Haruna Taratibu |
Mubarak Ghulum Mtangazaji Radio Kheri Akiwa Katika Matayarisho ya Kipindi Maalum cha Miaka 53 ya Uhuru wa Tanganyika |
![]() |
Kushoto Kwenda Kulia: Saleh Tambwe, Job Lusinde na Samweli Sitta |
Kutoka Kushoto: Iddi Faiz Mafongo, Sheikh Mohamed Ramiya, Julius Nyerere, Saadan Abdu Kandoro na |Haruna Taratibu Stesheni ya Reli Dodoma 1956 |
Mwandishi Akitoa Historia ya Maisha ya Shujaa Haruna Taratibu Muasisi wa TANU Jimbo la Kati (Central Province) 1954 Kipindi Maalum Kilirushwa na Radio Kheri Usiku wa Tarehe 8 Kuamkia 9 Desemba 2014 Kuadhimisha Miaka 53 ya Uhuru wa Tanganyika
KUMBUKUMBU
YA MIAKA 53 YA UHURU WA TANGANYIKA
Tunamkumbuka
Shujaa wa Uhuru wa Tanganyika
Haruna Taratibu Muasisi wa TANU Jimbo la Kati
(Central Province) 1954
Sifa kuu katika ujumbe wa Nyerere ilikuwa ni kule kueleweka kwa mantiki yake na kuweza kuwavutia wananchi wa kawaida. Hawa ndiyo walikuwa watu walioyageuza majumba yao kuwa ofisi za TANU, wakafanya kampeni kupata wanachama, wakauza kadi za TANU, na katika kufanya hivyo wakahatarisha maisha yao.
African Association mjini Dodoma ilikuwa
ikiongoza katika harakati baada ya Vita Kuu ya Pili. Ilikuwa na wanasiasa wenye
juhudi sana na wabunifu kuliko wanasiasa wengine wote waliopata kutokea katika
historia ya Tanganyika. Wanasiasa hawa walikuwa Ali Ponda, Mmanyema na Hassan
Suleiman, Myao, rais na katibu wake. Mwaka 1945 Ali Ponda alitoa wito kwa
Waafrika wote kuungana kama umma mmoja.[1]
Lakini kuanzia mwaka 1948 harakati za siasa mjini Dodoma zilififia, na TANU
ilipoanzishwa mnamo Julai, 1954, tawi la TAA Dodoma lilikuwa limedorora kiasi
kwamba kilishindwa hata kupeleka mjumbe kwenye mkutano ule wa TAA wa kuundwa
kwa TANU. Pamoja na ukweli kuwa mji wa Dodoma kulikuwa na Kikuyu Secondary School
(sasa Alliance Secondary School) ambako kulikuwa na walimu wa Kiafrika, wengi
wao kutoka Makerere, ambao kama wasomi, wangechukua juhudi kuihuisha African
Association. Labda kwa kuhisi kuwa hapakuwapo na ukinzani unaokwenda kinyume na maslahi yao katika mfumo wa kikoloni, walimu
wale waliamua kujitenga na siasa. Kwa hiyo basi, harakati dhidi ya serikali ya
kikoloni ziliachwa kuwa mikononi mwa wa Waislam wa mjini Dodoma, wengi wao
wakiwa wachache wa elimu.
Mwaka 1953, Haruna Taratibu, alikuwa na umri wa miaka 23. Wakati akifanya kazi
Public Works Department (PWD) kama mwashi, alijaribu kuunda chama cha
wafanyakazi kwa kuwahamasisha na kuwakusanya vibarua walioajiriwa katika kazi
za ujenzi. Kwa sababu ya harakati hizo za kutaka kuanzisha chama cha wafanyakazi,
Taratibu alionekana na wakoloni kama mtu mkorofi na mzusha vurugu. Hata hivyo
Taratibu hakufanikiwa kuanzisha chama hicho na matokeo yake akapewa uhamisho
kwenda Singida kama adhabu. Taratibu alivutiwa sana na harakati za Mau Mau
nchini Kenya na alizoea kufuatilia matukio yake katika gazeti lake alilokuwa
akilipenda sana, Baraza, gazeti la Kiswahili la kila wiki kutoka Kenya.
Ilikuwa katika Novemba 1954 wakati Taratibu
alipokuwa akipekuapekua gazeti hilo ndipo alioposoma habari kuhusu TANU.
Taratibu aliuliza pale Singida mjini kama kuna tawi la TANU. Taratibu
alifahamishwa kukuwepo kwa tawi la TANU
pale mjini na katibu wake alikuwa mzee mmoja kwa jina la Mzee Kinyozi.
Taratibu alikata kadi yake toka kwa huyo mzee na akawa mwanachama wa chama cha
siasa. Asubuhi iliyofuata Taratibu aliingia ofisini kwake na akaiweka kadi yake ya
uanachama wa TANU yenye rangi
nyeusi na kijani juu ya meza yake, kila mtu aione. Ofisa Mzungu wa PWD Singida
hakuweza kuvumila ufedhuli kama ule, alishauri Taratibu apewe uhamisho kurudi
Dodoma alikotoka, kabla hajaeneza sumu
yake kwa Waafrika wengine.
Mwaka 1955 wakati wimbi la utaifa wa Tanganyika
lilipokuwa limepanda sana nchini Tanganyika Omari Suleiman alikuwa na umri wa
miaka 43. Suleiman alikuwa fundi cherahani akifanya shughuli zake katika nyumba
moja katikati ya mji wa Dodoma. Mkabala na nyumba ambamo Suleiman alikuwa
amepanga chumba kimoja ilikuwa nyumba aliyopanga Taratibu. Mara baada ya kupewa
uhamisho kutoka Singida, Taratibu alimuuliza jirani yake, Suleiman, kama kuliwepo
na tawi la TANU pale mjini. Suleiman alimwambia Taratibu kuwa hapakuwepo na
tawi la TANU mjini Dodoma na alimjulisha habari kuwa kulikuwa na tetesi mjini
kuwa Hassan Suleiman amemuahidi na kumhakikishia DC kuwa yeye, akiwa katibu wa
Jimbo wa TAA, hatairuhusu TANU kusajiliwa katika Jimbo la Kati bila ya idhini
yake.
Lakini ukweli ulikuwa Hassan Suleiman alikuwa
tayari ameisajili TANU lakini hakumfahamisha mtu yoyote wala kufanya juhudi
yoyote kuitisha uchaguzi au kufanya mkutano. Hassan Suleiman kama, Omar
Suleiman alikuwa na umri wa miaka arobaini na tatu mwaka 1955. Tofauti na Omari
Suleiman, Hassan Suleimani alikuwa ameelimika na alikuwa mwanasiasa mwenye
uzoefu akiwa amekiongoza chama cha African Association. Halikadhalika alikuwa
amehudhuria mikutano ya African Association Tanganyika na Zanzibar. Baba yake
Hassan Suleimani, Taufik bin Suleiman alikutana na Burton, mvumbuzi mashuhuri,
kisiwani Zanzibar; na aliajiriwa kama mmoja wa wapagazi katika safari yake ya
kutafuta chanzo cha mto Nile. Alisafiri na Burton hadi Bagamoyo ambako kuanzia
hapo ndipo walipofunga safari ya bara. Taufik alifariki mwaka 1920 Hassan
Suleiman akalelewa na shangazi yake, Binti Taufik. Kisa cha kusoma kwa Hassan
Suleiman ni mfano mmoja muhimu sana unaoonyesha jinsi wazazi wa Kiislam
walivyokuwa waiuthamini Uislam. Hassan Suleiman alichaguliwa kuingia daraza la
sita St. Andrewís College Minaki, mwaka 1925. Shangazi yake alipopata taarifa
kuwa mtoto wa ndugu yake alikuwa anasoma shule ya wamishionari alipata hofu ya
kile ambacho huenda kitamtokea mwanae, yaani kubatizwa. Alitembea kwa miguu
kutoka Dar es Salaam hadi Minaki kumchukua mtoto wake. Siku hizo njia
iliyokuwapo kwenda Minaki kutoka Dar es Salaam ilikuwa njia ya miguu kupitia
vichakani. Hassan Suleiman alikuwa hajasoma hata majuma mawili mara akamuona
shangazi yake anaingia darasani kumtoa shule na akarudinae nyumbani. Sababu
aliyoitoa bibi mkubwa yule kwa mwalimu mkuu mmshionari ilikuwa, anahofu mwanae
atakuwa murtadi. Safari ya miguu ya kurudi Dar es Salaam iliwachukua siku
mbili.
Mwaka 1953 Nyerere alipokwenda Dodoma kuhudhuia
mkutano wa Kamati ya Elimu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Nyerere
alifikia kwa Hassan Suleiman na Nyerere akatambulishwa kwa wazalendo wengine
waliokuwa wakiondokea katika siasa kama Oscar Kambona, wakati huo akifundisha
katika Kikuyu Secondary School, Nsilo Swai na Kanyama Chiume ambao wote hapo
baadae walikuja kuwa mawaziri katika Tanganyika huru. Kanyama Chiume naye
vilevile alikuja kuwa waziri Nyasaland (Malawi) ilipopata uhuru.
Haruna Taratibu, Omari Suleimani na marafiki
zake wachache waliunda kamati ndogo kisha wakaandika barua kwenda makao makuu
ya TANU Dar es Salaam kuomba ruhusa ya kufungua tawi la chama. Katibu mwenezi
wa TANU, wakati ule Oscar Kambona, aliwaandikia kuwaeleza kuwa Hassan Suleiman
tayari alikuwa ameshaisajili TANU na ikiwa uchaguzi wa viongozi haujafanyika
basi waonanena na yeye pamoja na Ali Ponda. Omari Suleiman na Haruna Taratibu
hawakuridhika na majibu kutoka makao makuu ya TANU kwa hiyo walikwenda kutafuta
ushauri kwa Edward Mwangosi, aliyekuwa mwanachama mkongwe wa African
Association. Mwangosi aliishauri kamati ile iitishe mkutano Community Centre
ili kujadili kufungua tawi la TANU, na Hassan Suleiman na Ali Ponda waalikwe
kuhudhuria. Kadhalika Mwangosi aliishauri kamati ile kuwaalika walimu waliokuwa
wakifundisha Kikuyu Secondary School, wengi wao wasomi kutoka Makerere
kuhudhuria mkutano huo. Mwangosi
aliwaambia wajumbe wa kamati ile ndogo kuwa wasomi wa Makerere walikuwa ni
muhimu sana kwenye chama kwa kuwa wangetoa uongozi uliokuwa unatakiwa.
Karibu ya watu arobaini pamoja na wale wasomi wa
Makerere, miongoni mwao Job Lusinde walihudhuria mkutano ule. Lusinde alikuja
kuwa waziri, na Amon Nsekela, alikuja kushika nyadhifa muhimu katika serikali
na vilevile kuwa balozi wa Tanzania nchini Uingereza. Hassan Suleiman na Ali
Ponda hawakutokea mkutanoni. Wakati wanakusanyika kwa ajili ya mkutano, afisa
wa Community Centre aliwaambia kuwa alikuwa amepokea amri kutoka kwa DC kuwa
mkutano huo usifanyike. Kufuatia amri ile watu walitawanyika mara moja.
Alexander Kanyamara aliyekuwa Mwafrika
tajiri mjini Dodoma na rafiki wa John Rupia, wakati ule makamu wa rais wa TANU,
aliwataka kuahirisha mkutano huo kwa sababu ya kutokuwepo kwa viongozi wa juu
wa TAA, Hassan Suleiman na Ali Ponda.
Kutokana na sababu hii na vile vitisho vya DC, mkutano uliahirishwa bila
kupanga tarehe ya mkutano mwingine.
Asubuhi iliyofuata Taratibu alikamatwa na polisi
na kupelekwa kwenye ofisi ya DC, (hivi sasa ofisi hiyo ni ofisi ya Waziri
Mkuu). Taratibu alimkuta Hassan Suleiman pale ofisini akizungumza na DC, Bwana
Smith. DC alianza kumsaili Taratibu kwa kumuuliza kama alikuwa akijua
kuzungumza Kiingereza. Taratibu alijibu kuwa yeye hakusoma. Akizungumza
Kiingereza Hassan Suleiman alimwambia DC kuwa yeye ndiye katibu wa TANU mjini
Dodoma. DC, Bwana Smith, alimshutumu Taratibu kwa kuunda chama haramu na kwa
kuitisha mkutano usio na idhini ya serikali katika Community Centre jana yake
ambao ulielekea kuvuruga amani. Bila woga Taratibu alijibu kwamba yeye alikuwa
na mamlaka ya kuitisha mkutano kwa sababu alikuwa mwanachama wa chama cha siasa
kilichosajiliwa kihalali. Taratibu aliichomoa kadi yake ya TANU kutoka mfukoni
kwake yenye rangi nyeusi na kijani na kumwonyesha DC. Bwana Smith alimuuliza
Hassan Suleiman kama ikiwa na yeye pia alikuwa na kadi ya TANU. Hassan Suleiman
hakuwa nayo. Hassan Suleiman na DC walizungumza Kiingereza kwa muda baada ya
hapo aliwataka wote wawili kuandika maelezo yao. Baada ya kuandika maelezo yake
Taratibu aliruhusiwa kurudi nyumbani. Inasadikiwa kuwa wakati ule mwanachama
pekee wa TANU mjini Dodoma walikuwa Haruna Taratibu na Alexander Kanyamara
ambae yeye alikata kadi yake Dar es
Salaam.
Wasomi wa Makerere, ambao Mwangosi aliwaamini
sana katika kuunda TANU, walipopata habari kuhusu mkasa wa Taratibu na DC,
Bwana Smith, waliogopa. Waliamua kujiweka mbali kabisa na mambo ya siasa na kuendelea na kazi yao ya
kufundisha. Haruna Taratibu na Omari Suleiman sasa waliamua kugeuza mbinu, waliitisha
mkutano wa siri usiku nyumbani kwa Swedi bin Athumani.[1] Mkutano huu uliamua kuwa
Taratibu lazima aende makao makuu ya TANU Dar es Salaam akazungumze na Nyerere
ana kwa ana kuhusu matatizo yaliyokuwa yakiikabili TANU Dodoma. Mahdi Mwinchumu aliyekuwa mwanachama wa TANU
Dar es Salaam alijitolea kufuatana na Taratibu hadi makao makuu ya chama Dar es
Salaam kwa kuwa alikuwa akijuana na viongozi wa TANU. Said Mussa mjumbe
mwingine wa ile kamati ya siri alijitolea vilevile kufuatana na Taratibu na
Mwinchumu hadi Dar es Salaam. Siku ya kuondoka Job Lusinde alikwenda stesheni
ya gari moshi kuagana na ule ujumbe uliokuwa ukielekea Dar es Salaam, makao
makuu ya TANU. Lusinde aliuambia ule ujumbe kuwa jamaa wa Makerere wanaunga
mkono maamuzi yote yatakayoamuliwa na ile kamati ya siri.
Kwa bahati nzuri katika gari moshi lile lile
ambamo Taratibu na wenzake walikuwa wakisafiri kulikuwa na wajumbe wa TANU
kutoka Kigoma, Bukoba na Mwanza wakisafiri kwenda Dar es Salaam kuhudhuria
mkutano mkuu wa kwanza wa mwaka wa TANU. Wahudumu ndani ya gari moshi walipofahamu
kuwa walikuwa na wajumbe wa TANU kwenye gari moshi lile, waliwafanyia heshima
kubwa. Mmoja wa wahudumu wale alijitolea
kumpa malazi Salum Mussa nyumbani kwake Dar es Salaam. Mahdi Mwinchumu
aliwapeleka Haruna Taratibu na Said Mussa makao makuu ya TANU New Street ambako
walifanya mazungumzo na Nyerere pamoja na Rupia. Uongozi wa makao makuu
ulielezwa kwa ufupi matatizo yaliyokuwa yakikabili Dodoma katika kufungua tawi
la TANU. Papo hapo Nyerere alimwalika Taratibu kuhudhuria mkutano mkuu Hindu Mandal
Hall kama mjumbe wa Jimbo la Kati.
Mkutano ule ulimchagua Taratibu kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya
TANU. Taratibu na ujumbe wake walirudi
Dodoma washindi, walikwenda Dar es Salaam watu wasiojulikana na walirudi
nyumbani wakifuatana na mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa wa TANU, chombo cha juu
kabisa katika chama. Nyerere alimpa Taratibu dafari ya tasjili ya wanachama,
kadi mia moja hamsini za uanachama wa TANU na nakala hamsini za
Bill of Rights. Kazi ya kuwahamasisha na kuwaingiza watu TANU alipewa Omari
Suleiman, na fundi cherahani mwingine aliyejulikana kwa jina la Abdu Mohamed
Mkamba. Mara tu baba mwenye nyumba wake alipopata habari za kuwa mpangaji wake,
Haruna Taratibu alikuwa mwanachama wa TANU, alimfukuza kutoka kwenye nyumba
yake.
Baada ya kupata kikundi kidogo cha wanachama,
Taratibu alipiga simu makao makuu ya TANU na kuzungumza na kaimu katibu, Elias
Kissenge akaomba ruhusa ya kufanya uchaguzi. Kissenge hakuweza kutoa uamuzi
wowote wa maana kuhusu tatizo la uongozi wa TANU Dodoma. Taratibu alifanikiwa
kumpata Kambona ambae aliidhinisha uchaguzi ufanyike kwa shuruti moja la kuwa
Hassan Suleiman na Ali Ponda waruhusiwe kushiriki na kugombea uongozi wa chama.
Kusisitiza kwa Kambona juu ya uongozi wa zamani wa TAA kuongoza chama kipya
huenda kulishawishiwa na mafanikio ya zamani ya uongozi wa Hassan Suleiman mbae
alimfahamu huko Dodoma wakati Kambona alipokuwa mwalimu akifundisha Kikuyu Secondary School. Kwa bahati mbaya,
wanachama wa TANU waliokuwa wanainukia na chama pale mjini Dodoma waliwaona
Hassan Suleiman na Ali Ponda kama wasaliti kutokana na kutokushirikiana na
wenzao katika kuanzisha TANU.
Wakati ametatizwa na tatizo la uchaguzi wa TANU,
Taratibu alijulishwa na makao makuu kuwa makamo wa rais, John Rupia, atapita
Dodoma kwa gari moshi akiwa njiani kwenda Tabora kushughulikia mambo ya chama.
Gari moshi liliposimama Dodoma Rupia alishangazwa kuona kundi la wananchama wa
TANU wakimsubiri katika kituo cha gari moshi wakimtaka avunje safari waende
mjini kujadili na kutatua tatizo la uchaguzi. Rupia aliwaeleza wanachama wa
TANU wa Dodoma kuwa yeye hakuwa na
idhini kutoka makao makuu kufanya shughuli yoyote ya chama mjini Dodoma.
Wanachama wa TANU hawakutaka kusikia lolote na walimwambia Rupia kuwa wamechoshwa
na makao makuu kwa kushindwa kwake kutoa uamuzi wa tatizo la uchaguzi. Mizigo
ya Rupia ilishushwa chini kutoka kwenye gari moshi na Rupia akawa hana khiyari
isipokuwa kuwafuata wale wanachama wa TANU hadi mjini.
Ghafla mji mzima ukavuma tetesi kuwa makamu wa
rais wa TANU, John Rupia, yupo mjini kufungua tawi la TANU. Rupia alimwita
Hassan Suleimna na akamtaka alete hati ya tasjili ya TANU Hindu Mandal siku
inayofuata, mahali ambako mkutano utafanyika. Hassan Suleiman hakutokea
mkutanoni lakini alimtuma mtu apeleke ile hati. Ali Ponda alihudhuria mkutano
ule. Rupia alikuwa mwenyekiti wa mkutano na TANU ikafanya uchaguzi wake wa
kwanza. Alexander Kanyamara alichaguliwa
Rais; Haruna Taratibu Makamu wa Rais, Abdu Mohamed Mwamba, Katibu na Omari
Suleiman Mweka Hazina. Miongoni mwa wanachama waasisi alikuwa mwanamke mmoja wa
Kimanyema, Binti Maftah Karenga; wengine walikuwa Bakari Yenga, Maalim Khalfan,
mwanachuoni wa Kiislamu aliyekuwa akiheshimiwa sana, Idd Waziri na Said
Suleiman. Wale wasomi wa Makerere hata mmoja hakujitokeza kwenye mkutano huu wa
kuasisi TANU. Ali Ponda, mwanasiasa mkongwe alipuuzwa na hakuchaguliwa kushika
wadhifa wowote. Walipoona hawakupewa wadhifa wowote katika TANU, Ali Ponda na
Hassan Suleiman walijiunga na UTP kuipinga TANU.
Baada ya uchaguzi huo, wale mafundi cherahani
wawili, Abdu Mohamed Mkamba na Omari Suleiman, walianza kuhamasisha wananchi
wazi wazi kujiunga na TANU ili wapiganie uhuru wa Tanganyika. Tawi la TANU la
Dodoma baada ya kujizatiti pale mjini, lilituma wanaharakati kuwahamasisha watu
wa Kondoa ili wafungue tawi la TANU katika wilaya hiyo. Abdallah Jumbe
alizipenyeza kadi za TANU na kuzipeleka kwenye wilaya hiyo kwa siri akaanza
kuandikisha watu. D.C. wa Singida alikuwa jeuri sana kiasi kwamba ni baada ya
Mkutano Mkuu wa Tabora wa mwaka 1958 ndipo Abdallah Jumbe aliweza kufanikiwa
kufungua tawi mjini Singida. Wakati huo TANU ilikuwa na nguvu sana ikiwa na
wajumbe wake katka Baraza la Kutunga Sheria. Kwa ajili hii hakuna Mzungu
aliyethubutu kuwa fedhuli kwa TANU na kuwabughudhi wanachama wake.
Mzee Omar Suleiman na Rais Kikwete
|
No comments:
Post a Comment