Wednesday, 21 January 2015

MAHAKAMA YA KADHI: MAONI YA TAASISI ZA KIISLAM KWA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA UTAWALA


MAONI YA WAISLAM KUHUSU MUSWADA WA WRITTEN LAWS
(MISCELLANEOUS AMENDMENT)(NO. 2) ACT, 2014
…………………………………………………………
UTANGULIZI:
Kama taasisi ya Kiislam tumepitia muswada wa Written Laws (Miscellaneous Amendment)(No. 2) Act wa 2014 na malengo ya kuletwa kwake. Hapana shaka kwamba kwa kuwa sisi ni sehemu ya watanzania, na yote yaliyomo katika muswada huo yanatuhusu. Hata hivyo, kama asasi ya kidini, hususan ya Kiislam, tunaona kuwa tunahusika zaidi na Sehemu ya V ya muswada huo ambayo inahusu mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Islamic Law (Restatement Act), Sura ya 375 ya Mapitio ya 2002. Hivyo basi, tutatolea maoni eneo hilo la muswada huu.

SEHEMU YA KWANZA - MAELEZO YA JUMLA:
La kwanza tunapata faraja kuona kuwa hatimaye imefika wakati Serikali imetambua ukweli kuwa upo ulazima wa kupitishwa kwa sheria ya Mahakama za Kadhi hapa nchini. Hii ni hatua ndogo lakini muhimu katika safari ya kuelekea kujibu kiu ya Waislamu ya muda mrefu kutaka kuhukumiwa kwa mujibu wa Sheria inayoafikiana na mtazamo na imani yao katika masuala yanayohusu familia na hadhi binafsi kwa mujibu wa imani, mila na desturi zetu kama Waislamu.
Haja na kiu hii inatokana na mambo matatu makubwa: -

- Mosi, kuwa Uislam una mfumo wake kamili wa utoaji haki wenye sheria, misingi na taratibu zake. Kuchukua sheria peke yake na kuacha misingi na taratibu zake kumepelekea sheria za Kiislamu kutumika visivyo na hivyo kupelekea kupotosha haki, 

- Pili, Mfumo wa sasa unatoa nafasi kwa maafisa wa mahakama kama majaji na mahakimu kuhukumu masuala ya sheria ya Kiislamu ambapo mara nyingi maafisa hao hawana sifa, ujuzi na uzoefu wa kushika nafasi ya kuhukumu chini ya utaratibu wa Kiislamu. Moja ya kigezo muhimu ni majaji na mahakimu kuruhusiwa kuhukumu masuala ya sheria ya Kiislamu bila kuwa mejifunza sheria ya Kiislamu na nidhamu ya uhakimu, na

- Tatu, licha ya maafisa wa mahakama zetu kuwa hawajafunzwa sheria, misingi na taratibu za sheria za Kiislamu, lakini pia, wengi wao wamethibitika kutoridhika na kufuata ipasavyo Sheria za Kiislamu katika kusikiliza na kuamua mashauri ya Sheria ya Kislamu mpaka wengine hata kufikia kupotosha kwa makusudi kanuni na misingi ya sheria za Kiislamu. Ipo mifano mingi inayothibitisha hili.

- Kutokana na hali hiyo Waislamu wamekuwa wakidai kurudishwa kwa mfumo wa utoaji haki wa Kiislamu katika masuala ya familia na hadhi binafsi kama vile ndoa, talaka, matunzo ya mke, matunzo ya watoto, uzazi wa watoto, ulezi na usimamizi wa watoto, wosia, mirathi na wakfu. Serikali imekuwa ikikwepa suala hili kwa sababu mbalimbali zisizo waridhisha Waislamu.

Kwa hiyo ni faraja kuwa leo Serikali walau imefikia kutoa muswada huu unaohusu makahama za kadhi hapa nchini. Hata hivyo, ingawa tunafarijika kuona kuwa hatimaye Serikali inakiri umuhimu wa kuwepo kwa Mahakama ya kadhi inayotambuliwa na sheria za nchi, muswada huu una makosa, kasoro na udhaifu mwingi kiasi cha kutia shaka juu ya uthabiti wa nia ya Serikali wa kutaka kuleta sheria itakayowezesha mfumo wa utoaji haki wa Kiislamu kufanya kazi hapa nchini. Mfumo huu hautaweza kufanya kazi kwa ufanisi. Pia uhalali wa maamuzi yake utakuwa na shaka kubwa. Vilevile, utaleta migogoro, migongano na matatizo mengi baina ya makundi na asasi za Kiislamu.
Tutataja hapa chini makosa, kasoro na upungufu huo katika Sehemu ya Pili hapa chini. Badala yake, tunapendekeza kuwa marekebisho muhimu yafanywe katika muswada ili kuwezesha kupatikana kwa sheria ya mfumo wa utoaji haki wa Kiislamu unaoafikiana na mtizamo wa Waislamu na unaokidhi mahitajio ya kimuundo, kitaratibu na kiutendaji.

SEHEMU YA PILI: MAKOSA, KASORO NA UPUNGUFU WA MUSWADA:
1. MUSWADA HAUNA KIFUNGU CHA UANZISHAJI WA MAHAKAMA YA
KADHI:

1.1 HOJA:
Sheria yoyote inayotaka kuweka utaratibu wa kufanya kazi kwa mahakama Fulani, ni lazima iwe na kifungu kinachotamka kuwepo kwa mahakama hiyo. Vinginevyo, kama kusudio ni kutambua mahakama iliyopo, basi hakuna budi kiwepo kifungu kinachotoa tamko la kutambua kuwepo huko kwa mahakama hiyo. Muswada unaopendekezwa hauna tamko la kuanzisha au kuweka Mahakama ya kadhi wala tamko la kutambua kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi. Lakini, haitokuwa sawa kutoa tamko la kutambua kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi hapa nchini ilhali hakuna mahakama hiyo ambayo tayari imeanzishwa kwa utaratibu unaotambuliwa na sheria.

Ingewezekana tu kutambua kuwepo kwa mahakama ya kadhi kama Waislamu wa Tanzania kupitia jumuiya na taasisi zao zote za kitaifa wangekubaliana na kuanzisha mahakama hiyo. Makubaliano hayo hayapo. Ikiwa Serikali itambua kuwepo kwa mahakama ya kadhi iliyoanzishwa na BAKWATA kwa sasa, itakuwa ni sawa na kuitambua BAKWATA kuwa ndicho chombo halali cha kuwawekea Waislamu mahakama ya kadhi jambo ambalo linapingwa na sehemu kubwa ya Waislamu na taasisi nyingi za Waislamu. Kuipa BAKWATA nafasi ya kuwawekea Waislamu Mahakama ya Kadhi kutahesabiwa na waislamu kuwa ni hila ya Serikali kutaka kulazimisha mamlaka ya BAKWATA juu ya Waislamu hata wale wasioikubali taasisi hiyo. Jambo ambalo litakuwa limekiuka haki ya msingi ya kila Mtanzania kujumuika kwa  uhuru bila kutenzwa nguvu au kushinikizwa.Uhalali wa BAKWATA kuwa ndicho chombo kikuu cha uongozi wa waislamu nchini umehojiwa na Waislamu mara nyingi. Na hata BAKWATA yenyewe imetoa matamko mara kadhaa kuwa si chombo cha Waislamu wote. Ni ukweli uliowazi kuwa makadhi waliotangazwa na BAKWATA si makadhi halali kwa kuwa:-

- Wametangazwa kinyume na matakwa ya Waislamu walio wengi, - BAKWATA imetangaza makadhi wake kwa kukiuka utaratibu uliokuwa umekubaliwa na makundi mengi ya Waislamu wa majadiliano baina ya Serikali na Waislamu kwa kujitangazia makadhi peke yake na kusababisha kuvunjika kwa mchakato huo, - Serikali imearifiwa na wajumbe wa Jopo la Masheikh lililokuwa likijadiliana na Serikali wasiokuwa wajumbe kutoka BAKWATA kuwa BAKWATA imekiuka utaratibu na hivyo kutaka mchakato wa majadiliano uendelee lakini Serikali imepuuza.
Kwa maana hiyo basi, njia pekee ya kuweka chombo muhimu kama Mahakama ya Kadhi itakuwa ni kwa kupata ridhaa ya taasisi zote kubwa za Kiislamu nchini kwa maafikiano yao ya pamoja kama itakavyopendekezwa hapa chini. Hivyo basi, muswada huu una upungufu mkubwa kwa kukosa tamko la kuweka au kuanzisha au kutambua kuwepo kwa mahakama ya kadhi kwanza kabla ya kuanza kuipangia taratibu za utendaji. Kosa hili litapelekea mwenendo, maamuzi, hukumu na amri za mahakama hiyo kuwa batili kwa kuwa kimsingi yatakuwa yamefanywa na chombo kisichotambulika kisheria.

Iwapo atajitokeza mtu yeyote kupeleka malalamiko katika Mahakama Kuu ya Tanzania kutaka mapitio ya mwenendo, maamuzi, hukumu na amri za Mahakama ya Kadhi, Mahakama Kuu itabatilisha mwenendo, maamuzi, hukumu na amri hizo kwa kutolewa na chombo kisichotambuliwa na sheria.

Kutokana na hayo, muswada huu haukidhi haja na matakwa ya kisheria na kitaratibu ya kuwepo kwa mahakama ya kadhi kama chombo cha kimahakama hapa nchini. 

1.2 MAPENDEKEZO YETU:
i) Tunapendekeza kuwa kwa kuwa mahakama ya kadhi haipo kisheria, sheria iwe na tamko la kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi hapa nchini.

2. MUSWADA HAUWEKI MUUNDO WA MAHAKAMA INAYOKUSUDIWA:
2.1 HOJA:
Mahakama ni lazima iwe na muundo. Ijulikane mahakama hiyo ina ngazi zipi, ngazi yake ya chini ni ipi, kama kuna ngazi ya kati, na ngazi yake ya mwisho juu.

Inapasa pia ijulikane mashauri gani yanaanzia katika ngazi ya mwanzo chini na yapi mengine katika ngazi nyingine za juu. Pia muundo wake wa kijiografia unapasa ujulikane. Haya ni masuala muhimu sana kwa kuwepo kwa mahakama madhubuti inayoweza kukidhi haja za mfumo thabiti wa utoaji wa haki. Kinyume cha hivyo, mahakama hiyo itakuwa ni dhihaka katika utoaji haki na itapelekea migogogoro na migongano katika utendaji wake.

2.2 MAPENDEKEZO YETU:
Sheria iweke muundo wa mahakama inayokusudiwa. Kwa kuwa muundo wa mahakama ni jambo nyeti linaloamua pia masuala ya mamlaka (jurisdiction), ni lazima uwekwe na sheria mama, sio na kanuni zitakazowekwa chini ya sheria hiyo. Tuna pendekeza sheria iweke mfumo wa mahakama ya Kdhi yenye ngazi tatu kama ifuatavyo:

- Mahakama ya Kadhi ya Eneo (local Kadhi’s Court) itakayokuwa katika kila Kata
- Mahakama ya Kadhi ya Wilaya (District Kadhi’s Court) itakayokuwa katika kila Wilaya 
- Na Mahakama ya Kadhi Mkuu(Chief Kadhi’s Court) itakayokuwa ndiyo
mahakama ya juu kabisa. Hii itakuwa na Kadhi Mkuu (Chief Kadhi) na
makadhi waandamizi (Principal Kadhis) wane.

3. MUSWADA KUTOELEZA SIFA ZA KADHI:
3.1 HOJA:
Muswada huu umeacha mwanya kwa wasio kuwa na sifa kuteuliwa kuhudumu katika Mahakama za Kadhi. Haiyumkini watu muhimu wenye mamlaka ya kutoa haki wakateuliwa bila ya sheria kutaja sifa stahiki za wanaofaa kuchukua jukumu hilo na utaratibu wa kuwapata watu hao. Hili lazima lielezwe na sheria yenyewe inayounda Mahakama ya Kadhi au kanuni zitakazoundwa chini ya sheria hiyo na chombo chenye kuaminika na wananchi wote watakao tumia huduma ya Mahakama hiyo.

3.2 MAPENDEKEZO YETU:
Muswada utaje sifa za makadhi wa daraja mbalimbali na vigezo vya kuhudumu katika mahakama za kadhi za ngazi mbalimbali.

4. MASUALA YA UTEUZI WA MAKADHI:
4.1 HOJA:
Muswada unaeleza kuwa makadhi watateuliwa na “Mufti”. Hili lina kasoro nyingi zitakazoleta matatizo mengi. Baadhi ya kasoro ni hizi:

4.1.1 Mufti
i) Kwanza muswada unataja afisa aitwaye Mufti lakini hauelezi huyo Mufti ni nani na anapatikana vipi. Ni vyema Serikali ikatahadharishwa kuwa zipo taasisi nyingi za Kiislamu zilizoandikishwa na mamlaka mbalimbali za uandikishaji wa asasi huru na vyama vya kijamii (NGOs) zenye maafisa wenye cheo cha Mufti. 

Baadhi ya asasi hizo ni –

(a) Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania (BARAZA KUU),
(b)Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay-at), na
(c) Barza Kuu la Waislam wa Tanzania (BAKWATA).

Kwa hivyo kama sheria haikuweka wazi Mufti ni afisa gani na anapatikana vipi kunaweza kutokea mgongano na mgogoro mkubwa kwa kila asasi kutaka kutumia Mufti wake kuteua makadhi.

ii) Pili, si busara kuweka suala zito kama la uteuzi wa maafisa wa mahakama watakaokuwa na wajibu na dhima ya kutoa haki mikononi mwa mtu mmoja ambaye hata namna anavyopatikana haijulikani. Pia, huyu hachaguliwi na ummah wa Waislamu wote kama vile anavyochaguliwa Rais wa Jamhuri na wananchi wote wa Tanzania. Licha ya kuchaguliwa kwake na wananchi wote, bado
mapendekezo mengi yametolewa kuwa Rais apunguziwe madaraka ya uteuzi ukiwemo uteuzi wa majaji. Kwa hivyo hili ni jambo lisilokubalika. Utaona kuwa katika maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa na taasisi mbalimbali za Kiislamu juu ya mfumo wa uteuzi wa makadhi, zote zimependekeza kuwepo na baraza, jopo, bodi au chombo cha namna moja au nyingine kitakachokuwa ndiyo mamlaka ya kuteua makadhi. Hakuna hata taasisi moja iliyopendekeza kuwa uteuzi ufanywe na mtu mmoja, kwa cheo, hadhi au daraja yoyote aliyonayo. Kwa hiyo suala la uteuzi kuweka mikononi mwa mtu mmoja halikubaliki kwa sababu linatoa mwanya wa nafasi hiyo kutumika vibaya.

iii) Tatu, kuweka mamlaka ya uteuzi wa makadhi kwa afisa aitwaye Mufti hakukubaliani na utaratibu wa mfumo wa uongozi wa Kiislam. Kilugha, istilahi “mufti” maana yake ni alim mwenye upeo mkubwa wa elimu ya dini na sheria. Ni mtu aliyebobea katika taaluma za dini na sheria. Si afisa wa serikali wala hana dhima ya utawala au uongozi. Alim hutambuliwa kuwa Mufti na maulamaa wenzake wa eneo husika kwa kutambua upeo wake mkubwa katika fani za elimu ya dini na sheria. Alim akitambuliwa na kupewa hadhi ya mufti huchukuliwa kuwa ni marejeo kwa ajili ya kutolea ufafanuzi masuala ya elimu ya dini na sheria. Kwa hiyo mufti jukumu lake ni kufutu mas’ala ya dini na sheria. Si kuwa mtawala au mpangaji wa masuala ya utawala. Kwa upande wa pili, Kadhi ni cheo cha kimahakama na kiserikali. Ni afisa wa serikali au umma mwenye mamlaka. Katika taratibu za kiutawala za Kiislamu, kadhi ni cheo na hadhi kubwa kuliko mufti. Kwa maana hiyo si jambo linalokubalika, kwa mujibu wa mfumo wa utawala na uongozi wa Kiislam kupindua mizani na kuweka mufti juu ya kadhi. Kwa hivyo, Kiislamu, haifai makadhi kuteuliwa na Mufti.

4.2 MAPENDEKEZO YETU:
Sheria iunde Baraza la Sheria za Kiislam litakalokuwa na mamlaka ya kuteua makadhi na kusimamia nidhamu na maadili yao. Iwapo itaonekana kuwa ni lazima sheria iweke mamlaka ya kuteua makadhi juu ya afisa mmoja mkuu atakayetajwa na sheria, basi sheria ifanye kuwa ni lazima afanye hivyo kutokana na orodha itakayopendekezwa kwake na baraza au mamlaka itakayoundwa rasmi kwa ajili hii.

5. MUSWADA HAUELEZI KUHUSU AJIRA NA USALAMA WA AJIRA YA
MAKADHI:

5.1 HOJA:
Muswada hautaji popote iwapo kama hao makadhi watakuwa ni maafisa wa kuajiriwa au wa kujitolea. Na iwapo wanaajiriwa, basi wanaajiriwa na chombo gani. Ni jambo la lazima makadhi wawe wa kuajiriwa. Kufanya makadhi wawe wa kujitolea kutasababisha mfumo mzima kuingia dosari zinazotokana na shida na haja za kibinadamu za watu watakaokuwa wakihudumu kama makadhi. Muswada pia hauelezi ni nani mwenye mamlaka ya kumuondoa kadhi na utaratibu na vigezo au sababu za kumuondoa kadhi. Hili liaacha mwanya kwa makadhi kuingiliwa katika utendaji wao.

5.2 MAPENDEKEZO YETU:
Sheria iweke Bodi ya Ajira ya Makadhi ambyo ndiyo itakuwa mwajiri wa makadhi na ndiyo itakayowapa mafao yao ya ajira. Sheria pia ieleze wazi mamlaka ya nidhamu na udhibiti wa mwenendo na maadili ya makadhi kama inavyopendekezwa katika ibara ya 8 hapa chini.

6. MUSWADA UNAWEKA MAMLAKA YA KUWEKA KANUNI ZA MAHAKAMA KWA MUFTI:
6.1 Kasoro za kutegemeza mamlaka yahusuyo masuala ya Mahakama ya Kadhi kwa Mufti tumeshazitaja katika ibara ya 4 hapo juu. Kwanza kuwa Mufti mwenyewe hatajwi na sheria yoyote. Pili kuwa mamlaka muhimu kama hayo isingekuwa vyema kuyaweka mikononi mwa mtu mmoja. Hivyo basi, ni kasoro na kosa kubwa kuweka mamlaka ya kuweka kanuni za mahakama mikononi mwa Mufti.

6.2 MAPENDEKEZO YETU:
Sheria iunde Baraza la Sheria za Kiislam litakalokuwa na mamlaka ya kanuni za mahakama. Inapendekezwa kuwa Baraza la Sheria za Kiislam lililopendekezwa katika ibara ya 4.2 hapo juu ndilo liwe Baraza la Sheria za Kiislam ya kuweka kanuni za mahakama za Mahakama ya Kadhi. Iwapo itaonekana kuwa ni lazima sheria iweke mamlaka ya kutunga kanuni juu ya afisa mmoja mkuu atakayetajwa na sheria, basi sheria ifanye kuwa ni lazima afanye hivyo kutokana na orodha itakayopendekezwa kwake na baraza au mamlaka itakayoundwa rasmi kwa ajili hii. Tunapendekeza kuwa Baraza la Sheria za Kiislam la uteuzi ndilo liwe pia Baraza la Sheria za Kiislam la utungaji wa kanuni kama itakavyopendekezwa hapa chini.

7. MUSWADA UNAWEKA MAMLAKA YA KUWEKA KANUNI ZA KUKAZIA HUKUMU KWA WAZIRI:
7.1 HOJA:
Muswada unaweka mamlaka ya kuweka kanuni za kukazia amri, maamuzi na hukumu za makadhi kwa Waziri wa Sheria. Kasoro iliyopo ni kuwa muswada haumlazimishi waziri kushauriana na chombo au mamlaka yoyote ya Waislamu kabla ya kuweka kanuni hizo.Hili linaweza likapelekea migogoro na migongano kati ya Waislamu na Serikali. Kwanza kwa kuwa hili litahusu utekelezaji wa amri, maamuzi na hukumu za makadhi, litahusu pia kanuni na taratibu za Kiislam. Kwa hiyo kuna umuhimu mkubwa kuwahusisha wataalam na viongozi wa ummah wa Kiislam katika maandalizi ya kanuni za mahakama.

7.2 MAPENDEKEZO YETU:
Tunapendekeza kuwa sheria ieleze kuwa Waziri atashauriana na mamalaka au baraza linalotajwa katika ibara ya 4 hapa juu katika kuandaa kanuni za mahakama.

8. UDHIBITI WA NIDHAMU, MWENENDO NA MAADILI YA MAKADHI:
8.1 HOJA:
Muswada hauweki maelezo yanayohusu udhibiti wa mwenendo, nidhamu na maadili ya makadhi.
Ukisoma muswada, utaona kuwa waziri amepewa mamlaka ya kuweka kanuni za ukaziaji wa hukumu, maamuzi na amri za mahakama ya kadhi. Utaona pia kuwa Mufti amepewa mamlaka ya kuweka kanuni za mahakama (rules of court). Hakuna maelezo yanahusu kanuni za nidhamu, mwenendo na maadili ya makadhi.  Hii ni kasoro kubwa sana inayoweza kusababisha madhara makubwa sana katika utendaji wa mahakama hiyo.

8.2 MAPENDEKEZO YETU:
Tunapendekeza kuwa mamalaka au baraza linalopendekezwa katika ibara ya 4 hapo juu liwe ndicho chombo cha udhibiti wa nidhamu, mwenendo na maadili ya makadhi. Baraza la Sheria za Kiislam hilo pia liwe na mamlaka ya kuweka kanuni za nidhamu, mwenendo na maadili ya makadhi.

9. WIGO WA MAMLAKA WA MAHAKAMA YA KADHI:
9.1 HOJA:
Wigo wa mamlaka ya mahakama ya kadhi ni finyu sana. Kwa mujibu wa kifungu cha 3 cha Sheria mama kama kitakavyorekebishwa, mamlaka ya mahakama ya kadhi yataishia katika kusikiiza mashauri yanayohusu sheria ya Kiislamu katika maeneo yale tu yaliyomo katika matamko ya Waziri ya Sheria ya Kiislamu yanayoweza kutolewa chini ya kifungu cha 2 cha sheria hiyo.

“4.-(1) The statements of Islamic law published in the Gazette in terms of sections 2 and 3 shall be applied and given effect to by Kadhis Courts at any place within the geographical jurisdiction of such courts in any cases and matters to be determined relating to personal status, marriage divorce or inheritance”.

Hili liko wazi hata katika kauli ya madhumuni ya muswada: “In addition, it is proposed to amend section 4 so as to allow statements issued under sections 2 and 3 to be applicable and given effect by Khadhi Courts within geographical jurisdiction of the court on matters relating to personal status, inheritance, marriage, divorce and probate”.  Hii ni kasoro na upungufu mkubwa sana. Hasa ikizingatiwa kuwa waziri halazimishwi kutoa matamko katika maeneo yote ya sheria ya Kiislamu yanayohusu masuala ya familia na hadhi binafsi.

Utaona kuwa toka ilipopitishwa sheria ya Islamic Law (Re-Statement) Act mwaka 1964 kuna tangazo moja la matamko ya waziri ya Sheria ya Kiislamu nalo ni Tangazo la Serikali Na. 222 la 1967 linalohusu sheria ya ndoa ya Kiislamu. Na tangazo hilo nalo mpaka leo halijaanza kutumika kwa sababu Waziri wa Sheria hajatoa tangazo katika gazeti la Serikali la tarehe ya kuanza kutumika kwake. Hii inaonyesha kutokuwepo kwa nia thabiti upande wa Serikali wa kuwezesha mfumo wa Sheria za Kislam kufanya kazi ipasavyo hapa nchini.Hivyo, mahakama ya kadhi ikipitishwa leo, makadhi hawatakuwa na kazi ya kufanya mpaka Waziri wa Sheria atakapoamua kwa hiyari yake kutoa matamko ya sheria ya Kiislamu na kuyaanzisha kutumika. kwa hali hii, mahakama zilizopo sasa zina wigo mpana zaidi wa mamlaka kuliko mahakama ya kadhi kwa sababu mahakama za kawaida hazifungwi na matamko ya Waziri pekee. Na kwa sasa, mahakama ya kadhi haitakuwa na mamlaka kabisa.

9.2 MAPENDEKEZO YETU:
Mmlaka ya kawaida:
Wigo wa mamlaka ya mahakama ya kadhi upanuliwe. Mahakama ya kadhi iwe na mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri yanayohusu sheria ya Kiislamu katika maeneo yote ambayo mahakama za kawaida zina mamlaka bila kutegemea kuwepo kwa matamko ya waziri wa Sheria.

Mamlaka ya ziada:
Pia mahakama ya kadhi iwe na mamlaka ya kusikiliza na kuamua, kwa mamlaka ya hiyari, mashauri yoyote ya madai ikiwa ni pamoja na mashauri yanayohusu mikataba ya Kiislamu na masuala ya fedha ya Kiislamu pale pande zote husika zinapo hiyari kwa maandishi kuwa mashauri yao yasikilizwe na kuamuliwa na mahakama ya kadhi. Sheria iyape maamuzi ya Kadhi katika masuala ya hiayari kama inavyopendekzwa hapa uzito sawa na hukumu, maamuzi na amri zake
nyingine. 

10. MAMLAKA YA PEKEE:
10.1 HOJA:
Muswada unatoa hiyari kwa mdaawa Muislamu kufungua shauri lake la sheria ya Kislamu katika mahakama ya kadhi au mahakama nyingine. Hili lina hatari ya kuleta matatizo mengi. Likiachwa hivyo kunaweza kukatokea mgongano baina ya mahakama ya kadhi na mahakama za kawaida ikiwa kila upande katika mgogoro utaamua kufungua shauri katika mahakama tofauti.

10.2 MAPENDEKEZO YETU:
Sheria inapasa kuipa Mahakama ya Kadhi mamlaka ya kipekee (exclusive jurisdiction) kushughulikia migogoro inayohusu sheria za Kiislamu. Mahakama ya kadhi iwe na mamlaka ya kipekee pale sheria ya Kiislamu inapotumika.

11. UGHARIMIAJI WA MAHAKAMA YA KADHI:
11.1 HOJA:
Hoja ya kwanza ni kuwa mahakama haiwezi kujiendesha yenyewe. MUSWADA huu unaitaka mahakama ya kadhi ijiendeshe yenyewe badala ya kuendeshwa na serikali, jambo ambalo hatuna kumbukumbu ya kutokea kwake sehemu yeyote duniani kuwa chombo kama mahakama kujiendesha chenyewe. Mahakama si mradi wa kibiashara. Haiwezi kujiendesha yenyewe kwa sababu ima itabidi ifanye ada zake ziwe juu sana ili iweze kupata pesa ya kutosha kujigharimia, au itabidi iwe na miradi ya biashara, au iwe na taratibu za kutafuta pesa (fund raising). Haya yote hayatawezekana kwa sababu zifuatazo:-

- Chombo cha kutoa haki hakitakiwi kufanya huduma zake kuwa ghali kiasi cha kuwafanya wadaawa wanaotafuta haki washindwe kukiendea kwa sababu ya kutomudu gharama. Kufanya hivyo kutafunga mlango wa jumba la haki kwa wahitaji waliowengi. Hiyo itakuwa ni "denial of access to justice." Haki ya kupata haki ni haki ya msingi sana na ndiyo inayofanya dhana ya kuwepo na haki iwe na maana.

- Mahakama jukumu lake la msingi ni kutoa haki, sio kutafuta fedha kwa ajili ya kujiendesha. Mahakama ina wataalam wa sheria, sio wataalam wa miradi ya uchumi wala wataalam wa fund rasing. Kwa hiyo dhana ya mahakama kujiendesha yenyewe ni potofu. Hoja ya pili ni kuwa hakuna sababu kwa kwa mahakama ya kadhi kutogharimiwa na Serikali. Zipo sababu kadhaa za kupendekeza hivi:-

i) Katika mamlaka yake ya kawaida mahakama ya kadhi itasikiliza na kuamua mashauri yaleyale ya sheria ya Kiislam ambayo sasa yanasikilizwa na kuamuliwa na mahakama za kawaida za Serikali kwa gharama za Serikali. Tatizo kubwa ni kuwa mahakama hizo hazina sifa wala nia ya dhati ya kushughulikia migogoro ihusuyo Sheria ya Kiislam. Kwa hiyo kinachotakiwa sasa ni kushughulikia migogoro hiyohiyo kwa kupitia mahakama yenye sifa stahiki na utayari wa kufanya hivyo. Hakuna gharama mpya katika kuendesha mashauri haya kwani ni mzigo uleule utatolewa katika
mahakama za kawaida na kuwekwa katika mahakama za kadhi.

ii) Maeneo ya migogoro yanayopendekezwa kushughulikiwa na mahakama ya kadhi ni pamoja na ndoa, talaka, uzazi wa watoto, mirathi, ulezi na matunzo ya watoto, wakfu, na kadhalika. Wale wasiotumia sheria ya Kiislam nao pia wanayo migogoro katika maeneo haya na wanahudumiwa na mahakama za kawaida. Baada ya Mahakama ya kadhi kuanzishwa, wasiotumia sheria ya Kiislam wataendelea kuhudumiwa na mahakama za kawaida kwa gharama za Serikali. Lakini watumiaji wa Sheria ya Kiislam wawapo na migogogoro iliyosawa na hiyo ya wenzao, wao wanatakiwa wagharimie wenyewe. Hili linakinzana na dhana ya usawa mbele ya sheria. Wakati mashauri ya wengine yanagharimiwa na Serikali kwa kodi za wote, Waislam wanaambiwa wayagharimie ya kwao wao wenyewe. 

iii) Suala la Serikali kugharimia vitu vya watu wa dini moja si geni wala si jipya. Wakristo kupitia Memorandum of Understanding wanajipatia mabilioni ya shilingi kutoka katika bajeti ya Serikali kugharimia mahospitali yao na mashule na vyuo vyao. Kitendo cha kuyapa makanisa mapesa hayo yoyote kwa mkataba wa kipekee na wa siri baina yao na Serikali ambao hautoi fursa na wasiokuwa wakristo nao kupatiwa fedha kama hizo ni kitendo cha kibaguzi. Hapa hakuna usawa. Si sawa na suala la mahakama kwa kuwa watu wote wanapata fursa ya kutatuliwa migogoro yao kwa gharama za Serikali. Lakini makanisa yanapewa fedha ambazo wengine hawapewi sio kwa sheria bali kwa mkataba hususia. Huu ndio upendeleo halisi na ubaguzi. Kwa kutoa fedha kwa makanisa Serikali inaajingiza katika mambo ya kidini kwani hayo makanisa yanaita utoaji wa huduma hizo kuwa ni utume. Ukisoma machapisho mbalimbali ya makanisa husika utaona kuwa wanatumia huduma hizo kufikisha ujumbe wao wa kiroho. Kwa Serikali kujiingiza kuyapa fedha makanisa kwa ajili ya kuyasaidia katika kutoa huduma hizo inayasaidia kufanya kazi ya kidini.

iv) Mahakama ya Kadhi ipo na inafanya kazi Zanzibar katika Jamhuri hii hii. Zanzibar mahakama ya kadhi ni chombo cha kiserikali na inagharimiwa na serikali. Ikiwa ni halali Zanzibar, chini ya Katiba hii hii ya Jamhuri ya Muungano, itakosa vipi uhalali Tanzania Bara? Vipi mahakama iwe halali upande mmoja wa Muungano na ivunje katiba upande wa pili misingi ya kikatiba ni ileile.

v) Zipo mahakama za makundi ya watu maalumu ambazo zinaendeshwa kwa pesa za serikali ambazo ni kodi za watanzania wote. Mfano ni kama vile mahakama ya kazi, Ardhi, Biashara n.k ni kwanini mahakama itakayotafsiri sheria za Kiislamu iwe tofauti?

11.2 MAPENDEKEZO YETU:
Sheria iweke wazi kuwa mahakama ya kadhi itagharimiwa na Serikali sawa na zinavyogharimiwa mahakama nyingine. 

12. MAMLAKA YA WAZIRI KUTOA MATAMKO YA SHERIA YA KIISLAMU:
12.1 HOJA:
Sheria kama ilivyo sasa na hata baada ya marekebisho yaliyomo katika muswada inampa Waziri wa Sheria mamlaka ya kutoa matamko ya sheria ya Kiislamu. Sheria haimlazimishi waziri kufanya hivyo kwa kufuata muongozo wa maulamaa wa Kiislamu au baada ya kushauriana na chombo chochote cha Kiislamu. Hili si jambo zuri kwa sababu Waziri si mtaalamu wa sheria ya Kiislamu. Ni vyema Waziri katika kutekeleza hili akapata ushauri na mwongozo wa maulamaa wa Kiislamu kwa kuwa wao ni wataalamu katika fani hiyo. Sheria hii, The Islamic Law (Re-Statement) Act, sura ya Sura ya 375 inampa Waziri mamlaka ya kutoa matamko ya sheria ya Kiislamu. Lakini hakuna mamlaka ya kufanyia matamko hayo marekebisho pale itakapo bainika kuwa kuna makosa, kasoro au upungufu katika matamko hayo.

12.2 MAPENDEKEZO YETU:
Tunapendekeza kuwa Baraza la Sheria za Kiislam liliotajwa katika ibara ya 4 hapo juu ndiyo litaandaa matamko hayo, Waziri wa Sheria mamlaka yake yawe ni kuyapitisha matamko yaliyoandaliwa na Baraza la Sheria za Kiislam hilo kuwa kanuni. Pale Baraza la Sheria za Kiislam tajwa litakapobaini kuwa kuna kosa, kasoro au upungufu katika tamko lolote lile la Waziri, basi litaandaa marekebisho na kuyapendekeza kwa waziri ili ayapitishe.

13. ULAZIMA WA MAHAKAMA YA KADHI KUTAJWA NDANI YA
KATIBA:
13.1 HOJA:
Kutokutajwa ndani ya Katiba inayopendekzwa kunaweza kukaifanya mahakama ya kadhi kutokutambuliwa kama mahakama halali kikatiba. Hii inaweza kupelekea mgogoro mkubwa kwa mahakama nyingine kuweza kuhoji uhalali wa kikatiba wa mahakama ya kadhi. Mahakama nyingine, huhusan Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama ya Katiba zinaweza kubatilisha maamuzi yake na hata kutoa maamuzi ya kuifuta kabisa.

13.2 MAPENDEKEZO YETU:
Kuna ulazima wa kuiwekea mahakama ya kadhi msingi wa Kikatiba ili uhalali wa kuwepo kwake na utendaji wake usihojiwe na mahakama nyingine ili kuepusha migongano na migororo huko mbeleni.

SEHEMU YA TATU: PENDEKEZO LA MUSWADA ULIOREKEBISHWA:
Pamoja na maoni yetu haya tunawasilisha katika Kiambatanisho na. 1 pendekezo la muswada uliorekebishwa ili kukidhi matakwa tuliyoyaelezwa katika Sehemu ya Pili ya maoni haya.

Tunaomba kuwasilisha:

Jina Kamili /Taasisi /Wadhifa/ Sahihi
  1. Sheikh Suleiman A. Kilemile
  2. Hay Atul- Ulamaa Mwenyekiti 
  3. Sheikh Abdallah A. Bawazir Hay Atul -Ulamaa Makamu Mwenyekiti
  4. Sheikh Abdallah R. Ndauga Hay Atul - Ulamaa Mdhamini
  5. Sheikh Hassan Abbas Semkuya Shura ya Maimamu Makamu Amir
  6. Sheikh Hamad Iddi Almas Shura Ya Maimamu Imamu
  7. Dr. Said A Sima DUMT Makamu Mwenyekiti
  8. Musa M. Hans DUMT Katibu 
  9. Eng. Sherally H. Sherally BASUTA Mdhamini
  10. Sheikh Mohammed Issa BASUTA Naibu Katibu
  11. Sheikh Shams Elmi BASUTA Mjumbe
  12. Sheikh Shaaban Mussa BASUTA Katibu
  13. Eng. Alliy S. Kilima An-Nahl Trust Amir
  14. Dr. Hamdun Sulayman An-Nahl Trust Katibu
  15. Sheikh Mussa Yusuf Kundecha Baraza Kuu Amir Mkuu
  16. Maulana Ramadhan Sanze Baraza Kuu Katibu Mkuu
  17. Mwl. Fadhil Ally Chambo Jumuiya na Taasisi Mwenyekiti
  18. Ust. Jaffar Said Mneke Jumuiya na Taasisi Katibu
  19. Sheikh Khalfan Athuman Khalfan JASUTA Katibu Mkuu
  20. Sheikh Awadhi Mussa Mfinanga JASUTA Mdhamini
  21. Dr Pazi TAMPRO Katibu Mkuu Sheikh Karmal Msuya TAMPRO Kaimu Mwenyekiti
  22. Advocate Othman Kalulu IPC Katibu


No comments: