Thursday, 8 January 2015

SHEIKH ALI KOMORIAN: TAA ILIYOZIMIKA GHAFLA - ALHAJ ABDALLAH TAMBAZA

Sheikh Ali Mzee Comorian Akizungumza Katika Khitma Saigon Club 2012
Sheikh Ali Komorian:
Taa Iliyozimika Ghafla


Na Alhaj Abdallah Tambaza

WENGI wa wenyeji wa jiji la Dar es Salaam, hususan waumini wa dini ya Kiislamu, Jumapili ya Desemba 28, 2014 itakuwa siku ya kukumbukwa baada ya kuondokewa na mmoja wa masheikh mashuhuri wa jiji hili, Ali Mzee Komorian.

Kwa hakika jiji lilizizima baada ya habari za msiba ule mzito kusambaa miongoni mwa ndugu, marafiki na waumini wa dini ya Kiislamu— hasa wa maeneo ya Kariakoo— kwamba Sheikh wa ‘Darisalamu’(kama alivyopenda kujiita), hatunaye tena.

Nilikuwa ofisini kwenye Chumba cha Habari cha gazeti la Raia Mwema, Kinondoni, Dar es Salaam wakati simu yangu ya kiganjani ilipoashiria ujumbe mfupi:

“…msiba mzito wa mpenzi wa Mtume Sheikh Ali bin Mzee Komorian amefariki leo saa 5 asubuhi na mazishi bado kupangwa… Inna lillah…”

Alikuwa Alhaj Mussa Shaggow, aliyenitumia ujumbe ule kunipasha habari zile nzito ambapo baada ya hapo, simu nyingine nyingi zilifululiza kuleta habari zile za huzuni kubwa.  Haikuwa siku nzuri kwangu hata kidogo.

Maziko ya Sheikh Ali yalifanyika siku ya Jumatatu asubuhi na mwandishi huyu alikuwa miongoni mwa maelfu ya waombolezaji waliofurika kwenye Msikiti wa Makonde kupata fursa ya kuswalia jeneza lake.

Watu walikuwa wengi sana kiasi cha kusababisha wengine kuswalia nje barabarani na wengine kukosa fursa hiyo kabisa. Swala ya jeneza iliongozwa na rais mstaafu Sheikh Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa na uhusiano naye wa karibu mno.

Kama vile kuashiria namna fulani ya muujiza, jeneza lilobeba mwili wa marehemu lilipoanza kuwekwa mabegani tu, yakaanza kuanguka manyunyu mepesi mepesi ya mvua, kitu ambacho kilitafsiriwa na wengi kwamba ilikuwa ni bishara njema.

Mvua ile iliongezeka na kuwa kubwa iliyoambatana na mingurumo na radi zenye kutisha. Giza nene likatanda maeneo yote ya Kariakoo kuelekea makaburi ya Ngazija.

Allah (S.W.T), pengine alikuwa akituonyesha kwamba mja wake yule tunayekwenda kumzika hakuwa mtu wa kawaida.

Vyovyote vile iwavyo, mvua ile ilisababisha mimi na ‘sahib’ yangu Alhaj Mohamed Said, kushindwa kufika makaburini.

Gari letu lilikwama kwenye foleni maeneo ya Faya kwa zaidi ya saa nzima huku barabara zote za kuelekea Kisutu zikiwa zimejaa maji yasiyo kifani.

Mvua Kubwa Iliyonyesha Siku ya Maziko

Safari yetu iliishia hapo; tukamwombea dua ya ‘ghaib’ tukaelekea nyumbani kupumzika.

Said ‘Kilomoni’ Marjebi, yeye alikuwapo pale makaburini Ngazija wakati wa maziko. Nilikutana naye jioni— huku machozi bado yakimlengalenga – alinisimulia yaliyojiri: “… eh, bwana wee! Mungu katuonyesha utukufu wa Sheikh Ali kupitia mvua…“mwili wa marehemu ulipokuwa unashushwa kaburini, radi za vishindo ziliongezeka  …paa  …puu puu… mithili ya mizinga ile wapigiwayo watukufu wa kidunia wazikwapo,” alimaliza.   
           
Nilimfahamu Ali Mzee Komorian, (60), miaka miaka mingi iliyopita (1960s), sote tukiwa vijana wadogo, ingawa mimi ni mkubwa kwake kiumri.

Yeye alikuwa akisoma na wadogo zangu binamu, Ibrahim Mussa Pazi na Said Marjebi maarufu Said Kilomoni pale Shule ya Msingi Olympio, Upanga, jijini Dsm.

Kijana Ali, alikuwa akija kwetu mara kwa mara akiwa na rafiki zake hao, wakiwa ama wanakwenda au wanarudi kutoka shule wakati wa mchana wakicheka na kufurahi pamoja.

Lakini nikiangalia nyuma sawasawa (in retrospect), kumbukumbu zinanielekeza kwamba nilimfahamu mamake kwanza kabla ya kumjua Sheikh Ali mwenyewe.

Mwalimu Bahia, ndiye mama mzazi wa Sheikh Ali Komorian. Mama huyu, kwenye miaka ya 50 wakati nchi yetu ikiwa bado inatawaliwa na wakoloni, alikuwa akitembelea shule za msingi za Dar es Salaam kufundisha dini ya Kiislamu.   

Kuanzia mwaka 1958 mpaka mwaka 1961 nilipokuwa mwanafunzi pale Shule ya Mnazi Mmoja, alikuwa ni Mwalimu Bahia aliyekuwa akija kutufundisha somo la dini wanafunzi wote wa Kiislamu kwenye ‘holi’ la shule kila Ijumaa.

Kamwe siwezi kuisahau kazi hiyo ya mamake Sheikh Ali, kwani katika umri ule wa utoto, nilikuwa ‘nainjoi’ sana kashata nzuri za nazi ambazo mwalimu Bahia alikuwa akituuzia na sisi kuzila wakati darasa likiendelea.

Mwalimu Bahia, pia ndiye mwanamke anayeongoza shughuli nyingi za kidini jijini Dar es Salaam kwa upande wa wanawake wa Kiislamu.

Huwa mbele katika mazishi; huratibu na kuongoza shughuli za maulid kwa upande wa kina mama; na pia huwepo kwenye harusi upande wa kina mama iwe majumbani au kwenye maholi akiwa pamoja na watoto wake wa madrassa.

Katika miaka yangu ile ya ukuaji katika jiji la Dar es Salaam, nilimfahamu pia babake marehemu Sheikh Ali. Alikuwa msomi bobezi wa dini ya Kiislamu na mtunzi mahiri wa vitabu mbalimbali vya dini vikiwamo vya utenzi na mashairi ambayo sasa ni nadra au haiwezekani kabisa kumpata mtunzi wa kiwango cha bwana mkubwa yule.

Sheikh Mzee bin Ali (baba) pia ameacha kumbukumbu itakayodumu miaka mingi, kwani aliweza kutafsiri na kuyafanya Maulid ya Barzanji kuweza kusomwa Kiswahili kwa maghani yake yaleyale ya asili.

Marehemu Sheikh Ali bin Mzee bin Ali Komorian, alizaliwa mnamo mwaka 1954 mtaa wa Kibambawe, Kariakoo, Dar es Salaam akiwa mtoto mkubwa na pekee wa kiume kati ya watoto saba  familiani.

Habari zinasema, elimu yake ya madrassa (elimu ya dini) ya mwanzoni, aliipata nyumbani kwao kwa babake na mamake kabla ya kwenda kwa masheikh wengine akiwamo aliyewahi kuwa Mufti na Mudir wa Zanzibar Muslim Academy, Sayyid Omar Abdallah (Mwinyibaraka), Sheikh Ramadhan Abbas na masheikh wengi wengine jijini Dar es Salaam.     

Alijiunga na Shule ya Msingi Olympio ya Upanga, Dar es Salaam kwa masomo ya elimu ya kizungu na baadaye kumalizia elimu ya Sekondari, Kinondoni Muslim kwenye miaka ya 1970s.

Ukiachilia mbali mambo ya elimu, Ali Mzee, kama walivyo vijana wengi wa umri wake, alijiunga na vilabu mbalimbali vya watoto kucheza mpira.

Mwandishi huyu alimshuhudia akiwa golikipa machachari kwenye timu maarufu ya watoto ya West England iliyokuwa maeneo ya nyumbani kwao.

Timu hiyo ilikuwa ikiongozwa na kina Abdallah Katungunya, Ndege na Kocha Muharam Shakuku. 

Baadaye, Ali Komorian, alikuja kuwa mwanachama wa klabu ya Saigon ya Dsm, ambako alijijengea jina kwa kuwa kioo cha klabu hiyo kila zinapofanyika hafla mahala hapo.
Klabu ya Saigon, leo hii bado imeendelea kuwa kivutio na mfano wa kuigwa (exemplary) kwa kudumisha silka, silsila na tamaduni za watu wa ‘Kidarisalama’.

Saigon, kwa miaka mingi sasa imedumu katika kufanya kumbukumbu ya kuwaenzi na kuwaombea dua wazee, masheikh, pamoja na wanachama wenzao waliokwishatangulia mbele ya haki.


Kila mwaka, almarhum Ali Komorian amekuwa mshereheshaji mkubwa kwenye hafla hizo— piga ua atakuwa mzungumzaji au mtoaji dua wa mwisho.  

Bila shaka, katika hafla itakayofanyika mwaka huu jina lake litakuwa miongoni mwa warehemewa wa mwanzo kabisa.

Daima ilikuwa ni hapo Saigon ambapo mara nyingi amekuwa akihubiri upendo, subira na kukemea maovu miongoni mwa jamii. Hakupenda hasama na mifarakano baina ya watu.

Hili lilidhihirika katika maudhui ya tungo zake za mashairi na Qassida  alizozitunga zikiwa na maneno mazito yenye mafunzo hayo.

Msomaji zingatia beti hizi hapa chini:

“Ugomvi wa nini; patana…patana…
Tutagombana mpaka lini…
Patana…patana…patana
Ni khasara leo na kesho kiyama…”

KHITMA YA SAIGON CLUB


Sheikh Ali bin Sheikh Mzee Comorian Akizungumza Katika Khitma ya
Saigon Club Tarehe 24 Juni 2012

Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi Akiwasili Katika Khitma Saigon Club



Wa Pili Kushoto Kwenda Kulia - Stephen Rupia (Mpuya) Alhaj Abdallah Tambaza
na Alhaj Ali Momba
Mbele ni Alhadi Mussa Sheikh wa BAKWATA Mkoa wa Dar es Salaam
na Kulia ni Boi Juma Risasi.
Nyuma ni Mufti wa BAKWATA Sheikh Shaaban Simba Akisindikizwa na Muharram Mkamba
Hao Watatu Wenye Kanzu ni Wahudumu Katika Khitma
Kushoto Kwenda Kulia: Abdulbari, Juma Abeid na Alhaj Musa Shagow
Pembeni Yao Kushoto ni Stone na Kulia ni Simba



Aliyevaa Kashda Kushoto ni Shariff Hussein Badawiy na Kulia kwake ni Iddi Simba na
Kushoto Kwake ni Hamza Kassongo
Balozi Abbas Sykes Akizungumza na Mwinyi Mangara
Kutoka Kushoto: Dk. Tamim Bushiri, Mohamed Said, Abdallah Miraj na Mbwana



Maneno ya mashairi hayo hapo juu yameweza kusaidia kupatanisha watu wengi sana waliokuwa wamegombana na kushindwa kupatana kirahisi.

Miongoni mwa tungo zake nyingi nyengine ambazo zitadumu kupendwa na kuenziwa na jamii ni; ‘Usisikitike Allah alilokadiri…’ na ‘Haya Tumpendeni…’ wenye kumsifu na kumtukuza Mtume Muhammad (S.A.W).

Ali Komorian, alikuwa mpenzi mkubwa wa Mtume Muhammad (SAW), kiasi cha kufikia kujiita (self proclaimed) Ahbabi Rassul (mpenzi wa Mtume).

Alikuwa kweli mpenzi wa Mtume na wala alikuwa hafanyi mzaha; kwani katika uhai wake hakuchoka kuhudhuria hafla za Maulid kila zilipofanyika na yeye kupata habari zake.

Almarhum Sheikh Ali, alikuwa si mtu wa kupenda kujikweza na kupenda ukubwa na utukufu. Fahari na majivuno pia vilimpitia mbali.

Akikazia nukta hiyo ya udhalili (simplicity) wa Ali Komorian, Imam Mkuu wa Msikiti wa Mtoro, Sheikh Zubeir Yahya aliyepewa fursa ya kutoa wasifu wa rafiki yake kwenye khitima anasimulia kisa hiki:

“…kuna tajiri mmoja anaitwa Zakaria alimwita marehemu na kumpa gari la kifahari liwe mali yake limsaidie katika maisha yake marehemu alilikataa gari lile na kumjibu Zakaria kwamba yeye hufurahi zaidi  anapokanyaga kwenye ardhi ya Allah…
Marehemu alichelea huenda gari lile likamfanya ajione bora na kuwa mtu wa majivuno kitu ambacho hakukipenda,’’ alisimulia Sheikh Zubeir na kuuliza;“Je, ni nani kati yetu hapa msikitini, nikiwamo mimi na wewe, anaweza kupewa gari kama hilo na alirudishe namna hiyo?”

Mvua kubwa iliyonyesha asubuhi ile ya maziko ilimzuia Rais Jakaya Kikwete kufika makaburini kuzika. Kufuatia hali hiyo, rais alielekea nyumbani kwa marehemu kwenda kutoa mkono wa tahania kama vyombo vya habari vilivyomwonyesha akiwa pale na ndugu wa marehemu.
Tunamwomba Mungu awape subira na uvumilivu wafiwa wote na marehemu ampumzishe kwenye pepo yake ya Firdaus:

Yailahi Yasatari Tustiri Yalatwifu,
Utupe riziki za kheri viumbe vyako dhaifu;
Kila jema liwe ndilo tusamehe Mola wetu;
Mikono tumeinua kukuomba  Yakarimu;
Utakalo Mola huwa pasi dakika kutimu.


Simu: 0715 808 864 /0784 808 864          

No comments: