kijana wa kiasi cha miaka 25 akifanya kazi ya uashi. Huo ndio ulikuwa wakati wa siasa za ASP na Hizbu zimepamba moto. Mzee Mkwawa alikuwa mmoja wa wachezaji wa ngoma ile hata kama alikuwa anatoka Tanganyika. Dkt. Ghassany akavushwa na kuletwa pwani ya Kipumbwi na Sakura ambako Mzee Mkwawa alikuwa akisimamia kambi ya mafunzo iliyokuwa msituni ya wakata mkonge, wengi wao wakiwa Wamakonde, kambi ambayo ilitoa askari waliotumika kuipindua serikali ya Mohamed Shamte, 12 Januari 1964.
Dkt. Ghassany hakuwa amejitayarisha kwa haya. Alishangwazwa na uwezo wa kumbukumbu wa Mzee Mkwawa, akitaja majina na mahali na akirudia mazungumzo neno kwa neno kati yake na maofisa wa serikali ya Tanganyika kutoka vyombo vya usalama waliomtia katika operesheni maalum ya kuipindua Zanzibar kutoka Tanganyika. Majina ya Abdulla Kassim Hanga, Jumanne Abdallah, Ali Mwinyi Tambwe, Victor Mkello, Oscar Kambona na wengine yakawa yanadondoka moja baada ya lingine. Taarifa hizi ndizo zilizommaliza Dkt. Ghassany na kumsawajisha uso.
Mimi binafsi nilipigwa na butwaa. Nilibaini, kama alivyobaini Dkt. Ghassany, kuwa Mzee Mkwawa alikuwa hazina na tulikuwa tumevumbua mgodi wa dhahabu. Kazi yetu sasa ilikuwa kuchimba tu.
Kumekuwa na uvumi kwa miaka mingi katika duru za wanasiasa wapya na wa zamani na katika wanafunzi wa historia ya Tanzania na Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Ali Mwinyi Tambwe alihusika sana katika kupinduliwa kwa serikali ya Zanzibar, lakini hakuna aliyejuwa ni kwa kiwango gani na alihusika vipi. Lakini zito ni kuwa yeye mwenyewe akiudhika sana mtu akimuuliza habari zile. Kwa nini ilikuwa hivyo? Kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru cha Dkt Ghassany kimekuja kutoa majibu. Hakuna binadamu apendae historia yake ihusishwe na mauaji na dhulma na kufutwa kwa nchi yake.
Kwa kipindi cha takriban miaka saba, Dkt. Ghassany alikuwa akija Tanga kwa mahojiano na Mzee Mkwawa na katika kipindi hicho Mzee Mkwawa alitupeleka Kipumbwi na Sakura na kutuonyesha sehemu zile ambazo walikuwa na kambi na wakifanya mazoezi ya kivita na matumizi ya silaha. Mkahawa, ambao wale wakata mkonge walikuwa wakila chakula cha usiku kabla ya kuvushwa kwa vyombo vya bahari kwenda Unguja, bado upo hadi leo ingawa kwa sasa kijumba kile hakitumiki tena kama mkawaha. Endapo itakuja siku serikali ya Zanzibar itataka kuhifadhi historia ya Mapinduzi ya Zanzibar, bila shaka moja ya vitu vitakavyokuwa katika makumbusho ni picha ya hicho kibanda.
Victor Mkello
Kipumbwi haijabadilika. Iko kama vilevile iliyokuwa miaka ya 1960. Kipumbwi imebaki vilevile kama kijiji cha uvuvi. Mzee Mkwawa alitupeleka hadi sehemu ambapo bahari imeingia katika kijiji lakini sehemu hiyo imefunikwa na mikoko mingi na vichaka. Tuliingia ndani na kuangalia mandhari ya pale mahali. Hakika pale palikuwa sehemu nzuri ya kujificha. Leo imekuwa sehemu hii ni maarufu kwa watu wa magendo. Mzee Mkwawa alitueleza kuwa hapo ndipo walipojificha na ndipo walipopandia vyombo vyao kwa usiri mkubwa wakati wote wakiwa wamevaa nguo matambara na kofia za makuti kama wavuvi. Tanga ilikuwa kituo muhimu cha kufanikisha mapinduzi ya Zanzibar. Haikuwa bure kuwa Ali Mwinyi Tambwe, Jumanne Abdallah na Victor Mkello walikuwa hapo na wala haistaajabishi kwa Dkt. Ghassany kutueleza kuwa vinara wa mapinduzi kwa upande wa bara, Mkello na wenzake, walisubiri taarifa za mapinduzi katika mkesha ndani ya ofisi ya TANU Tanga.
Napenda kukiri kuwa sikupata kushiriki kama msikilizaji wa mahojiano wakati wa utafiti wa Kwaheri Ukoloni,Kwaheri Uhuru. Kazi yangu kubwa sana ilikuwa kufungua milango ya gari na kumwendesha daktari. Kwa ufupi, kazi yangu ilikuwa kumwekea mwandishi mazingira mazuri ili kazi yake iwe nyepesi. Kwa hakika ilikuwa kazi ambayo na mimi vilevile nilisoma, kujifunza mengi na kupata faida kubwa.
Katika haya nakumbuka sakata la kumtafuta Victor Mkello. Leo si wengi wanaomjua Victor Mkello au hata kupata kusikia jina lakelikitajwa. Lakini kwa sisi tuliokuwa wadogo tukiwa shule katika miaka ya 1960, Mkello alikuwa hapungui katika magazeti ya Ngurumona Mwafrika. Mzee Mkwawa ndiye aliyetusaidia kumtafuta alipo. Victor Mkello ndiyo aliyekuwa “Amiri Jeshi Mkuu” wa lile jeshi la Wamakonde lililokuwa na makao yake makuu katika mashamba ya mkonge ya Sakura na Kipumbwi. Bila ya kupata kauli ya Mkello, kitabu kisingeweza kuandikika.
Ilichukua muda kuweza kumpata. Kwanza tulikwenda Muheza ambako ndiko kwao. Huko tukaambiwa kuwa hakuwapo hapo, bali kwa muda mrefu alikuwa Tanga. Mwishowe tulimkuta nyumbani kwake, Nguvu Mali. Mkello alikuwa katika kitanda cha mauti. Kisukari kilikuwa kikimla kiwiliwili chake. Hakuwa anaweza kunyanyuka kitandani wala kukaa. Kwa hakika alikuwa anasikitisha.
Huyu hakuwa Victor Mkello niliyekuwa namsoma katika magazeti wala yule ambae Mzee Mkwawa alikuwa akituelezea. Mtu mjanja aliyepambana na Magiriki wamiliki wa mashamba ya mkonge akitetea haki za Waafrika katika miaka ya 1960. Huyu kwa kweli hakuwa yule Victor Mkello aliyekuwa akisaidiana na TANU na Mwalimu Julius Nyerere kupigania uhuru wa Tanganyika. Hiki mbele yetu kilikuwa kivuli chake. Hapakuwa na wasiwasi wowote Victor Mkello alikuwa akisubiri malaika wa mauti amtembelee na yeye hilo alikuwa akilijua fika.
Victor Mkello na Mzee Mkwawa wanamapinduzi waliofutwa katika historia walitazamana na wakasalimiana kama vile hakuwapata kujuana. Jicho la Mkello lilikwenda kwa Dkt. Ghassany kisha likaangukia kwangu kisha likarudi kwa mwanamapinduzi mwenzake Mzee Mkwawa. Baada ya utambulisho uliofanywa na Mzee Mkwawa nilihisi woga na wasiwasi kwenye sura ya Victor Mkello. Hakuwa anaamini kuwa Dkt. Ghassany katoka Maskati kwa ajili ya utafiti wa historia na hili lilijidhihirisha alipofunua kinywa kuzungumza. Victor Mkello alikuwa na hisia kuwa alifuatwa kukamatwa kwa vifo vya Waarabu vilivyotokea Zanzibar wakati wa mapinduzi ili apelekwe Mahakama ya Kimataifa. Baadaye, Dkt. Ghassany alinifahamisha kuwa jinsi Waingereza walivyomueleza katika taarifa zao za siri ambazo yeye alizisoma London zimeafikiana kabisa na jinsi alivyomuona pale. Waingereza walimsifia Mkello kwa kusema kuwa alikuwa bingwa wa kuteleza kama samaki ndani ya maji.
Kufupisha maelezo. Ilichukua karibu miaka mitatu kwa Victor Mkello kukubali kuzungumza kuhusu mapinduzi ya Zanzibar. Dkt Ghassany akienda Maskati na kurudi Tanga na kila akienda kwa Victor Mkello, Mkello hakuwa tayari kueleza kile alichokijua kuhusu mapinduzi ya Zanzibar. Kila nilipokwenda na Dkt Ghassany kumuona Mkello hali yake ilikuwa inazidi kudidimia. Sasa alikuwa kakatwa mguu mmoja kwa ajili ya kisukari. Ilikuwa katika hali ile katika siku zake za mwisho ndipo siku moja alipomwambia Dkt Ghassany aje siku ya pili na yeye atazungumza na angependa azungumze mbele ya mkewe ili amkumbushe pale atakapokuwa kasahau kitu.
Hapa ndipo ilipo moja ya sehemu tamu kabisa ya kitabu hiki, Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru. Victor Mkello, Amiri Jeshi Mkuu wa Mamluki wa Kimakonde alizungumza. Mimi sikushiriki katika mazungumzo yale, nilijiweka pembeni ili Mkello azungumze na Dkt. Ghassany kwa utulivu. Nilikuwa nimeegesha gari yangu karibu ya msikiti jirani ya nyumba ya Mkello nikimsubiri daktari akamilishe upasuaji mgonjwa apate nafuu. Mwendo wa Dkt Ghassany wa kudunda alipokuwa ananijia pale nilipoegesha gari ulidhihirisha furaha yake.
Haukupita muda mrefu baada ya mazungumzo yale na Dkt Ghassany, Victor Mkello akaaga dunia kimya kimya. Hakuna mtu aliyejua kifo chake kama ilivyokuwa vifo vingi vya mashujaa waliopigania uhuru wa Tanganyika. Hakuna hata gazeti moja lililotoa taazia yake wala hotuba hazikusomwa kaburini kwake. Mkello aliondoka katika historia ya Tanzania kimya kama jinsi mamluki wake walivyokuwa wakiingia Zanzibar kimya kimya usiku mkuu na kwa siri, mapanga yao makali ya kukata mkonge yakiwa chini ya nguo zao za ndani yakisubiri kuivamia Zanzibar na kuua watu wasio na hatia. Kazi hii kwao haikuhitaji mafunzo kwani mafunzo walikuwanayo muda mrefu katika kazi yao ya kukata mkonge katika mashamba ya mkonge ya Tanga. Pigo moja lilitosha kuangusha chini jani zito la mkonge seuze kiungo cha binadamu.
Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru ni kitabu kilichoandikwa kwa staili ya pekee ya wahusika wenyewe wa matokeo katika mapinduzi kujitolea kueleza kile kilichotokea katika mapinduzi, kabla na baada yake. Kuanzia mipango ya kuangusha serikali ya Zanzibar hadi katika kuwaua wale waliokuja kushukiwa kuwa ni maadui wa mapinduzi hadi kufikia hata kuweka wazi jinsi walivyoshiriki katika mengi ya kusikitisha kupelekea hata msomaji kujiuliza: kwa nini hawa watu baada ya miaka yote hiyo kupita wameamua kueleza yote hayo? Vipi Abdallah Kassim Hanga, Othman Shariff, Mdungi Ussi, Jaha Ubwa, Abdulaziz Twala na wengineo walivyouliwa, nani alitoa amri ya mauaji, nani aliwauwa na katika mazingira gani. Kifo cha Karume mwenyewe kwa mtutu wa bunduki hakikuwekewa pazia na chanzo cha kuamuliwa kuwa auawe ni tofauti ya kilichozoeleka kuelezwa. Karume hakuuawa na “wapinga mapinduzi” kama ilivyozoeleka kuelezwa katika historia rasmi.
Kwa kumaliza, tusubiri mapitio ya kitabu hiki na ni wazi kuwa wasomaji watapata mengi ya kuelimisha na kuhuisha. Tunategemea wasomi wa somo la historia watakaopitia kitabu hiki watatufanyia hisani kubwa kwa kuwaleta katika picha wahusika wakuu wa mapinduzi – Mwalimu Julius Nyerere – fundi mkuu mwenye kishindo kikubwa lakini hakisikiki, mkono wake wa chuma hauonekani, uso wake nyuma ya pazia, Abdallah Kassim Hanga – kiongozi hasa na mpangaji wa mapinduzi, Victor Mkello – mtumishi wa Hanga na Nyerere bila ya yeye mwenyewe kujua kati ya hao wawili nani aliyekuwa bingwa kumshinda mwenzake katika mchezo mchafu wa siasa ya kuiuwa Zanzibar na Wazanzibari na wengineo.
Lakini juu ya hayo yote mipango hii ilikuwa ni ya akina Nyerere, Hanga na Mkello pekee? Dkt. Ghassany anaeleza nini kuhusu mkono wa Waingereza, Algeria, Misri, Wachina, Warusi, Marekani na Mayahudi? Nini kilichowasukuma hao wote katika mapinduzi ya Zanzibar? Nini kilimsukuma Nyerere, kuwapindua Waislam walioupigania Uhuru wa Tanganyika na baadae kuwapinduwa Waislam walioupigania Uhuru wa Zanzibar na kuendelea kuwadhibiti hata baada ya kuipindua Zanzibar? Nini kilichowasukuma Waingereza na Wamerekani kuachia mapinduzi yafanyike? Lakini kubwa zaidi, kipi kilichowasukuma Wayahudi kuingia na kusaidia mapinduzi, ni ile chuki yao ya asili dhidi ya Waarabu au kulikuwa na jengine ambalo liliwatia khofu? Na kwanini kitabu kiitweKwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru: Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia? Kitabu kina majibu ya maswali haya na mengine ambayo bado hayajaulizwa na chemchemu mpya za utafiti.
Dkt. Ghassany anastahili pongezi kubwa sana kwa kuinusuru historia ya mapinduzi ya Zanzibar na kuwaamsha Wazanzibari na Watanganyika toka lepe zito la usingizi ili wajitambue na wamjue adui yao. Anastahiki pongezi kubwa zaidi si kwa kukiandika kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru, bali kwa kutumia mrengo usiokuwa na mrengo. Huna pa kumuweka Dkt. Ghassany na baada ya kumaliza kukisoma kitabu ukaridhika napo. Kama utafikiria kuwa kitabu ni cha CUF, basi baada ya kusoma mpaka mwisho utavunjika moyo. Kama utamtumbukiza ndani ya CCM, basi ataelea. La kama unataka upae nje ya masunduku na mapakacha, basi utamuona katulia ndani ya uhuisho wa umoja wa Zanzibar na Tanganyika Mpya – Tanzania Mpya.
Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru ni ngoma nzito ambayo watu wameanza kuicheza hata mdundo haujaanza kupigwa! Tayari imeshaingia katika rikodi za Hansard za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tayari imeshasikika katika Sauti ya Marekani. Tayari daktari anafuatilia kwa karibu ukweli wa Maridhiano na kuwa kwa mara nyengine tena ukweli wake umeshaanza kupotoshwa na waroho na tayari historia mpya na kubwa zaidi hata kuliko ile ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 imeshaanza kuvurugwa.
Watengenezaji wa filamu Hollywood wana mtindo wa kumaliza senema zao za matokeo ya kweli kwa kueleza katika maandishi yale yaliyowafika wahusika wa kisa kilichotengenezwa hiyo senema. Huonyesha majina na mwisho wa hao wahusika, kama wahai, wako wapi, wamekufa na kama wamekufa ni kwa kuuliwa au kwa amri ya Mungu nk.
Katika Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru majina ya wahusika machache ambayo yametajwa katika makala haya yako kama hivi:
Mohamed Omar Mkwawa: Yu hai na anaishi Makorola Tanga

Abeid Amani Karume: Ameuawa 1972

Abdallah Kassim Hanga: Ameuawa 1967/68
Mustafa Songambele: Yuhai anaishi Songea
Victor Mkello: Amekufa kifo cha kawaida
Ali Mwinyi Tambwe: Baada ya mapinduzi, alikuja kuhusika katika mchakato wa kuunda muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Amekufa kifo cha kawaida.
Jumanne Abdallah: Alitumikia serikali kwa muda mrefu hadi alipofariki kifo cha kawaida
Oscar Kambona: Aligombana na Nyerere na akakimbia nchi mwaka 1967 na kwenda kuishi uhamishoni Uingereza

Kuna vigogo kadhaa ambavyo viko hai na kwa sasa wameomba majina yao yahifadhiwe.

About Zanzibar Daima

Zanzibar Daima, Jana, Leo na Kesho