Thursday, 22 January 2015

ALHAJ ABDALLAH TAMBAZA AZUNGUMZIA HISTORIA YA BABU ZAKE


Alhaj Abdallah Tambaza

Kushoto Kwenda Kulia: Jumbe Mohamed Tambaza, Mshume Kiyate
Dossa "The Bank" Aziz
Gazeti la Raia Mwema la tarehe 21 Januari 2015

''Mzee Saleh Abdallah Tambaza, ni babu ya mwandishi huyu, ambaye pamoja na kaka yake Mzee Kidato Tambaza, walikuwa wanamiliki ardhi kubwa sana  Upanga, jijini Dar es Salaam wakati wa ukoloni na kabla ya hapo. Eneo hilo lilianzia Selander Bridge, mahala walipokuwa wakivua samaki, Palm Beach, Sea View na kuzunguka mpaka maeneo ya Mahakama ya Kisutu, maeneo ya Diamond Jubilee, makao makuu ya Jeshi na Hospitali ya Tumaini. Miembe mikubwa ya miaka mingi, minazi, mikungu na mizambarau ambayo ipo bado hadi sasa ni kielelezo tosha (classic example) ya dhulma ya wazungu. Wakoloni waliwataka babu zangu wahame hapo kwa sababu tu hapafai kukaa mtu mweusi tuwaachie Wahindi upepo wa bahari. Wazungu nao peke yao wakawa wanaburudika kule Oysterbay (sasa Masaki).''


''Mzee Mwinjuma Mwinyikambi na Jumbe Tambaza hawa ni babu zangu katika ukoo wetu. Jumbe Tambaza anakuwa binamu ya babu yangu mzaa baba. Kwa hiyo nawafahamu vizuri sana wazee hawa wa Kimashomvi. TANU likuwa ni wao na wao ni TANU. Hawa wazee wawili walikuwa na nafasi za kudumu (permanent seats) katika Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya TANU siku hizo; siyo kwa kupigiwa kura na mtu, bali kwa heshima na nyadhifa zao tu.'' - Alhaj Abdallah Tambaza

''Katika siku za mwanzo za harakati za kudai uhuru, chama cha TAA na baadaye TANU hakikuwa na fedha za kujiendesha kufanikisha shughuli zake kubwa na ndogo za kila siku. Katika kufanya hayo, chama kiliwategemea watu wachache ambao walikuwa na uwezo wa kifedha kwa wakati huo. Miongoni mwa watu hao ni Mzee John Rupia, Dossa Aziz, Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate, Mwinjuma Mwinyikambi, Haidar Mwinyimvua pamoja na familia ya kina Sykes. Hawa wote kwa wakati huo walikuwa ni Waafrika wazalendo wenye kumiliki mali kama mashamba, majumba na biashara mbalimbali. ''


''Mzee Haidar Mwinyimvua alikuwa akiishi Wadigo Street Kisutu, jijini Dar es Salaam, jirani na mahala alipozaliwa mwandishi huyu. Mzee Haidar alikuwa fundi cherehani lakini pia alimiliki majumba (landlord) yaliyotapakaa jijini Dar es Salaam wakati huo. Alikuwa pia Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU kwenye miaka ya 50. Habari zinasema alipata kuuza nyumba yake na fedha kuzipeleka katika harakati za ukombozi wa taifa hili kutoka minyororo ya ukoloni. Mzee Haidar, alikuwa na watoto wasiopungua 12 hivi waliohitaji kula, kulala na kusoma; lakini kwa mapenzi ya nchi hii na kuuchukia ukoloni, aliona bora awalaze njaa wanawe lakini nchi yetu iwe huru.''

''Mmoja wa Waafrika waliokuwa na pesa nyingi kabla ya uhuru ni Mzee John Rupia. Huyu alimiliki mashamba jijini Dar es Salaam pamoja na nyumba kadhaa, ikiwamo ya ghorofa (Rupia Building) pale mtaa wa Kitchwele (sasa Uhuru street). Huyu alikuwamo tokea TAA na wakati TANU ilipoanzishwa alikuwa Makamu wa Rais. John Rupia alitoa fedha zake nyingi sana kwa chama kama vile kilikuwa cha kwake binafsi na Julius Nyerere ni mfanyakazi tu.'' 

''Mshume Kiyate, yeye pamoja na mambo mengine, alichukua jukumu la kumlisha Nyerere kila siku akipeleka kapu kubwa lililosheni kila aina ya chakula nyumbani kwa Mwalimu pale Magomeni, ili kazi ya kutafuta riziki isimwondoe Nyerere kwenye kufikiria kazi za chama. Aliifanya kazi hiyo kwa muda wote wa kudai uhuru na mpaka mwaka 1961 ulipopatikana, alitaka kuendelea kumpelekea Nyerere chakula pale Ikulu, lakini Nyerere akamwambia ‘Mzee Mshume sasa basi tena pumzika’. ''



''Dossa Aziz, ni mtu mwingine aliyekuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere wakati huo. Dossa ni mtoto mkubwa wa Mzee Aziz Ali wa Mtoni Dar es Salaam. Wengine  mashuhuri ni Hamza na Ramadhani Aziz. Aziz Ali, alikuwa Mwafrika tajiri wakati wa ukoloni akimiliki magari na majumba mjini. Mwanawe, Dossa Aziz hakuwa tu mfadhili mkubwa wa TANU, lakini pia ndiye aliyetoa gari yake binafsi iwe gari ya mwanzo kabisa kwa matumizi ya chama na Nyerere wakati huo. Ilikuwa gari ya Dossa Aziz aliyopanda Nyerere siku aliporudi kutoka safari yake ya kihistoria ya Umoja wa Mataifa alikotoa hotuba ya kusisimua, kuhusu mustakabali wa watu wa Tanganyika na kujitawala wenyewe, hotuba ambayo— habari zinasema— ilikuwa imeandikwa mapema mwaka 1950 na Abdulwahid Sykes akishirikiana na Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Hamza Kibwana Mwapachu, Dr. Vedasto Kyaruzi, Stephen Mhando, Said Chaurembo  wazalendo waliokuwa katika TAA Political Subcommittee.''



Abdulwahid Kleist Sykes (1924 - 1968)

"Mwaka 1954 wakati TANU ilipoasisiwa, Ally Sykes ndiye aliyebuni na kugharimia ununuzi wa kadi za chama kipya yeye mwenyewe akiwa na kadi namba 2. Kakake Abdulwahid namba 3, Dossa namba 4 na kadi namba 1 ikiwa ya Nyerere. Vipi taifa makini linaweza kuwafanyia hiyana watu wa namna hiyo? Watu waliohatarisha uhai wao ili leo ili sisi tuwe huru; haiingi akilini kwamba nchi inaweza kuwasahau kiasi hiki. Mimi bado nakumbuka, pale mchana ule wa Jumamosi, Oktoba 12, 1968 mji wa Mzizima ulipozizima baada ya habari kuzagaa kwamba Abdul Sykes ameaga dunia. Alikuwa mtu mashuhuri sana jijini Dar es Salaam, si tu kwamba alikuwa mwanasiasa lakini kipenzi na rafiki wa watu wengi akiwemo baba wa mwandishi huyu. Alizikwa na maelfu ya watu Jumapili Oktoba 13, katika makaburi ya Kisutu katika mazishi ambayo yalihudhuriwa pia na Mwalimu Nyerere na waasisi wengine wa taifa hili."

(Makala hii imenyambuliwa kutoka makala ya Alhaj Abdallah Tambaza Iliyochapwa katika Raia Mwema la tarehe 21 Januari 2015)

No comments: